Pigo Chadema |
Thursday, 05 April 2012 10:56 |
LEMA AVULIWA UBUNGE ARUSHA MJINI, JAJI AMZUIA KUGOMBEA MIAKA MITANO, VILIO MAHAKAMANI Waandishi Wetu, Arusha MAKAHAMA Kuu Kanda ya Arusha, imetengua matokeo ya ubunge yaliyompa ushindi mgombea wa Chadema, Godbless Lema baada ya kuridhika kuwa alitumia lugha ya kashfa na udhalilishaji dhidi ya aliyekuwa mpinzani wake katika uchaguzi huo wa mwaka 2010, Dk Batilda Burian. Lema ni mbunge wa nne nchini kuvuliwa ubunge na mahakama katika kipindi cha miaka 16 iliyopita kutokana na kasoro zilizojitokeza katika mchakato wa uchaguzi. Akisoma hukumu yake jana iliyochukua zaidi ya saa nzima, Jaji Gabriel Rwakibarila alimtia hatiani Lema kwa makosa mawili kati ya manne aliyokuwa akikabiliwa nayo, huku akitupa mawili kwa kukosa ushahidi. Ndani ya ukumbi wa mahakama uliojaa wanachama, wafuasi na wapenzi wa Chadema, Jaji Rwakibarila alimvua ubunge Lema baada ya kuridhika na ushahidi kuwa alitumia maneno ya kashfa na ubaguzi wa jinsia dhidi ya aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk Batilda Burian. Jaji Rwakibarila katika hukumu yake hiyo, pia alimwamuru Lema kulipa gharama za kesi hiyo na kwamba ana haki ya kukata rufaa ikiwa hajaridhika na hukumu hiyo. Uamuzi wa Jaji huyo ni kama umetia doa shamrashamra za Chadema ambazo zilikuwa zikiendelea baada ya chama hicho kushinda kiti cha ubunge katika uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki, kupitia kwa mgombea wake, Joshua Nassari. Makosa ya Lema Lema alitiwa hatiani kwa kudaiwa kusema kuwa Dk Burian hakustahili kuchaguliwa kuwa mbunge kwa sababu mila na desturi za makabila ya Waarusha (Wamaasai na Wachaga), mwanamke hawezi kuongoza wazee. Sababu ya pili aliyotumia Jaji kutengua ubunge wa Lema kutoa maneno ya kashfa dhidi ya Dk Burian kuwa ni mwanamke asiye mwaminifu, aliyezaa nje ya ndoa na alikuwa na mimba nyingine na bwana huyo aliyezaa naye ambaye siyo mumewe. Jaji Rwakibarila alitupilia mbali madai mawili ya kutumia lugha na maneno yenye mwelekeo wa ubaguzi wa kidini na ubaguzi wa makazi. Kuhusu ubaguzi wa kidini alikataa madai ya walalamikaji Mussa Mkanga, Agness Mollel na Happy Kivuyo kuwa kauli ya Lema kuwataka wapiga kura wa Arusha kujihadhari na wanaovaa vitambaa na hijabu wasije kujikuta wanachagua Al Qaida kuwa haihusiani na dini ya Kiislamu. “Mwanamke kuvaa kitambaa kichwani haina uhusiano wowote na dini ya Kiislam wala Al Qaida kwani ni dhahiri wanawake wengi ambao baadhi yao siyo Waislam wanavaa vitambaa. Kwanza ni heshima kwa wanawake kuvaa vilemba hivyo madai haya nayatupilia mbali,” alisema Jaji Rwakibarila katika hukumu yake. Kuhusu tofauti ya ukaazi kati ya Lema na Dk Burian aliyedaiwa kuolewa na kuishi Zanzibar, Jaji huyo alisema hoja hiyo isingeharibu wala kwenda kinyume na maadili ya kampeni kwani kisheria Mtanzania ana haki ya kuishi upande wowote wa Jamhuri ya Muungano, yaani Bara na Visiwani. Katika shauri hilo namba 13/2010, wadai waliowakilishwa mahakamani na Mawakili Alute Mughwai na Modest Akida, waliomba mahakama kutengua matokeo yaliyompa ushindi Lema kwa madai kuwa alitumia lugha na kauli za matusi, kashfa na udhalilishaji dhidi ya Dk Burian wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita. Jaji Rwakibarila alisema baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi 14 wa upande wa wadai na wanne wa upande wa utetezi, aliridhika kuwa Lema alitamka maneno ya kibaguzi, kijinsia na kashfa dhidi ya Dk Burian katika mikutano yake minane ya kampeni kati ya mikutano zaidi ya 60 aliyofanya. Kabla ya kuanza kusikilizwa mbele ya Jaji Rwakibarila, shauri hilo lilikuwa mbele ya Jaji Aloyce Mujulizi aliyejitoa baada ya Lema kueleza kutokuwa na imani naye kutokana na wabunge wa Chadema kuwahi kuituhumu kampuni yake ya uwakili ya IMMA aliyokuwa akifanyia kazi kabla ya kuteuliwa kuhusika na ufisadi wa akaunti ya EPA katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Jaji Rwakibarila alianza kusikiliza shauri hilo mfululizo kuanzia mapema Februari kutokana na kutakiwa kulimazika kabla ya Mei 3, mwaka huu kutokana na mahitaji ya kisheria inayoelekeza kesi za uchaguzi zisikilizwe na kuamuliwa ndani ya mwaka mmoja tangu kufunguliwa. Licha ya kuibuka washindi kwa uamuzi wa Jaji jana, wadai katika shauri hilo pamoja na mawakili wao walionekana kupigwa bumbuwazi mahakamani bila kuamini kilichotokea hadi watu walipoanza kuondoka baada ya Jaji kutoka ndipo waliposimama na kuanza kukumbatiana na kupongezana. Baada ya mwaka mmoja kukamilika Novemba, mwaka jana, Msajili wa Mahakama Kuu, Herbert George aliandika barua kwa Waziri mwenye dhamana ya sheria ambaye aliongeza kipindi cha ziada cha miezi sita kinachomalizika Mei 3, mwaka huu. Mkanganyiko kwenye hukumu Jaji Rwakibarila kwa upande mwingine anadaiwa kujichanganya katika vifungu vya sheria alivyotumia katika uamuzi wake. Akitoa uamuzi wake jana, Jaji huyo alisema Lema alithibitika kutenda kosa la kutumia maneno yasiyostahili kwenye kampeni zake za Uchaguzi Mkuu mwaka 2010. Kwa kauli ya kisheria, Jaji alisema Lema anatiwa hatiani kwa kosa la ‘Illegal Campaign’ kwa kutoa kauli za kumbagua kijinsia Dk Burian akitumia tofauti yao ya kimaumbile ya yeye kuwa mwanamme na mwenzake mwanamke aliposema mila na desturi za Waarusha na Wachaga haziruhusu mwanamke kuongoza wanaume. Alisema hata kauli ya Lema kuwa Dk Burian siyo mwanamke mwaminifu aliyezaa nje na kupata mimba nje ya ndoa ilikuwa ya kashfa dhidi ya mgombea huyo wa CCM na kutafsiri kosa hilo kama ‘Illegal Campaign’ aliyosema inatosha kutengua matokeo ya uchaguzi. Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi, makosa yote mawili yanaangukia kwenye kifungu cha 108, kifungu kidogo cha pili aya ‘A’ ambayo humruhusu aliyevuliwa ubunge kugombea kwenye uchaguzi mdogo utakaoitishwa. Lakini katika majumuisho ya hukumu yake, Jaji Rwakibarila alitumia kifungu cha 114 cha sheria ya uchaguzi inayozungumzia “Illegal Practice” ambayo yanaangukia kwenye makosa yanayohusiana na vitendo vya rushwa kwa wapiga kura, watendaji wa Serikali na watumishi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Wakili wa Lema, Method Kimomogoro alithibitisha utata huo na kusema atafuatilia kujua iwapo Jaji Rwakibarila alijichanga katika kutaja vifungu hivyo vyenye maana na adhabu tofauti kisheria. “Anayehukumiwa kwa makosa yanayoangukia kwenye kifungu cha 108 (II) (A) kama ilivyotokea kwa mteja wangu (Lema) anaruhusiwa kugombea kwenye uchaguzi, lakini kwa mshangao wakati akihitimisha hukumu yake jaji alitaja kifungu cha 114 ambacho ni kinyume na makosa aliyokutwa nayo Lema,” alidai Wakili Kimomogoro. Bila kutaka kuingia kwa undani katika suala hilo hadi atakapopata nakala ya hukumu hiyo, Kimomogoro alidai hadi jana jioni alikuwa hajapata maelekezo yoyote kutoka kwa mteja wake kuhusu hatua za kuchukua dhidi ya uamuzi huo. Kimomogoro alieleza kuwa iwapo hukumu hiyoitaachwa kubakia kwenye kifungu hicho cha 114 ina maana mteja wake Lema hataruhusiwa kugombea ubunge kwa kipindi kisichopungua miaka mitano, jambo ambalo siyo haki kwa sababu hakushtakiwa wala kukutwa na hatia ya kujihusisha na rushwa wakati wa kampeni. Kwa upande wake, wakili wa wadai Alute Mughwai aliyekuwa akisaidianana Modest Akida alieleza kuridhishwa na uamuzi huo ingawa aliahidi kuwasiliana na wateja wake kuangalia uwezekano wa kukatia rufaa hoja mbili za ubaguzi kimakaazi na kidini zilizotupwa na mahakama. Happy Kivuyo aliyekuwa mdai wa tatu katika shauri hilo nambo 13/2010 alieleza kufurahishwa na hukumu hiyo aliyodai imewatendea haki wote waliochukizwa na matusi, kashfa na udhalilishaji uliofanywa na Lema dhidi ya Dk Burian. Kauli ya Mbowe Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, amevitaka vyombo vyenye Mamlaka ya Maamuzi nchini, ikiwepo Mahakama kusoma alama za nyakati kabla ya kutoa uamuzi ambao unaweza kusababisha nchi kuingia katika machafuko. Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za Chadema Mkoa wa Arusha, eneo la Ngarenaro, kuhusu hukumu ya Jaji Rwakibarila, Mbowe alisema ni hatari pale watu wanapoanza kutilia shaka vyombo vya uamuzi kama Mahakama Kuu. “Sitaki kuingilia uamuzi ya mahakama, lakini ni kweli kuwa uamuzi wa hukumu hii ulivuja hata kabla ya kusomwa, tulipewa taarifa za ubunge wa Lema kutenguliwa, sasa hili ni jambo la hatari kama tutaendelea kuvujisha uamuzi wa kisheria, nchi inaweza kuingia kwenye machafuko pale watawala wanapoingilia vyombo vya kisheria,”alisema Mbowe. Alisema Serikali na vyombo vingine vyenye Mamlaka, ni lazima wajue kuwa, enzi za kuwaburuza watu zimepitwa na wakati. “Mahakama zisifikiri zinaweza kufanya kila ambacho zinataka bila kuzingatia, sheria, taratibu na matakwa ya umma, mimi sitaki tukife huko,”alisema Mbowe. Alisema katika kesi hiyo ya Lema, wanaamini uamuzi ya mahakama umeingiliwa na chombo kingine jambo ambalo ni hatari katika utawala wa Sheria. Kukata rufani Kuhusu Chadema kuukatia rufaa uamuzi wa Lema kuvuliwa ubunge, Mbowe alisema bado wanasubiri nakala ya hukumu ya kesi hiyo na wanafanya majadiliano kupitia mawakili wa chama hicho na viongozi wengine na kisha watatoa uamuzi ambao utatangazwa kesho Jumamosi kwenye mkutano wa hadhara. Mbowe alisema, ingawa wananchi wengi wa Arusha wanataka kurejewa haraka kwa uchaguzi, lakini, hawafahamu kama Mbunge wao Lema, kulingana na hukumu hiyo ataruhusiwi kugombea tena. “Kabla ya kufikia uamuzi wowote tumeona ni busara kwanza, tukae kwani Lema ambaye wanamtaka kwa hukumu hii ni lazima tukate rufani,”alisema Mbowe. Hata hivyo, aliwaomba wananchi wa Arusha, kutulia kwa sasa na kutofanya vurugu zozote ili kuthibitisha Chadema sio chama cha vurugu na ni chama cha wanademokrasia wa kweli. Alisema katika mkutano wa Jumamosi, watatoa tamko la pamoja kama watakata rufani au watatoa nafasi kwa wanachama wengine wa Chadema kujitokeza kumrithi Lema. Kabla ya kukutana na waandishi wa habari, Mbowe alizungumza na mamia ya wakazi wa Jiji la Arusha nje ya Uwanja wa ofisi za Chadema, ambao pia aliwataka kutulia wakati chama hicho kinatafakari uamuzi wa kuchukua. Chaguzi zilizowahi kutenguliwa Mwaka 1996 aliyekuwa mbunge wa Temeke, Ramadhani Ali Kihiyo alivuliwa ubunge baada ya Mahakama kumtia hatiani kwa kosa la kughushi cheti na nafasi yake ilichukuliwa na Augustine Mrema, wakati huo akiwa Mwenyekiti wa Chama cha NCCR- Mageuzi. Vivyo hivyo Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba ilitengua ubunge wa aliyekuwa mbunge wa Biharamulo Magharibi kwa tiketi ya Chama Cha Tanzania Labour (TLP), Phares Kabuye. Kabuye aliyefariki dunia kwa ajali ya gari akiwa njiani kuelekea jijini Dar es Salaam, alivuliwa ubunge baada ya mahakama kuthibitisha kuwa katika mchakato wa uchaguzi mwaka 2005, alimdhalilisha mgombea mwenzake, Anatoly Choya. Desemba 28, 2007 Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, kupitia kwa Jaji Josephat Mchome ilitengua matokeo ya aliyekuwa mbunge wa Mwibara Charles Kajege kutokana na kutiwa hatia kwa rushwa. Kesi ya kupinga matokeo ya hayo ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea wa jimbo hilo kupitia TLP, Mtamwega Mgaywa, (TLP) aliyeshindwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2005. Hata hivyo, Septemba 25, 2009, Mahakama ya Rufaa chini ya majaji watatu, wakiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania wakati huo, Agustino Ramadhani, January Msofe na Jaji Mbaruku, walimrejeshea Kajege ubunge kutokana na rufaa aliyokata dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu. Habari hii imeandaliwa na Mussa Juma, Arusha, Peter Saramba, Moses Mashalla |
CHANZO CHA HABARI NI GAZETI LA MWANANCHI
NA CHIWAMBO AUSI R.
Karbu siku mzima Arusha na Tanzania kwa ujumla siku tatu zilizopita vichwa vya watu viligonga mwamba kuhusiana na kitendo cha mahakama kubatilisha ubunge wa Mh. Godbless Lema. Tukumbuke kwamba katika nchi yetu ni ya demokrasia. Na ikumbukwe kuwa katika nchi ya Tanzania kuna mihimili mikuu mitatu ambayo ni Serikali, mahakama na bunge. Hivyo basi hukumu ya mahakama haiwezi kuingiliwa na muhimili mungine. Hivyo ule usema wa lema kuwa zilikuwa ni njama za serikali ikuru ya Tanzania ilikanusha maneno yake kama inavyoonekana hapa chini katika barua iliyoandaliwa na ikuru;
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI |
Katika mahojiano yake leo, Alhamisi, Aprili 5, 2012, na Redio One, ikiwa ni kauli yake ya kwanza baada ya Mahakama Kuu ya Arusha kutangaza kumvua ubunge, aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Bwana Godbless Lema, amedai kwa jazba sana kuwa hukumu ya Mheshimiwa Jaji Gabriel Rwakibalira imetokana na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Ikulu.
Kauli hii ya Bwana Lema ni upuuzi. Siyo Mheshimiwa Rais Kikwete wala Ikulu imeingilia kati kesi yake kwa namna yoyote ile, iwe ni kwa kupiga simu ama kuzungumza na Mheshimiwa Jaji Rwakibalira.
Kwa hakika, haijapata kutokea Mheshimiwa Kikwete, tokea alipoingia madarakani, Desemba 21, 2005, akaingilia, kwa namna yoyote ile, mwenendo wa kesi yoyote ile katika Mahakama yoyote na ya ngazi yoyote katika Tanzania. Na wala hakusudii kufanya hivyo wakati wote wa muda wake uliobakia wa uongozi. Siyo kazi ya Rais kutoa hukumu ama kuelekeza namna ya kutoa hukumu katika kesi zilizoko Mahakamani. Rais hana madaraka wala mamlaka hayo.
Aidha, kauli ya Bwana Lema ni ukosefu mkubwa wa adabu na heshima kwa Mahakama ambao ni Muhimili Huru usioingiliwa na Serikali ama na Muhimili mwingine katika maamuzi yake. Bwana Lema amekuwa kiongozi kwa muda sasa, hivyo ni lazima atambue jambo hili kubwa na muhimu katika mfumo mzima wa utawala wa nchi yetu.
Ni jambo lisilokuwa na mshiko wala tija, na kwa kweli ni bahati mbaya, kwamba Bwana Lema anajaribu kuingiza mambo yasiyohusika katika jambo la dhahiri kabisa kuwa ni la kisheria ambalo msingi ni hoja na maelezo mahakamani.
Bwana Lema asitafute visingizio kwa yaliyomfika kwa sababu hakuna mtu mwingine wa kumbebea msalaba huu. Badala ya kutafuta mchawi asiyekuwepo, ni vyema Bwana Lema angekaa chini na kuangalia ni sababu zipi za kisheria zilizomfanya ashindwe na kama ameridhika kuwa hakutendewa haki akate rufani kwa mujibu wa sheria na taratibu. Tunaomba wananchi wampuuze. Ameshindwa kesi kwa makosa yake aliyofanya hana mtu wa kumlaumu bali ajilaumu mwenyewe.
Mwisho.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
05 Aprili, 2012
No comments:
Post a Comment