Friday, February 15, 2013

Ashangaa Serikali kutumia takwimu za kale



MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba amesema ni aibu kwa Tanzania kutumia takwimu za miaka ya nyuma ambazo zinatumia gharama kubwa kifedha na muda mwingi badala ya kuwa njia mbadala na rahisi ya kupata takwimu kwa wakati.

Lipumba alisema hayo juzi wakati akizungumza machache kwenye hafla fupi ya uzinduzi wa Mpango wa Sauti za Wananchi ambapo alitoa pongezi kwa Taasisi ya Twaweza kwa juhudi zao za kutumia simu za mkononi ili kupata maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi.

Profesa huyo alisema jitihada hizo zitawawezesha kukusanya taarifa kwa njia ya simu ambayo itatumia gharama ndogo lakini kwa ufanisi pia ina uwezo wa kuwafikia Watanzania waishio kila upande wa nchi. “Tunahitaji kujua taarifa halisi zinazogusa maeneo ya wananchi ambayo Serikali inatakiwa kuyafanyia kazi kupitia sera zake,mfano Sera ya Serikali ya wazee ambayo inawataka wapate matibabu bila malipo, je inafanya hivyo…,hivyo kupitia mpango huu tunaweza kupata taarifa halisi,”alisema.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kariuki alitoa pongezi kwa niaba ya Serikali kwa Twaweza ambao ndio waandaaji wa mpango huo akisema una umuhimu kwa wananchi na kwa Serikali pia katika kupata maoni yao na kuandaa sera ambazo zinakidhi haja na matakwa ya wananchi.

Kariuki alisema mpango huu ni wakupata maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi hususani yanayohusu afya,elimu na maji, ili kujua ni jinsi gani sekta hizi zinatoa huduma kwao namna ambavyo Serikali inawajibika.
Source: www.mwananchi.co.tz

No comments: