Sunday, August 25, 2013

Jaji Mihayo: Rushwa imekithiri

Dar es Salaam. Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Thomas Mihayo amesema kushamiri kwa matukio ya uuzwaji, ununuaji wa dawa za kulevya, sambamba na upitishaji wa dawa hizo katika viwanja mbalimbali vya ndege nchini, kunachangiwa na rushwa iliyokithiri katika Mahakama na Polisi.

Amesema matukio mengi ya mauaji ya raia wasio na hatia pamoja na upitishwaji wa wanyamapori (Twiga) katika viwanja vya ndege mbalimbali nchini hayachukuliwi hatua stahiki kwasababu rushwa imetawala, “Kuzungumzia rushwa siyo hoja, tatizo ni kuwa matendo yetu ni tofauti na kauli tunazotoa.” Katika maelezo yake alisema anamuonea huruma Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, kwani licha ya kuonyesha wazi kutaka kupambana na watu wanaoingiza dawa za kulevya kupitia katika viwanja vya ndege, hataweza kwa maelezo kuwa rushwa ndiyo inafanikisha mipango yote ya uingizwaji wa dawa hizo.

Jaji Mihayo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) aliyasema hayo jana katika mahojiano maalumu na Mwananchi Jumapili, huku akitoa mifano ya kesi mbalimbali ambazo watuhumiwa waliachiwa huru katika mazingira yanayoonekana wazi kuwa Mahakimu walipewa rushwa.

“Twiga kusafirishwa kupitia viwanja vya ndege maana yake ni rushwa ilitembea na siyo uzembe. Sasa tunaona mauaji ya watu wasio na hatia lakini vyombo vya dola vinafumba macho na hakuna kinachofanyika.Katika nchi inayofuata sheria mambo kama haya lazima yafanyiwe kazi, lakini ukiona kimya maana yake rushwa imetawala” alisema na kuongeza;

“Rushwa imetoka huko sasa imeingia katika dawa za kulevya, Watanzania wengi wanadhani dawa za kulevya kupita katika uwanja wa ndege ni uzembe wa wasimamizi, hilo siyo kweli yamepita kwa sababu ya rushwa.”
“Hawa watu polisi wanawajua lakini wanawalinda…, ndiyo wanalindwa na haohao polisi” alisisitiza.

Akitolea mfano tukio la Julai 5 mwaka huu la upitishaji wa mabegi tisa ya dawa za kulevya katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) lililoanikwa na hadharani na Dk Mwakyembe, ambapo watu mbalimbali walitajwa kuhusika, wakiwemo maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa ambao walidaiwa kuchelewesha mbwa kwa ajili ya kukagua mizigo alisema, “Mbwa hawawezi kupokea rushwa na kama wangekuwepo katika uwanja wa ndege. Ni wazi kuwa wangeweza kubaini dawa hizo za kulevya.”

Alifafanua, “Dk Mwakyembe alieleza wazi kuwa mbwa walichelewa kufika uwanja wa ndege, swali la kujiuliza kwa nini walichelewa? Sababu za kuwachelewesha zinaweza kuwa nyingi tu, unaweza kusema gari liliharibika.”

Alisema haoni uwezekano wa Dk Mwakyembe kufanikiwa katika mapambano hayo, kwani hata kama viwanja vya ndege vitafungwa mashine za kubaini waliobeba dawa hizo, kama wasimamiaji watapokea rushwa hakuna atakayekamatwa.

“Kama kutakuwa na sheria kali za kudhibiti dawa za kulevya basi watekelezaji wa sheria hizo wanatakiwa kuwa waaminifu na kuichukia rushwa. Pia tunaweza kuwa na sheria kali lakini ndiyo rushwa ikaongezeka zaidi” alisema Jaji Mihayo
“Watanzania watafanikiwa kuikomesha rushwa kama wakiichukia. Nasema hivi kwa sababu siku hizi mtu aliyekithiri kwa kupokea rushwa anashabikiwa na wenzake. Mahakama zetu nazo zinatakiwa zitekeleze wajibu wake ipasavyo” alisema
Rushwa katika Mahakama
Huku akitoa mifano halisi, Jaji Mihayo alisema kuwa hivi karibuni alisomewa hukumu moja ya kesi ya dawa za kulevya na Dk Mwakyembe, hukumu aliyodai kuwa inaonekana wazi hakimu alipewa rushwa.

Bila kutaja Mahakama wala hakimu aliyetoa huku hiyo alisema, “ Kuna mtu mmoja alikamatwa na dawa za kulevya akiwa amezimeza baadaye alifikishwa mahakamani huku dawa zile alizokutwa nazo zikitumika kama ushahidi,”
“Cha ajabu wakati wa hukumu ya kesi hiyo hakimu alimuachia huru mtuhumiwa kwa maelezo kuwa hakukuwa na ushahidi wa kutosha kwamba dawa zile za kulevya zilikuwa zimemezwa na mtuhumiwa huyo. Mimi ni Jaji nilisikiliza uchakachuaji wa kesi hiyo nilijua tu kuna rushwa ilitembea.”

Alisema kesi nyingine ambayo uamuzi wake ulikuwa ya utata, alielezwa na ofisa mmoja wa Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
“Yule ofisa wa Takukuru alinieleza kuwa kuna jamaa mmoja aliombwa rushwa na Sh1milioni. Kutokana na hali hiyo mtu huyo alikwenda kuripoti Takukuru ambao waliandaa mpango wa kumkamata mwomba rushwa kwa kumweka mtego wa Sh500,000” alisema na kuongeza;
“Yule mtu aliyeomba rushwa alikamatwa na kufikishwa mahakamani, ila cha kushangaza hakimu alimwachia huru mtuhumiwa, kwa maelezo kuwa aliomba Sh1 milioni lakini alipewa Sh500,000. Hiki ni kichekesho kweli yaani kwasababu fedha aliyoomba siyo aliyopewa basi akaachiwa huru.”

Chanzo: Mwananchi

No comments: