Dar es
Salaam. Tanzania imemkataa Balozi mteule wa Ujerumani
ambaye alitakiwa kuja kufanya kazi nchini.
Balozi huyo, Margit Hellwig-Boette
alikuwa amemaliza muda wake nchini Kenya
na alitakiwa kuja kuiwakilisha nchi yake Tanzania.
Balozi Hellwig-Boette alikaririwa na
Gazeti la Standard la Kenya
akieleza kuwa anajipanga kurudi kwao baada ya kukataliwa na Serikali ya Tanzania.
Alipoulizwa juu ya suala hilo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alikataa
kuzungumzia suala hilo
akisema: “Watu wa Wizara ya Mambo ya Nje ndio wanaoshughulika na hayo mambo,
waulizeni.”
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mkumbwa Ally alisema wizara
yake haijapata taarifa za kukataliwa kwa balozi huyo.
“Suala hilo linahusu ofisi ya Rais, mambo ya uteuzi
ni ya Rais. Wizara ya Mambo ya Nje haina hiyo taarifa na hata kama
ingekuwapo hiyo taarifa siyo ya `public’.
“Siyo taarifa ya umma kwa maana
kwamba, mchakato wake ni wa siri na hayo mambo hayana kuuliza kwa nini. Ukileta
jina la mtu unayetaka aje kuwa balozi likikataliwa, hakuna kuuliza eti ni kwa
nini.
“Unachofanya ni kuleta jina jingine,
hata Rais hapa akipeleka jina la mtu kwenye nchi nyingine lisiporudi, hakuna
kuuliza unachofanya ni kuteua tu jina jingine,” alisema Mkumbwa.
Alikariri Kifungu cha Nne cha Azimio
la Vienna
ambacho kinaruhusu nchi kukataa balozi wa nchi nyingine bila ya kutoa sababu.
“Nchi inayopeleka balozi katika nchi
nyingine inatakiwa kutoa jina mapema kwa nchi nyingine. Hata hivyo, nchi hiyo
ina uwezo wa kumkubali au kukataa uteuzi,” kinaelekeza kifungu hicho.
Balozi Mjerumani alonga
Gazeti hilo
la The Standard, lilimkariri Balozi Hellwig-Boette akisema kuwa amekataliwa
kuja Tanzania
bila ya kuelezwa sababu.
“Ndiyo, Tanzania
imekataa uteuzi wangu. Kwa mujibu wa itifaki za kidiplomasia, nchi husika ina
haki ya kumkataa mtu aliyeteuliwa kwenda kuwakilisha nchi yake au kumkubali.
Tanzania imenikataa lakini haijatoa sababu
yoyote ya kufanya hivyo.
“Nitaondoka Nairobi kurudi Berlin
Alhamisi (leo) asubuhi ili nikapangiwe sehemu nyingine,” lilieleza gazeti hilo.
Hivi karibuni aliyekuwa Waziri Mkuu
wa Kenya, Raila Odinga
aliandaa chakula cha jioni, lengo likiwa ni kumuaga balozi huyo baada ya
kumaliza kipindi cha miaka minne akiwa anaiwakilisha Ujerumani nchini Kenya.
Misimamo yake imemponza
Gazeti hilo
limesema Hellwig-Botte ambaye alikuwa Balozi wa Ujerumani nchini Kenya tangu
mwaka 2009, alikuwa anajulikana kutokana na misimamo yake na hasa kupinga
ukiukwaji wa haki za binadamu na mara nyingine kuunga mkono vyama vya upinzani.
Anadaiwa kutokuwa na uhusiano mzuri
na Serikali ya Kenya kutokana na msimamo wake wa kuunga mkono Rais wa nchi
hiyo, Uhuru Kenyatta na Naibu wake, William Ruto kushtakiwa kwenye Mahakama ya
Makosa ya Jinai ya Kimataifa huko The Hague, Uholanzi kutokana na kuhusishwa na
vurugu za uchaguzi wa mwaka 2007 nchini Kenya.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment