Monday, August 19, 2013

Serikali inapoteza Sh700 bilioni kwa risiti za mkono



Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu (PAC), Zitto Kabwe.

Serikali hupoteza zaidi ya Sh700 bilioni kwa mwaka kutokana na utaratibu wa kukusanya mapato kwa kutumia stakabadhi zinazoandikwa kwa mkono.

Taarifa iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu (PAC), Zitto Kabwe imesema kwa sasa Serikali hukusanya Sh741 bilioni kwa mapato yasiyo ya kikodi ambayo ni nusu tu ya mapato ambayo Serikali ingestahili kupata.

Zitto, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), ameishauri Serikali itumie risiti za elektroniki kwa kukusanya maduhuli.
"Utaratibu wa kutumia risiti za elektroniki utaongeza maradufu mapato ya Serikali na kuifanya kuachana na mtindo wa kupandisha kodi kwenye bidhaa muhimu kwa wananchi.

"Uamuzi wa Kamati za Bunge za Hesabu wa kuitaka Serikali kukusanya maduhuli yake kwa kutumia risiti za elektroniki unapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania," ilisema taarifa hiyo ya Zitto.
Alisema walipitia mpango wa Serikali na kugundua kuwa mapato yasiyo ya kikodi yamekadiriwa kuwa ni Sh741 bilioni kutoka wizara, idara na mikoa.
"Serikali inapata Sh383 bilioni kutoka kwenye halmashauri za wilaya, miji na manispaa. Hatukuweza kupata mapato ya mashirika ya umma maana hayaletwi kwenye Bajeti za Serikali," alisema.
Wizara zinazoongoza kwa mapato (mapato kwenye mabano ni Nishati na Madini (Sh220 bilioni), Fedha (Sh126 bilioni), Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi (Sh100 bilioni), Maliasili na Utalii (Sh84 bilioni), Mambo ya Ndani (Uhamiaji Sh92 bilioni na Usalama Barabarani Sh17 bilioni), Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi (Sh19 bilioni), Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (Sh16 bilioni).
Hata hivyo, Zitto alisema mapato ya Serikali yameongezeka kwa asilimia 60 kutoka Sh500 bilioni mpaka Sh800 bilioni.

Maazimio
Pia kamati tatu zinazosimamia hesabu za Serikali zimetoa maazimio 14 baada ya kumalizika kwa mafunzo yaliyofanyika Bagamoyo wiki iliyopita.
Kamati hizo za PAC, Bajeti na ile ya Serikali za Mitaa (LAAC), zimeagiza kuwapo kwa mkutano kati ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Hazina, Hesabu za Bunge, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ili kupata usahihi wa deni la taifa.
Pia kamati hizo zimesema kuna umuhimu wa kuandaa mkutano wa kutathmini mafanikio na changamoto za mfumo wa bajeti ya mwaka huu na kukutana na maofisa masuuli hatarishi (risk based) ili kutathmini utendaji wao.

Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge na Tamisemi zimetakiwa kuanza kuratibu mikutano na mafunzo ya wakurugenzi wa halmashauri na kuanzishwa kwa mfumo wa kutunza kumbukumbu za hesabu na nyaraka mbalimbali katika Serikali Kuu na halmashauri.
"Kamati zimetaka CAG akague mara kwa mara sehemu zote zenye matatizo, pia wametaka taarifa za mwaka za kamati za Bunge ziwe na kipengele cha kiwango cha utekelezaji wa mapendekezo ya kamati yaliyotolewa awali.
"Pia mikataba katika ngazi ya Serikali za Mitaa iandikwe kwa Kiswahili. Serikali inatakiwa kufanya jitihada za ziada kuzalisha wataalamu wa fani ya ununuzi na bajeti ya Bunge iongezwe kupitia Mfuko wa Bunge na iwasilishwe bungeni na Naibu Spika na siyo Ofisi ya Waziri Mkuu," iliongeza taarifa hiyo.

Kamati hizo pia zimeitaka Serikali iandae mjadala wa kitaifa wa kutafuta ufumbuzi wa kukabiliana na vitendo vya rushwa na mmomonyoko wa maadili na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma iweke uwazi wa kutangaza umiliki wa mali za viongozi.
Pia kamati hizo zimetaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani kuhakikisha askari wa usalama barabarani wanatumia utaratibu wa kisasa wa kutoa risiti za malipo za elektroniki. Ofisi za Serikali zifanye ununuzi wake kwa wafanyabiashara wanaotumia mashine za kielektroniki pekee.

TRA pia imetakiwa kuhamasisha wananchi na wafanyabiashara umuhimu wa matumizi ya risiti za elektroniki na Serikali idhibiti kampuni za uwakala wa kupakia na kupakua mizigo.
Kamati hizo pia zimeshauri Sheria ya Kupambana na Utakatishaji wa Fedha ya 2006 irekebishwe ili iweke viwango vya fedha ambazo mtu anaweza kuingia au kutoka nazo nchini bila kuzitaja.
Source: www.mjengwablog.co.tz

No comments: