California/Johannesburg. Wakati Rais
Jakaya Kikwete akisema Serikali yake haitawatetea Watanzania wanaokamatwa
wakijishughulisha na biashara ya dawa za kulevya, Watanzania wawili Agnes
Masongange na mwenzake, Melisa Edward jana walinyimwa dhamana na Mahakama Kuu
ya North Gauteng katika kesi ya dawa ya
kukamatwa na dawa hizo.
Rais Kikwete alisema Serikali yake
itakabiliana na biashara hiyo kwa nguvu zote kwa kuwa ni haramu na ni kinyume
na sheria za nchi.
Alisema hayo juzi usiku alipokutana
na Watanzania wanaoishi katika Jimbo la California,
Marekani...“Serikali yangu haitawatetea watu wanaojishughulisha na ubebaji wa
dawa za kulevya na kusafirisha nje ya nchi. Hii ni biashara haramu na inavunja
sheria za nchi yetu.”
Masogange na Melisa walikamatwa Julai
2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Oliver Tambo, Afrika Kusini wakituhumiwa
kusafirisha kilo 150 za dawa za kulevya zenye thamani ya Sh6 bilioni.
Aidha, amesema hayo siku chache baada
ya meli ya mizigo ya Gold Star iliyosajiliwa nchini kukamatwa na maofisa
forodha na askari wa doria wa Italia katika Pwani ya Sicily, Bahari ya Mediterranean ikiwa na
tani 30 ya dawa ya kulevya aina ya bangi zenye thamani ya Paundi za Uingereza
50 milioni (Sh125 bilioni).
Pia, Agosti 31, mwaka huu,
mshambuliaji nyota wa zamani wa timu ya soka ya Simba na Taifa, Joseph Kaniki
‘Golota’ na bondia Mkwanda Matumla walikamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Bole, Addis Ababa walipokuwa wakijiandaa kwenda Paris, Ufaransa wakituhumiwa kubeba dawa za
kulevya.
Juzi, Rais Kikwete alisema ni wajibu
wa Watanzania wanaoishi ughaibuni kuwa raia wema, kufuata na kuheshimu sheria
katika nchi wanazoishi kwa sababu wakizivunja, Serikali yake haitawatetea.
“Ukikamatwa na dawa za kulevya
hatukutetei kwa sababu hata sheria za nchi yetu zinazuia biashara hiyo. Sisi
hatuwezi kuendelea kuwa na sifa ya kufanya biashara za ovyoovyo kiasi hicho.
Serikali itawatetea Watanzania wanaoishi nchi za nje ikiwa wataonewa. Lakini
ukifanya biashara ya dawa ya kulevya au kubaka watu hatukutetei kamwe,”
alisema.
Masogange, Melisa wakwama dhamana
Masogange na mwenzake Melisa jana
walikosa dhamana baada ya kupandishwa kizimbani katika Mahakama Kuu ya North
Gauteng, Afrika Kusini kujibu mashtaka ya kusafirisha dawa zinazodaiwa kutumika
kutengenezea dawa aina ya amphetamine (maarufu kama
tik).
Taarifa kutoka Mahakama hiyo
zinaeleza kuwa, Masogange na Melissa walirudishwa rumande na kesi yao itasikilizwa tena
Novemba mwaka huu.
Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za
Kulevya cha Polisi nchini, Kamanda Godfrey Nzowa alithibitisha kuwa watuhumiwa
hao walipanda kizimbani jana kujibu mashtaka yanayowakabili ya kusafirisha dawa
za kulevya na kwamba wamerudishwa rumande hadi Novemba.
Awahoji akina Masogange
Nzowa alisema alikwenda Afrika Kusini
kuwahoji Melisa na Masogange kabla ya kupandishwa kizimbani lakini alisema
hawakumpa ushirikiano.
Kamanda huyo alisema imebainika kuwa
mzigo walioubeba wasichana hao haukuwa dawa halisi za kulevya, bali kemikali
zinazotumika kutengeneza dawa zinazoitwa amphetamine. Kutokana na madai hayo,
Nzowa alisema wanaweza kupewa dhamana na kesi yao kuendelea kusikilizwa nchini baada ya
yeye (Nzowa) kushauriana na Kitengo cha Dawa za Kulevya cha Afrika Kusini.
Alisema, inawezekana watuhumiwa
wakapewa hukumu nyepesi kidogo kutokana na kosa hilo.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment