NA EVARIST CHAHALI, USKOCHI
Makala yangu
katika RAIA MWEMA Tole la Feb 13 "Tishio la uhai mlangoni kwangu"
JUMAMOSI Februari 2 mwaka huu itabaki katika kumbukumbu
zangu kwa muda mrefu, pengine katika uhai wangu wote.
Majira ya saa 3 asubuhi nilikurupushwa usingizini na kelele
za mlango uliokuwa ukigongwa kwa nguvu. Wakati ninajiandaa kwenda kufungua
mlango, nikasikia sauti yenye dharura ikisema, “bwana Chahali, polisi hapa,
tafadhali fungua mlango.”
Nilichanganyikiwa kwani tangu nifike nchi hii zaidi ya miaka
10 iliyopita sijawahi kufanya kosa lolote au kukwaruzana na vyombo vya
dola/sheria.
Baada ya kufungua mlango, askari waliovalia kiraia
walijitambulisha na kuonyesha vitambulisho vyao. Pia walinisihi kuwa nisiwe na
hofu ya kudhani kwamba nimefanya kosa lolote.
Kwa kifupi, walinieleza kuwa wamepewa ujumbe kutoka moja ya
taasisi za intelijensia za hapa kuwa kuna tishio la uhakika dhidi ya maisha
yangu. Hata hivyo, walieleza kuwa kwa vile wao walipewa tu ujumbe huo na
kutakiwa kuuwasilisha kwangu, hawakuwa na maelezo ya ziada. Walisisitiza kuwa
nichukue tahadhari muhimu na kunipa maelekezo ya mawasiliano ya dharura.
Kwa vile nilikurupushwa usingizini, awali taarifa hiyo
ilionekana kama ndoto iliyokuwa inaendelea hata baada ya kutoka usingizini.
Ilinichukua takriban saa tatu kuzinduka kutoka katika mshituko huo, na kutambua
uzito wa taarifa niliyopewa na polisi hao.
Nikaamua kwenda kituo kimoja cha polisi kupata ufafanuzi
zaidi. Mara baada ya kujitambulisha, mazingira ya namna suala hilo lilivyokuwa
likishughulikiwa kituoni hapo lilinipa picha kuwa jambo hilo lina uzito. Kwa
kifupi, baada ya kitambo nilipewa ufafanuzi ambao haukutofautiana na maelezo
niliyopewa awali na polisi walionitembelea katika makazi yangu.
Kikubwa ni kuwa taarifa hiyo ilionyesha kuwa tishio hilo
dhidi ya maisha yangu linatokea huko nyumbani. Swali linaloendelea kunisumbua
kichwa ni KWA NINI iwe hivyo.
Wakati si vigumu kwangu kuhisi wahusika wa mpango huo wa
kijahili, napata shida kuelewa kwanini wahusika hao watumie fedha za walipakodi
kuandaa operesheni ya kutaka kunidhuru ilhali ninaamini kwa asilimia 100 kuwa
mimi si tishio kwa usalama wa Taifa letu.
Ndiyo, baadhi ya ninayoandika kwenye makala zangu na tweets
zangu huko kwenye mtandao wa kijamii wa twitter yanaweza
kuwachukiza baadhi ya watu, lakini kwa hakika kuchukizwa huko si sababu ya
kutaka kunidhuru.
Hadi wakati ninaandika makala hii nimekuwa nikiishi kwa
tahadhari kubwa. Faraja kubwa kwangu inatokana na sababu tatu za msingi.
Kwanza, kwa vile nilizaliwa na kukulia katika familia inayomtanguliza Mungu
katika kila jambo, nina imani kubwa kuwa mamlaka pekee kuhusu uhai wangu (yaani
kuwa hai au kufa) ni Mungu pekee. Hakuna mwanadamu anayeweza kupora jukumu hilo
la Mungu na kufanikiwa kufupisha uhai wa yeyote.
Pili, nina imani kubwa na taasisi za usalama za hapa
Uingereza. Kimsingi, wenzetu hawa wanathamini sana usalama na uhai wa binadamu
pasi kujali mhusika ni mzaliwa wa hapa au ni ‘mgeni’ kama mimi. Ushauri na
sapoti ninayoendelea kupata inanipa matumaini makubwa kuwa nipo kwenye ‘mikono
salama.’
Lakini tatu ni ukweli kwamba takriban miaka mitano sasa
nimekuwa nikiishi na uelewa kwamba kuna baadhi ya watu huko nyumbani wanaoniona
kama kimelea cha maradhi hatari ambacho kikiachwa bila kudhibitiwa kitazua
balaa.
Kwa sababu hiyo, tangu wakati huo nimekuwa nikiishi kwa
tahadhari japo si kubwa kama hii ninayolazimika kuichukua sasa. Lakini ili
uweze kuchukua tahadhari ni lazima uwe na mbinu na ujuzi wa kuchukua tahadhari
husika. Kwa bahati nzuri, watu hao wanafahamu fika kuwa nina ujuzi wa kutosha
na kuelewa na kumudu fika mbinu za kuishi kwa tahadhari.
Hata hivyo, kumudu mbinu ni suala moja na kuishi kwa kutumia
mbinu hizo ni kitu kingine. Si jambo la kupendeza hata kidogo kuishi ukiwa na
uelewa kuwa siku moja, mahala fulani unaweza kukumbana na madhara fulani.
Lakini kadri unavyolazimika kuishi kwa namna hiyo inakuwa kama sehemu muhimu ya
maisha yako, na ndivyo ilivyo kwangu.
Pamoja na kuchukulia kwa uzito taarifa hizo za tishio dhidi
ya uhai wangu, nimechukua hatua nyingine kadhaa ikiwa ni pamoja na
kuwafahamisha watu ninaohisi kuwa ndio wahusika wa mpango huo dhalimu kwamba ni
ukosefu wa busara wa hali ya juu kupoteza fedha za walipa kodi kutaka
kunidhuru.
Ingekuwa vema raslimali zinazotumika kufanikisha mpango huo
zikaelekezwa kwenye uchunguzi wa mabilioni ya fedha za Watanzania yaliyofichwa
kwenye mabenki nchini Uswisi huku nchi yetu ikikabiliwa na deni kubwa la ndani
na nje la zaidi ya shilingi trilioni 30!
Licha ya kuwa na mwangaza kuhusu mahala linakoanzia tishio
hilo kutoka huko nyumbani, sina hakika kama ni mkakati wa kitaasisi au ndiyo
yaleyale niliyowahi kuandika katika makala yangu moja huko nyuma juu ya kuwapo
kwa rogue elementskatika taasisi zetu nyeti.
La muhimu kwangu kwa sasa ni kuhakikisha kuwa majahili hao
hawafanikiwi katika azma yao. Pia sioni haja ya kuvifahamisha rasmi vyombo vya
dola huko nyumbani. Itoshe tu kusema hapa kwamba mipango kama hii katika zama
hizi haina tena tija.
Hakika suala hili limenikera sana lakini ninajitahidi
kuzingatia busara za mwandishi wa Laws of Power, Robert Greene, ambapo kanuni
ya 21 inausia kuwa “Play a Sucker to Catch a Sucker – Seem Dumber than your
Mark” (yaani, kwa tafsiri isiyo rasmi, jifanye mjinga kumnasa mjinga).
Kanuni hii inasema, ninanukuu, “No one likes feeling
stupider than the next persons. The trick, is to make your victims feel smart –
and not just smart, but smarter than you are. Once convinced of this, they will
never suspect that you may have ulterior motives” (hakuna mtu anayependa
kuonekana mpumbavu zaidi ya mtu mwingine. Ujanja ni kumfanya mlengwa wako
ajione mwerevu, na si mwerevu tu bali mwerevu zaidi yako. Pindi akaamini hivyo,
hatohisi kuwa una nia kubwa zaidi yake).
Nimalizie makala hii kwa kusisitiza kuwa vitisho kama hivi
kamwe havitonizuwia kusimamia ukweli na kuuhubiri pasi kumhofia mtu au taasisi.
Ninatambua yaliyowakumba baadhi ya waandishi wa habari wa
nyumbani.
Kwangu hizo ni chachu za kuendeleza walichoanzisha.
Kadhalika, ni vema walioandaa mpango huo dhalimu wakatambua
kuwa licha ya kitendo hicho kuwa na uwezekano wa kuharibu ‘mahusiano ya
kiusalama’ kati ya nchi yetu na Uingereza (kwa kuwatwisha mzigo usio wa lazima
kuhakikisha mimi kama mkazi wa nchi hii sidhuriwi), lakini pia kinakwaza kiapo
changu cha utii kwa nchi yangu (nilipokuwa mtumishi wa umma) ‘kuyaacha mambo
fulani yaendelee kubaki yasiyopaswa kuongelewa hadharani.’ Laws of
Power ya 19 inasisitiza, “Never offend a wrong person” (kamwe
usimkorofishe mtu asiyestahili).
"If you're not ready to die for it, take the word
'freedom' out of your vocabulary" ~ Malcom X
Souece:
Gazeti la Raia Mwema & www.chahali.com
No comments:
Post a Comment