Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali
Said Mwema (kulia) akiagana na Wenyeviti wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim
Lipumba wa CUF (kushoto)Freeman Mbowe wa Chadema (wapili kulia) na James Mbatia
wa NCCR-Mageuzi, jijini Dar es Salaam jana. Picha Fidelis Felix
Dar es Salaam. Vyama vya siasa vya upinzani vya
Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, leo vitafanya mkutano wa hadhara katika Viwanja
vya Jangwani kuhamasisha wananchi wapinge kile wanachodai ni hujuma dhidi ya
Mchakato wa Katiba Mpya.
Hatua ya kufanya mkutano huo,
ilifikiwa jana baada ya wenyeviti wa vyama hivyo kumvamia Mkuu wa Jeshi la
Polisi nchini (IGP), Said Mwema ofisini kwake wakipinga kitendo cha Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Dar es Salaam
kupiga marufuku maandamano waliyokuwa wayafanye leo jijini humo.
Katika mkutano wao na IGP Mwema,
viongozi hao walikubaliana maandamano hayo yasitishwe kwa sababu za kiusalama,
lakini wafanye mkutano huo wa hadhara.
Wenyeviti hao wa vyama vya Upinzani,
James Mbatia wa NCCR-Mageuzi, Freeman Mbowe (Chadema) na Profesa Ibrahim
Lipumba (CUF), ambao walikutana na Mwema jana mchana.
Hatua ya viongozi hao ilitokana na
tamko lililotolewa juzi na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam, Suleiman Kova kusitisha
maandamano ya vyama hivyo yasifanyike.
Kova alitaja sababu za uamuzi huo
kuwa ni kuhofia yatasababisha kusitishwa kwa shughuli za kiuchumi pamoja na
kuwepo taarifa za kiintelijensia kwamba yatakuwa na vurugu.
Tamko hilo
liliwakera viongozi wa vyama hivyo vitatu vilivyotangaza kushirikiana katika
kupinga kile wanachodai ni uporaji wa haki ya wananchi kutunga Katiba yao.
Mazungumzo wenyeviti hao na IGP
yalianza saa 6 mchana na kumalizika saa 11 jioni, ambapo walitoa taarifa ya
pamoja kuhusu waliyokubaliana.
Akitangulia kutoa taarifa hiyo, kwa
niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba alisema: “Tumekubaliana
kesho tutafanya mkutano Viwanja vya Jangwani. Tumekubaliana kusitisha
maandamano hadi Oktoba 5, (mwaka huu).”
Aliongeza kuwa wamekubaliana pia
kwamba watafanya mkutano mwingine wa hadhara Visiwani Zanzibar, Jumatano ijayo.
Hata hivyo, katika taarifa ya pamoja,
ulitokea kuhitilafiana kwa kauli, pale IGP Mwema alipokuwa akitoa ya upande
wake.
Hali hiyo ilitokana na kauli ya
Profesa Lipumba kusisitiza kuwa mikutano na maandamano ni haki ya msingi kwa
vyama vya siasa na kwamba wanachopaswa ni kutoa taarifa kwa polisi na wala siyo
kuomba kibali.
Awali, wakati Mwema akihitimisha
taarifa hiyo ya pamoja alisema kuwa wanasiasa hao wanapaswa kuomba kibali cha
maandamano hayo ya Oktoba 5.
Alisisitiza kuwa kazi ya polisi ni
kuhakikisha usalama wa raia na mali
zao, hivyo wanasiasa hao wanapaswa kuomba kibali na baada ya polisi kuchunguza
watakuwa na mamlaka ya kuridhia au kukataa ombi lao.
Mwema alisema haoni haja ya kuwepo
malumbano na wanasiasa hao katika suala hilo
kwa sababu lengo lao ni moja nalo ni kudumisha ustawi wa jamii.
“Wote tunajenga nyumba moja, sioni
sababu ya kugombania fito,” alisema Mwema.
Mzozo wa Katiba
Mzozo wa vyama vya siasa vya upinzani
ulianzia kwenye Mkutano wa 12 wa Bunge uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma, lakini sasa
umehamia nje ya Bunge na vyama hivyo vimetangaza azma ya kuanza kampeni ya
kuuhamasisha umma kudai maridhiano kabla ya kuendelea na mchakato wa Katiba
Mpya.
Viongozi hao wa upinzani wanadai
kwamba wabunge wa CCM waliongeza baadhi ya mambo kupitia majedwali ya
marekebisho.
Wanadai kuwa hali hiyo inatoa mwanya
kwa Serikali inayoongozwa na CCM kupitia kwa rais kuwa na mamlaka zaidi ya
uteuzi wa wajumbe husika.
Vyama hivyo viliazimia kuanza rasmi
leo harakati za kuhamasisha umma kupitia maandamano na mikutano ya hadhara.
Ndoa hiyo ya wapinzani waliifunga,
Septemba 15, kwa kuandika historia nyingine mpya kwenye tasnia ya siasa za Tanzania
wakipinga Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka
2013.
Wanadai mapendekezo mengi yaliyomo
katika Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
yalipendekezwa na vyama hivyo, hivyo havitakuwa tayari kuona maoni hayo pamoja
na ya Watanzania wengi yakichakachuliwa.
Wanasema muungano wao ni mwanzo wa
kuunganisha umma wa Watanzania kufanya uamuzi wa kunusuru utekaji madaraka na
mamlaka ya nchi kutoka kwa wananchi.
Vyama hivyo vinadai kuwa vinaungwa
mkono na makundi mbalimbali yakiwamo asasi za kiraia, taasisi za dini, vyama
vingine vya siasa, wasomi na taasisi za elimu.
Makundi mengine ni pamoja na vyama
vya wafanyakazi, jumuiya za wakulima, wafugaji, wavuvi, sekta binafsi, watu
wenye ulemavu, jumuiya za wanawake, vijana na wastaafu.
Misimamo ya wenyeviti
Profesa Lipumba anasema
wanachopigania ni kuurejesha mchakato wa Katiba Mpya mikononi mwa umma,
anaongeza kuwa suala hilo
kwa sasa limehodhiwa na CCM.
“Tunamshauri Rais Kikwete asisaini
muswada huu, aurejeshe bungeni ufanyiwe marekebisho yenye kujenga kuaminiana na
mwafaka wa kitaifa kwenye mchakato wa mabadiliko ya Katiba. Hatutakwenda
kumwona, ila aurejeshe bungeni,” anasema Lipumba na kuongeza:
“Mchakato huu unahitaji uvumilivu,
staha na hekima na usitawaliwe na nia mbaya, ubabe, mabavu, kejeli na dharau
hasa kutoka kwa watawala. Misingi hii ikipuuzwa mchakato mzima unaweza
kutumbukiza taifa letu katika mpasuko, migogoro na hata machafuko.”
Mbatia anasema historia ya nchi
inaonyesha kuwa waasisi wa kutaka sauti, kauli na mawazo ya umma isikike katika
kudai Katiba Mpya ni vyama vya upinzani.
“CCM ndio nini… Wanatakiwa kujua kuwa
Tanzania kwanza vyama
baadaye, vyama vya siasa vilivyokuwa vikitawala nchini Kenya, Zambia vimekufa, lakini nchi hizo
bado zipo. CCM inaweza kufa, lakini Tanzania itaendelea kubakia”
anasema na kuongeza;
“CCM wakisema wapinzani tunafanya
vurugu wanakosea, hatuwezi kuangamiza wazo letu la kutaka Katiba Mpya, katika
taifa hili Watanzania hawajawahi kuandika Katiba iliyotokana na mawazo yao.”
Mbowe anasema wameamua kuweka pembeni
tofauti zao kwa ajili ya kudai Katiba Mpya ya Watanzania wote, kwamba hata
wanahabari wanatakiwa kuweka pembeni itikadi za vyombo vyao vya habari
vinavyomilikiwa na vyama vya siasa, kuwa wakweli katika kudai Katiba Mpya.
“Waandishi wa habari msiwe vipaza
sauti vya watawala bila kutafakari kwa kina Tanzania
ya miaka 100 ijayo itakuwaje, wanahabari mnaweza kutunyima Katiba Mpya au
mkatunyima kama ikitumika vibaya,” anasema.
Anaongeza kuwa amani ya nchi inaweza
kuvurugwa kama mchakato wa katiba utahodhiwa
na chama kimoja cha siasa (CCM), “Ikiwa hivyo, sisi hatutakubali kuwa kondoo.
Wanaohubiri amani watambue kuwa kuna misingi ya kuipata amani hiyo, amani
inapatikana kunapokuwepo na haki.”
Huku akinukuu kitabu cha Mwalimu
Julius Nyerere cha ‘Freedom and Unity’, anasema, “Ni rahisi mno kuliwasha taifa
la watu ambao wamekwazika, taifa hili watu wamekwazika sana. Mchakato wa katiba unaweza kutibu
majeraha makubwa ambayo yanalikabili taifa.”
Anasema fursa adimu ya kupata Katiba
Mpya inapotezwa na bunge na CCM na anasisitiza kwamba wapinzani watatumia kila
aina ya mbinu kuwaelewesha Watanzania kinachoendelea ili washiriki katika
kuidai katiba iliyotokana na mawazo yao.
“Wapinzani hatutarudi nyuma na
hatutakubali nchi kurejeshwa chini ya uongozi wa katiba ya sasa. Hilo wenzangu (wenyeviti
wenzangu) naomba mnielewe, Chadema hatukubali na naomba na nyinyi msikubali,
maana ndani ya CCM kuna kundi linataka kurudi katika katiba hii
tunayoilalamikia,” alisema.
Anasema katika kitabu hicho, Mwalimu
Nyerere alisema, ‘Kuna siku wananchi watachagua kifo kama
viongozi hawatakuwa makini’, kwamba hoja ya kutaka Amani itaharibiwa na wale
wenye dola, siyo vyama vya upinzani.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment