Saturday, April 5, 2014

Nyalandu: Wafanyakazi pambaneni na ujangili

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amewataka wafanyakazi wa wizara hiyo kuhakikisha wanatumia kila mwanya uliopo kisheria kufanikisha mapambano dhidi ya vitendo vya ujangili.

Alitoa kauli hiyo mjini Morogoro jana wakati akifungua baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo, na kusema vitendo vya ujangili vimekuwa vikiathiri taswira ya maliasili, na kwamba hali hiyo itabadilika iwapo wafanyakazi wenyewe watawajibika ipasavyo.

Aliwataka wafanyakazi hao kubadilisha mwelekeo wa wizara hiyo na kupandisha morali ya kazi, kwani wizara ina rasilimali nyingi zinazoweza kuliingizia pato taifa kwa asilimia 70.

Alisema pamoja na serikali kuwa na mkakati wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), amewaasa watendaji wa wizara hiyo kujiwekea mikakati yao wenyewe kiwizara, ili kufanya kazi kwa tija.

Alisema kuanzia Mei mwaka huu hadi Julai, wizara itaanza kutoa mafunzo maalumu ya kupambana na ujangili kwa kutumia helikopta.

Chanzo: Tanzania Daima

No comments: