HATIMAYE Msajili wa Vyama vya Siasa,
Jaji Francis Mutungi ameanza kuonyesha makali, baada ya kukipa onyo kali Chama
Cha Mapinduzi (CCM) na kukitaka kuacha mara moja kutumia viongozi wa
kidiplomasia kwenye shughuli za kisiasa.
Hatua ya Jaji Mutungi, imekuja siku
chache baada ya CCM kumtumia Balozi wa China, Dk. Lu Youping katika shughuli
za kisiasa mkoani Shinyanga wiki iliyopita.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya
habari mjini Dar es Salaam
jana, ilisema suala la ushiriki wa raia wa kigeni ikijumuisha wanadiplomasia
katika shughuli za kisiasa nchini, halikubaliki.
Alisema ofisi yake, inaunga mkono kwa
dhati hatua iliyochukuliwa na Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, kukemea jambo hilo.
"Tamko la Serikali limezingatia
sheria na wajibu wa wanadiplomasia, wakati wa uwepo wao hapa nchini, mimi
nikiwa mlezi wa vyama vya siasa, ninakemea kitendo cha CCM kumshirikisha Balozi
wa China
katika shughuli za kisiasa," alisema Jaji Mutungi.
Alisema katika tukio hilo,
CCM kuruhusu raia wa kigeni kutumia jukwaa lake
ni dhahiri limezua hali ya taharuki
kwa wananchi, japo sheria ya vyama vya siasa kwa upande wake iko kimya katika
suala hilo.
"Naviasa vyama vya siasa kwa
ujumla wake, kuzingatia na kufuata sheria na taratibu stahiki katika
utekelezaji wa shughuli zao za kisiasa.
"Napenda kuujulisha umma kwamba,
ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa wakati huu ipo kwenye mchakato wa
marekebisho ya sheria husika ya vyama vya siasa, ambayo imebainika kuwa na
upungufu....lengo ni kukabiliana na changamoto zilizopo likiwemo suala
hili," alisema Msajili, Jaji Mutungi katika taarifa yake aliongeza sasa
hivi ofisi yake inaendelea kukusanya maoni ya wadau katika jitihada za
kufanikisha marekebisho ya sheria hiyo.
Suala la CCM kumshirikisha Balozi wa China katika
masuala ya kisiasa, lilizua mjadala mkubwa hali iliyosababisha CHADEMA kutoa
tamko na kuandika barua ya malalamiko UN wakitaka aondolewe kwa kupoteza sifa
za kuwa balozi, baada ya kuvunja mkataba wa Umoja wa Mataifa wa 1961
unaosimamia nchi na nchi.
CHADEMA waliandika barua nyingine
kwenda Serikali ya China na Tanzania,
wakitaka msimamo na hatua zitakazochukuliwa dhidi ya balozi huyo kuvunja
mkataba huo ibara ya 41(1-3), kinachokataza balozi kujihusisha na siasa katika
Taifa ambalo yuko.
Chadema imesema inalaani kitendo
hicho na itachukua hatua kwenda Umoja wa Mataifa na pia kupata maelezo toka
Serikali ya China kama imemtuma balozi huyo kujihusisha na mambo ya siasa
za ndani za vyama au kuiwakilisha nchi.
Akijibu tuhuma hizo, Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema alichofanya balozi huyo ni
kitendo cha kuungwa mkono, maana alikuwepo kwa nia ya kuangalia maeneo ya
uwekezaji wa zao la Pamba katika Mkoa wa Shinyanga.
Alisema uwekezaji kutoka China,
utasaidia kuondoa tatizo sugu la ajira, kupanda kwa bei ya zao la pamba ambacho
kimekuwa kilio kikubwa cha wakulima pamoja na ujengwaji wa viwanda vya nguo na
kuchuja mafuta.
Hivyo ni vema kumpongeza balozi huyo
na kuunga juhudi za CCM za kuwatafuta wawekezaji wa nje, badala ya kusingizia
uvunjaji wa Mkataba wa Vienna
ili kupata umaarufu wa kisiasa:
chanzo mtanzania
No comments:
Post a Comment