Friday, September 20, 2013

TBS yadai ‘oil’ ya magari haifai



Dar es Salaam. Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Agness Mneney amebainisha kuwa asilimia 90 ya mafuta ya kulainisha mitambo (oil) ya magari yamechakachuliwa au kutengenezwa chini ya kiwango, hivyo kuhatarisha usalama wa magari hayo na watumiaji kwa jumla.

Hayo yameelezwa jana na Naibu Mkurugenzi huyo alipokuwa akifungua mkutano wa watengenezaji na wafanyabiashara wa mafuta hayo, uliofanyika kwenye ofisi za TBS makao makuu Dar es Salaam.

Mneney alisema, tatizo hilo limebainika kutokana na utafiti ulifanywa na TBS katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, wakizingatia vigezo vya msingi vinavyopendekezwa na Chuo cha Utafiti cha Petroli cha Amerika (API).

“Hata hivyo utekelezaji wa kiwango ndiyo changamoto inayotukabili. Sisi wote ni mashahidi wa mafuta yaliyopo chini ya kiwango katika soko hapa nchini. Katika utafiti ilibainika bayana kuwa kuna mahitaji yanayopaswa kuainishwa katika utendaji,” alisema Mneney.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Starpeco, Grantian Nshekanabo aliitaka TBS ichukue hatua za kiutendaji ili kuhakikisha mafuta yanayoingizwa sokoni yanakidhi viwango vinavyotakiwa ili kuepusha hasara wanayoipata watumiaji hasa wamiliki wa magari.
“TBS ihakikishe kikosi chake kinaondoa mafuta yasiyo na viwango ambayo hununuliwa kutokana na bei kuwa chini na injini za magari kuharibika.”

No comments: