Utangulizi
Ndugu Wananchi;
Kama ilivyo ada naomba tuanze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwenye Rehema,
kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kuzungumza kwa mara nyingine kwa kutumia
utaratibu wetu huu mzuri wa mawasiliano baina ya Rais na wananchi wa Tanzania
kila mwisho wa mwezi. Siku ya leo nitazungumzia safari yangu ya Ufaransa,
Uswizi na Ethiopia. Pia nitazungumzia ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi
asili kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam.
Safari za Kikazi Nje ya Nchi
Ndugu Wananchi;
Safari
yangu ya Ufaransa, Uswizi na Ethiopia ilikuwa na manufaa makubwa kwa nchi
yetu. Nchini Ufaransa licha ya kuimarisha uhusiano wa kirafiki baina ya
nchi zetu, tumepata wawekezaji wengi wakubwa wenye nia thabiti ya kuja kuwekeza
hapa nchini. Pia tumekubaliana kuanza mazungumzo ya kuwa na mpango
mwingine wa ushirikiano. Mpango wetu wa sasa ulioanza mwaka 2006 uliisha
mwaka 2010. Mpango ule ulitusaidia sana kuboresha huduma za maji katika
miji ya Utete mkoani Pwani na Mpwapwa mkoani Dodoma.
Katika mkutano wa Kongamano
la Uchumi wa Dunia uliofanyika Davos, Uswizi, tumehakikishiwa ushirikiano
katika kuendeleza juhudi zetu za kuleta mapinduzi ya kijani ili tujihakikishie
usalama wa chakula na kupunguza umaskini vijijini na kukuza uchumi wa nchi
yetu. Aidha, tulipata bahati ya kushirikishwa katika mjadala wa kuanzishwa
kwa programu kubwa ya kuzisaidia nchi za Afrika kutatua matatizo ya upatikanaji
wa umeme. Naamini programu hiyo ikitekelezwa na wakubwa kuheshimu kauli
na ahadi zao itakuwa msaada mkubwa kwa maendeleo ya nchi za Afrika zilizo
Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Ndugu Wananchi;
Nchini Ethiopia tulishiriki
katika mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika na katika kikao
cha African Peer Review Mechanism (APRM) ambapo taarifa ya tathmini ya utawala
bora ya Tanzania na Zambia iliyofanywa na APRM ilijadiliwa. Kwa jumla
hatuna mahali tuliponyooshewa kidole kuwa tunafanya vibaya. Tumepongezwa
katika mambo mengi na tumepewa ushauri kwa baadhi ya maeneo waliyoona hatuna
budi kuyaboresha. Nilipata nafasi ya kusema ambayo niliitumia kufafanua baadhi
ya mambo yaliyokuwamo kwenye taarifa. Niliwashukuru na kuahidi kuufanyia
kazi ushauri uliotolewa. Tathmini ya nchi yetu ilipitishwa kwa kauli
moja.
Vurugu za Kupinga Gesi
Kusafirishwa Kutoka Mtwara
Ndugu wananchi;
Kama mtakavyokumbuka tarehe 8 Novemba, 2012 kule Kinyerezi, Wilaya ya Ilala
hapa Dar es Salaam, niliweka jiwe la msingi la ujenzi wa bomba la kusafirisha
gesi asili kutoka Mtwara na Songosongo kuja Dar es Salaam. Karibu na
mwishoni mwa Desemba, 2012 kukafanyika maandamano mjini Mtwara kupinga ujenzi
wa bomba hilo. Katika maandamano yale na baadaye kwenye kauli za
wanasiasa na wanaharakati yakatolewa madai kuwa gesi hiyo itumike kwa maendeleo
ya Mtwara na kwamba yale yanayotakiwa kufanyika Dar es Salaam yafanyike
Mtwara. Pia, zilitolewa shutuma nyingine dhidi ya Serikali eti kuwa kwa
miaka mingi imewasahau na haiwajali wananchi wa Mikoa ya Kusini na ujenzi wa
bomba hilo ni muendelezo wa hayo. Kauli mbalimbali za wanasiasa na wanaharakati
ni kama vile ziliongeza mafuta kwenye kaa la moto na kuuchochea mpaka kukatokea
matukio yaliyotusikitisha na kutshtua sote. Baadhi ya ndugu zetu
wamepoteza maisha na mali za watu na Serikali kuharibiwa.
Ndugu Wananchi;
Katika hotuba yangu ya kuaga mwaka 2012 na kuukaribisha mwaka 2013, tarehe
31 Desemba, 2012, nililisemea jambo hili. Leo mwezi mmoja baadae, napenda
kusisitiza mambo mawili. Kwanza kwamba, si kweli kuwa Serikali inapuuza
Mikoa ya Kusini. Na pili, kwamba kujenga bomba la kuipeleka gesi Dar es
Salaam hakuinyimi Mikoa ya Mtwara na Lindi fursa ya kunufaika na gesi iliyopo
Mtwara.
Ndugu Wananchi;
Serikali imefanya, inafanya na
ina mipango ya kufanya mambo mengi mazuri kwa ajili ya kuleta maendeleo katika
Mikoa ya Mtwara na Lindi. Ipo mipango ya kuboresha miundombinu, huduma za
kiuchumi na kijamii pamoja na kukuza uchumi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa
viwanda vikubwa na vidogo. Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya uongozi wa
Rais Mstaafu, Mheshimiwa Benjamin Mkapa, ilijenga daraja katika Mto Rufiji
maarufu kama Daraja la Mkapa. Hii ilikuwa ni hatua kubwa ya awali katika
safari ya kutatua matatizo ya usafiri ya Mikoa ya Kusini. Serikali
ninayoiongoza mie iliachiwa kazi ya kukamilisha ujenzi wa barabara za lami
kufikia darajani na kuunanisha Mkoa wa Mtwara na Mkoa wa Ruvuma. Kazi
hiyo, tumeitekeleza vizuri na sasa tunakaribia kuimaliza. Tulikamilisha
ujenzi wa barabara ya kutoka Mnazi-Mmoja hadi Nangurukuru. Mwaka 2009
tukaanza ujenzi wa barabara ya kilomita 56 kutoka Somanga hadi
Ndundu (darajani). Ujenzi wa kilometa 36 za mwanzo ulienda
vizuri. Bahati mbaya ujenzi wa kilomieta 20 za mwisho
umechelewa sana kwa sababu ya mmiliki wa kampuni iliyokabidhiwa kufanya kazi
hiyo kufariki. Kwa sababu hiyo, kampuni ilipata mtikisiko kiasi na
kusababisha kazi kutotekelezwa kwa kasi tuliyoitarajia. Sasa mambo
yametengemaa na kazi inaendelea kwa kasi nzuri. Matumaini yetu ni kuwa
ifikapo mwezi Desemba, 2013 kazi hiyo itakuwa imekamilika.
Hali kadhalika, Rais Mstaafu, Mzee Benjamin Mkapa alituachia jukumu la
kumaliza ujenzi wa Daraja la Umoja katika mto Ruvuma na ujenzi wa barabara ya
lami kuanzia Mikoa ya Mtwara na Ruvuma. Tumelikamilisha Daraja hilo na
ujenzi wa barabara ya lami kutoka Masasi hadi Mangaka umekamilika.
Mchakato wa kujenga barabara ya kwenda Songea na kwenda Darajani umefikia
mahala pazuri. Tenda ya ujenzi wa barabara kutoka Tunduru hadi Mangaka
mpaka Darajani imeshatangazwa. Kama mambo yataenda sawa miezi mitatu
ijayo mjenzi atapatikana. Wakati huo huo ujenzi wa barabara kutoka
Namtumbo hadi Songea – Mbinga na Namtumbo – Tunduru unaendelea. Hivyo
basi, kwa barabara ya “Mtwara Corridor” kazi iliyobaki ni kutoka
Mbinga kwenda Mbambabay ambayo tutaifanya wenyewe kama tulivyofanya kwa Mnazi
Mmoja – Nangurukuru na Somanga – Ndudu na Daraja la Umoja.
Ndugu Wananchi;
Ipo pia mipango ya kuipanua na kuijenga upya bandari ya Mtwara ili iweze
kuhudumia mahitaji ya utafutaji na uchimbaji wa gesi baharini, kuhudumia na
kuvifanyia matengenezo vyombo vinavyotumika katika utafiti, uchimbaji na
uendelezaji wa gesi. Pia iweze kuhudumia shughuli za kiuchumi
zitakazotokana na uchumi wa gesi pamoja na zilizopo sasa. Nilipozungumza
na makampuni ya utafutaji gesi pale Mtwara tarehe 25 Julai, 2011 waliomba
nikubali bandari ya Mtwara iwe mahali pa kuhudumia vyombo vyote vinavyofanya
shughuli ya utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta katika pwani ya Afrika ya
Bahari Kuu ya Hindi. Pia waliomba kuwa sehemu hiyo ya bandari iwe bandari
huru. Niliwakubalia bila ya kusita na tayari eneo la hekta 110 zimeshatengwa
na kutangazwa rasmi kuwa bandari huru. Vile vile waliomba wapewe sehemu
ya bandari ya sasa kuendeshea shughuli na eneo la kujenga kituo cha mitambo ya
kuchakata gesi na kusafirisha nje.
Ndugu Wananchi;
Baada ya kuzungumza na makampuni ya utafutaji gesi na mafuta na kuelezwa
mahitaji yao nilibaini kuwa bandari ya Mtwara inahitaji kupanuliwa na kujengwa
upya. Bahati nzuri viongozi wa Mamlaka ya Bandari walikuwepo na
walinihakikishia kuwa watafanya hivyo.
Tayari eneo la bandari limeongezwa kutoka hekta 70.68 hadi 2,693.68.
Eneo la bandari huru limeshatengwa hivyo hivyo na eneo la
kampuni ya Dangote na makampuni ya gesi yaliyopo. Aidha, mchakato wa
kupanua bandari iliyopo, kujenga gati mpya na kuendelea na ujenzi hadi maeneo
ya Msanga Mkuu ipo katika hatua mbalimbali za matayarisho na utekelezaji.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa Mkoa wa Lindi
mipango ya kupanua na kuijenga upya bandari ya Lindi imefikia hatua
nzuri. Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Dkt. Charles Tizeba alithibitisha hayo
tarehe 1 Desemba, 2012 nilipotembelea bandari hiyo wakati wa ziara yangu ya
Mkoa wa Lindi ya tarehe 1 mpaka 5 Desemba, 2012. Hali kadhalika mipango
ya kujenga bandari ya Kilwa iko mbioni. Tena kwa upande wa Mkoa wa Lindi
moja ya makampuni yaliyogundua gesi baharini wameamua kujenga bandari na kituo
cha kuchakata na kusarifisha gesi nje ya mkoa huo kama ilivyo kwa Mtwara.
Naambiwa wametambua maeneo matatu, kilichobakia ni kuamua mojawapo ili ujenzi
uanze.
Ndugu Wananchi;
Nilipotoka bandari ya Mtwara,
siku ile nilitembelea Chuo cha VETA na kuzungumza na viongozi wa VETA taifa na
wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuhusu kuwa na mitaala ya kutoa mafunzo
mahsusi yanayohitajika na sekta ya gesi na mafuta. Nilisisitiza kwamba
tuwapatie vijana wetu mafunzo yatakayowawezsha kuajiriwa na makampuni ya gesi
na yale yatakayokuwa yanatoa huduma kwa makampuni hayo. Nilisema
tusipofanya hivyo, makampuni hayo yataajiri watu kutoka nje na hatutakuwa na
sababu ya kuwalaumu wala kulalamika.
Nafurahi kwamba agizo langu hilo limefanyiwa kazi ipasavyo. Hivi sasa
katika chuo cha VETA Mtwara mafunzo hayo yanatolewa. Kampuni ya
PetroBrass ya Brazil inaendesha mafunzo ya sekta ya gesi kwa vijana 25 kutoka
mkoani Mtwara. Aidha, chuo cha VETA kwa kushirikiana na Kampuni ya Gesi
ya Uingereza (British Gas) na Volunteers Service Overseas ya Uingereza,
kinatekeleza programu ya miaka mitatu iitwayo Enhancing Employerbility
Through Vocational Training. Programu hii inalenga kutoa
kozi zitakazowafanya wahitimu kuweza kuajiriwa katika sekta ya gesi.
Programu hii ilifunguliwa na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib
Bilal, tarehe 26 Novemba, 2012.
Ndugu Wananchi;
Chini ya programu hii, walimu wa masomo yanayohusiana na gesi wanaongezewa
ujuzi ili waweze kufikia viwango vya kimataifa. Vile vile, Wizara ya
Nishati na Madini imetoa upendeleo maalum wa kudhamini wanafunzi 50
kutoka mkoa wa Mtwara kusoma chuoni hapo ambao tayari wameshahitimu mafunzo ya
msingi ya uunganishaji vyuma viwandani. Mchakato wa kuwapata wanafunzi
50 kwa ajili ya mafunzo kama hayo kutoka mkoa wa Lindi
unaendelea. Nimeambiwa mpaka wameshawapata vijana 25 bado 25.
Hali kadhalika, Wizara ya
Nishati na Madini inadhamini wanafunzi 10 kupata mafunzo katika Chuo Kikuu cha
Dodoma ambako kozi za mafuta na gesi zinatolewa. Kipaumbele kwa udhamini
huu unatolewa kwa wanafunzi wa mikoa ya Mtwara na Lindi wenye sifa za
kudahiliwa katika mafunzo haya. Wamepatikana watatu. Wataalamu hawa
na wengine wa fani mbalimbali za gesi na mafuta watafundishwa kwa kiwango cha
shahada ya kwanza na baadae uzamili na uzamivu ili nchi yetu ijitosheleze kwa
wataalamu wa sekta hii.
Kupanga Mji wa Mtwara
Ndugu Wananchi;
Baada ya kutembelea bandari
ya Mtwara na Chuo cha VETA, nilikaa na kuzungumza na viongozi wa Serikali na
Manispaa ya Mtwara. Katika mazungumzo yangu nao niliwasisitizia umuhimu
wa kuwa na mpango kabambe wa kuendeleza mji wa Mtwara – (Mtwara Masterplan)
Mpango ambao utawezesha kujengwa mji mkubwa wa kisasa unaokidhi mahitaji ya mji
wa uchumi wa gesi. Niliwataka wahakikishe kuwa kuna maeneo ya viwanda,
biashara, makazi, mahoteli, huduma za afya, elimu, mapumziko na burudani,
viwanja vya michezo na kadhalika. Kazi ya kutayarisha Masterplan
hiyo imeanza na Manispaa ya Mtwara inashirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Makazi.
Kwa upande wa uwekezaji nafahamu kuwa mpaka sasa makampuni 51
yameonyesha nia ya kuwekeza Mtwara katika viwanda, hoteli, shughuli za uchukuzi
na huduma hasa kwa sekta ya gesi. Wanachosubiri ni kutengewa maeneo ya
kujenga, waanze. Hivyo kukamilika mapema kwa Masterplan ya mji
wa Mtwara kutasaidia kuongeza kasi ya uwekezaji huu kufanyika. Viwanda
hivi vyote vitasaidia kuongeza ajira kwa vijana wa Mtwara na Watanzania kwa
jumla. Nimeambiwa kwa mfano, wakati wa ujenzi wa kiwanda cha saruji watu
zaidi ya 7,000 wataajiriwa.
Ndugu Wananchi;
Kabla hata
ya ugunduzi wa gesi iliyoko baharini, tulikuwa na mipango ya kutumia gesi ya
Msimbati (Mnazi Bay) kwa ajili ya kuzalisha umeme, kuzalisha mbolea na kutumika
katika kiwanda cha saruji. Kwa upande wa umeme kulikuwa na mpango wa
kujenga mtambo wa kuzalisha Megawati 300 kwa kushirikiana na
mwekezaji binafsi. Bahati mbaya wakati wa matatizo ya kifedha ya dunia
mwaka 2009 mwekezaji huyo akashindwa kupata mkopo, hivyo mradi ukasimama
kutekelezwa. Haukufa wala haukuhamishiwa Dar es Salaam au Bagamoyo kama
ambavyo imekuwa inapotoshwa kwa makusudi. Mradi huo bado upo, tena mpango
wa sasa ni kujenga Megawati 600 zitumike Mtwara na zingine
kuziingiza kwenye gridi ya taifa kupitia Songea.
NduguWananchi;
Kwa upande wa kiwanda cha mbolea, wawekezaji wengi wameshajitokeza tangu
mwaka 2008 mpaka sasa. Mchakato umefanyika wa kuchambua wawekezaji wenye
sifa na kutambuliwa. Mambo mawili yamechelewesha utekelezaji
kuanza. Jambo la kwanza ni wawekezaji na kampuni ya Artumas iliyokuwa
mbia na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (T.P.D.C) wakati ule,
kushindwa kukubaliana nao juu ya bei ya kuwauzia gesi. Wawekezaji
walitaka bei ya gesi ipunguzwe, lakini kampuni ya Artumas na T.P.D.C. hawakuwa
tayari kupunguza zaidi ya kiasi walichopunguza, ambacho wawekezaji bado waliona
hailipi kwa kuzalisha mbolea.
Sababu ya pili ni matatizo ya kifedha yaliyoikumba kampuni ya Artumas
katika kipindi hicho. Kufuatia machafuko ya masoko ya fedha na mdororo wa
uchumi wa dunia mwaka 2008/2009 kampuni ya Artumas iliathirika na kulazimika
kuuza hisa zake kwa wawekezaji wengine. Katika kipindi hicho ilichopitia
kampuni, mazungumzo na uwekezaji wa kiwanda cha mbolea hayakuweza kupewa kipaumbele.
Mtazamo wa sasa wa wabia wapya na T.P.D.C. ni kuwa wao wenyewe sasa wawekeze
katika ujenzi wa kiwanda cha mbolea. Serikali imekubali rai yao hiyo na
wanaendelea na matayarisho.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande
wa kiwanda cha Saruji kitakachojengwa na kampuni ya Dangote ucheleweshaji
ulikuwa kwa sababu mbili. Kwanza, kampuni ya Dangote iliomba eneo zaidi
ya ililokuwa imeomba na kupewa. Hoja yao ilikuwa kwamba eneo la ziada
walilokuwa wanaliomba ndilo lenye malighafi nyingi na bora kwa utengenezaji wa
saruji. Hivyo, waliamua kusubiri mpaka watakapopewa eneo hilo.
Bahati mbaya eneo hilo lilikuwa linamilikiwa na mtu mwingine na alikuwa na
hati miliki nalo. Halmashauri ya Mtwara iliomba Serikali eneo hilo
litwaliwe na baadaye ipewe kampuni ya Dangote. Serikali ilikubali. Hata
hivyo, mchakato ulichukua muda na hata pale ulipokamilika mwenye eneo aliupinga
uamuzi wa Serikali Mahakamani. Kesi ilichukua muda kusikilizwa na
kumalizika. Bahati nzuri Serikali ikashinda na mara baada ya uamuzi wa
Mahakama ndipo kampuni ya Dangote ikamilikishwa eneo hilo.
