UKIWA unapita Barabara ya Morogoro, labda unatoka Arusha, Morogoro, Iringa au Mbeya, ukishaumaliza Mkoa wa Pwani, utakutana na bango kubwa barabarani limeandikwa ‘Karibu Dar es Salaam’.
Kama hiyo haitoshi utakutana na
mabango mengine madogo madogo yakisomeka “Sasa umeingia Dar es Salaam’.
Baada ya Mbeya
City kuwa vidume katika Mkoa wa Mbeya
na hata kuikomalia Yanga, sasa si vibaya kama tukiikaribisha timu hiyo jijini Dar es Salaam kwa kusema
“Karibu Dar es Salaam’.
Mbeya City wameingia Dar es Salaam kwa mara ya
kwanza tangu waanze Ligi Kuu Bara.
Kila kona ya Dar es Salaam na Tanzania wanaizungumzia mechi yao dhidi ya Simba leo Jumamosi itakayopigwa
Uwanja wa Taifa.
Licha ya kuwa imeshacheza mechi nne
za awali, mashabiki wanaamini kuwa wikiendi hii ndiyo Mbeya City
wanaanza ligi kwa kucheza mechi ya kwanza ngumu zaidi nje ya mkoa wake na ndani
ya Dar es Salaam tena dhidi ya timu ngumu ya Simba.
Mbeya City ilishangaza wengi kwa kutoka sare ya
bao 1-1 na mabingwa watetezi Yanga kwenye Uwanja wa Sokoine, wikiendi iliyopita
mjini Mbeya kabla ya kulazimisha suluhu dhidi ya Mtibwa mjini Morogoro Jumatano
wiki hii.
Mambo hayo yameongeza mvuto na hamasa
kwa mashabiki kwenye mechi dhidi ya Simba, ambayo imebatizwa jina la ‘Karibu
Dar es Salaam’.
Mbeya City
iliingia Mkoa wa Pwani juzi Alhamisi na kupiga kambi ya muda kabla ya jana
Ijumaa mashushushu wake kuanza kutua Dar
es Salaam na baadaye wakafuatiwa na timu yenyewe.
Kocha Juma Mwambusi amesisitiza kuwa
mchezo huo utakuwa mgumu lakini amewatengeneza kisaikolojia wachezaji wake
kukabiliana na presha ndani na nje ya uwanja na wanaamini watapata matokeo
mazuri.
Straika msomi na hatari wa Mbeya City
aliyemfunga Ally Mustapha ‘Barthez’, Mwagane Yeya amepania kumtungua, kipa wa
Simba, Abel Dhaira na kuandika historia katika Ligi Kuu Bara. Kiungo wa Mbeya City,
Steven Mazanda amesema lazima wawafanye kitu mbaya Wekundu hao wa Msimbazi.
Mbali na tambo hizo za wachezaji,
mashabiki wa Mbeya City kutoka Mbeya, wamesema watafurika kwa wingi
Uwanja wa Taifa kuishangilia timu yao.
Yeya, ambaye ni mwalimu wa Shule ya
Sekondari Iduda Uyole, aliliambia Mwanaspoti kuwa: “Mbeya City
ni vijana wa kazi, kwetu matokeo ni jambo la mwisho. Lakini malengo yangu ni
kuhakikisha napigana, kama niliweza kumfunga,
Barthez hata Dhaira (Abel) atafungika tu.”
Straika wa Simba, Tambwe Amisi
amesisitiza kuwa ameshazitambua klabu za Tanzania na sasa inamuwia rahisi
kukabiliana na mabeki.
Mchezaji huyo amesisitiza kuwa haijui
Mbeya City
lakini anaamini hakuna timu ambayo haifungiki huku kocha wake msaidizi, Jamhuri
Kihwelu ‘Julio’ akisema; “Simba imekamilika, vijana wako fiti sana na ni vipigo tu, hatuangalii jina la
timu wala ushabiki sisi tunataka pointi tu.”
HOFU YA KIPIGO
Wachezaji wa Mbeya City
wamekuwa na hofu kubwa huenda mashabiki wa Yanga wakawafanyizia kulipa kisasi
cha basi lao kuvunjwa kioo wikiendi iliyopita katika Uwanja wa Sokoine mjini
Mbeya.
Lakini hofu yao nyingine ni kucheza kwa mara ya kwanza
kwenye Uwanja wa Taifa, ambao una uwezo wa kubeba mashabiki 60,000 tena na timu
ambayo imeshinda mabao 6-0, Jumatano.
JEZI ZA MBEYA CITY
Kwa wauzaji wa jezi ni kwamba, jezi
za Mbeya City ni dili kubwa jijini Mbeya na watu
wanazishambulia kuliko za Simba na Yanga. Mbeya City
klabu mpya, imejizolea wapenzi wengi wa soka na robo tatu ya watu wa Mbeya
wanaishabikia klabu hiyo mpya ya Ligi Kuu Bara.
Mwanaspoti ilipita katika mitaa
mbalimbali ya Jiji la Mbeya na kujionea uuzwaji wake. Mmiliki wa duka la vifaa
la Mbaspo, Salum Haroun alisema: “Jezi za Mbeya City
hapa ni dili kubwa. Hapa dukani kwangu zimeisha na watu wanaziulizia sana, ukileta tu
hazikai.”
Naye mchuuzi wa barabarani, Jastine
Kisongi alisema: “Asikwambie mtu, kwa sasa jezi za Mbeya City
ndiyo zina dili hapa Mbeya, ukiwa nazo una uhakika wa kuuza tofauti na hizi za
Simba na Yanga.”
MECHI ZA LEO JUMAMOSI
Mgambo vs Rhino
Prisons vs Mtibwa
Kagera vs Ashanti
Simba vs Mbeya City
Chanzo: Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment