Thursday, October 31, 2013

Serikali kutorudisha majeshi ya Kongo

 

na Happiness Mnale
SIKU chache baada ya kutokea kwa kifo cha mwanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Rajabu Mlima, aliyekuwa katika operesheni ya kulinda amani Mashariki mwa Kongo (DRC), serikali imesema haitatetereka wala kurudi nyuma kwa kurudisha majeshi yake nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati wa kuaga mwili wa marehemu Mlima katika viwanja vya jeshi Lugalo, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, alisema serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wanajeshi waliobakia nchini humo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa kulinda amani ya wananchi wa Kongo.

“Kama serikali tunasikitika kwa kifo cha mwanajeshi wetu, lakini hili halitufanyi kushindwa kuendelea kulinda raia wa Kongo na bado tunaendelea kutoa hamasa kubwa kwa wanajeshi waliobaki waendelee na majukumu yao kama kawaida.
“Kikubwa tutaendelea kutoa ushirikiano kwa familia ya marehemu kwa kuhakikisha shughuli zote za mazishi zinaenda sawa pamoja na kuwa nao karibu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi,” alisema Nahodha.

Awali akisoma salamu za rambirambi kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi Nchini (CDF), Davis Mwamunyange, Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi, Luteni Jenerali, Samuel Ndomba, alisema marehemu Mlima alipigwa risasi Oktoba 27, saa 5:00 asubuhi, akiwa katika milima ya Cavana iliyoko mashariki mwa Kongo na kufa papo hapo.
Chanzo; Tanzania Daima


Abwao amshika pabaya Lukuvi




na Salehe Mohamed, Dodoma
UTARATIBU wa mawaziri kuwa wabunge jana ulionesha udhaifu wake baada ya kusababisha mvutano mkubwa bungeni kati ya Mbunge wa Viti Maalumu, Chiku Abwao (CHADEMA), na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.

Mvutano huo ulitokea baada ya Abwao anayetoka Mkoa wa Iringa kuuliza swali la uhaba wa maji katika Jimbo la Isimani linaloongozwa na Lukuvi.
Abwao alilielekeza swali hilo kwa Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), akitaka kufahamu ni lini vijiji vilivyomo katika Jimbo la Isimani vitapata huduma ya maji safi na salama.

Wakati akiuliza swali hilo wabunge kadhaa walikuwa wakipiga makofi kumshangilia, hali iliyomfanya Spika wa Bunge, Anne Makinda, kumtaka aliulize tena, kwa madai kuwa hakulisikia.
Mbunge huyo alilazimika kulirudia swali hilo ambalo lilijibiwa na Waziri Stephen Wassira, ambaye alisema tatizo hilo si la Isimani pekee bali ni la nchi nzima na kwamba serikali itahakikisha vijiji vyote vinapata maji.

Baada ya Wassira kutoa jibu hilo, Lukuvi alisimama kushibisha majibu ya waziri mwenzake, lakini baadhi ya wabunge walikuwa wakipiga kelele kupinga uamuzi wake huo.

Licha ya kelele hizo, Spika alimpa nafasi ya kuzungumza, akimtaka azungumze kama mbunge lakini Lukuvi alisema angelizungumza kwa kofia ya uwaziri.
“Mimi ni waziri, ninaweza kuzungumzia jambo la wizara yoyote ile, hivyo hawa wenzangu wanaona nimekiuka kanuni, wanakosea, nataka waelewe vizuri mambo haya,” alisema.

Lukuvi alisema serikali inafahamu tatizo la maji la jimbo hilo na inatekeleza mradi wa sh bilioni tatu huku mbunge wake (yeye) akishiriki kikamilifu kutafutia ufumbuzi.
Alibainisha kuwa tayari vimekwisha kuchimbwa visima 25 vya maji kwa jitihada zake binasfi na mpango mwingine wa kuchimba visima vingine 10 unaendelea.
“Mipango hii yote ikikamilika kila kijiji kitakuwa na uhakika wa maji pamoja na kuwa na kisima kimoja cha akiba,” alisema.

Majibu hayo ya Lukuvi yalizusha vifijo na kuzomeana ndani ya Bunge kulikokwenda sambamba na kurushiana maneno baina ya wanaomuunga mkono na wale wa Abwao, ambao walidai kuwa ana masilahi na Jimbo la Isimani.
Mara baada ya Lukuvi kumaliza kutoa ufafanuzi wake huo, Makinda alisema kuwa kila mbunge ana haki ya kutoa maelezo juu ya jimbo lake anapoona kuna mwenzake kalizungumzia.

Hata hivyo, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), alisimama na kuomba mwongozo kuhusiana na hatua hiyo ya Lukuvi kutumia kofia mbili kujibu swali ambalo hakuulizwa.

Akitumia kanuni ya 68 (7), Mnyika alihoji sababu ya Lukuvi kusimama na kutumia mamlaka ya ubunge kujibu hoja hiyo wakati yupo kwa ajili ya nafasi ya uwaziri.
“Nimesimama kwa kanuni ya 68 (7), wakati wa kipindi cha maswali alisimama Mheshimiwa Lukuvi kujibu swali la Mheshimiwa Abwao, lakini alijibu akitumia cheo chake cha ubunge, wakati kanuni ya 39 (1) inatoa ruhusa kwa waziri kujibu maswali na hoja za wabunge na si wabunge.

“Kanuni ya wabunge kujibu maswali inahusu wabunge walioulizwa na walioteuliwa kwa kazi maalumu, kilichotokea leo inaonyesha wazi kuwa mchanganyiko wa vyeo unaleta madhara, waziri atakiwe kuepuka kutumia nafasi; nilikuwa naomba mwongozo wako,” alisema Mnyika.
Katika mwongozo wake, Makinda alisema Lukuvi yuko sahihi mpaka hapo Katiba itakapotenganisha kofia ya ubunge na uwaziri.

Utoro wa mawaziri
Katika hatua nyingine, kumejitokeza tukio la kushangaza la mawaziri wengi kutokuonekana bungeni wakati wa mjadala wa mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2014/2015, hatua iliyowafanya wabunge wakiongozwa na Spika Anne Makinda kuwashambulia kwa utoro.

Juzi jioni wakati akiahirisha mjadala huo, Makinda aliwaonya baadhi ya mawaziri kuwa kutokuwapo kwao bungeni kutaiathiri serikali katika kujibu hoja za wabunge.
“Nyinyi mawaziri msidhani huu mjadala na mpango huu unamhusu Waziri Wassira peke yake…hapana, huu unahusu wizara zote, maana litaulizwa swali ambalo Wassira hana jibu lake, lazima muwepo,” alisema.

Licha ya onyo hilo, jana hali ilikuwa mbaya zaidi ambapo mawaziri na manaibu waliokuwapo ndani ya ukumbi idadi yao ilikuwa haizidi saba wakati baraza zima wako zaidi ya 50.

Kutokana na utoro huo, wabunge wengi waliochangia mjadala walisema utoro huo umesababisha kutowajibika ipasavyo, hivyo maendeleo kusuasua.
Waliongeza kuwa utoro huo unadhihirisha dharau walizonazo na kwamba hao ndio kikwazo cha mipango mizuri inayoandaliwa na serikali.
Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alisema serikali inaonesha ina mchoko mkubwa ndiyo maana mawaziri waliomo ndani ya Bunge wakifuatilia mjadala huo hawazidi wanne.

Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, alisema haoni kama mpango huo utafanikiwa kwa kuwa wasimamizi na watekelezaji wa mpango huo hawapo bungeni.
Kombo Hamis Kombo (CUF), alisema mawaziri na manaibu wao wanafanya mchezo wa kuigiza katika mambo muhimu kwa taifa, badala ya kuweka mkazo kwenye kusikiliza mapendekezo ya wabunge kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Taifa.
Kutokana na mashambulizi hayo, Waziri asiye na wizara maalumu, Profesa Mark Mwandosya, aliwakingia kifua mawaziri na manaibu wao akisema wanafuatilia mijadala hiyo kupitia runinga.