Kampuni nayo ilichukua muda kuanza. Hivi sasa, timu yake ipo kwenye
eneo na mradi uko tayari kuanza kutekelezwa. Niliambiwa kuwa katika
magari yaliyopigwa mawe katika fujo za Mtwara ni pamoja na lile la mradi
huu. Huo ndiyo ukweli kuhusu ujenzi wa kiwanda cha saruji cha
Dangote. Madai kuwa kiwanda hicho kimehamishiwa Bagamoyo si ya
kweli. Ni uzushi wa makusudi wa watu wenye nia mbaya na
Serikali. Huwezi kudai kuwa mtetezi wa wananchi wa Mtwara kwa hoja za
uongo na kufanya upotoshaji wa makusudi kabisa.
Ndugu Wananchi;
Ujenzi wa
bomba la gesi ndiyo uliozua mzozo wote huu. Zilijengwa hisia kuwa gesi
yote inapelekwa Dar es Salaam na kwamba Mtwara itakosa gesi na maendeleo
yatayotokana na gesi hiyo. Na, wengine wakasema gesi inapalekwa Bagamoyo
ili kuzidisha chumvi na kupandikiza chuki kwa wananchi dhidi ya Serikali kwamba
Rais anapeleka gesi kwao. Kwanza, Kinyerezi iko Ilala na siyo Bagamoyo.
Pili, ukweli ni kwamba pale Mtwara kuna gesi nyingi ya kutosheleza mahitaji ya
Mtwara, Lindi na Dar es Salaam na kubaki. Gesi itakayoletwa Dar es Salaam
ni asilimia 16 tu ya gesi yote iliyoko Mtwara kwa miaka
ishirini ijayo. Hivyo asilimia 84 ya gesi itabaki Mtwara
kwa ajili ya kuuzwa nje ya nchi na kupelekwa kwingineko nchini.
Kwa sababu hiyo, ndugu zetu
wa Mtwara hawana sababu ya kuwa na wasiwasi. Ipo gesi ya kutosha kwa mahitaji
ya sasa na ya miaka mingi ijayo. Viwanda vinavyotumia gesi kama mali
ghafi na vile vinavyohitaji gesi kama nishati vyote vitapata gesi ya
kutosha. Kwa upande wa uzalishaji umeme hali kadhalika ipo gesi ya
kutosha kuzalisha umeme mwingi zaidi. Hivi sasa tunacho kituo
kinachozalisha umeme wa megawati 15 unaotumika Mtwara, Lindi,
Tandahimba, Newala, Masasi, Nachingwea, Ruangwa, na Mtama. Bado umeme huo
hautumiki wote hivi sasa.
Ndugu Wananchi;
Nayaeleza
yote haya kuwathibitishia wananchi wa Mtwara kuwa tunawathamini sana na kuwajali.
Mimi nitakuwa mtu wa mwisho kuwapuuza na kuwatupa mkono wananchi wa Mikoa ya
Kusini. Aidha, sitakuwa tayari kuwaruhusu watu au mtu ye yote Serikalini
kuwapuuza wananchi wa Mikoa ya Kusini au mkoa wo wote hapa nchini. Hiyo
haitakuwa sawa. Nilishasema siku za nyuma na napenda kurudia tena leo
kuwa kwangu mimi hakuna mkoa ulio bora kuliko mwingine. Ni kutokana na
msimamo wangu huo ndiyo maana tumeelekeza nguvu na rasilimali nyingi za
Serikali katika mikoa iliyokuwa inadaiwa kuwa imesahauliwa. Kazi ya
ujenzi wa barabara za lami iliyofanyika na inayoendelea kufanyika katika mikoa
ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Rukwa, Kigoma na Kagera inajieleza yenyewe. Mipango
ya kuboresha Kiwanja cha Ndege cha Mtwara kufikia hadhi ya kimataifa na
uboreshaji wa viwanja vya ndege vya Lindi na Kilwa ni ushahidi mwingine kati ya
mambo mengi tunayoweza kuyataja.
Ndugu Wananchi;
Haya
niliyoyasema ni sehemu ndogo tu ya yale yaliyofafanuliwa na kuelezwa kwa kina
na Mawaziri na Wakuu wa Idara husika za Serikali na Mashirika ya
Umma pale Mtwara katika mkutano wa Waziri Mkuu na viongozi wa Serikali, dini,
vyama vya siasa na wazee wa Mkoa wa Mtwara tarehe 29 Januari, 2013.
Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa
Mizengo Pinda, kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanya kule Mtwara. Uvumilivu
wake, usikivu wake na utulivu wake vimesaidia sana kulivusha taifa katika moja
ya mitihani mikubwa ambayo ingeikuta nchi yetu tangu Uhuru. Nawapongeza
Mawaziri na Wakuu wa Mashirika ya Umma na Idara za Serikali kwa mchango wao
muhimu walioutoa, uliosaidia kufafanua masuala ambayo yalikuwa hayaeleweki
vizuri. Kwa wao nawasisitiza na kuwakumbusha wajibu wao wa kuelimisha
jamii kuhusu shughuli wazifanyazo. Wakifanya hivyo mara kwa mara
migongano haitakuwepo na wapotoshaji hawatapata nafasi.
Ndugu Wananchi;
Nitakuwa
mwizi wa fadhila kama sitawashukuru viongozi wa Serikali, vyama vya siasa,
madhehebu ya dini, viongozi wa jamii, wazee, wana-Mtwara na makundi mbalimbali
ya jamii, kwa muda waliotumia kuzungumza na Waziri Mkuu na kuwasikiliza
wasaidizi wake wakifafanua masuala mbalimbali. Uvumilivu wao na uelewa
wao npyo vilivyosaidia kurejesha hali kuwa ya kawaida. Nawaomba nao sasa,
wote kwa pamoja washirikiane na Serikali kuelimisha umma kuhusu ukweli wa
mambo. Pia watumie nafasi hiyo kutahadharisha jamii na kuwataka watu kuwa
waangalifu na kupima maneno wanayoambiwa na watu. Wajiepushe na maneno au
vitendo vinavyofarakanisha, kuchonganisha na kupandikiza chuki dhidi ya watu au
Serikali. Waambieni kuwa ghasia hukimbiza wawekezaji kwani wakipata hofu kuwa
hali ya amani na usalama ni ya mashaka, watatoka kwenda kuwekeza
kwingine. Vyema iwe hapa hapa nchini, lakini wanaweza kwenda nchi
nyingine na sisi kupoteza kabisa.
Ndugu Wananchi;
Nawapa pole wananchi wa
Mtwara na Masasi kwa usumbufu walioupata kutokana na ghasia zilizofanywa.
Nawapa pole waliofiwa na kujeruhiwa. Nawapa pole waliopoteza au
kuharibiwa mali zao. Kwa kweli inasikitisha na kufadhaisha kuona watu wanafanya
vitendo vya kuua, kuchoma moto nyumba za watu na majengo ya Serikali pamoja na
, kuharibu na kuiba mali za watu. Huu ni uhalifu ambao hauna maelezo na
haukubaliki. Tunaviachia vyombo husika vya dola na sheria kutimiza wajibu
wao. Kwa waliohusika iwe fundisho kwao na kwa wengineo kutokubali
kutumika kwa maslahi ya watu wengine siku zijazo. Sasa wameachwa pekee
yao wakati wenzao wako huru na kufaidi maisha
Ndugu Wananchi;
Hili sakata la bomba la gesi limefika mahali pazuri. Yaliyopita si
ndwele tugange yajayo.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni Sana kwa
Kunisikiliza!
No comments:
Post a Comment