Seif al-Islam Gaddafi
Mtoto wa kiume wa dikteta wa Libya
aliyeuwawa Moamer Gaddafi Alhamisi (19.09.2013) amefikishwa mahakamani katika
mji wa Zintan kwa mashtaka ya kuvuruga usalama na kesi yake imeahirishwa hadi
tarehe 12 mwezi wa Disemba.
Seif al-Islam pia alikuwa anatarajiwa
kufikishwa katika mahakama ya Tripoli kwa ajili
ya kutajwa kwa kesi yake ya mashtaka ya usalama kuhusiana na uasi wa mwaka 2011
uliompinduwa baba yake lakini kuna wasi wasi iwapo waasi wa zamani waliomteka
na kumshikilia huko Zintan watakubali kumpeleka Tripoli.
Mwendesha mashtaka wa Libya Abdulqader Radwan hapo Jumatano aliamuru
Seif al -Islam ahamishiwe katika mahakama ya Tripoli kutoka ya Zintan ilioko kilomita 180
kusini magharibi mwa nchi hiyo.
Mrithi huyo wa zamani wa uongozi wa
Gaddafi na washtakiwa wengine zaidi ya 30 akiwemo kiongozi wa zamani wa ujasusi
Abdullah al Senussi wanashtakiwa kwa madai ya uhalifu waliofanya wakati wa uasi
wa mwaka 2011 uliomn'gowa madarakani Gaddafi.
Kesi muhimu katika historia ya Libya
Baghdadi al -Mahmudi waziri mkuu wa
mwisho katika kipindi cha Gaddafi na Mansur Daw ambaye alikuwa akiiongoza
Kikosi cha Ulinzi cha Wananchi pia ni miongoni mwa washtakiwa katika mojawapo
ya kesi muhimu kabisa ya kisheria katika histroria ya Libya.
Mwendesha mashtaka wa Libya Radwan
ameuambia mkutano wa wandishi wa habari kwamba wametuma agizo la kuhamisha kesi
hiyo katika mahakama ya Tripoli
kwa mamlaka zinazoshugulikia watu
wanaohusishwa na kesi nambari 630
akiwemo Sef al-Islam.Inaripotiwa kwamba mazungumzo yalifanyika hadi usiku wa
manane hapo jana kwa ajili ya kumhamisha Seif mjini Tripoli
kwa masaa kadhaa.Duru zilizo karibu na kesi hiyo zimesema suala hilo litategemea zaidi
hali ya usalama.
Mashtaka makuu yanayowakabili
watuhumiwa ni pamoja na mauaji yaliofanyika wakati serikali ilipokuwa
ikipambana na uasi ambao ulizuka katika mji wa mashariki wa Benghazi hapo mwezi wa Februari mwaka 2011.
Seif al-Islam yuko mikononi mwa
serikali
Gaddafi alitekwa na kuuwawa na waasi
katika mji alikozaliwa wa Sirte mwezi wa Oktoba mwaka huo.
Mtoto wake huyo wa kiume alitekwa
mwezi uliofuatia na kundi la waasi wa zamani kutoka eneo la milimani la Zintan
na amekuwa akishikiliwa huko tokea wakati huo.Serikali ya sasa ya nchi hiyo ya
Afrika Kaskazini ilijaribu mara kadhaa kutaka kuhamishiwa Tripoli kwa mtoto huyo wa Gaddafi bila ya
mafanikio.
Hata hivyo serikali hiyo imekuwa
ikisisitiza kwamba Seif al-Islam anashikiliwa na serikali.
Wakati huo huo shirika la kimataifa
la kutetea haki za binaadamu Amnesty International limetaka kukabidhiwa haraka
kwa Seif al Islam na Senussi kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu.
Shirika hilo
limesema mfumo wa mahakama nchini Libya unatakiwa kufanyiwa mageuzi
makubwa na kuna wasi wasi mkubwa juu ya uwezo wa serikali kuhakikisha kesi
zinafanyika kwa haki kutokana na kuwepo kwa hali mbaya ya usalama nchini humo.
Jumla ya nyaraka 40,000 na kurasa
4,000 za maelezo ya usaili zitazingatiwa na mahakama ambayo itasikiliza kesi
hiyo katika eneo la siri katika mji mkuu wa Libya.
Iwapo watuhumiwa watapatikana na
hatia wanaweza kuhukumiwa adhabu ya kifo.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP
Mhariri: Josephat Charo
Chanza: DW
No comments:
Post a Comment