Wednesday, April 9, 2014

Mkono aikoromea serikali

Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM),Nimrod Mkono.

Aishangaa kutumia nguvu kubwa kulinda wanyamapori kuliko binadamu

Mbunge  wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono, ameishutumu serikali kwa kushindwa kudhibiti mauaji ya kikatili wanayofanyiwa wanawake katika baadhi ya vijiji vya tarafa ya Nyanja jimboni mwake akisema imekuwa ikitumia nguvu kubwa kulinda wanyama pori kuliko binadamu.

Mkono alitoa kauli hiyo juzi katika kijiji cha Mugango baada ya watu wasiojulikana kumnyonga hadi kufa kwa kutumia upande wa khanga, Anastazia Mang’ombe (42), baada ya kumbaka shambani kwake.

Mauaji ya mwanamke huyo ni mwendelezo wa mauaji ya kinyama na kikatili yanayotokea katika vijiji vya mwambao wa Ziwa Victoria vya Nyakatende, Etaro, Nyegina,  Mkirira katika tarafa hiyo yakihusisha wanawake.

Mpaka sasa, hao ni mauaji ya pili kutokea katika kipindi cha wiki mbili katika jimbo hilo.

Katika tukio la kwanza, mwanamke mwingine mkazi wa kijiji Kamguruki kata ya Nyakatende wilayani humo, aliuawa katika mazingira yanayofanana na hayo.

Alisema tangu kuibuka kwa wimbi la mauaji hayo ya kinyama ambayo hadi sasa yanahusishwa na imani za kishirikina, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na serikali licha ya viongozi wake kutoa kauli za kisiasa ambazo zimeshindwa kumaliza mauaji hayo na hivyo kuongeza hofu kubwa kwa jamii hasa wanawake.

“Jamani, mauaji haya ya wanawake mwisho wake utakuwa lini, hivi serikali iko wapi, mbona tembo mmoja tu akiuawa tunasikia filimbi na ndege zinaruka huku na huku kuwasaka wauaji? Iweje leo binadamu hasa hawa wanawake wanauawa bila hatia hatujasikia serikali imechukua hatua?

“Akina mama zangu wanauawa, wanachinjwa kama kuku, sijaiona serikali ikichukua hatua. Sasa ni wakati wa Waziri Mkuu na Rais wetu waje hapa ili kutusaidia kukomesha mauaji haya ya kikatili…hivi niwaweke wapi akinamama ambao sasa wanaishi kwa hofu kubwa?,” Alisema Mkono huku akibubujikwa na machozi.

Kwa sababu hiyo, mbunge huyo alisema serikali inaonekana kuwapuuza wananchi hao wanauawa kinyama kwani ina vyombo vya kuwabaini wauaji wote na kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Nakwenda bungeni kupigania hili kwani ni janga la kitaifa. Ikiwezikana serikali itangaze operesheni maalum kama ilivyofanya katika kupambana na ujangili,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Butiama,  Angelina Mabula, pamoja na kulaani vikali mauaji hayo, amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili kuhakikisha wauaji hao wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

“Kwa kweli hali ni mbaya, nawaomba muwe watulivu kwani matukio haya yametuchanganya. Wiki iliyopita wanawake wawili wameuawa hivi hivi ukiangalia matukio yote yanafanana na yanafanyika wazi. Sasa lazima tujiulize wote hapa kuna nini?," Alihoji.

Aliongeza: “Hata tufanyaje polisi hawawezi kutosha kulinda wote, lazima tuweke mikakati ya pamoja katika kushughulikia mauaji haya...kwa muda mfupi tu kwa eneo hili la kata nne, wanawake wanane wameuawa kikatili na mauaji yote yanafanana,” alisema.

Kwa msingi huo, aliwaomba wananchi kutoa taarifa za kina kwa vyombo vya dola zikiwamo ofisi za viongozi katika kuhakikisha mauaji hayo yanakomeshwa.

Hata hivyo, litoa agizo kwa wanaume kuwasindikiza wake zao mashambani na katika shughuli nyingine za kutafuta kipato wakati vyombo vya dola vikipambana na vitendo hivyo.

Alisema viongozi wa serikali sasa wameshindwa kuhamasisha shughuli za maendeleo kwani muda wote wamekuwa wakishughulikia matukio ya mauaji kila uchao.

Kwa mujibu mujibu wa Mkuu huyo wa Wilaya, hadi sasa watu watano wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji kama hayo huku wanne wakishikiliwa polisi kwa uchunguzi.

Naye katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Butiama, Mercy Mollol, aliomba serikali kutangaza eneo hilo kuwa kanda maalum ya kipolisi ili kuongeza idadi ya askari wa kukabiliana na mauaji hayo.

“Kama Chama tumesikitishwa sana na mauaji haya yanayoendelea katika eneo hili. Sasa tunaitaka serikali chini ya Rais Jakaya Kikwete na IGP Mango, kutangaza operesheni ya watu wanaoua wanawake kabla hatujatangaza maandamano makubwa ya kupinga ukatili huu,” alisema.

Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Ferdinand Mtui, akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Kamanda Mtui alisema hadi sasa watu watatu wanashikiliwa polisi kwa mahojiano.
Chanzo: Nipashe

No comments: