Sunday, April 6, 2014

Hukumu Chalinze Kujulikana Leo

TAMBO, mbwembwe na kejeli zilizokuwa zikitolewa kwenye mikutano ya kampeni za kuwania ubunge wa Chalinze leo zinatarajia kufikia kikomo wakati wakazi wa jimbo hilo watakapopiga kura
Wagombea watano kutoka vyama vya CCM, CHADEMA, CUF, NRA na AFP  ndio watakaomenyana kwenye kinyang’anyiro hicho.

Wagombea hao ni Mathayo Torongey (CHADEMA), Phabian Skauki wa (CUF), Vuniru Hussein (NRA), Ramadhani Mgaya (AFP) pamoja na Ridhiwani Kikwete (CCM).

Uchaguzi huo unafanyika kutokana na kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Said Bwanamdogo, kufariki Januari 22, mwaka huu.

Msimamizi wa uchaguzi huo ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo,  Samuel Salianga, alisema vituo vitakavyotumika kupigia kura ni 288 na idadi ya wapiga kura waliojiandikisha ni 92,939.

Salianga alisema maandalizi ya uchaguzi huo yamekamilika kwa asilimia 95 na tayari vifaa vyote muhimu vimeshafika na kusambazwa katika vituo vya kupigia kura.

Alibainisha kwamba vituo vitakavyotumika ni vile vilivyotumika katika uchaguzi uliofanyika katika mwaka Uchaguzi Mkuu 2010.

Dk. Slaa afunga kampeni

Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, jana alifunga kampeni za kuwania ubunge wa Chalinze kwa kuwaomba wananchi wamchague mgombea ubunge wake, Mathayo Torongey.

Dk. Slaa, alisemaTorongey akichaguliwa ataongeza nguvu ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na baadaye kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwakilisha masilahi na matakwa ya wananchi.

Aliwataka wasikichague Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mgombea wake, kwani kufanya hivyo ni ‘kuhalalisha’ kuwa wanakubaliana na hali ngumu inayoikabili nchi, ikiwemo ugumu wa maisha na ufisadi unaotishia amani ya nchi.

Akizungumza kwenye mkutano huo wa ufungaji wa kampeni hizo uliofanyika jana Chalinze mjini, kwenye Uwanja wa Masoko, Slaa alisema uchaguzi huo mdogo ni fursa ya kudhihirisha nguvu ya wanyonge dhidi ya watawala.

Alisema kuwa matatizo ya huduma za jamii wanayokabiliana nayo wananchi wa Chalinze ni kielelezo cha wazi cha kushindwa kwa Rais Jakaya Kikwete, CCM na serikali yake, kuweka mazingira ya wananchi kujitafutia maendeleo.

Dk. Slaa, alikebehi ahadi zinazotolewa na CCM na mgombea wake, akisema kuwa amepitia vitabu vya bajeti ya serikali ya taifa na Wilaya ya Bagamoyo, ambapo amebaini kuwa hazimo kwenye makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kuu na serikali za mitaa.

Alisema ahadi hizo ni ulaghai wa ahadi ambao wamekuwa wakifanyiwa kwa miaka mingi sasa.

“Nimekuwa nikiambiwa kuwa kwenye kampeni hizi CCM wametoa ahadi karibu kila kijiji, kila wameahidi kila mahali, nataka kuwaambia kuwa huu ni mwendelezo wa tabia ya ufisadi inayoendekezwa na chama hicho, kwa sababu kutoa ahadi za uongo pia ni ufisadi.

“Nimelazimika kufanya utafiti na kupitia vitabu vyote vya bajeti, serikali kuu na serikali za mitaa, ahadi wanazotoa CCM kwenye uchaguzi huu wa Chalinze hazimo kwenye bajeti. Hivyo hazitekelezeki. Hapo ni kitu kimoja kati ya viwili au vyote…ama hawajui kusoma bajeti au wanataka kufanya ufisadi ili watekeleze,” alisema Dk. Slaa.

Dk. Slaa pia alitumia fursa hiyo kujibu madai ya kwamba CHADEMA  kimemtelekeza mgombea wake, kwa viongozi wakuu wa chama hicho kutofika kwenye kampeni, ambapo alisema kuwa yeye ndiye aliyezindua kampeni kwenye Kijiji cha Miono akiwa ametokea Kalenga, kisha kampeni zikaongozwa na Makamu Mwenyekiti Said Issa Mohamed.

DK. Shein afunga CCM

Makamu Mwenyekiti wa CCM (Zanzibar), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar Dk. Mohamed Shein,  amewataka wakazi wa Jimbo la Chalinze,  kutosahau mabadiliko yaliyofanywa na wabunge wa chama hicho waliowahi kuongoza jimbo hilo na waendelee kuenzi fadhila hizo kwa kumchagua Ridhiwani Kikwete.

Dk. Shein alitoa ombi hilo wakati akifunga zoezi la kampeni za chama hicho katika Kata ya Miono wilaya ya Baganoyo.

Alisema kuwa tangu jimbo hilo lianzishwe limekua likiongozwa na wabunge wa CCM na kuleta mabadikiko katika kipindi chote hicho, na hivyo ili kuenzi fadhila hizo wanatakiwa kumchagua Ridhiwani Kikwete aweze kuwa mbunge katika jimbo hilo.

Aliwaomba kumpa kura mgombea huyo katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika leo ili aendelee kutekeleza ilani ya chama hicho kwa yale ambayo hayajakamilika.

Alisema wananchi wanatakiwa kuchagua CCM ili iendelee kuenzi muungano ambao sasa unaenda kusherehekewa kutimiza miaka 50.

Alisema wapo watu ambao wanajidai hawaufahamu muungano huo lakini inatakiwa itambuliwe kuwa upo  na kila mmoja analitambua hilo.

Aliongeza kuwa muungano huo upo katika msingi mkubwa.

Aliwataka wananchi kuheshimu uchaguzi kwa kufanya kwenda kupiga kura kwa utulivu na amani.

Naye Ridhiwani aliwaomba wananchi kijitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura na wamchague kuwa mbunge wa jimbo hilo.

Aliwashukuru wananchi wa jimbo hilo kwa kujitokeza kwa katika mikutano ya kampeni aliyoifanya tangu Machi 14, mwaka huu.

Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika leo kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo,  Said Bwanamdogo aliyefariki dunia Januari 22 mwaka huu.

Aidha, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, aliwahakikishia wananchi hali ya usalama na kusema kuwa ulinzi umeimarishwa.


Matei alisema kuwa katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo ulinzi umeimarishwa na wananchi wanatakiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi hilo bila hofu.

No comments: