Saturday, April 5, 2014

Mjumbe alazimishwa kupiga kura ya wazi

WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikiendelea kumwandama kwa kejeli Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, mmoja wa makamishna wa tume hiyo naye ameonja ‘joto ya jiwe’ kwenye kamati za Bunge Maalumu la Katiba.

Mjumbe huyo ni Al- Shymaa Kweigyir (mbunge), ambaye jana  alishulutishwa na wajumbe wenzake wa CCM kupiga kura ya wazi ili kukataa kuafiki ibara ya kwanza ya sura ya kwanza ya rasimu.

Kwa mujibu wa chanzo chetu, Kwegyir alikumbana na zahama hiyo wakati wa kupiga kura katika kamati yake namba 12 inayoongozwa na Paul Kimiti.

Ingawa Kimiti ambaye amekuwa mgumu kutoa taarifa za kamati yake kwa waandishi hakupatikana kuthibitisha tukio hilo, gazeti hili lilidokezwa kuwa Kwegyir aliomba kupiga kura ya siri ambayo CCM wanaikwepa akitaka kulinda uhuru wake kwa sababu ana masilahi na tume.

Kwa kawaida, Kwegyir kama mmoja wa wajumbe wa tume iliyoandaa rasimu  lazima angepiga kura ya kuunga mkono mapendekezo yao.

Kamati namba 12 ina wajumbe 53 ambapo 36 wanatoka Bara na 17 Zanzibar na ili kufikia theluthi mbili ya kura kwa Bara zilitakiwa 24 na Zanzibar 12.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, zilipopigwa kura za kuamua ibara ya kwanza ya sura ya kwanza, theluthi mbili haikupatikana kwa pande zote, ndipo CCM wakaaza kusaka ‘mchawi’ anayekwamisha.

Tanzania Daima lilidokezwa kuwa baadhi ya wajumbe wa CCM wakiwemo mawaziri walianza kumzomea Kwegyir wakimwita msaliti kwa sababu ndiye alipiga kura ya siri tofauti na msimamo wa chama chao.

“Hali hiyo ilimkasirisha Kwegyir hadi akafikia hatua ya kutoa machozi, akishangaa kuona ananyimwa haki yake wakati kanuni zinaruhusu mjumbe kupiga kura aitakayo kati ya wazi na siri.

“Baada ya hali kuwa mbaya, wajumbe wa upinzani waliingilia kati wakipinga kitendo hicho ingawa CCM waliendelea kumwandama wakitaka atamke wasikie kama anakubali pendekezo la ibara hiyo au hapana,” alisema msiri wetu.

Hata alipolazimishwa kupiga kura ya wazi kwa kutamka, inadaiwa kuwa Kwegyir alilikubali pendekezo la tume kuhusu muundo wa muungano wa serikali tatu.

Mjumbe Edward Lowassa (Mbunge wa Monduli) ndiye anadaiwa kuokoa jahazi hilo baada ya kuingilia kati na kuwasihi wajumbe wenzake kutulia, hivyo shughuli ya upigaji kura kusimama kwa muda.

Miongoni mwa viongozi wakubwa wa CCM wanaounda kamati hiyo ni, Prof. Anna Tibaijuka (waziri), Pandu Ameir Kificho (Spika Zanzibar), Binilith Mahenge (naibu waziri) na Aden Rage (mbunge).

Wapo pia Michael Laizer (mbunge), Ahmed Shabiby (mbunge), Amos Makalla (naibu waziri), Seleman Jaffo (mbunge), Henry Shekifu (mbunge na mwenyekiti wa CCM Tanga), Jesca Msambatavangu (mjumbe na mwenyekiti wa CCM Iringa) na wengine.

Theluthi mbili Zanzibar utata

Theluthi mbili ya kuamua ibara na sura za rasimu ya Katiba imekuwa kikwazo kwa kamati nyingi za Bunge Maalumu la Katiba hususan upande wa wajumbe wa Zanzibar.

Hali hiyo ilijitokeza jana wakati kamati hizo 12 zilipopiga kura ya kuamua vifungu vya ibara za sura ya kwanza na sita huku ibara ya kwanza inayopendekeza muundo wa serikali tatu ikileta mgawanyiko.

Katika ibara ya kwanza ya sura ya kwanza (1), rasimu inapendekeza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi na Shirikisho lenye mamlaka kamili ambalo limetokana na Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ambazo kabla ya hati ya makubaliano ya muungano ya mwaka 1964, zilikuwa nchini huru.

Wakizungumza na waandishi wa habari jana, baadhi ya wenyeviti wa kamati hizo walisema kuwa licha ya wajumbe kuafikiana katika baadhi ya ibara, lakini katika suala hilo la shirikisho waligawanyika kulingana na pande za muungano.

Hadi jana mchana hakuna kamati hata moja iliyokuwa imepata theluthi mbili kwa pande zote za muungano katika suala hilo la shirikisho ambapo wajumbe wengi wa CCM wanataka pendekezo hilo lifutwe kwa madai inakwenda kinyume cha hati ya makubaliano ya Muungano.

Ili kufikia theluthi mbili kwenye kamati yenye wajumbe 52 au 53, upande wa Tanzania Bara wenye wajumbe kati ya 33 hadi 37 unatakiwa kupata kura zaidi ya 23 za ndiyo na upande wa Zanzibar wenye wajumbe kati ya 15 hadi 19 zinahitajika kupata zaidi ya 10.

Kwa upande wa Bara ni rahisi kwa CCM kupata theluthi mbili kwa sababu ina wajumbe kati ya 23 hadi 28 kila kamati bila kutegemea za wajumbe wa kundi la kuteuliwa lakini kwa Zanzibar ni vigumu kwani idadi ya wajumbe wake inalingana na ile ya CUF.

Kutokana na msimamo wa vyama hivyo kuwa tofauti katika suala la muundo wa muungano ni vigumu kupata theluthi hiyo ya kura kwa upande wa Zanzibar.

Ibara ya pili kuhusu eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya tano kuhusu tunu za taifa zilizua ubishano mkali katika kamati nyingi kiasi cha baadhi ya wajumbe kuleta majedwali ya marekebisho wakiongeza na kupungua baadhi ya vitu.

Mwenyekiti wa kamati namba moja, Ummy Mwalimu, alisema kuwa katika sura ya kwanza yenye ibara tisa, ni ibara mbili za sita na tisa ambazo zilipata theluthi mbili ya kukubalika kwa pande zote.

Mwenyekiti wa kamati namba tano, Hamad Rashid Mohammed, alisema kwa sura ya kwanza, ibara ya pili, tano na saba zilikataliwa kwa theluthi mbili huku ibara ya kwanza ikikosa idadi hiyo ya kura kwa upande wa Bara.

Naye Anna Abdallah, mwenyekiti wa kamati namba 10, alisema hawakukubaliana kwa ibara nyingi na hivyo kufanya theluthi mbili  kushindikana hasa upande wa Zanzibar.

Hali kama hiyo ya wajumbe kutofautiana kuhusu muundo wa muungano ilijitokeza pia kwa kamati namba 11 inayoongozwa na Anne Killango Malecela na nane ya Job Ndugai, ambazo wajumbe wake walitarajiwa kupiga kura jana jioni.

Chanzo: Tanzania Daima

No comments: