Friday, April 4, 2014

Lembeli: Nitasimamia ninachoamini bila hofu ya kushughulikiwa

Dodoma.Uamuzi wa kupiga kura umepita kwa makubaliano ya kupiga kura mseto utakaoruhusu mjumbe kupiga kura kwa aina anayoitaka; kupiga kura ya wazi au ya siri.

Uamuzi huo  ni wa kihistoria kwa kuwa haujawahi kutumika kokote duniani. Baadhi ya wajumbe wameonyesha kufurahishwa nao na wengine kuupinga.

Kwa sehemu kubwa kura ya wazi ilikuwa ni msimamo wa wajumbe wanaotoka kundi la wanasiasa hasa wanaotoka Chama cha Mapinduzi (CCM).

Hata hivyo, miongoni mwa wajumbe hao wa CCM, wapo ambao walipinga tangu mwanzo suala hilo, wakisema mfumo huo unawakandamiza na hauna tija kwa taifa.

Miongoni mwa wajumbe ni Alli Keissy, Kangi Lugola, Deo Filikunjombe, Esther Bulaya, Juma Kapuya na James Lembeli.

Hatua ya wajumbe hao kupingana hadharani na matakwa ya chama chao, inaweza kuchukuliwa kama ujasiri wa kipekee, kwani wanafanya hivyo, wakijua ndani ya chama chao baadhi ya wajumbe wameadhibiwa kutokana na kutofautiana kimtazamo na chama.

Kura ya mseto ilipitishwa kwa kila mjumbe kuitwa jina lake na kueleza kukubali au kukataa. Hapo ndipo misimamo ya wengi ilionekana.

Wabunge Kangi Lugola na Deo Filikunjombe walionyesha misimamo yao hadharani baada ya kupingana na matakwa hayo ya chama kwa kupinga kura ya wazi. Wakati kura hiyo inapigwa, wajumbe James Lembeli na Profesa Juma Kapuya hawakuwapo ukumbini.

Nikiwa bungeni nimepata fursa ya kuzungumza na Lembeli nikitaka kujua msimamo wake ulikuwa upi kama angekuwapo bungeni siku hiyo ya kupiga kura na yafuatayo ni mahojiano yetu:

Swali: Mheshimiwa Lembeli, pole na shughuli za hapa bungeni wakati wa kupitisha kanuni za 38 na 39, sikubahatika kusikia sauti yako mle ukumbini hivi uliunga mkono kura ipi?

Jibu: Asante, sijapoa maana kazi ndio imeanza, lakini na ninyi mmeanza uchokozi…(kicheko). Kweli haukunisikia kwa sababu sikuwepo.

Swali: Kama ungekuwepo kura yako ilikuwa katika mrengo upi mheshimiwa?

Jibu: Hata siku moja siwezi kula matapishi yangu. Nimekuwa nikisimamia ukweli na ukweli ndio utakaoniweka huru siku zote za maisha yangu. Mimi nataka kura ya siri na ndiyo ambayo ningeitaka siku hiyo bila hofu.

Swali: Kura ya siri inapingwa na chama chako, ni vipi uendelee kuing’ang’ania kwani huogopi kushughulikiwa kisiasa?

Jibu: Vijana msipende kutishwa na jambo la kushughulikiwa. Anayeshughulika na mwanadamu ni Mungu pekee si mtu mwingine. Hapa tunafanya kazi za kujifurahisha tu jamani.

Ukisikia mtu anasema atakushughulikia, jiulize mara nyingi anashughulika na wewe kwa namna gani au juu ya jambo gani, je ni kwa jambo la ukweli au lile la kinafiki.

Swali: Kwa nini unasema hivyo, una maana chama chako hakina uwezo wa kufanya hivyo?

Jibu: Kinao, lakini najiuliza hivi mtu anashughulika nami kwa jambo gani? Je, kwa matakwa ya wananchi au kwa lipi hasa? Mimi nakipenda sana chama changu kuliko wengi wanavyofikiri lakini nasimamia ukweli ambao chama pia kinautaka.

Swali: Kwa mtazamo wa wengi ni kwamba Tanganyika uliyokuwa ukiishabikia sasa ndiyo imezikwa rasmi kutokana na wingi wa kura za wanaopinga rasimu hii, wewe unasemaje?

Jibu: Haiwezi kufa ili mradi watu wanataka ife. Subirini mle ndani mtatuona, nitaanzia kwenye kamati yangu hadi tutakaporudi humu ndani. Nasema historia huwa haikarabatiwi.

Swali: Sasa umeshindwa kuonyesha msimamo wako kwa wapiga kura ambao unasema ndio watu wa kuwaheshimu zaidi. Je, unawaahidi nini katika mchakato huu?

Jibu:Nasisitiza kuwa msimamo wangu haupingani na wapiga kura walionituma bungeni na nikipingana kwa kupiga kura ya wazi hapo watakaponihukumu, lakini nikiwa pamoja na mawazo yao lazima watanitendea haki.

Swali: Lakini umekuwa na mawazo kinzani wakati wote kuhusu Rasimu ya Katiba, nguvu ya aina hii unaipata wapi?

Jibu: Siyo mawazo kinzani. Naishi kwa kujifunza na kuangalia watangulizi wetu walisema nini, mfano Mwalimu Nyerere aliwahi kusema Watanzania wanataka mabadiliko na wasipoyapata ndani ya CCM wanaweza kutafuta kwingine. Kwa hiyo mabadiliko ni lazima yaanzie kwetu sisi wa chama tawala.

Chanzo: Mwananchi

No comments: