Wednesday, April 9, 2014

Hofu yatanda malumbano makali kuibuka kesho

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa,Peter Kuga Mziray.
Mwenyekiti  wa Baraza la Vyama  vya Siasa, Peter Kuga Mziray, ameonyesha wasiwasi wake kwamba huenda mvutano mkubwa ukazuka bungeni kesho na Ijumaa wakati kamati 12 za Bunge Maalum la Katiba zitakapowasilisha taarifa bungeni baada ya kupitia na kuchambua sura mbili za Rasimu ya Katiba, ya kwanza na ya sita.

Sura ya kwanza inazungumzia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Alama na Sikukuu za Taifa, Lugha za Taifa na lugha za alama na Tunu za Taifa.

Sura ya sita inazungumzia muundo wa Muungano, vyombo vya utendaji vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mamlaka ya serikali ya Muungano, mambo ya Muungano, nchi washirika, mamlaka ya nchi washirika, mahusiano kati ya nchi washirika, mawaziri wakaazi, mamlaka ya wananchi na wajibu wa kulinda Muungano.

Akizungumza na NIPASHE jana, Mziray alisema mambo yalikwenda vizuri katika vikao vya kamati, lakini kujadili sura hizo mbili ndani ya bunge zima mabishano yataanza.

“Hizo sura mbili ndizo zinaleta ugumu, ndipo kwenyewe,” alisema Mziray ambaye pia ni Mjumbe wa Bunge hilo na kuongeza: “Hali bado siyo nyepesi, bado sura hizo ndizo ngumu na ndizo zinaleta mambo.”

Aprili Mosi, mwaka huu kamati 12 za Bunge hilo zilitawanyika katika maeneo manne kwa ajili ya kuchambua na kujadili sura ya kwanza na ya sita ambazo ndizo zenye mvutano mkali.

Miongoni mwa mambo ambayo yalizua utata katika Sura ya Kwanza ni ibara 1(1)  inayosema  Tanzania ni nchi na Shirikisho lenye mamlaka kamili ambalo limetokana Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambazo kabla ya Hati ya Makubalino ya Muungano ya mwaka 1964 zilikuwa nchi huru.

Katika ibara hiyo wajumbe kadhaa walitaka neno shirikisho ilitoke badala yake iwe Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi yenye mamlaka kamili.

Hali hiyo ilisababisha baadhi ya kamati kukosa theluthi mbili ya kura kutoka katika kila upande wa muungano ambazo zinatakiwa kwa mujibu kanuni 64 (1).

Eneo lingine lililozua mvutano ni Ibara  1(3) inayosema Hati ya Makubaliano ya Muungano iliyorejewa katika Ibara ndogo ya kwanza ndiyo msingi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba hii kwa kadri itakavyorekebishwa, itakuwa ni muendelezo wa makubaliano hayo.

Kutokana na hali hiyo, wajumbe kadhaa walitaka ufafanuzi kuhusu Hati ya Muungano na kutaka kuiona.

Hali hiyo ilisababisha kamati Na 2 na 8 kumuita aliyekuwa Katibu wa Bunge wakati wa Muungano, Pius Msekwa, kwenda kutoa maelezo. Hata hivyo, suala hilo bado halijapata ufumbuzi hususani mahali ilipo hati hiyo na madai ya utata wa saini.

Katika hatua nyingine, Mziray alisema kuwa baraza lake liliandaa mkutano wa dharura wa viongozi wa vyama vya  siasa kwa ajili ya kupata mwafaka na kuwekana sawa kufuatia matukio kadhaa ya mivutano katika Bunge Maalumu la Katiba Jumatatu iliyopita, lakini uliahirishwa kutokana na uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Chalinze na Siku ya Kumbukumbu ya Karume.

Alisema siku inayoweza kupangwa ni Jumapili ambayo ni rahisi kuwapata viongozi wengi kwa kuwa hakuna vikao vya Bunge.

Naye Katibu wa Baraza hilo, Jaji Francis Mutungi, aliiambia NIPASHE kuwa wanauandaa tena mkutano huo ili ufanyike kati ya Aprili 22 na mwisho wa mwezi.

Jaji Mutungi ambaye pia ni Msajili wa Vyama vya Siasa, alisema watawawaalika watu wengine wakiwamo viongozi wa dini na kwamba kabla ya mkutano huo, atakutana na baadhi ya makatibu wakuu wa vyama vya siasa.


CHANZO: NIPASHE

No comments: