Wednesday, August 21, 2013

Wenje mbaroni Mwanza Kutokana na Maandamano ya Chadema yaliyosababisha Polisi kutumia Nguvu dhidi ya Waandamanaji



Na Sitta Tumma, Mwanza

SIKU moja baada ya Jeshi la Polisi mkoani hapa kulazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya wananchi na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), waliokuwa wakiandamana kutoka Uwanja wa Furahisha kuelekea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, mbunge wa Nyamagana jijini Mwanza, Ezekiel Wenje (CHADEMA), amekamatwa akituhumiwa kutenda makosa mawili.

Wenje alishikiliwa jana majira ya saa 5 asubuhi kwa mahojiano na Jeshi la Polisi yaliyodumu takribani saa nne.

Mbunge huyo aliitwa polisi kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na tuhuma za kuchochea maandamano na yeye kuandamana bila kibali, jambo lililosababisha ghasia na uvunjifu wa amani.

Inadaiwa na polisi kwamba mbunge huyo juzi aliongoza maandamano ya wafuasi wa CHADEMA na wananchi kutoka Uwanja wa Furahisha kuelekea ofisi ya mkuu wa mkoa, yalikokuwa yakifanyika mazungumzo baina ya Mkuu wa Mkoa Evarist Ndikilo na ujumbe ulioongozwa na mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia kuhusu hatima ya meya, naibu wake, na madiwani watatu waliofukuzwa kinyume cha sheria.

Wenje aliyeongozana na mwanasheria wake, Charles Kiteja, baadhi ya madiwani wa Nyamagana na Ilemela na viongozi wa CHADEMA Kanda ya Ziwa Magharibi, alifika katika ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Mwanza (RCO), majira ya saa 5 asubuhi.Akiwa huko, RCO Joseph Konyo na baadhi ya maofisa wengine wa jeshi hilo, walitumia takribani dakika 45 wakimhoji mbunge huyo kuhusiana na tuhuma hizo dhidi yake.

Wenje ambaye anasifika kwa msimamo na ushawishi mkubwa kwa wananchi ndani na nje ya jimbo lake la Nyamagana, aliliambia gazeti hili kwamba: “Polisi wanadai nimewaambia wananchi kwamba Ndikilo na Matata ni adui wa wananchi, na wakiwaona wawazomee.

“Wananituhumu pia kuongoza waandamanaji kutoka viwanja hivyo vya Furahisha kisha kuelekea ofisi za mkuu wa mkoa, pamoja na kusababisha barabara ya Nera-Makongoro Mission kuzibwa kutokana na ghasia zilizoibuka.”

Alipoulizwa kuhusiana na kushikiliwa kwa mbunge huyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, na Naibu Kamishna wa jeshi hilo, Ernest Mangu alikiri Wenje kushikiliwa.

“Kweli mheshimiwa Wenje tumemshikilia kwa mahojiano. Anatuhumiwa mambo mawili ya kuchochea maandamano na yeye kuandamana bila kibali cha polisi.

“Tunataka mheshimiwa Wenje atueleze alipata wapi idhini ya kuandamana bila kibali, na aliandamana na akina nani. Asipotutajia alioandamana nao tutamng’ang’ania yeye hadi kieleweke,” alisema RPC Mangu.

Juzi majira ya alasiri, ziliibuka ghasia baada ya Jeshi la Polisi kulazimika kutumia mabomu ya machozi, kuwatawanya wafuasi wa CHADEMA.

Ghasia hizo zilitokea wakati wa maandamano ya chama hicho yaliyolenga kupinga uchaguzi ‘batili’ wa Meya wa Manispaa ya Ilemela, Henry Matata na Naibu wake, Swila Dede, pamoja na kupinga kufukuzwa madiwani watatu wa chama hicho kinyume cha taratibu, kanuni na sheria za nchi.

Madiwani waliofukuzwa na Matata kinyume cha sheria na kata zao kwenye mabano ni Abubakar Kapera (Nyamanoro), Malietha Chenyenge (Ilemela), na Dany Kahungu (Kirumba).

Tarime hakukaliki

Wakati sakata la meya huyo likizidi kuchemka jijini Mwanza, Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika hatua inayozidi kuushangaza umma, kimeingilia kati na kuingizwa madiwani wake watatu wa viti maalumu kinyume na utaratibu katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

Hatua hiyo ilipingwa vikali na madiwani wa CHADEMA wakiongozwa na Charles Ndesi Mbusiro wa Kata ya Turwa, waliosusia kikao cha uchaguzi na kuitaka serikali izingatie hati ya awali iliyotolewa na Katibu wa Bunge, Thomas Kashililla iliyotaka utaratibu wa uwiano wa idadi ya kila madiwani wa vyama waliochaguliwa katika kata mbalimbali kutimia moja ya tatu yao.

“Sisi tumesusia kikao cha kuchagua mwenyekiti wa halmashauri hiyo na makamu wake na kuamua kupanga mipango yatu thabiti kwa ajili ya kuipinga hati iliyowaingiza madiwani wa viti maalumu; Prischal Matinde, Saluma Abubakari na Adina Chambiri ili utumike ule ulioletwa na Katibu wa Bunge Kashilila wa kutumia moja ya tatu ya madiwani wa kuchaguliwa kisheria,” alisema Ndessi.

Wajumbe wa halmashauri hiyo waliosusia kikao hicho ni Peter Marwa Chacha (Kata ya Nyandoto), Mbusiro (Turwa), Christopher Chomete (Sabasaba), Thobias Elias Ghati (Nyamisangura) na Mbunge wa viti maalumu, Esther Nicholous Matiko.

Hatua hiyo ilisababisha kikao kubaki na wajumbe wake saba, wote wakiwa madiwani wa CCM wakiwamo mbunge wa Jimbo la Tarime Nyambari Chacha Nyangwine na Waziri wa Ajira na Kazi, Gaudensia Kabaka hivyo kufikisha idadi ya wajumbe 12, na hivyo kuendesha uchaguzi uliomchagua diwani Daudi Mrimi Wangwe (mdogo wa marehemu Chacha Wangwe) kuwa mwenyekiti wa halmashauri na makamu wake Godfrey Michael Masubo.

Uchaguzi huo umekuja baada ya hati yake kukabidhiwa kwa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Venance Mwamengo Agosti 16 mwaka huu baada ya kuvunjwa kwa baraza la madiwani na mwenyekiti wake Amos Sagara, kulipotangazwa rasmi Julai 1, mwaka huu na Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Gabriel Tuppa.

Source: www.freemedia.co.tz/daima/

No comments: