Tuesday, April 8, 2014

DK. SLAA: UPINZANI HATUNA LENGO LA KUVUNJA MUUNGANO

Na Hudugu Ng'amilo
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia (Chadema), Dk. Willibroad Slaa, amewataka Watanzania kutambua kuwa hakuna chama cha upinzani ambacho kina lengo la kuvunja Muungano bali yanayoelezwa ni njama ya kudhoofisha msimamo wa kuwapo kwa serikali tatu.

Alitoa kauli hiyo jana katika viwanja vya Tangamano, alipokuwa akiwahutubia wakazi wa jiji la Tanga, baada ya kuongoza timu ya viongozi wa juu wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) mjini hapa na kuwataka wakazi wa jiji hilo kukataa hadaa zinazofanywa kwa lengo la kukanyaga rasimu ya katiba, ambayo waliitolea maoni yao.

Alisema kilichofanywa na Rais Jakaya Kikwete, wakati akilihutubia Bunge Maalumu la Katiba kuiponda rasimu ya katiba ni kumdhalilisha aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, ambaye ni kiongozi mwenye heshima Tanzania na nje ya nchi na kwamba, Ukawa itazunguka nchini kote kumtetea.

Dk. Slaa ambaye ni Mwenyekiti wa Ukawa nje ya Bunge hilo, alisema Rais Kikwete anawahadaa wananchi anaposema wanaotaka serikali tatu wana lengo la kuvunja Muungano na kusisitiza kuwa hakuna chama chochote cha upinzania, ambacho kinataka Muungano uvunjike.

"Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na wananchi wote wa Tanzania Bara na hata visiwani, hakuna anayetaka Muungano uvunjike, bali kinachofanywa na CCM ni kuwachonganisha kwa wananchi ili waonekane ni maadui wa Muungano," alisema Dk. Slaa.

Alisema inasikitisha kuona kuwa kuna baadhi ya wajumbe kutoka Zanzibar ndani ya Bunge hilo wakidanganywa kuahidiwa kupewa fedha za kuwasomesha ili waunge mkono msimamo wa kupiga kura ya serikali mbili jambo ambalo ni kinyume cha malengo ya uwakilishi wao kwa Watanzania.

"Chini ya Umoja wao wa Ukawa wanachofanya ni kutetea maoni ya wananchi yaliyotolewa kwenye Tume ya Katiba kwa kuwa Tanzania ni nchi ya wote na hakuna, ambaye akifa atazikwa nje ya nchi hii. Hivyo, ni lazima kutetea maslahi ya wananchi," alisema Dk. Slaa.

KAIMU KATIBU MKUU WA CUF ANENA
Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Shaweji Mketo, alisema Tume ya Maridhiano ya Zanzibar inayoundwa na viongozi kutoka CCM na CUF ikiongozwa na Nassoro Moyo, imetoa tamko la kumtaka Rais asidhani Watanzania ni watu wa kuhadaiwa, bali watatetea serikali tatu kwa kuwa ina lengo la kuimarisha Muungano uliopo.

CHANZO: NIPASHE.

NEWZZZZ: Jela kwa mapenzi ya jinsia moja Misri

            Wanne wahukumiwa kifungo jela kwa kosa la kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja nchini Misri

Mahakama moja nchini Misri imewahukumu watu wanne kifungo cha hadi miaka minane jela kwa kosa la vitendo vya kufanya mapenzi ya jinsia moja.
Watu hao wanashutumiwa kuhudhuria au kupanga tafrija za vitendo vya ngono, na kuvaa mavazi ya kike na kujipodoa.

Sheria ya Misri haitamki kupiga marufu vitendo vya mapenzi ya jinsia moja, lakini waendesha mashitaka wametumia sheria ya Misri inayokataza mambo fulani kufanyika hadharani kuwahukumu wapenzi wa jinsia moja.
Hukumu hiyo imeshutumiwa na wanaharakati wa haki za binadamu.
Mmoja wa watu hao amehukumiwa na mahakama mjini Cairo, kifungo cha miaka mitatu jela na kazi ngumu.

Kikundi cha kutetea haki za binadamu chenye makao yake nchini Marekani, Human Rights First , kimesema hukumu hizo zinasikitisha na kukatisha tamaa.
"Misri ni taifa linalobadilika katika eneo la nchi za Kiarabu; kinachotokea Misri kinaweka hali ya kuenea katika ulimwengu wote wa nchi za Kiarabu," kimesema kikundi hicho katika taarifa yake.

Kikundi hicho kimesema tangu kung'olewa madarakani Rais Mohammed Morsi mwezi Julai 2013 kumekuwa na ongezeko la watu kukamatwa kwa misingi ya jinsia zao.
Hukumu ya sasa inakumbushia kesi ya mwaka 2001 ya watu 52 kushutumiwa kwa vitendo vya mapenzi ya jinsia moja na makosa mengine chini ya sheria ya Misri.
Watu ishirini na watatu walihukumiwa kifungo cha kufikia miaka mitano jela pamoja na kazi ngumu, hukumu ambayo ilishutumiwa kimataifa.

Kikundi kimoja cha kutetea haki za binadamu nchini Misri kimesema adhabu kali zilizotolewa kwa watu hao Jumatatu ni sehemu ya msako unaoendelea dhidi ya uhuru binafsi.

Chanzo: BBC Swahili

Zaidi ya watu elfu nne wakamatwa Kenya

                 Watu waliokamatwa katika msako mjini Nairobi wakiingizwa uwanja wa mpira wa Kasarani

Serikali ya Kenya imesema kwa sasa inawashikilia zaidi ya watu elfu nne kufuatia operesheni usalama nchini humo.
Msako huo wa kamatakamata ulianza baada ya mashambulio ya magruneti wiki iliyopita katika eneo la Eastleigh jijini Nairobi, ambalo wakaazi wake wengi ni wa jamii ya Kisomali.

Wengi wa watuhumiwa ni Wasomali.
Wengi wao wanashikiliwa kwa siku tatu katika uwanja wa mpira wa Kasarani jijini Nairobi. Umoja wa Mataifa, makundi ya kutetea haki na ndugu wa watu waliokamatwa wamesema wamenyimwa nafasi ya kukutana na watuhumiwa hao.
Waziri wa mambo ya Ndani wa Kenya, Joseph Ole Lenku, amesema wale ambao hawana vitambulisho kuhusu ukaazi au uraia wao wa Kenya, watafikishwa mahakamani na huenda wakarejeshwa Somalia.

Chanzo: BBC Swahili

Msako wa wageni Kenya waendelea


Maafisa wa Polisi nchini Kenya wanasema wamekamata zaidi ya watu elfu tatu katika msako dhidi ya wageni nchini humo .
Msako huo ulianza Ijumaa, baada ya mashambulizi ya gurunade wiki iliyopita katika eneo la Eastleigh linalokaliwa zaidi na wasomali katika mji mkuu Nairobi.
Wengi wa waliokamatwa ni wasomali .

Inspekta mkuu wa polisi , David Kimaiyo, amesema kuwa watu 450 bado korokoroni asili mia kubwa yao ikiwa katika uwanja wa michezo wa Kasarani huku waliosalia wakiruhusiwa kwenda zao baada ya kuchunguzwa na maafisa
wa usalama na wale wa uhamiaji kubaini uhalali wao .

Umoja wa Mataifa, makundi ya kutetea haki za binadamu na jamaa wa watu hao wanasema hawajapewa ruhusa ya kuwaona wapendwa wao.
Waziri wa mambo ya ndani wa Kenya Joseph Ole Lenku, anasema wale ambao hawana vibali vya kuishi nchini watachukulia hatua zaidi.

Sitini na tisa wamepelekwa mahakamani kwa madai ya kuwepo nchini Kenya bila idhini au kumiliki stakabadhi gushi.
Mwandishi wetu Robert Kiptoo ambaye amezuru mtaa huo wa Eastleigh ametueleza kuwa msako wa polisi dhidi ya wahamiaji haramu na washukiwa wa ugaidi bado unaendelea .

Msemaji wa polisi nchini Kenya Masoud Mwinyi amekanusha madai kuwa polisi wanalenga jamii moja ama watu wa dini moja.
Mashirika ya kijamii na yale ya kutetea haki za kibinadamu yanalalamika kuwa yamenyimwa fursa ya kuwatembelewa washukiwa hao waliokamatwa.
Miongoni mwa waliokamatwa ni raia wa Kenya, Uganda, Sudan, Sudan Kusini ,hata hivyo idadi kubwa inatoka Somalia.

Aidha ripoti zinasema kuwa wageni wengi wamekimbilia miji mingine nchini Kenya kukwepa msako huo wa polisi lakini.
Serikali imetoa onyo kwa Wakenya kutowasaidi watu ambao wanawashuku kuwa wageni.

Serikali ya Kenya imeonya kuwa haitawavulimia wakimbizi mijini ikisema kuwepo kwao mijini kunahujumu usalama wa taifa.

Chanzo: BBC Swahili

Waasi watimuliwa Kharkiv,mashariki ya Ukraine

                                     Vikosi maalum vya Ukraine vikiwatuimua waasi huko Kharkiv
                                    Waandamanaji wanaopigania kujiunga na Urusi mashariki ya Ukraine
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Sergey Lavrov walipokutana Paris Marchi 30 iliyopita

Polisi ya Ukraine imewatimuwa wanamgambo wanaoelemea upande wa Urusi huko Kharkiv, lakini wanamgambo wenzao wanaendelea kuyakalia majengo ya serikali huko Donetsk na Luhansk.

Ukraine ikiungwa mkono na Marekani na nchi za Umoja wa ulaya inaituhumu Urusi kusimamia machafuko katika eneo la mashariki na kuyarejea yale yale yaliyopelekea Moscow kuimeza raasi ya Crimea mapema mwezi uliopita.Kama ilivyotokea Crimea,waandamanaji wameyavamia majengo ya serikali jumapili usiku huko Kharkiv,Donetsk na Luhansk wakishinikiza kura ya maoni iitishwe.

Urusi iliyokusanya wanajeshi wake karibu na mpaka wa Ukraine imewaonya viongozi wepya wa mjini Kiev wasipuuze madai ya majimbo yenye wakaazi wengi wanaozungumza kirusi-kusini mashariki ya Ukraine, kitovu cha viwanda na migodi ya Ukraine.

Waziri wa ndani wa Ukraine Arsene Avakov amesema wanamgambo wanaoelemea upande wa Urusi wametimuliwa Kharkiv katika opereshini ya kupambana na magaidi iliyodumu dakika 18.
Waziri wa ndani Arsene Avakov amewatwika rais Vladimir Putin wa Urusi na rais wa zamani wa Ukraine Viktor Yanukovich jukumu la kukaliwa majengo hayo.

Urusi yalaumiwa kuwa nyuma ya uasi huo
Wanamgambo 70 waliokamatwa wanatuhumiwa na serikali ya Ukraine miongoni mwa mengineyo kuhusika na "harakati haramu za uasi,kuchochea fujo miongoni mwa jamii na kusababisha madhara kwa afya ya binaadam.

Hata hivyo waasi wanaendelea kuyashikilia majengo ya serikali huko Donatsk na Luhansk ambako walivunja jengo la idara ya upelelezi na kunyakuwa silaha.
Hali mashariki ya Ukraine inaangaliwa kwa jicho la wasi wasi na nchi za magharibi,zinazohofia Urusi isije ikaitumia biashara ya gesi kama turufu dhidi ya nchi za Umoja wa ulaya.

Marekani imeionya Urusi isiingilie kichini chini katika mzozo wa mashariki ya Ukraine ambako kwa maoni ya ikulu ya Marekani kuna ishara za kuaminika zinazoonyesha wanamgambo wa Ukraine wanalipwa ili wafanye fujo.

Msemaji wa uikulu ya Marekani Jay Carney anasema:"Ikiwa Urusi itaingia mashariki ya Ukraine naiwe moja kwa moja au kichini chini, hali ya mambo itazidi kuwa mbaya.Tunamtolea wito rais Putin na serikali yake waache kuchochea vurugu nchini Ukraine.Na tunawatahadharisha pia dhidi ya kuingilia kijeshi."

Katibu mkuu wa jumuia ya kujihami ya NATO Anders Fogh Rasmussen nae pia ameionya Urusi akisema itafanya "kosa la kihistoria" ikiamua kuivamia tena Ukraine.

Ishara njema yaanza kuchomoza
Ishara pekee ya kutulia hali ya mambo,waziri Serguei Lavrov amethibitisha mkutano wa pande nne utakaozileta pamoja Urusi,Marekani,Ukraine na umoja wa ulaya huenda ukaitishwa haraka kusaka ufumbuzi wa mzozo wa Ukraine.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP/AP

Mhariri: Josephat Charo

MILIPUKO YAUWA WATU SITA NAIROBI

Milipuko mitatu katika mji mkuu wa Kenya wa Nairobi imesababisha vifo vya watu 6 na karibu darzeni mbili kujeruhiwa jumatatu usiku katika mtaa mkubwa wenye wakazi wengi wa asili ya Kisomali wa Eastleigh.

Mkuu wa polisi wa County ya Nairobi Benson Kibue anasema milipuko hiyo ilitokea takriban saa moja na nusu usiku na kwa karibu wakati mmoja katika migahawa ya Sheraton CafƩ na The New Kwa muzairua Grill.

Kufuatana na mmiliki wa Sheraton CafƩ Bw. Patrick Gakuyu watu walikuwa wanatizama taarifa ya habari ya saa moja kwenye televisheni wakati aliposikia milipuko miwili na umeme kuzimika na kuwa katika kiza. Anasema anadhani ni grunetti mbili zilizorushwa ndani ya mgahawa wake.

Jumapili usiku karibu na mtaa huo mtu anayedhaniwa ni gaidi aliuwawa alipokuwa anatengeneza milipuko yake pamoja na wenzake watatu. Na gruneti moja ilipatikana siku hiyo hiyo ya jumapili katika mji wa pwani wa Lamu ndani ya kanisa moja.
Usalama umeimarishwa katika miji mikuu ya Kenya na hadi hivi sasa haijulikani aliyehusika na mashambulio ya jumatatu.

Chanzo: Mjengwablog

Mhariri Mkuu DW: Rwanda ilikuwa na makovu mazito

                                       Mhariri Mkuu wa DW Alexander Kudascheff .

Rwanda ilikuwa ni nchi yenye makovu mazito. Anasema hivyo Mhariri Mkuu wa DW Alexander Kudascheff ambaye alikuwako Rwanda mwaka 1994 akiwa mwandishi wa kwanza wa DW kurepoti baada ya mauaji ya halaiki nchini humo

Katika mahojiano na Dirke Kƶpp wa DW anazungumzia juu ya fikra zake kuhusu mauaji hayo na dhima ya jumuiya ya kimataifa wakati huo na hivi sasa. Muda mfupi baada ya kutokea kwa mauaji hayo ya halaiki Kudascheff aliripoti kutoka Rwanda kwa ajili ya Deutsche Welle ambapo alizunguka nchini kote kwa kutumia gari na hadi Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wakati huo ikijulikana kama Zaire kuona hali ya wakimbizi.

Wakati huo waandishi wengi wa habari wa kigeni walikuwa hawako Rwanda bali walikuwa wakirepoti juu ya kile kilichokuwa kikitajwa kama balaa la wakimbizi huko Goma. Wale waliokuwa Rwanda utashi wao mkubwa ulikuwa msako wa wauaji wa Kihutu ambao walikuwa wamekimbilia mafichoni.

Akiwa na dereva wake kutoka Uganda wameitembelea nchi nzima na hadi hii leo jambo moja limekuwa na mvuto wa kudumu kwake:kwamba Rwanda ni nchi zuri ajabu na kujuwa kwamba watu wake ni wa kupendeka kweli licha ya kuwa kwenye hali ya kuathirika vibaya.

Umegunduwa kwamba watu nchini humo walikuwa wanapendeka ....jambo ambalo wasafiri wengi wamelizungumzia. Lakini wakati huo huo Wanyarwanda wengi wakati wa mauaji ya halaiki walidiriki kutenda unyama usiosemeka Uliweza kuitafakari vipi hali hiyo?

Yumkini tulikutana na wale waliokuwa wahanga.Kwa vyo vyote vile ni vigumu pia hata kufahamu vipi Wajerumani walithubutu kuwapeleka watu milioni sita ili wakauwawe kwenye vyumba vyenye gesi ya sumu.Nafikiri wakati huo nililiona jambo hilo kama aina fulani ya mripuko wa machafuko na wakati ulipomalizika watu walirudi tena kwenye fahamu zao.

Rwanda ilikuwa ni nchi yenye makovu mazito.Wakati unapozunguka na gari unapishana na mrundiko wa mabufuru na unawasikia watu wakizungumzia juu ya jinsi ndugu zao walivyokufa au kuuwawa.Kila unapokuweko unagunduwa kwamba watu walikuwa wakitaka kuzungumzia juu ya kile kilichowakumba. Ulikuwa ukiona kile kiliomo mawazoni mwao,mchanganyiko wa furaha na aibu kwa kuweza kunusurika halikadhalika hofu juu ya mustakbali wao.Kipi kiko mbele yetu ?
Hata hivyo wakati wa mauaji hayo ya halaiki macho ya ulimwengu yalikuwa hayako kwa Rwanda. Pia kwa kuangalia yaliyopita kama mwandishi habari, mtu inabidi aone aibu kwa kutoweka nadhari kubwa juu ya kile kilichokuwa kinatokea nchini humo wakati huo.Lakini walioko kwenye nafasi za uwajibikaji wakati huo wana sababu ya kuona aibu zaidi:hususan Umoja wa Mataifa ambayo ilishindwa kabisa kuchukuwa hatua.Lakini vivyo hivyo kwa mataifa ya magharibi,Jumuiya ya Kujihami ya NATO na hasa Ubelgiji mkoloni wa zamani wa Rwanda.Ubelgiji ina uhusiano wa muda mrefu na Rwanda na pia walijiuliza wapi tulipokosea?Kwa nini hawakuweza kuyakomesha mauaji hayo ya halaiki au angalau kuyazwiya?

Paul Kagame amekuwa rais wa Rwanda tokea mwaka 200. Amekuwa akijaribu kuleta upatanishi,miongoni mwa mambo mengine kwa kupiga marufuku watu kujitambulisha kwa misingi ya ukabila. Una fikra gani kuhusu mtizamo huo?

Nakubaliana na fikra ya msingi kutofikiria kwa kuzingatia makundi ya kikabila.Kwa njia hii mtu huondokana na mila za kibaguzi. Lakini je hiki ni kitu kinachoweza kuamrishwa kutoka juu kwenda chini?Nchi za Kisoshalisti zimelijaribu jambo hilo mara kwa mara bila ya mafanikio kwa sababu mara tu ujamaa unapokuwa umeondoka matatizo yote ya utaifa huibuka upya.

Ningelichukuwa mtizamo tafauti kwa Paul Kagame.Kwa upande mmoja sera yake za kiuchumi ni za mafanikio makubwa.Kwa upande mwengine yeye ni kiongozi kutoka mojawapo ya makundi ya kikabila na sio rahisi kwa wengine kumkubali. Katika mahojiano niliyofanya na Kagame miaka mitano au sita iliopita alinipa hisia kuwa ni mtu mwenye amani na nafsi yake. Alionekana kuwa ni mtu ambaye yumkini alihisi kuwa yeye pia alikuwa amefanya makosa lakini aliamini kwamba sera zake zilikuwa muhimu na sahihi. Aidha hii iwe ndio hali ilivyo au iwapo makundi mawili ya kikabila yameondokana na tafauti zao ni jambo ambalo yumkini likadhihirika katika kipindi cha baada ya Kagame.

Wakati ilipokabiliwa na mauaji hayo ya halaiki hapo mwaka 1994 Jumuiya ya Kimataifa ilishindwa vibaya sana kuyakabili. Kutokana na kushindwa huko kukaibuka kanuni ya wajibu wa kutowa ulinzi.Kwa kiasi gani Jumuiya ya Kimataifa hivi sasa inatimiza wajibu huo?

Haitimizi wajibu huo. Kibahati sambamba na mauaji hayo ya halaiki tulikuwa na mzozo huko Balkan ambapo tulijiuliza masuali hayo hayo.Tamko mashuhuri la Katibu Mkuu wa zamani wa NATO Manfred Wƶrner kufuatia shambulio la kuvizia lililofanyika kwenye uwanja wa soko huko Sarajevo - "Wakati wa kuchukuwa hatua umefika" imekuja kuzama kwenye mawazo ya watu wengi.

Kiuadilifu nafikiri hakuna chochote cha mjadala hapa.Ilibidi kila kitu kifanyike kuwasaidia watu hao.Pia tulijiuliza wenyewe suala hili kwa kuangalia nyuma historia yetu. Je majeshi ya Muungano yalipaswa kushambulia njia za reli zinazoelekea kwenye kambi ya mateso ya Auschwitz?

Ukiniuliza kama mwandishi habari mwangalizi kwa kutumia busara kutowa maoni ya dhati iwapo nafikiri kuingilia kati kungelisaidia na kuwa na maana kwa kuzingatia kipindi cha muda mrefu au kwa hatua ya kujenga taifa ingelinibidi niseme 'Hapana siamini ingelisaidia'. Unaweza kuingilia kati kwa muda mfupi kujaribu kutuliza hali, kujaribu kuzuwiya mripuko wa volkano wenye maafa.Lakini baada ya hapo inabidi uondoke haraka kadri inavyowezekana ili kwamba wale wanaoishi kwenye volkano hiyo waweze kukabiliana na hali hiyo wao wenyewe.Mwanzoni mambo yalikwenda vizuri Afghanistan na hata kwa wafanya kazi wa misaada lakini baadae katika mwaka 2004 au 2005 hali ilibadilika kabisa.

Kulikuwa na hatua za kuingilia kati zilizoshindwa kabisa kama vile Somalia na nyengine kushindwa kwa kiasi fulani kama vile Bosnia na mahala pengine ambapo matokeo yake bado hayako wazi mfano Kosovo.Hatuwezi kusema mambo yatakuwaje Jamhuri ya Afrika ya Kati au nchini Mali.

Baadae Jumuiya ya Kimataifa ilikuja kuendeleza uchunguzi kuhusu mauaji ya halaiki na kurudisha haki kwa kupitia Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kwa ajili ya Rwanda. Nchini Ujerumani na hata Ufaransa kesi za mauaji ya halaiki zimekuwa zikiendeshwa. Una mawazo gani juu ya majaribio haya yaliochelewa kukabiliana na kile kilichotokea?

Nafikiri ni vyema kwa dunia hii kwamba watu wanaohusika na uhalifu wa ukubwa huo wanakuwa hawana sababu ya kuamini kuwa wanaweza kuachiliwa bila ya kuadhibiwa.Hiyo ndio sababu kwa mfano kwa nini nafikiri kwamba mlinzi wa zamani wa kambi ya mateso ya Auschwitz mwenye umri wa miaka 90 bado anapaswa kushtakiwa.Kwani wakati fulani aliwahi kuwalazimisha hata watoto wadogo wa miaka miwili wakauliwe kwenye vyumba vya gesi ya sumu ........kwa hiyo kwangu mimi umri haujalishi.Kwa hiyo fikra ya kuwepo kwa Mahakama hiyo ya Kimataifa ya Uhalifu kuona kwamba dunia haitomuachilia mtu akwepe kuhukumiwa kwa uhalifu wa aina hiyo ni sahihi.

Aidha mahakama hiyo ni ya mafanikio au la hilo ni suala jengine.Kwa vyovyote vile wengi wa wahalifu hao wako huru na wanakwenda watakako tena chini ya uwezo wa Jumuiya ya Kimataifa kuwatia nguvuni. Wengi hawashtakiwi hadi pale hali zao zinapodoofika. Wengine katu hawakuwahi kabisa kufunguliwa mashtaka.
Mwandishi : Dirke Kƶpp/Mohamed Dahman
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Urusi Yaonywa Isiingilie Mzozo wa Ukraine

                                      Mapigano yamezuka kati ya wabunge wa Ukraine mjini Kiev


Hali inatisha mashariki ya Ukraine ambako wanaharakati wanaoelemea upande wa Urusi wamejitangazia "Jamhuri ya Donetsk". Urusi imeonya dhidi ya hatari ya kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe Ukraine ikiingilia kati.

"Waasi wanaobeba silaha,wanaopigania kujitenga maeneo ya mashariki,walioyavamia majengo ya serikali wataandamwa kuambatana na katiba na sheria na kulinganishwa na magaidi na wahalifu" amesema hayo rais wa mpito Olexandre Turtchinov.
Akihutubia bungeni hii leo rais Turtchinov amesisitiza jeshi halitoshamiri silaha dhidi ya watu wanaoandamana kwa amani katika wakati ambapo wanaharakati wanaoelemea upande wa Urusi wanadhibiti majengo ya serikali maashariki ya nchi hiyo nayo Urusi inaonya dhidi ya hatari ya kuripuka vita vya wenyewe kwa wenyewe.

 Rais Turtchinov amethibitisha silaha na maguruneti yametumiwa dhidi ya vikosi vya wanajeshi waliowekwa kulinda majengo ya serikali katika mji wa Kharkiv na kwamba wanajeshi kadhaa wamejeruhiwa. Ameelezea matumaini yake kuyaona majengo ya setrikali yakikombolewa haraka huko Lougansk na shughuli za tawala kuendelea kama kawaida katika mji wa Donetsk ambako wanaharakati wanaoelemea upande wa Urusi wametangaza "jamhuri yao".

Urusi imeitaka Ukraine iache maandalizi ya kuingilia kijeshi katika maeneo hayo ya mashariki. Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Urusi inahoji watumishi wa shirika la kibinafsi la Marekani wanashiriki katika opereshini hizo.

Jumuia ya Kimataifa itakutana Haraka kuzungumzia Ukraine
Katika wakati ambapo Urusi inaonya dhidi ya hatari ya kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe katika maeneo ya mashariki ya Ukraine,jumuia ya kujihami ya NATO imeitolea wito Moscow iwarejeshe nyuma wanajeshi wake waliokusanywa karibu na mpaka wa nchi hizo mbili.

Wakati huo huo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry amezungumza kwa simu na waziri mwwenzake wa urusi Sergei Lavrov na kumuonya Washington inafuatilizia kwa wasi wasi mkubwa yanayotokea Mashariki ya Ukraine.Waziri Kerry ameitaka Urusi ijitenganishe na wanaopigania kujitenga eneo hilo,wanaofanya fujo na kuchochea mizozo.

Mawaziri hao wawili wamezungumzia umuhimu wa kuitishwa mkutano kati ya Ukraine, Urusi, Marekani na Umoja wa Ulaya ili kumaliza mivutano.

Bendera za Urusi zapepea Mashariki ya Ukraine
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinemeir anasema:"Tunabidi tufanye bidii kuisaidia Ukraine kiuchumi na kisiasa. Juhudi hizo hazitafanikiwa mtengano ukitokea nchini humo.

Yadhihirika kana kwamba hilo ndilo linalotokea;bendera za Urusi zinapepea katika majrengo yote yanayokaliwa na waasi mashariki ya Ukraine.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters
Mhariri: Josephat Charo

UN yalaani mauaji ya maafisa wake

Wawili hao waliuawa katika eneo la Galkayo katika mpaka na Puntland
Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Nicholas Kay, ameshutumu mauaji ya washauri wawili wa Umoja wa Mataifa ambao wamekuwa wakifanyakazi katika kitengo cha Ofisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC).

Washauri hao wawili wa kimataifa walikuwa Galkayo kusaidia jitihada za Ofisi ya UNODC katika eneo hilo wakati walipouawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana katika uwanja wa ndege wa Galkayo, Puntland, Somalia.
Umoja wa Mataifa umesema unawalaani wauaji hao.

"Wafanyakazi wenzetu wa Umoja wa Mataifa walikuwa wakifanyakazi ya kuwasaidia wananchi wa Somalia kufikia ndoto yao ya kuwa na taifa lenye amani na imara. Hakuna uhalali wowote wa kufanyika shambulio hilo.
Natoa wito kwa serikali kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini wahalifu hao na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria bila kuchelewa".Amesema Bwana Kay.

"Natoa salamu zangu za pole kwa familia na marafiki wa watu hao waliouawa.
Umoja wa Mataifa umedhamiria kuendelea na msaada wao wa dhati kwa wananchi wa Somalia ambao wanatoka katika mgogoro uliodumu kwa miongo kadhaa," amesema Mwakilishi huyo Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bwana Kay.
Habari kutoka Mohadishu, Somalia, zinasema kikundi cha wapiganaji wa al-Shabab kimepongeza mauaji hayo na kudai kufurahishwa na taarifa hizo za kuuawa kwa raia wa kigeni katika mji wa Galkayo, katikati mwa Somalia Jumatatu.


"TUnapongeza na kufurahishwa na mauaji ya maafisa wa Umoja wa Mataifa, leo. Mashirika ya Umoja wa Mataifa daima ni maadui wa Waislam na Wasomali na vifo vyao vimelifurahisha kundi la wapiganaji wa Mujahdeen" wamesema.
Walipoulizwa kama wanahusika na mauaji hayo, al-Shabab wamesema kwa sasa hawapingi wala kudai kuhusika na mauaji hayo”

Chanzo: BBC Swahili

Monday, April 7, 2014

KATUNI YA LEO NA Chiwambo's Blog


Wataka waandishi wa aljazeera kuachiwa

Al Jazeera English journalists Peter Greste, Mohamed Fahmy, and Baher Mohamed have been held in jail in Egypt for 100 days.

Mashirika ya vyombo vya habari yamerejelea wito wa kutaka kuachiliwa huru kwa waandishi watatu wa habari wa shirika la al-Jazeera ambao wamekuwa wakishikiliwa kwa siku 100 sasa tangu wakamatwe nchini Misri.

Waandishi hao watatu, akiwemo mwandishi wa habari wa zamani wa BBC, Peter Greste, walifunguliwa mashitaka mwezi Februari, wakituhumiwa kusambaza habari za uongo na kukisaidia kikundi cha ugaidi.

Wamekana mashitaka hayo, ambayo al-Jazeera imeyaita kuwa ni "upuuzi."
Kesi hiyo imechochea shutuma kutoka vyombo vya habari vya kimataifa na makundi ya kutetea haki za binadamu duniani kote.

Waandishi hao watatu ni miongoni mwa watu 20 wanaokabiliwa na mashitaka kama yao. Ni watu wanane tu ambao mpaka sasa wako gerezani, ambapo wengine 12 wamesomewa mashitaka bila kuwepo mahakamani.

Mwandishi wa nne wa al-Jazeera, Abdullah al-Shami, ambaye anafanyia chaneli ya Kiarabu, anashikiliwa tangu mwezi Agosti bila ya kufunguliwa mashitaka.
Bwana al-Shami amekuwa katika mgomo wa kula na mke wake amesema afya yake inazorota.

Source: Al Jazeera

Waasi Libya waridhia mafuta yauzwe


Waasi wakubaliana na serikali ya Libya kuuza mafuta

Makubaliano yameafikiwa kuondoa kizuizi cha kusafirisha mafuta mashariki mwa Libya. Mauzo ya mafuta katika nchi za ngambo nchini humo yaliathirika pakubwa katika kipindi cha miezi minane iliyopita baada ya kufungwa kwa bandari zilizo katika eneo la mashariki linalotawaliwa na makundi ya wanamgambo.

Katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyiwa katika jiji la Beghazi, Waziri wa Maswala ya Haki wa Libya, Salah Al-Maghani, alithibitisha kuondolewa kwa muda kwa vizuizi vya kuuza mafuta. Vituo vya mafuta vya Hureiga na Zuetina vilivyo na uwezo wa kuzalisha mafuta mapipa 200,000 kwa siku hivi sasa vimesimamiwa na Serikali.

Vituo viwili vilivyo vikubwa zaidi nchini humo vya Mashariki mwa nchi vya Ras Lanuf na Sidra vitafunguliwa kwa muda wa majuma machache yajayo, kulingana na Waziri.

Mapatano yaliafikiwa kati ya makundi ya wapiganaji yaliyosababisha kufungwa kwa vituo hivyo na kundi ambalo Serikali ililitaja kama "wapatanishi".
Msemaji wa Waziri Mkuu ameambia BBC kuwa Serikali imekubali kuwalipa mishahara walinzi wa vituo hivyo vya mafuta.

Juhudi za mwezi uliopita za kufikia mapatano ya kuanza kuuza mafuta tena katika vituo hivyo hazikufaulu.
Wale wanaozuia mafuta kuuzwa katika vituo hivyo wamekuwa wakilalamika kuwa sekta ya mafuta nchini Libya inakabiliwa na ufisadi mkubwa, lawama ambayo imekanushwa na maafisa wa Serikali.

Wapiganaji hao pia wamekuwa wakisema kuwa wakaazi wa Mashariki wanahitaji mapato makubwa zaidi kutoka kwa mauzo ya mafuta. Waziri wa Haki sasa anasema kuwa Serikali itachunguza lawama za ufisadi.
Libya imepata hasara ya zaidi ya Dola Bilioni tisa tangu kufungwa kwa vituo hivyo vya mafuta. Eneo la Mashariki ndilo linalozalisha kiwango kikubwa cha mafuta.

Chanzo: BBC Swahili

Miaka 20 baada ya Mauwaji ya halaiki Rwanda


                                                                    Majeneza ya wahanga wa mauwaji
Katika wakati ambapo Rwanda inatafakari miaka 20 baada ya mauwaji ya halaiki, taasisi ya wanasheria ya Ufaransa imefanikiwa kumhukumu mmojawapo wa waandalizi wa mauaji hayo ya halaiki Pascal Simbikangwa.

Kesi ya kwanza ya mnyarwanda aliyekuwa akituhumiwa kuhisika na mauwaji ya halaiki ni hatua muhimu kwa jopo hilo maalum la mjini Paris linaloshughulikia masuala ya aina hiyo na ambalo linaanza kupanua shughuli zake-anasema naibu mwendesha mashtaka mkuu AurƩlia Devos.

Pascal Simbikangwa,myarwanda wa kwanza kuhukumiwa nchini Ufaransa kwa makosa ya kushiriki katika mauwaji ya halaiki ya watu wa kabila la tutsi mnamo mwaka 1994,alihukumiwa kifungo cha miaka 25 jela Marchi 15 iliyopita,na kuipatia jaza ya kwanza taasisi hiyo inayoshughulikia masuala ya mauwaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya ubinaadamumbele ya mahakama ya mjini Paris.

Ikiundwa mapema mwaka 2012,taasisi hiyo imejiwekea lengo la kupambana dhidi ya mitindo ya kutoandamwa kisheria wahalifu wa vita ambao wamekimbilia nchini Ufaransa nchi yenye idadi kubwa ya wahamiaji.

"Ni hatua muhimu" amesema AurƩlia Devos ambae ni mkuu wa taasisi hiyo ya masuala ya sheria."Kesi dhidi ya Pascal Simbikangwa imebainisha kwa mkumbo mmoja kwamba ni halali na ni jambo linalowezekana kumfikisha mahakamani nchini Ufaransa mgeni yoyote,kwa makosa aliyoyafanya katika pembe nyengine ya dunia."

Hata hivyo kesi hiyo ya kwanza sio anzilishi,anahisi mwanasheria huyo na kusisitiza kwamba taasisi yake-mojawapo ya mashirika madhubuti barani Ulaya,yenye majaji watatu,wanasheria wawili na wasaidizi wao na wachunguzi 12 wanaokutana tangu mwezi wa februari katika ofisi yao kuu,wanashughulikia masuala tofauti yanayopindukia yale yanayohusiana na Rwanda.

Shabaha ni kurejesha uhusiano pamoja na Ufaransa
Kesi nyingi-27 kati ya 35 wanazozishughulikia zinawahusu watuhumiwa wa mauwaji ya halaiki ya Rwanda waliohamia Ufaransa."Lakini nijuavyo mie haijawahi kuwa taasisi inaoshughulikia suala la Rwanda tu" amehakikisha AurƩlia Devos.Mashirika kadhaa yamekuwa yakiituhumu taasisi hiyo tangu ilipoanzishwa kuwa chombo kinachoshughulkia kutuliza uhusiano kati ya Paris na Kigali.


                                                            Mafuu ya wahanga wa mauwaji ya halaiki ya Rwanda

Uhusiano mbaya kati ya Ufaransa na Rwanda ulikwenda umbali wa kuvunjwa uhusiano wa kibalozi kati ya nchi hizo mbili mwezi Novemba mwaka 2006.Uamuzi huo ulipitishwa baada ya jaji mmoja wa kifaransa kutangaza waranti wa kukamatwa maafisa tisa wa Rwanda kuhusiana na uchunguzi wa shambulio la April, sita mwaka 1994 lililopelekea kuuwawa rais wa zamani wa kihutu JuvƩnal Habyarimana-chanzo cha kuzuka siku ya pili yake mauaji ya halaiki nchini Rwanda.

Watuhumiwa wengine pia wanaandamwa
Katika wakati ambapo Pascal Simbikangwa amehukumiwa kifungo cha miaka 25 jela,mnyarwanda mwengine Charkes Twagira ametiwa korokoroni baada ya kukutikana na hatia ya kuhusika na mauwaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya ubinaadam.

Wanasheria wake wanatumia wakati mwingi kutathmini hali ya isiasa,kihistoria,kiuchumi na kisaikolojia ya nchi ambako uhalifu umetokea.Na kwa upande wa Rwanda mtu anaweza kusema ni kadhia moja inayowahusu watuhumiwa 27.Anasema.Kadhia nyenginezo ambazo wanasheria wa taasisi hiyo wanazishughulikia ni pamoja na ile ya Iraq, Libya,Tchad,Congo Brazaville,jamhuri ya Afrika kati,Cambodjia na Maroko.


                                 Pascal Simbikangwa ahukumiwa kifungo cha miaka 25 jela nchini Ufaransa

Na kadha nyengine kadhaa zinazohitaji uchunguzi wa awali.Mojawapo ya kadhia hizo inahusu biashara ya zana za ukaguzi iliyofanywa na kampuni ya Ufaransa Amesys kwa utawala wa zamani wa Muammar Gaddafi nchini Libya-kampuni inayotuhumiwa na mashirika yasiyomilikiwa na serikali,kusaidia katika kuwatesa wapinzani wa serikali.

"Hatujaribu kupanua uwanja wa shughuli zetu-zipo tayari,anasisitiza mwanasheria huyo AurƩlia Davos. Uwaja huo umepata nguvu kutokana na kuongezeka vusa vya uhalifu dhidi ya ubinaadam.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Maoni : Mauaji ya halaiki Rwanda - Kushindwa kwa Jumuiya ya Kimataifa

                                     Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili (DW) Andrea Schmidt.

Jambo hilo lisingelipaswa kutokea: Mauaji ya halaiki mbele ya macho ya ulimwengu! Hata watoto wachanga na vikongwe waliuwawa. Wanamgambo waliteketeza hata nyumba za ibada ambapo watu walikuwa wamejihifadhi.

Katika kipindi cha siku 100 serikali ya wakati huo na wanamgambo wake waliwauwa zaidi ya watu 800,000. Hususan walioandamwa walikuwa ni watu wa jamii ya Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani ambao walikuwa wamejaribu kuwasaidia majirani na marafiki zao.

Lakini suala ni kwa nini hakuna mtu aliechukuwa hatua licha ya kutolewa kwa tahadhari na mapema?Takriban miezi mitatu kabla ya kuzuka kwa mauaji hayo,mkuu wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa(UNAMIR) nchini Rwanda Romeo Dallaire alituma ujumbe kwa wakuu wake walioko New York ambapo alionya katika kile kinachojulikana kama "Fax ya Mauaji ya Halaiki " yenye kufafanuwa mipango ambapo kwayo wanamgambo wakiwa kwenye makundi ya kuanzia watu 40 wanaweza kuuwa zaidi ya watu 1,000 katika kipindi kisichozidi dakika 20.

Wakati mauaji hayo yalipokuwa yamepamba moto,Dallaire alituma tena ujumbe wa dharura kwa Umoja wa Mataifa wa kuisihi itume wanajeshi zaidi wa kulinda amani na kuwapa mamlaka thabiti ya kulinda wananchi.Badala yake Umoja wa Mataifa ukaanza hata kupunguza vikosi vyake vilioko nchini humo yumkini kutokana na hofu ya kuja kukabiliana na balaa la kushindwa kama lile lililowakuta wakati ilipoingilia kati nchini Somalia na wakayafumbia macho mauaji hayo na kukataa kukiri juu ya ouvu huo uliokuwa ukitokea.

Wakati huo huo Ufaransa iliendelea kuipelekea silaha serikali ya nchi hiyo hadi mwezi wa Juni yaani badala ya kuchukuwa hatua ya kuingilia kati kijeshi kwa "Operesheni ya Turquoise(Takwaz)" ili kuwalinda raia,jeshi la Ufaransa liliwachilia wanamgambo waliohusika na mauaji ya halaiki kuondoka na silaha zao na kukimbilia Congo iliokuwa ikijulikana kama Zaire wakati huo.

Wajibu mpya wa kulinda wananchi
Hususan Umoja wa Mataifa ulikuwa umefedheheka kwa kushindwa kutimiza wajibu wake.Lakini wamejifunza nini kutokana na hilo?Kutokana na kuboronga huko Rwanda,Umoja wa Mataifa na juhudi zake za Kuwajibika kutowa Ulinzi hapo mwaka 2005 umebuni mfumo mpya ambapo mataifa yanawajibishwa kulinda wananchi wake dhidi ya ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu, mauaji ya halaiki na kuangamiza jamii.Iwapo nchi inashindwa kutimiza wajibu huo wa kutowa ulinzi jumuiya ya kimataifa inaweza kutimiza wajibu huo na kuingilia kati kijeshi.

Lakini msimamo wa uadilifu pekee hautoshi.Umoja wa Mataifa haukuzuwiya mauaji ya raia wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sri Lanka .Hata hivi sasa kuna maeneo ya vita ambayo ni changamoto kwa jumuiya ya kimataifa kuthibitisha kile ilichojifunza kutokana na Rwanda.Kwa mfano maangamizi ya jamii yanayofanyika Jamhuri ya Afrika ya Kati au hali ya machafuko nchini Sudan Kusini.

Lakini kwa nini shughuli za kulinda amani za Umoja wa Mataifa bado zinakosa mamlaka thabiti ya kutekeleza majukumu yake?Changamoto ni pamoja na umuhimu wa kuzingatia tahadhari zinazotolewa na mapema kama vile matumizi ya nguvu kupita kiasi.Kuweka viashiria kabla ya hali kuwa mbaya,wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wawe wamepatiwa mafunzo vizuri, kupatiwa silaha na kuwa tayari kukabiliana na hali hiyo kwa ufanisi na uwajibikaji.

Congo ni mfano
Kikosi cha Umoja wa Mataifa kilioko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kinaweza kutumiwa kama mfano wa mambo yote kwa matatizo na njia zinazoweza kutumika kwa ufumbuzi katika shughuli za kulinda amani.Kwa miaka mingi kikosi hicho kimekuwa kikishutumiwa kwa ukosefu wake wa ufanisi na moja kwa moja kuchukiwa na wananchi wa nchi hiyo.Kutokana na kutokuwa na mamlaka thabiti ya kutekeleza majukumu yake mara nyingi hujifanya hawaoni wakati watu wanapouwawa na wanawake kubakwa. Hata hivyo hapo mwaka 2013 kutokana na kuwepo kwa kikosi kipya cha kuingilia kati haraka cha wanajeshi kutoka Afrika chenye mamlaka mpya hali hiyo imebadilika.

Hususan shughuli za kulinda amani za Umoja wa Mataifa hazipaswi kushindwa kutokana na ukosefu wa fedha na rasilmali.Jumuiya ya Kimataifa lazima ijitolee kwa kila hali kutowa msaada kwa haraka na kuwa na ufanisi hususan kulinda haki za binaadamu katika nchi husika.Matumizi mabaya kutokana na sababu za kisiasa au za kiuchumi lazima yaepukwe.

Jumuiya ya Kimataifa hapo mwaka 1994 ilitenda kosa kubwa sana.Lazima isifumbie macho tena uhalifu wa aina hiyo.Mauaji ya halaiki yamegharimu maisha ya watu 800,000 nchini Rwanda. Watu wengine milioni tatu wameuwawa katika vita vya Congo ikiwa ni matokeo ya mauaji hayo ya halaiki.Jambo hilo pia halipaswi kusahauliwa.
Mwandishi: Andrea Schmidt/Mohamed Dahman

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

NEWZZZ: Hatimaye Nigeria yaipita Afrika Kusini kiuchumi

Nigeria imekuwa taifa kubwa zaidi kiuchumi barani Afrika, na kuipiku Afrika Kusini, baada ya takwimu mpya kupandisha pato la jumla la ndani la taifa hilo hadi kufikia dola za marekani zaidi ya bilioni 500.

Wakala wa takwimu wa Nigeria ulitangaza pato jipya la taifa hilo linaloongoza kwa uzalishaji mafuta barani Afrika kuwa ni dola za Marekani bilioni 509.9, karibu mara mbili ya kiwango kilichokuwa kinakadiriwa kabla ya kukokotolewa upya. Thamani hii mpya ya pato la ndani la Nigeria inajumlisha sekta kama vile mawasiliano, habari na teknolojia, muziki, biashara za mtandaoni na fillamu za Nollywood, ambazo hazikuwepo wakati mahesabu ya mwisho yalipofanyika mwaka 1990.


Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan.
Wakati huo kulikuwepo na simu za mezani 300,000. Hivi sasa Nigeria ina watumiaji wa simu za mkononi milioni 100. Takwimu hizo mpya zinazingatia ukuaji katika sekta za kilimo na utalii, ambazo zimekuwa kwa kiasi kikubwa tangu nchi hiyo iliporejea kwenye mkondo wa demokrasia mwaka 1999, na kukomesha miongozo kadhaa ya utawala wa kidikiteta.

Afrika Kusini yaachwa mbali
Nigeria sasa imeipiku Afrika Kusini ambayo pato lake la jumla la ndani la dola za Marekani bilioni 353 ndiyo lilikuwa linahesabiwa kuwa kubwa zaidi barani, na ambayo ndiyo nchi pekee ya Kiafrika mwanachama wa kundi la mataifa 20 yaliyoendelea kiuchumi G20.

Meneja wa uwekezaji Kevin Daly kutoka shirika la usimamizi wa mali la Aberdeen la nchini Uingereza, na ambalo linawekeza Nigeria, alisema mafanikio ya Nigeria ni ukumbusho kuwa Afrika inasonga mbele licha ya changamoto inazokabiliana nazo kwa sasa. Daly alibainisha kuwa ni bilionea wa Kinigeria Aliko Dangote, ambaye anajenga kiwanda kikubwa zaidi binfasi cha kusafisha mafuta barani Afrika.

Wawekezaji watavutiwa na ukweli kwamba, wakati mafuta yanaendelea kuwa chanzo kikuu cha mapato ya serikali, kwa asilimia 80, uzalishaji wa mafuta unapungua wakati sekta za kilimo na huduma za mawasiliano zinazidi kushamiri.

Nigeria imekuwa mpokeaji mkubwa zaidi wa uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni barani Afrika licha ya matatizo mengi yanayoikabili, kuanzia rushwa iliyokithiri na wizi wa mafuta vinavyoigharimu nchi karibu dola milioni 20 kila siku, hadi kwenye uasi wa kundi la Kiislamu kaskazini-mashariki, ambao umewaua watu zaidi ya 1,200 mwaka huu peke yake, na umeme usiyo wa uhakika, unaozifanya biashara zitegemee majenereta.

Waziri wa fedha Ngozi Ikonjo-Iweala aliuwambia mkutano wa waandishi wa habari jana kuwa takwimu hizo mpya zinaifanya Nigeria kuwa nchi ya 26 kwa uchumi mkubwa duniani, na zinapandisha pato lake la mtu mmoja mmoja hadi kufikia dola za Marekani 2,688, na kushika nafasi ya 121 duniani kutoka 135.

Maskini hawanufaiki
Hata hivyo kiwango hicho bado ni kidogo ikilinganishwa na Afrika kusini ambayo pato lake la mtu mmoja mmoja ni dola za Marekani 7,336 kwa wakaazi wake milioni 48. Mchambuzi wa masuala ya fedha Bismark Rewane aliyaita marekebisho hayo kuwa ni majivuno tu, na kwamba maisha ya raia hayataboreka kesho kwa sababu ya tangazo hilo.
Licha ya mafanikio ya kiuchumi, Nigeria bado inakabiliwa na changamoto kubwa zikiwemo miundombinu duni

Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa kiwango cha ukosefu wa ajira nchini Nigeria kilipanda kutoka asilimia 12.7 mwaka 2007 hadi asilimia 23.9 mwaka 2011, wakati benki ya dunia ikisema ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana ni asilimia 38, lakini wachambuzi wanasema kinakaribia asilimia 80 katika maeneo mengi ya nchi.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/ape,rtre,afpe

Mhariri: Hamidou Oummilkheir.