Aliongeza kuwa kutokuwapo kwao na watendaji wengine bungeni si kikwazo cha utekelezaji wa mpango huo, kwa kuwa serikali inafanya kazi kwa njia mbalimbali, ikiwamo hiyo ya runinga.
Waziri huyo alisema kila kinachosemwa bungeni kinaandikwa na maofisa wa serikali ambao hukifikisha katika ngazi husika kwa ajili ya utekelezaji zaidi.
Chanzo: Tanzania Daima

Mageuzi sekta ya elimu



•  Madaraja ya ufaulu yapanguliwa, sifuri lafutwa

na Lucy Ngowi
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imefanya marekebisho katika upangaji wa viwango vya alama za matokeo ya wanafunzi wa kidato cha nne kwa kufutwa daraja sifuri na kuwekwa daraja la tano, ambalo litakuwa la mwisho katika ufaulu.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Sifuni Mchome, alitangaza mageuzi hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu upangaji wa viwango vya alama, matumizi ya alama endelevu ya mwanafunzi na ufaulu.

Alisema kwa muundo mpya, daraja la kwanza litabakia kuanzia pointi 7 hadi 17 kama ulivyokuwa muundo wa zamani, ambalo ni kundi la ufaulu uliojipambanua na bora sana, daraja la pili litaanzia pointi 18 hadi 24, badala ya pointi 18 hadi 21 kama zamani na likiwa ni kundi la ufaulu mzuri sana.

Pia daraja la tatu pointi zake zitaanzia 25 hadi 31, badala ya zile za zamani za 22 hadi 25 na kundi hili litakuwa la ufaulu mzuri wa wastani.
Kwa mujibu wa Prof. Mchome, daraja la nne litaanzia pointi 32 hadi 47, badala ya zile za zamani za kuanzia pointi 26 hadi 33, na kundi hilo litajulikana kama la ufaulu hafifu.
Daraja jipya lililoongezwa ni lile la tano, litakaloanzia pointi 48 hadi 49, litakalofuta daraja sifuri la zamani, lililokuwa na pointi 34 hadi 35, na sasa litajulikana kama kundi la ufaulu usioridhisha.

Prof. Mchome alifafanua kuwa mabadiliko hayo yamefanyika ili kuendelea kuimarisha mfumo wa elimu na kuweka wazi taratibu mbalimbali kwa ajili ya mitihani na masuala mengine.

Pia alisema wataalamu wa mifumo ya mitihani wataufanyia kazi zaidi muundo huo wa madaraja ili uweze kutumika kwa ufanisi katika kipindi hiki cha mpito.
“Yapo mambo mengi mengine ambayo hayana budi kuendelea kuimarishwa, ukiwamo mfumo wa mitaala, walimu, mazingira ya kujifunzia na kufundishia pamoja na vitabu na vifaa vingine muhimu katika elimu,” alisema.

Awali alisema kuwa wizara imekusanya maoni ya wadau wa elimu kuhusu upangaji wa viwango vya alama katika mitihani ya kuhitimu kidato cha nne na cha sita pamoja na matumizi ya alama za tathmini endelevu ya mwanafunzi.
Alisema maoni hayo ya wadau yamekusanywa kwa sababu kwa muda mrefu sasa upangaji wa viwango vya alama vinavyotumika na utaratibu wake katika mitihani hiyo yote ni vya elimu ya sekondari.

“Sera ya elimu na mafunzo ya 1995 imeelekeza kwamba katika kuamua kiwango cha ufaulu wa mwanafunzi wa elimu ya sekondari, alama za tathmini endelevu ya mwanafunzi zitachangia asilimia 50 na mtihani wa mwisho asilimia 50.
“Kwa upande wa Zanzibar alama hizo zimekuwa zikiandaliwa kwa mfumo wa asilimia 40 na mtihani wa mwisho asilimia 60. Pamoja na kwamba baraza halijawahi kuitumia mifumo hii tokea ilipowekwa, kumekuwa na mitazamo, maoni na mapendekezo tofauti katika muundo na matumizi ya alama hizo,” alisema.

Vilevile alisema kuwa wadau wengi walishauri muundo uliopo sasa wa madaraja uimarishwe ili kuanza kutumia muundo wa wastani wa alama katika ufaulu (GPA), kwa kuwa ni rahisi kueleweka na kuuandaa kuliko muundo wa madaraja.
Pia kwa kutumia muundo huo wa GPA inakuwa rahisi katika kukadiria uwezo wa mwanafunzi kielimu na kufanya uamuzi mbalimbali ikiwamo kuendelea na masomo katika ngazi mbalimbali za elimu.

Wakati huo huo, Prof. Mchome alisema kuwa mtihani wa kidato cha nne na mtihani wa maarifa mwaka huu unatarajiwa kufanyika nchini kote kwa siku 18 kuanzia Novemba 4 hadi 21.
Alisema jumla ya watahiniwa walioandikishwa kufanya mtihani huo ni 427,906, ambapo kati yao 367,399 ni watahiniwa wa shule na 60,507 ni wa kujitegemea.

Kwa mujibu wa katibu mkuu huyo, hadi sasa maandalizi na usafirishaji wa mitihani hiyo hadi ngazi ya mkoa yamekamilika.
Alitoa wito kwa kamati za mitihani za mikoa yote kuhakikisha kuwa taratibu zote za utunzaji, uhifadhi na usafirishaji wa mitihani hiyo zinazingatiwa.
Chanzo: Tanzania Daima

Mahakama iliyoibuliwa na Mwananchi kuwa ni chakavu kuvunjwa



Hali ilivyo katika sehemu ya kuhifadhia mafaili ya kesi katika Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo. Picha na Editha Majura

Na Editha Majura, Mwananchi
Bagamoyo.Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kiponzi amesema jengo la Mahakama ya wilaya ya Bagamoyo ambalo liliripotiwa na gazeti hili miezi kadhaa iliyopita kuwa linatishia uhai wa watu wanaofanya shughuli humo kutokana na uchakavu litavunjwa ili kujengwa nyingine mpya.

Anasema kuwa jengo hilo ni chakavu kwa sababu ni la muda mrefu na kwamba wameshaunda kamati ya kulishughulikia.
Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake Bagamoyo, Kiponzi anasema kasi ya utendaji wa kamati hiyo katika kushughulikia upatikanaji wa jengo mbadala la mahakama ya Wilaya ilipungua, baada ya aliyekuwa hakimu wa wilaya hiyo, Said Ali Mkasiwa kwenda masomoni nje ya nchi.

Tayari kimetengwa Kiwanja kitakachotumika kwa ujenzi wa jengo jipya, litakalokuwa mbadala wa jengo linalotumiwa sasa kwa shughuli za mahakama ya wilaya.
Hata hivyo hakutaja eneo kilipo kiwanja hicho kwa maelezo kuwa hiyo ni moja ya taarifa zitakazotolewa na kamati ya kushughulikia upatikanaji wa jengo jipya la mahakama hiyo, itakayokutana punde.

Anasema tayari mchoro wa ramani ya jengo litakalokuwa la mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo umekamilishwa na kwamba kilichobaki ni kamati kujadili na kutekeleza hatua zilizosalia katika kukamilisha ujenzi huo.

“Usifikiri ni maneno tu, (akitoa kabrasha la michoro ya ramani ya jengo la mahakama na kumkabidhi mwandishi wa makala hii) unaweza kushuhudia mwenyewe mchoro wa ramani ya jengo litakalojengwa kwa ajili ya mahakama ya wilaya; tupe muda kidogo bila shaka utakapofuatilia tena utakuta mabadiliko na tutakupa taarifa nzuri zaidi ya hizi,”anaeleza Kiponzi.

Kwa mujibu wa Kiponzi, kamati hiyo inafanya kazi chini ya uongozi wake kama mwenyekiti huku hakimu mfawidhi wa wilaya hiyo akiwa Katibu na kwamba kutokana na nafasi iliyoachwa na Mkasiwa kuzibwa na hakimu mfawidhi, Liad Chamshama; utendaji wa kamati hiyo utarejea kwenye kasi inayotakiwa.

Shughuli za Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo zinaendeshwa ndani ya jengo la enzi za utawala wa kikoloni. Limechakaa na kuchoka kiasi ambacho kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana mahakamani hapo zinasema mhandisi wa wilaya hiyo, ameishaeleza tena kwa maandishi kuwa halistahili kutumika.

Mkazi wa kijiji cha Miono ambaye ni miongoni mwa watumiaji wa mahakama hiyo, Kilo Khamis Mdete (42) anasema jengo hilo kufanywa ofisi ya wataalamu, wanaotoa haki na adhabu kwa mujibu wa sheria, ni sawa na udhalilishaji.
Anashauri Serikali kutumia rasilimali zake kuwezesha upatikanaji wa haraka wa jengo jipya.
Chanzo: Mwananchi