Wenyeviti wa vyama vya Upinzani,Freeman Mbowe wa Chadema(Kulia) na Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF(wapili kulia)wakiagana na viongozi wa Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu jijini Dar es Salaam jana baada ya mazungumzo kuhusu kupinga Rais kusaini Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba.Picha na Fidelis Felix
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo,
atamshangaa Rais Kikwete ikiwa atasikiliza kelele za wapinzani kwa sababu
walishirikishwa kupitia kamati na hata bungeni kabla ya kupitishwa kwake.
“Nitamshangaa sana
Rais Kikwete kama atashindwa kusaini muswada
huo kwa sababu ya kelele za wapinzani. Tuliwashirikisha katika kila mchakato
kabla na baada ya kuuwasilisha bungeni,” alisema Chikawe.
Alisema kitendo cha wapinzani hao
kujiunga pamoja na kuanzisha kampeni za kuwahamasisha wananchi ili waukatae
muswada hakisaidii lolote, kwa sababu sheria zote zinatungwa bungeni na siyo
kwenye Viwanja vya Jangwani wala Ikulu.
Vyama vyampinga JK
Wakati Chikawe akisema hayo, viongozi
wa Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi wameshikilia msimamo wao kwamba wataendelea
kupinga muswada huo uliopitishwa na Bunge, Septemba 6, mwaka huu.
Wakizungumza Dar es Salaam jana
walipokutana na Shura ya Maimamu ikiwa ni mwendelezo wao wa kukutana na asasi
za kiraia, viongozi wakuu wa vyama hivyo, walisema kamwe kasi yao ya kutaka
kutosainiwa kwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
haiwezi kupunguzwa kwa namna yoyote kwa kuwa wanatetea masilahi ya Watanzania
na siyo mtu binafsi.
Kauli yao imekuja siku moja baada ya Rais Kikwete
kusema kuwa baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakisema uongo kuhusu mchakato wa
Katiba unavyokwenda.
Wanasiasa pia hao wamepinga matumizi
ya kauli za kibabe kwenye mchakato huo na kuonya kuwa nguvu ya dola haiwezi
kushindana na nguvu ya umma.
Mbali na hayo, wanasiasa hao
walisisitiza kwamba hawatapiga magoti kuomba Katiba Mpya, kwani ni ya
Watanzania wote na si mali
ya wanasiasa, chama cha siasa wala wabunge.
Rais Kikwete alikaririwa na magazeti
mbalimbali jana akipinga madai ya wapinzani kuwa hakuzingatia maoni yao wakati wa uteuzi wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Nafahamu kwamba tunaambiwa tunasema
uongo, lakini ni vizuri ifahamike wazi kuwa hatuwezi kupunguzwa nguvu na kauli
hizo alizozitoa Rais Kikwete, kwani msimamo tulionao ni kuendelea kutetea
Watanzania,” alisema Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Mbowe alimshauri Rais Kikwete atumie
busara kwa kutosaini mkataba huo ili mchakato uende vizuri.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim
Lipumba alisema mikutano wanayoifanya na asasi za kiraia imebainisha kwamba
uteuzi wa Tume ya Katiba ulifanyika kwa ubaguzi.
“Tunafahamu kwamba Rais ana nguvu ya
kuteua wajumbe wa tume hiyo kwa mujibu wa sheria, lakini kuna taasisi zimekosa
wawakilishi kwenye tume, mfano hai ni Shirikisho la Vyama vya Watu wenye
Ulemavu (Shivyawata), walitakiwa wapeleke majina ya watu watatu, lakini hakuna
hata mtu mmoja kati yao
aliyeteuliwa,” alisema Profesa Lipumba.
Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James
Mbatia alisema viongozi wa Shivyawata waliwaeleza wazi kuwa hawana mwakilishi
kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Wanasiasa hao leo wanatarajia
kukutana na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (Tec).
Nape alonga
Akizungumzia madai hayo ya upinzani,
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema kama
wanataka waaminike, watoe ushahidi kuthibitisha wanachokidai.
“Hawa watu ni vigeugeu. Kwanza, Rais alipoteua wajumbe wa Tume, Chadema
walijitokeza hadharani na kupongeza. Baadaye haohao waliibuka na kuanza
kuishutumu Tume wakisema kuwa imekosa weledi.
“Wakati wa mchakato wa kukusanya
maoni, Chadema haohao, ambao waliiona Tume haina weledi, wakapeleka maoni yao hukohuko. Ukifuatilia
haya mtu unashindwa kuelewa msimamo wa watu hawa ni upi hasa,” alisema Nape
mkoani Simiyu.
Imeandikwa na Patricia Kimelemeta,
Aidan Mhando na Rachel Shempemba.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment