Watu wenye silaha wavamia jengo la
maduka mji mkuu wa Kenya Nairobi (21.09.2013) na kuuwa takriban watu 20 na
kujeruhi wengine zaidi ya 50 kwa kile serikali inachosema linaweza kuwa
shambulio la kigaidi.
Wafanya manunuzi walikimbia jengo la
Westgate. (21.09.2013).
Watu wengine wengi walikimbilia
barabarani, madukani na sinema kusalimisha maisha yao.Kundi la wanamgambo wa
Somalia la Al Shabaab lilikuwa limetishia kushambulia jengo hilo la maduka la
Westgate ambalo ni mashuhuri kwa jumuiya ya wataalamu wa kigeni mjini
humo.Lakini hakuna kundi lililodai mara moja kuhusika na shambulio hilo na Al
Shabaab imekataa kuzungumzia shambulio hilo.
Helikopta za polisi zilikuwa
zikizunguka juu ya anga ya eneo la jengo hilo
wakati polisi wakisikika wakipiga makelele wakitaka watu watoke nje ya jengo hilo na huku watu wengi waliokuwa wakifanya manunuzi
wakilikimbia jengo hilo.Moshi ulikuwa ukifuka kwenye mlango wa jengo hilo na watu walioshuhudia tukio hilo wamesema walisikia miripuko ya
maguruneti.
Wengine wamesema wamewaona watu
watano wenye silaha wakilivamia jengo hilo
la maduka la Westgate na kwamba linaonekana kuwa ni shambulio na sio wizi wa
kutumia silaha.
Milio ya risasi ilikuwa ikisikika
kutoka hapa na pale ikiwa ni saa mbili baada ya mashambulio ya risasi kuanza
wakati polisi ikilipekuwa jengo hilo
wakiwasaka washambuliaji kutoka duka moja hadi jengine.
Watu wanashikiliwa mateka
Baadhi ya vituo vya televisheni
nchini humo vimeripoti kwamba kulikuwa na watu waliokuwa wameshikiliwa mateka
lakini hakuna uthibitisho rasmi kutoka serikalini.
Yukeh Mannaseh ambaye alikuwa ghorofa
ya juu ya jengo hilo wakati mashambulizi hayo ya
risasi yalipoanza amekaririwa akisema "Hawaonekani kama majambazi,hilo sio tukio la
wizi". Ameendelea kusema kwamba "Inaonekana kama ni shambulio.Walinzi
waliowaona wamesema walikuwa wakifyatuwa risasi ovyo."
Shahidi mwengine aliyejitambulisha
kwa jina la Taha amesema amesikia milio ya breki za gari iliofuatiwa muda mfupi
baadae na mripuko na milio ya risasi katika ghorofa ya chini ya jengo hilo.Mtu
mwengine aliyenusurika katika shambulio hilo
amesema amepigwa risasi na mtu mwenye sura ya Kisomali.
Baadhi ya watu waliokuwa wakifanya
manunuzi kwenye jengo hilo walikimbilia ngazini
na kwenye lifti na kujicha kwenye ukumbi wa sinema wa jengo hilo
wakati wengine polisi iliwagunduwa wakiwa wamejificha chooni kwenye ghorofa ya
kwanza ya jengo hilo.
Takriban watu 24 waliojeruhiwa
walitolewa nje kwa machela na vigari vya kufanyia manunuzi.Wengi wa wahanga
walikuwa na majeraha mengi madogo madogo waliyoyapata kutokana na vitu
vilivyorushwa kutokana na mripuko.Wengine walitoka nje wakitembea wenyewe kwa
miguu huko nguo zao zilizorowa damu zikifunika majeraha yao.
Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya
limeliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba takriban watu 15
wameuwawa na kuna uwezekano wengine waliouwawa bado wangaliko ndani ya jengo
hilo.Katibu Mkuu wa Chama cha Msalaba Mwekundu nchini Kenya Abbas Gullet
amesema idadi ya maafa na majeruhi ni kubwa na ile waliyokuwa nayo ni ya wale
walioko nje. Gullet alitowa kauli wakati milio ya risasi ilipokuwa ikiendelea
kurindima ndani ya jengo hilo.
Kuna maafa ndani ya jengo
Kenya imekuwa ikilaumu kundi la al Shabaab
na wafuasi wao kwa mashambulio kadhaa ya risasi, mabomu na maguruneti dhidi ya
makanisa na vikosi vya usalama tokea jeshi la Kenya
lilipoingia Somalia
kusaidia kupambana na wanamgambo wenye mafungamano na kundi la Al Qaeda miaka
miwili iliopita.
Al Shabaab huko nyuma ilitishia
kushambulia majengo ya ghorofa refu mjini Nairobi
na maeneo ya starehe na burudani vikiwemo vilabu vya usiku kucha na mahoteli
ambayo hupendelewa na watu wa mataifa ya magharibi walioko katika mji mkuu huo.
Lakini hadi sasa wameshindwa kufanya mashambulizi ya aina hiyo.
Mwanajeshi mmoja wa zamani wa
Uingereza aliyekuweko katika eneo hilo
amesema yeye mwenyewe binafsi aliyapapasa macho ya watu wanne na walikuwa
tayari wamekufa akiwemo mtoto mmoja.
Amesema kuna mauaji makubwa kwenye
jengo hilo.
Mwanamgambo mmoja wa jeshi la
serikali alipoulizwa iwapo hilo
lilikuwa ni tukio la wizi amejibu "Hapana huo ni ugaidi".Hata hivyo
hakuna taarifa rasmi kutoka kwa polisi kuhusiana na dhamira ya washambuliaji
hao.
Polisi imelizingira jengo na barabara
zilioko karibu na jengo hilo lilioko kwenye
kitongoji cha Westlands katikati ya mji wa Nairobi.Wizara ya mambo ya ndani
imesema huenda hilo ni tukio la kigaidi na
tayari jeshi la Kenya
limefika katika eneo la mkasa kushirikiana na polisi kudhibiti hali hiyo.
Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters
Mhariri:Caro Robi
Chanzo: DW/De/Kiswahil