Friday, April 4, 2014

MICHEZONI: Kaseja agomea mechi Yanga

WAKATI kipa nguli wa timu ya Yanga, Juma Kaseja, akijisalimisha kambini Bagamoyo, wachezaji wengine wanne wakiwemo Haruna Niyonzima na Nadir Haroub ‘Canavaro’ hawapo kambini kutokana na kuwa wagonjwa.

Wachezaji Emmanuel Okwi, Kelvin Yondani na Athuman Idd ‘Chuji’ pia inadaiwa hawapo kambini kutokana na matatizo mbalimbali.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana mjini Bagamoyo jana kutoka kwa mmoja wa wachezaji wa timu hiyo, alithibitisha kuwa Kaseja amerudi kambini jana jioni, lakini Niyonzima na Canavaro wameondolewa kutokana na kuumwa.

“Huku tupo vizuri, tunafanya mazoezi kama kawaida, lakini kwa sasa morali umeshuka, si unajua tena kufungwa na Mgambo imekuwa tabu, Canavaro, Niyonzima hawapo wanaumwa, Yondani naye ameondolewa kuelekea mechi ijayo kwani anatumikia adhabu ya kadi mbili za njano,” alisema mchezaji huyo.

Alisema idadi yao imepungua ukilinganisha na mechi mbili zilizopita ambapo hata Chuji na Okwi hawaonekani kambini na wakimuuliza Meneja wao, Hafidh Salehe, hakuwa tayari kueleza chochote.

Alipoulizwa Ofisa Habari wa timu hiyo, Baraka Kizuguto, kuhusu wachezaji hao watano, alisema hana taarifa zozote kwani hakuwa amewasiliana na daktari wa timu tangu ilivyoondoka jijini Dar es Salaam.

Alisema anachojua timu imefika salama Bagamoyo na kuendelea na mazoezi na kwamba hata idadi ya wachezaji walioingia kambini juzi mjini humo haifahamu.

Chanzo: Tanzania Daima

No comments: