Ndugu zangu,
Ndugu Kingunge Ngombale Mwiru ni
mmoja wa wanasiasa ninaowaheshimu sana. Nimemsikia Kingunge tangu nikiwa na
miaka saba.
Lakini, kama ilivyokuwa kwa Mwalimu
Nyerere, hakuwa malaika, Kingunge naye ni mwanadamu kama wengine. Si malaika.
Nimeyasikia mawazo ya Kingunge juu ya
Serikali Tatu na hata Uraia wa Nchi Mbili. Ni mawazo yake, nayaheshimu, ingawa,
kwa mtazamo wangu, Kingunge hayuko sahihi kwenye yote mawili.
Na hapa nitalizungumzia hili moja tu
la mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba juu ya muundo wa Muungano wa
Serikali Tatu.
Kimsingi haya ni mapendekezo yenye
kutokana na maoni Wananchi. Hivyo, Tume imewasilisha tu. Si mapendekezo ya Jaji
Warioba au wajumbe wake.
Hii ni tofauti kubwa na mazoea ya '
Ukale' ya Mzee Kingunge ambayo hata sasa anataka yafuatwe; kuwa jambo kubwa la
muundo wa Muungano liachiwe Chama Cha Mapinduzi na vikao vyake.
Ni jambo jema kwa mwanadamu kujifunza
kutokana na historia, lakini, si jambo jema kwa mwanadamu kuwa mtumwa wa
historia. Ni bahati mbaya, kuwa Mzee wetu mpendwa, Kingunge Ngombare Mwiru,
anataka tubaki kwenye utumwa wa historia. Hatutaki.
Na hakika Mzee Kingunge anapaswa
kuelewa, kuwa nchi hii ni zaidi ya Chama cha Siasa. Na chama cha siasa kilicho
madarakani hakiongozi mawe. Na hata kama kingekuwa kinaongoza tumbiri, bado
kingekumbwa na changamoto ya uwepo wa tumbiri wenye kutaka mabadiliko,
kulingana na mahitaji ya wakati.
Tukubali, kuwa yalifanyika makosa
makubwa ya kiuongozi huko nyuma. Ni pale masuala makubwa ya kitaifa kuachwa
maamuzi yake kufanywa na kundi dogo la watu kwa kutumia nyadhifa za uongozi wa
chama. Kwenye masuala makubwa ya nchi Chama kiliamua juu ya vichwa vya watu
bila kushirikisha mawazo ya wananchi wenyewe, iwe kwa kupitia kura za maoni au
kukusanya tu maoni ya makundi wakilishi. Huo ni msingi wa manung'uniko mengi ya
sasa.
Kwangu mimi, Jakaya Kikwete ni
mwanamageuzi wa kweli ambaye, kama kiongozi, ameonyesha ujasiri mkubwa wa
kuzipa mgongo fikra za ukale na kuiangalia zaidi nchi na mustakabali wake kwa
miaka mingi ijayo. Anafanya hivyo bila kujali nani au chama gani kitakuwa
madarakani.
Wakati Mzee Kingunge na wahafidhina (
wasiotaka mabadiliko) wengine ndani ya mfumo uliopo wanatoka mahandakini huku
wakihaha kujaribu kuurudisha nyuma mshale wa mabadiliko chanya kwa jamii ,
Jakaya Kikwete anaonekana, kuwa sio tu amesimama imara katika kuhakikisha
mshale wa saa ya mabadiliko chanya kwa nchi unakwenda mbele, bali, unakwenda
mbele kwa kasi.
Ni imani yetu, Wananchi walio wengi,
kuwa Jakaya Kikwete hatakatishwa tamaa wala kuyumbishwa katika kukamilisha
ajenda yake njema ya mabadiliko chanya kwa jamii ya Watanzania kuelekea miaka
50 ijayo.
Mzee Kingunge aelewe pia, kuwa wakati
umebadilika. Kuwa ya mwaka 1974 alipojiunga na TANU ni tofauti na ya sasa,
mwaka 2013. Huu ni wakati wa kiongozi kuonyesha uwezo wa kusoma alama za
nyakati. Hivyo, kujitahidi kuendana na mabadiliko ya nyakati.
Hiyo pia ndio tafsiri ya kuwa ' Kiongozi
wa Kisasa na Kimaendeleo'- A modern and progressive leader. Jakaya Kikwete kwa
sasa yumo kwenye kundi hilo.
Na wenzake ndani ya CCM wakimsaidia
katika kazi yake, basi, ni fursa pia kwa Chama chao kuiteka tena mioyo ya
Wananchi wengi, mijini na vijijini. Maana, kati ya ambayo yanawachosha wananchi
ni kukosekana kwa mawazo ya usasa na ya kimaendeleo kutoka kwa miongoni mwa
viongozi wa CCM. Ni moja ya sababu ya chama hicho kupungukiwa na mvuto hususan
kwenye kundi kubwa la vijana.
Na hakika, hata kama hatuoni leo,
historia itakuja kumkumbuka Jakaya Kikwete kama mmoja wa viongozi Wana-Mageuzi
ndani ya Chama chake CCM, na nchi kwa ujumla.
Maggid.
Iringa.
Iringa.
MAKALA HII IMEANDIKWA NA MAGGID
Chanzo: mjengwablog.com