Saturday, September 21, 2013

Mbeya City Timu Inayong'aa waambiwa Karibu Dar es Salaam


 

UKIWA unapita Barabara ya Morogoro, labda unatoka Arusha, Morogoro, Iringa au Mbeya, ukishaumaliza Mkoa wa Pwani, utakutana na bango kubwa barabarani limeandikwa ‘Karibu Dar es Salaam’.

 Kama hiyo haitoshi utakutana na mabango mengine madogo madogo yakisomeka “Sasa umeingia Dar es Salaam’.
Baada ya Mbeya City kuwa vidume katika Mkoa wa Mbeya na hata kuikomalia Yanga, sasa si vibaya kama tukiikaribisha timu hiyo jijini Dar es Salaam kwa kusema “Karibu Dar es Salaam’.

Mbeya City wameingia Dar es Salaam kwa mara ya kwanza tangu waanze Ligi Kuu Bara.
Kila kona ya Dar es Salaam na Tanzania wanaizungumzia mechi yao dhidi ya Simba leo Jumamosi itakayopigwa Uwanja wa Taifa.

Licha ya kuwa imeshacheza mechi nne za awali, mashabiki wanaamini kuwa wikiendi hii ndiyo Mbeya City wanaanza ligi kwa kucheza mechi ya kwanza ngumu zaidi nje ya mkoa wake na ndani ya Dar es Salaam tena dhidi ya timu ngumu ya Simba.
Mbeya City ilishangaza wengi kwa kutoka sare ya bao 1-1 na mabingwa watetezi Yanga kwenye Uwanja wa Sokoine, wikiendi iliyopita mjini Mbeya kabla ya kulazimisha suluhu dhidi ya Mtibwa mjini Morogoro Jumatano wiki hii.

Mambo hayo yameongeza mvuto na hamasa kwa mashabiki kwenye mechi dhidi ya Simba, ambayo imebatizwa jina la ‘Karibu Dar es Salaam’.
Mbeya City iliingia Mkoa wa Pwani juzi Alhamisi na kupiga kambi ya muda kabla ya jana Ijumaa mashushushu wake kuanza kutua Dar es Salaam na baadaye wakafuatiwa na timu yenyewe.

Kocha Juma Mwambusi amesisitiza kuwa mchezo huo utakuwa mgumu lakini amewatengeneza kisaikolojia wachezaji wake kukabiliana na presha ndani na nje ya uwanja na wanaamini watapata matokeo mazuri.

Straika msomi na hatari wa Mbeya City aliyemfunga Ally Mustapha ‘Barthez’, Mwagane Yeya amepania kumtungua, kipa wa Simba, Abel Dhaira na kuandika historia katika Ligi Kuu Bara. Kiungo wa Mbeya City, Steven Mazanda amesema lazima wawafanye kitu mbaya Wekundu hao wa Msimbazi.

Mbali na tambo hizo za wachezaji, mashabiki wa Mbeya City kutoka Mbeya, wamesema watafurika kwa wingi Uwanja wa Taifa kuishangilia timu yao.
Yeya, ambaye ni mwalimu wa Shule ya Sekondari Iduda Uyole, aliliambia Mwanaspoti kuwa: “Mbeya City ni vijana wa kazi, kwetu matokeo ni jambo la mwisho. Lakini malengo yangu ni kuhakikisha napigana, kama niliweza kumfunga, Barthez hata Dhaira (Abel) atafungika tu.”

Straika wa Simba, Tambwe Amisi amesisitiza kuwa ameshazitambua klabu za Tanzania na sasa inamuwia rahisi kukabiliana na mabeki.
Mchezaji huyo amesisitiza kuwa haijui Mbeya City lakini anaamini hakuna timu ambayo haifungiki huku kocha wake msaidizi, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ akisema; “Simba imekamilika, vijana wako fiti sana na ni vipigo tu, hatuangalii jina la timu wala ushabiki sisi tunataka pointi tu.”

HOFU YA KIPIGO
Wachezaji wa Mbeya City wamekuwa na hofu kubwa huenda mashabiki wa Yanga wakawafanyizia kulipa kisasi cha basi lao kuvunjwa kioo wikiendi iliyopita katika Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Lakini hofu yao nyingine ni kucheza kwa mara ya kwanza kwenye Uwanja wa Taifa, ambao una uwezo wa kubeba mashabiki 60,000 tena na timu ambayo imeshinda mabao 6-0, Jumatano.

JEZI ZA MBEYA CITY
Kwa wauzaji wa jezi ni kwamba, jezi za Mbeya City ni dili kubwa jijini Mbeya na watu wanazishambulia kuliko za Simba na Yanga. Mbeya City klabu mpya, imejizolea wapenzi wengi wa soka na robo tatu ya watu wa Mbeya wanaishabikia klabu hiyo mpya ya Ligi Kuu Bara.

Mwanaspoti ilipita katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Mbeya na kujionea uuzwaji wake. Mmiliki wa duka la vifaa la Mbaspo, Salum Haroun alisema: “Jezi za Mbeya City hapa ni dili kubwa. Hapa dukani kwangu zimeisha na watu wanaziulizia sana, ukileta tu hazikai.”

Naye mchuuzi wa barabarani, Jastine Kisongi alisema: “Asikwambie mtu, kwa sasa jezi za Mbeya City ndiyo zina dili hapa Mbeya, ukiwa nazo una uhakika wa kuuza tofauti na hizi za Simba na Yanga.”

MECHI ZA LEO JUMAMOSI
Mgambo vs Rhino
Prisons vs Mtibwa
Kagera vs Ashanti
Simba vs Mbeya City
Chanzo: Mwanaspoti

No comments: