Mkuu wa Kitengo cha
Polisi cha Kuzuia na Kudhibiti Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa
Johannesburg. Watanzania Agness Masogange na Melisa
Edward waliokamatwa kwa kutuhumiwa kubeba dawa za kulevya huko Afrika Kusini
wameachiwa kwa dhamana.
Mkuu wa Kitengo cha Dawa za Kulevya
Afrika Kusini, Kamishna Toto Mangaleni aliithibitishia Mwananchi jana kuwa
watuhumiwa hao wameachiwa kwa dhamana,lakini wataendelea kubaki Afrika Kusini
wakati kesi yao ikiendelea.
Mangaleni alisema wanawake hao ambao
juzi pia walipanda kizimbani, walipata dhamana hiyo jana kutoka Mahakama Kuu ya
Gauteng iliyoko eneo la Kempton
Park jijini Johannesburg.
Hata hivyo, Kamishna Mangaleni
alisema hawezi kuzungumzia zaidi kuhusu kesi hiyo kwa sababu hataki kuharibu
uchunguzi ambao unaendelea dhidi ya Watanzania hao, ambao ni wasanii.
Marafiki wa karibu wa Masogange
wanaoishi maeneo ya Midland Johannesburg ambao walikataa kunukuliwa majina yao, walithibitisha kuwa
wanawake hao wameachiwa kwa dhamana.
“Ni kweli wameachiwa leo asubuhi.
Lakini hatuwezi kuongelea kwa kina habari hizi kwa sababu hatutaki matatizo na
polisi. Hii kesi bado inaendelea na wataendelea kubaki hapa hadi kesi yao itakapomalizika,”
alisema mmoja wa marafiki zake.
Naye Masogange aliandika kwenye
mtandao wa ‘Facebook’.
“Namshukuru Mungu nimeamini wewe
ulikuwa pamoja na mimi katika maombi yangu na nashukuru kwa wote mliokuwa
mkiniombea Mungu kapokea maombi yenu.”
Masogange na Melissa walikamatwa
Julai 2 mwaka huu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo jijini Johannesburg wakiwa wana
mabegi sita makubwa ya dawa zinazoaminika kuwa ni `Crystal Methyl Amphetamine’.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Polisi cha Kuzuia
na Kudhibiti Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa aliiambia Mwananchi jijini Dar es
Salaam kuwa alikuwa amepata taarifa za kuachiwa kwa wasichana hao, lakini
alikuwa anawasiliana na watu wa Afrika Kusini ili kupata uhakika.
Nzowa, hata hivyo alilidokeza gazeti
hili juzi kuwa kuna uwezekano wanawake hao wangepata dhamana au kufungwa
kifungo chepesi kwani dawa walizokamatwa nazo ni kemikali zinazotumika
kutengeneza dawa za aina tofauti kwa matumizi ya binadamu ingawa pia na dawa za
kulevya.
Mamlaka yapinga uamuzi wa Mahakama
Msemaji wa Mamlaka za Huduma za
Mapato Afrika Kusini(SARS), Marika Muller alisema wana uhakika asilimia 100
kuwa akina Masogange walikamatwa na dawa za kulevya.
“Timu yetu ilifanya kazi vizuri na
ilitambua kuwa mzigo huo ulikuwa wa dawa za kulevya ila tunaiachia mahakama
kuendelea na uchunguzi wake,” aliongeza Muller.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment