Friday, February 15, 2013

Katibu wa Bunge, Spika Makinda wapingana Juu ya Kutorusha Runingani Vipindi Vya Bunge


Katibu wa Bunge, Thomas Kashilillah.

KATIBU wa Bunge, Thomas Kashilillah amepingana hadharani na bosi wake Spika wa Bunge, Anne Makinda kuhusu kurushwa moja kwa moja matangazo ya Vipindi vya Bunge.
Juzi katika mkutano na waandishi wa habari katika Ofisi za Bunge, Kashilillah alisema kuwa ofisi yake inakusudia kutoonyesha matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge vinavyofanyika mjini Dodoma kutokana na baadhi ya wabunge kukiuka kanuni za kibunge kwa kuvunja maadili.
Hata hivyo, kauli ya Kashilillah inapingana na ile ya Makinda aliyoitoa mjini Dodoma, Februari 8 wakati wa kuahirisha kikao cha 10 cha Bunge aliposema: “Naipongeza TBC (Shirika la Utangazaji la Taifa) kwa kuonyesha moja kwa moja matangazo na yote yanayoendelea bungeni.
“Kutokana na vurugu zilizotokea, ninaiomba Serikali kuiongezea ruzuku TBC ili kupata mitambo ya kisasa waweze kuonyesha vizuri matangazo yake, safari hii matangazo yalikuwa yanakatika katika sana,” alisema Makinda.
Hata hivyo, kauli hiyo wakati wa kufunga Bunge ilikuwa ni ya pili kwa Makinda kwani baada ya kutokea vurugu zilizoongozwa na baadhi ya viongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Makinda aliisifu TBC kwa kuonyesha kila kilichotokea bungeni na kuweka msisitizo kuwa lazima TBC isaidiwe ili kila kinachotokea ndani ya Bunge kionekane kwa wananchi.
Akizungumza jana kwenye Ofisi za Bunge, Kashilillah alisema kuwa vikao vinavyofanyika sasa mara nyingi vinakiuka kanuni na maadili ya shughuli za Bunge, jambo ambalo limesababisha baadhi ya wabunge kuinuka na kutoa kauli mbalimbali wakati mijadala ikiendelea.
Kashilillah alisema, utaratibu unafanyika na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ili kuangalia namna ambavyo wataweza kuonyesha shughuli za Bunge kwa vipande vipande vilivyorekodiwa kwa maeneo yanayofuata kanuni na maadili ili kuficha taswira mbaya itakayojitokeza kwa wananchi.
“Kuna ukiukwaji mkubwa wa kanuni na maadili ya vikao vya Bunge, na si kwamba wanaofanya hivyo hawafahamu, isipokuwa wanafanya makusudi au wanatafuta umaarufu kupitia vikao hivyo. Kutokana na hali hiyo, tumeamua kukaa na TCRA ili kuangalia namna ambavyo tunaweza kurusha vikao vilivyorekodiwa badala ya moja kwa moja,” alisema.
Simu za matusi na kashfa
Akizungumzia suala la Spika Makinda kutukanwa na kukashifiwa, Dk Kashililah alisema kuwa, kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali ameshawafahamu wote waliofanya hivyo na taratibu za kuwakamata zinaandaliwa.
“Tumeshawabaini, tunafahamu wanakoishi na namba zao tayari zimeanza kushughulikiwa. Hasa wale wote waliotuma ujumbe wa matusi au kupiga simu,” alisema.
Kuvunjwa kwa kamati
Kuhusu kuvunjwa kwa baadhi ya Kamati za Bunge, alisema kuwa Spika wa Bunge anaweza kuzivunja kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo utendaji wake au ushauri unaotoka kwa viongozi wa vyama vyenye uwakilishi bungeni.
Alisema kutokana na hali hiyo, waliangalia kamati ambazo zinafanya kazi kwa mwingiliano na kuhamishia shughuli zile kwenye kamati nyingine kama ilivyokuwa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ambayo shughuli zake zimehamishiwa kwenye Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC).
“Kabla ya kufanya uamuzi wa kuvunja kamati hizo, tulishirikiana na viongozi wa vyama vyote vyenye uwakilishi bungeni, hii ilisaidia kumpa mamlaka Spika Makinda kutangaza kuvunjwa kwa kamati hizo, huku baadhi majukumu yake kuhamishiwa kwenye kamati nyingine,” alibainisha.
Alisema kutokana na hali hiyo, kamati hiyo itaongezewa nguvu ili ziweze kufanya kazi kwa mujibu wa kanuni kama ilivyokuwa awali, jambo ambalo ni sawa na uboreshaji wa kazi zao.
“Hii si mara ya kwanza kufanyika suala hilo, hata kipindi cha Spika Adam Sapi aliwahi kuvunja kamati hizo na kuhamishia shughuli zake kwenye kamati nyingine.”
Hoja ya Mnyika
Alisema kuwa kitendo cha Spika Makinda kuiondoa hoja ya Mbunge wa Ubungo, John Mnyika si ukiukwaji wa kanuni, bali hoja yake ilijibiwa na Waziri wa Maji, Prof Jumanne Maghembe.
“Wakati Mnyika anawasilisha hoja yake, anayejibu hoja ni mwakilishi wa Serikali na wakati ule alikuwa Waziri Maghembe na kusema kuwa, hoja ya hiyo tayari imo kwenye mpango mkakati wa utekelezaji wa mradi wa maji wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mnyika alipaswa kuwasilisha mabadiliko ya hoja ili iweze kuzaa  hoja, lakini alishindwa badala yake Spika akaiondoa mezani,”alifafanua.

Source: www.mwananchi.co.tz

No comments: