Dar es Salaam. Shahidi wa Waziri wa Fedha wa
zamani, Basil Mramba, Kamishna wa zamani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
Felician Busigara, jana alizua mvutano mkali kati ya mawakili wa mashtaka na
wale wa utetezi.
Busigara ambaye ni shahidi wa pili wa
Mramba, alipanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ili kumtetea
Mramba katika kesi ya matumizi mabaya ya madaraka katika ofisi za umma na
kuisababishia Serikali hasara.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo
ni, Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu wa zamani
wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja.
Wanakabiliwa na mashtaka ya kuisamehe
kodi isivyo halali, Kampuni ya Ukaguzi wa Madini ya Alex Stewart (Assayers) ya
Uingereza na kuisababishia Serikali hasara ya Sh11.7 bilioni.
Mvutano huo ulizuka baada ya upande
wa mashtaka, kumpinga shahidi huyo, kutoa ushahidi wake kama mtaalamu wa
masuala ya kodi, ukidai kuwa upande wa utetezi haukufuata taratibu za utoaji wa
maoni kama mtaalamu.
Wakati akitoa ushahidi wake huku
akiongozwa na Wakili Herbert Nyange, anayemtetea Mramba, Wakili wa Serikali
Mkuu, Oswald Tibabyekomya, alikuwa akinyanyuka mara kwa mara na kuweka
pingamizi shahidi huyo kutoa ushahidi kama mtaalamu.Mbali na Wakili
Tibabyekomya kupinga, mahakama pia ilikuwa ikihoji sababu za shahidi huyo kutoa
ushahidi kama mtaalamu.
Akiongozwa na Wakili Nyange, Busigara
alidai kuwa sheria ya kodi ya mapato inamtaja mwenye mamlaka ya kusamehe kodi
kuwa ni Waziri wa Fedha.
“Nyange kuna haja gani ya kumleta
shahidi anayezungumzia sheria, sheria zipo katika vitabu, hata wakili unaweza
kuzungumzia hizo sheria katika majumuisho yako, mashahidi wako wasituambie
kuhusu sheria,” alihoji Jaji Rumanyika.
Shahidi aliendelea kutoa ushahidi kwa
kusoma kipengele kimoja cha mkataba kati ya Alex Stewart na BoT, akidai kuwa
mkataba huo ulionyesha kwamba atakayelipa kodi ni benki na kampuni itapata
fedha yake baada ya kodi.
Jambo lililosababisha Jaji Rumanyika
kuingilia tena kati.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment