Wednesday, April 9, 2014

Uganda yatuma ujumbe polisi wake kuvamia Tanzania

Ujumbe  wa askari wa Jeshi la Polisi la Uganda umewasili nchini kwa kile kinachodaiwa kuja kufanya mazungumzo ili kupata maridhiano kufuatia kitendo cha askari wake wakiwa na bunduki kuvamia eneo la Mutukula, mkoani Kagera, na kurusha risasi ovyo zilizojeruhi Watanzania wawili.

Habari zilizopatikana jana zinaeleza kuwa askari hao ujumbe wa askari hao umewasili nchini wakiongozwa na mmoja wa viongozi wakuu wa Jeshi la Polisi Mbarara, nchini humo.

NIPASHE, ambayo ilifika katika Kituo Kikuu cha Polisi jana asubuhi iliwashuhudia askari wanne wa Uganda waliovalia sare, wakiwa nje ya kituo hicho, ambako mwenzao mmoja anashikiliwa kwa tuhuma hizo.

Hata hivyo, habari nyingine zilieleza kuwa mbali na kuja kutafuta maridhiano baina yao na wenzao wa Tanzania, ujumbe huo pia umekuja nchini kwa ajili ya kumchukulia dhamana mwenzao anayeshikiliwa na polisi wa Tanzania.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, George Mayunga, alipotakiwa jana kuelezea suala hilo, alisema hadi jana alikuwa hajapata kibali cha kuzungumzia suala hilo kutoka Makao Makuu ya Polisi, jijini Dar es Salaam.

Msemaji wa Jeshi hilo nchini, Advera Senso, jana hakupatikana kuzungumzia kinachoendelea kuhusiana na kadhia hiyo na hata alipopigiwa simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita bila kupokelewa.

Hata hivyo, juzi alikaririwa akisema kinachopfanywa na Jeshi la Polisi ni kuchunguza ili kujua sababu za askari hao kuendesha operesheni hiyo nchini bila kuwaarifu wenzao wa Tanzania kama sera ya Interpol (Polisi wa Kimataifa) inavyotaka.

Askari saba kutoka Uganda Jumamosi wiki iliyopita wakiwa na silaha hizo, walivamia eneo hilo kwa kile kilichodaiwa kuwa walikuwa wakiwatafuta watuhumiwa wa wizi wa pikipiki waliokimbilia Tanzania.

Chanzo: Nipashe

No comments: