Mbunge wa Musoma Vijijini
(CCM),Nimrod Mkono.
Aishangaa kutumia nguvu kubwa kulinda
wanyamapori kuliko binadamu
Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono,
ameishutumu serikali kwa kushindwa kudhibiti mauaji ya kikatili wanayofanyiwa
wanawake katika baadhi ya vijiji vya tarafa ya Nyanja jimboni mwake akisema
imekuwa ikitumia nguvu kubwa kulinda wanyama pori kuliko binadamu.
Mkono alitoa kauli hiyo juzi katika
kijiji cha Mugango baada ya watu wasiojulikana kumnyonga hadi kufa kwa kutumia
upande wa khanga, Anastazia Mang’ombe (42), baada ya kumbaka shambani kwake.
Mauaji ya mwanamke huyo ni mwendelezo
wa mauaji ya kinyama na kikatili yanayotokea katika vijiji vya mwambao wa Ziwa
Victoria vya Nyakatende, Etaro, Nyegina,
Mkirira katika tarafa hiyo yakihusisha wanawake.
Mpaka sasa, hao ni mauaji ya pili
kutokea katika kipindi cha wiki mbili katika jimbo hilo.
Katika tukio la kwanza, mwanamke
mwingine mkazi wa kijiji Kamguruki kata ya Nyakatende wilayani humo, aliuawa
katika mazingira yanayofanana na hayo.
Alisema tangu kuibuka kwa wimbi la mauaji
hayo ya kinyama ambayo hadi sasa yanahusishwa na imani za kishirikina, hakuna
hatua zozote zilizochukuliwa na serikali licha ya viongozi wake kutoa kauli za
kisiasa ambazo zimeshindwa kumaliza mauaji hayo na hivyo kuongeza hofu kubwa
kwa jamii hasa wanawake.
“Jamani, mauaji haya ya wanawake
mwisho wake utakuwa lini, hivi serikali iko wapi, mbona tembo mmoja tu akiuawa
tunasikia filimbi na ndege zinaruka huku na huku kuwasaka wauaji? Iweje leo
binadamu hasa hawa wanawake wanauawa bila hatia hatujasikia serikali imechukua
hatua?
“Akina mama zangu wanauawa,
wanachinjwa kama kuku, sijaiona serikali ikichukua hatua. Sasa ni wakati wa
Waziri Mkuu na Rais wetu waje hapa ili kutusaidia kukomesha mauaji haya ya
kikatili…hivi niwaweke wapi akinamama ambao sasa wanaishi kwa hofu kubwa?,”
Alisema Mkono huku akibubujikwa na machozi.
Kwa sababu hiyo, mbunge huyo alisema
serikali inaonekana kuwapuuza wananchi hao wanauawa kinyama kwani ina vyombo
vya kuwabaini wauaji wote na kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Nakwenda bungeni kupigania hili
kwani ni janga la kitaifa. Ikiwezikana serikali itangaze operesheni maalum kama
ilivyofanya katika kupambana na ujangili,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati
ya Ulinzi na Usalama ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Angelina Mabula, pamoja na kulaani vikali
mauaji hayo, amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili
kuhakikisha wauaji hao wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
“Kwa kweli hali ni mbaya, nawaomba
muwe watulivu kwani matukio haya yametuchanganya. Wiki iliyopita wanawake
wawili wameuawa hivi hivi ukiangalia matukio yote yanafanana na yanafanyika
wazi. Sasa lazima tujiulize wote hapa kuna nini?," Alihoji.
Aliongeza: “Hata tufanyaje polisi
hawawezi kutosha kulinda wote, lazima tuweke mikakati ya pamoja katika
kushughulikia mauaji haya...kwa muda mfupi tu kwa eneo hili la kata nne,
wanawake wanane wameuawa kikatili na mauaji yote yanafanana,” alisema.
Kwa msingi huo, aliwaomba wananchi
kutoa taarifa za kina kwa vyombo vya dola zikiwamo ofisi za viongozi katika
kuhakikisha mauaji hayo yanakomeshwa.
Hata hivyo, litoa agizo kwa wanaume
kuwasindikiza wake zao mashambani na katika shughuli nyingine za kutafuta
kipato wakati vyombo vya dola vikipambana na vitendo hivyo.
Alisema viongozi wa serikali sasa
wameshindwa kuhamasisha shughuli za maendeleo kwani muda wote wamekuwa
wakishughulikia matukio ya mauaji kila uchao.
Kwa mujibu mujibu wa Mkuu huyo wa
Wilaya, hadi sasa watu watano wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji kama
hayo huku wanne wakishikiliwa polisi kwa uchunguzi.
Naye katibu wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) wilaya ya Butiama, Mercy Mollol, aliomba serikali kutangaza eneo hilo
kuwa kanda maalum ya kipolisi ili kuongeza idadi ya askari wa kukabiliana na
mauaji hayo.
“Kama Chama tumesikitishwa sana na
mauaji haya yanayoendelea katika eneo hili. Sasa tunaitaka serikali chini ya
Rais Jakaya Kikwete na IGP Mango, kutangaza operesheni ya watu wanaoua wanawake
kabla hatujatangaza maandamano makubwa ya kupinga ukatili huu,” alisema.
Kamanda wa Polisi mkoani Mara,
Ferdinand Mtui, akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu, alithibitisha kutokea
kwa tukio hilo.
Kamanda Mtui alisema hadi sasa watu
watatu wanashikiliwa polisi kwa mahojiano.
Chanzo: Nipashe