HATIMAYE Tanzania imewekwa kando
rasmi na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), katika kuunda
Shirikisho la Kisiasa litakaloziongoza nchi hizo. (HM)
Tayari marais wa nchi hizo, Paul
Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda, Uhuru Kenyatta wa Kenya na Pierre
Nkurunzinza wa Burundi wamekwishafikia makubaliano ya kuanzisha mchakato wa
kuandikwa kwa Rasimu ya Katiba ya Shirikisho la Kisiasa la nchi wanachama wa
EAC, bila kuishirikisha Tanzania.
Waziri wa Serikali za Mitaa wa
Rwanda, James Musoni, amekaririwa na vyombo vya habari vya nchi hiyo akieleza
kuwa makubaliano ya kuanzishwa kwa mchakato wa kuandikwa kwa Rasimu ya Katiba
ya Shirikisho la Afrika Mashariki, yalifikiwa Septemba 12 mwaka huu, mjini
Kampala na marais wa Rwanda, Kenya na Uganda na hivi karibuni Rais wa Burundi
ambaye alialikwa katika mkutano huo na kushindwa kuhudhuria, naye sasa
amethibitisha ushirika wake katika shirikisho hilo jipya.
Gazeti la The Sunday Times la Rwanda,
limemnukuu Waziri Musoni kuwa marais wa nchi hizo wamekubaliana kukamilisha
rasimu hiyo ndani ya muda mfupi.
Musoni ambaye alikiri kushiriki
katika mkutano wa marais hao ulioshirikisha pia maofisa waandamizi wa nchi hizo
isipokuwa Tanzania, alisema
uamuzi uliofikiwa katika mkutano huo ambao ni wa pili kufanyika, ni moja ya
maagizo ya uamuzi uliofikiwa kwenye mkutano wa kwanza uliofanyika pia mjini Kampala.
"Tumekubaliana juu ya kanuni za
kisheria na mpango mzima utakaotuongoza ili kupata Rasimu ya Katiba
itakayoliongoza shirikisho hilo
la kisiasa," alikaririwa Musoni.
Alieleza kuundwa kwa kikosi kazi
maalumu kitakachojulikana kwa jina la High Level Task Force (HLTF), ambacho
kitajumuisha wataalamu wa nyanja mbalimbali watakaoandika Rasimu hiyo kwa namna
ile ile ya ulivyoandaliwa mpango wa Itifaki ya soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Musoni alisema mawaziri wa nchi
wanachama waliopangiwa kushughulikia shirikisho hilo,
wanatarajiwa kuelezea mwelekeo wa mafanikio ya mpango huo katika mkutano
mwingine uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Oktoba huko Kigali
Rwanda.
Kwa mara ya kwanza, marais Kagame,
Museveni na Kenyatta walikutana kufikia makubaliano ya kuharakisha uundwaji wa
shirikisho la kisiasa kwa nchi zao kwa kuondoa vikwazo vya kiuchumi na kuweka
hati ya vitambulisho vya pamoja na ushirikiano wa kibiashara sambamba na
kuzindua mradi wa ujenzi wa gati ya Bandari ya Mombasa.
Waziri Sitta ashangaa
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, alipoulizwa kuhusu hatua ya nchi hizo kuanza kuitenga Tanzania kuelekea kwenye Shirikisho la Kisiasa, alisema Katiba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ibara ya 7 (e) ya mkataba inaruhusu nchi wanachama kufanya jambo la haraka kama nchi nyingine zinachelewa kufanya hivyo.
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, alipoulizwa kuhusu hatua ya nchi hizo kuanza kuitenga Tanzania kuelekea kwenye Shirikisho la Kisiasa, alisema Katiba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ibara ya 7 (e) ya mkataba inaruhusu nchi wanachama kufanya jambo la haraka kama nchi nyingine zinachelewa kufanya hivyo.
Sitta alilieleza Jumatano kuwa,
taratibu za Tanzania
haziruhusu kibali cha utambulisho kutumika katika nchi zote wanachama, kwa
sababu lazima raia wa nchi wanachama anapoingia Tanzania kufuata taratibu za
uhamiaji.
Alisema licha ya hatua
zinazochukuliwa na nchi wanachama wa EAC za kuitenga Tanzania katika baadhi ya mambo,
itabakia na msimamo wake na haitakubaliana kuingia kwenye Shirikisho la Kisiasa
huku masuala ya ushuru wa forodha, soko la pamoja na sarafu moja,
hayajatengamaa.
"Huo ndio msimamo wa Tanzania,
hivi vitu vinne vilikuwa bado havijakamilika, matumizi yake hayajaenda sawasawa
na makubaliano ya kila nchi sasa wanaharakisha Shirikisho la Kisiasa, waache
waende kwa sababu Katiba inawaruhusu na wana ajenda zao za siri.
"Hatuoni suluhisho katika suala hilo, ni vigumu kuanza kusuluhisha matatizo ya jumuiya kwa
sasa kama ilivyo vigumu kusuluhisha matatizo ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
"Ukitazama sasa tunapambana
kuendeleza Muungano na Zanzibar,
hili la nchi zote nne litakuwaje? Mali zinatoka nchi nyingine, vivyo
hivyo kwa upande wa bidhaa, kwa maana hiyo hatuwezi kufika kwenye shirikisho
kabla hatujamaliza vikwazo hivi vingine," alisema Sitta.
Tanzania yailima barua EAC
Waziri Sitta pia alieleza kuwa Tanzania imeiandikia barua sekretarieti ya baraza la mawaziri wa nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki, ikilalamikia baadhi ya mambo yanayoendeshwa kwa usiri na baadhi ya nchi katika jumuiya hiyo.
Waziri Sitta pia alieleza kuwa Tanzania imeiandikia barua sekretarieti ya baraza la mawaziri wa nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki, ikilalamikia baadhi ya mambo yanayoendeshwa kwa usiri na baadhi ya nchi katika jumuiya hiyo.
Alisema barua alikabidhiwa katika
kikao cha baraza la mawaziri kilichofanyika Agosti 28 mwaka huu, mkoani Arusha,
ikitaka wahusika kuweka wazi mambo yanayoendelea ndani ya jumuiya kwa
kuzishirikisha nchi zote.
Aidha, Sitta alieleza kuwa wakati
barua hiyo ikiwa imekwishawasilishwa kwa Sekretarieti, viongozi ambao
wamekubaliana kuanza mchakato wa kuandika Rasimu ya Katiba ya Shirikisho la
Kisiasa, wanapaswa kutambua kuwa Katiba itakayopatikana itakuwa batili kwa
sababu haikuamuliwa na wananchi wa nchi husika bali watawala. Chanzo: Mtanzania
No comments:
Post a Comment