Friday, October 11, 2013

ICC:Mawakili wa Kenyatta wataka kesi ifutwe



Mawakili wa Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, wameitaka mahakama ya kimataifa ya jinai kusimamisha mashtaka ya Rais huyo kabla ya kesi yake kuanza mwezi ujao.
Wanasheria hao wamesema mashahidi wa utetezi wamekuwa wakitishwa, na kwamba wanao ushahidi wa kutosha kuthibitisha ukiukwaji wa taratibu za mahakama hiyo.

Rais Kenyatta na Naibu wake William Ruto, wanatuhumiwa kuchochea wimbi la vurugu za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.
Takriban watu1,200 walifariki na wengine laki sita kuachwa bila makao wakati wa ghasia hizo.

Kesi dhidi ya Kenyatta inatarajiwa kuanza tarehe 12 mwezi Novemba.
Naibu Rais pia yuko mbele ya mahakama hiyo na yeye ndiye afisaa mkuu wa kwanza wa serikali kufikishwa mbele ya mahakama ya ICC.

Mawakili wa Kenyatta waliwasilisha nyaraka za kurasa 38 siku ya Alhamisi kwenye mahakama hiyo wakiitaka kesi hiyo kutupiliwa mbali.
Nyaraka hizo zilisema kuwa upande wa utetezi una ushahidi wa kutosha kuonyesha kuwa mahakama imekua ikiendelea kukiuka taratibu zake.

Pia zilisema kuwa kuna ushahidi wa kutosha kuonyesha kuwa mashahidi wa upande wa mashitaka na mwengine mmoja walihusishwa na njama ya kutaka kuhujumu sheria.
Mawakili wa uetetzi aidha walituhumu upande wa mashitaka kwa kuwasilisha kesi ambayo ni ya kifisadi na sio ya haki dhidi ya Rais Kenyatta.

Upande wa mashitaka sasa unatarajiwa kujibu madai hayo na mahakama ya ICC huenda ikaamuru jopo la kusikilizwa kwa madai hayo kuyathibitisha.
                                                        Chanzo: Mjengwablog

Ndege zisizo na rubani kupelekwa DRC



Ndege zisizokuwa na rubani maarufu Drones,zitapelekwa mashariki mwa jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo mwezi ujao. Ndege zisizo na rubani zijulikanazo kama Drones.

Kamanda wa kijeshi wa tume ya kulinda amani ya umoja wa mataifa nchini Kongo,Monusco amesema kwamba ndege hizo zitahusika na kuchunguza mpaka wa Kongo na Rwanda. Wakati huohuo shirika la kimarekani la Enough Project limetuhumu waasi wa M23 kuendelea na biashara haramu vya madini. Kwenye ripoti yake ilotolewa hii leo shirika hilo limesema kila mwaka waasi hao na washirika wao kutoka Uganda na Burundi wameuza dhahabu ya zaidi ya dola milioni mia tano.

Sikiliza taarifa kamili kutoka kwa mwandishi wetu Salehe Mwanamilongo kwa bonyeza alama ya spika za masikioni hapo chini.
Mwandishi: Salehe Mwanamilongo
Mhariri: Saumu Mwasimba

UCHAMBUZI WA HOTUBA YA JK NA MGONGANO WA MASWALI





Hotuba iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete na kuzungumzia kwa undani mchakato wa Katiba Mpya, imeacha maswali mengi huku ikiashiria kutokuwapo kwa mawasiliano madhubuti ndani ya Serikali kuhusu suala hilo.

Kadhalika, hotuba hiyo imeibua mambo mawili ambayo ni hofu ya kuahirishwa kwa Bunge Maalumu la Katiba na kuzidi kwa lawama dhidi ya wabunge wa CCM pamoja na uongozi wa Bunge, hususan Naibu Spika, Job Ndugai.

Itakumbukwa kuwa mara baada ya muswada wa awali kupitishwa, baadhi ya mawaziri walinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari wakisema kusingekuwapo na mwanya kwa Rais Kikwete kukutana na wapinzani kwani upitishwaji wa sheria hiyo ulifuata taratibu zote za kibunge.

Hata hivyo, Rais Kikwete katika hotuba yake ya Septemba mwaka huu kwa taifa, alitangaza kuwapo fursa ya majadiliano baina ya Serikali na viongozi wa vyama vya upinzani; Chadema, CUF na NCCR Mageuzi ambavyo tayari vilikuwa vimeungana kupinga mchakato huo.

Viongozi wa vyama hivyo, Freeman Mbowe (Chadema), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na James Mbatia (NCCR Mageuzi) walichukua hatua ya kuhamasisha umma kutokubaliana na mchakato huo, wakirejea kutoridhika na jinsi Bunge lilivyoshughulikia Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Kauli ya Rais Kikwete kuwaalika wapinzani kwenye meza ya mazungumzo, inatafsiriwa na baadhi ya wasomi kuwa ni aibu kwa Bunge na wabunge waliopitisha sheria hiyo na kwamba ni dhahiri kwamba itarejeshwa bungeni kufanyiwa marekebisho.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut), Mwanza, Steven Dasu alisema Rais Kikwete ameridhia kuzungumza na wapinzani baada ya kubaini kuwapo udhaifu katika mchakato wa kupitisha sheria husika bungeni na kwamba hatua hiyo itawezesha kupatikana kwa Katiba yenye tija kwa nchi.

Hata hivyo, Ndugai jana alitetea uongozi wake bungeni huku akisema: “Bunge limefanya kazi yake, inawezekana liliamua vibaya au liliamua vizuri lakini uamuzi ulifanyika. Sasa kama sheria iliyopitishwa ina kasoro inaweza kurekebishwa tu kulingana na taratibu zilizopo”.

Pia aliwaponda wapinzani kwa kile alichokiita kuwa ni kukimbilia kwa Rais, badala ya kujenga hoja zao ndani ya Bunge na kwamba lazima watambue kuwa tabia hiyo haitawapeleka mbali.

Lawama kwa wabunge
Wakili wa kujitegemea, Dk Rugemeleza Nshala alisema wabunge hawakuwa makini na kwamba miswada inayotungwa na Bunge kurudishwa kwenye chombo hicho cha kutunga sheria kabla ya kuanza kutumika “ni aibu kwa mhimili huo”.

Pia Dk Nshala alisema hatua hiyo ni matumizi mabaya ya fedha za umma kwani wabunge wanapokaa na kufanya kazi bila umakini inalazimu warudi tena kufanya kazi ileile huku wakilipwa.

Naye mwanasheria wa siku nyingi wa Moshi Mjini, Peter Shayo alisema: “Tafsiri ya uamuzi huu wa Rais ni kuwapo kwa incompetence (upungufu) kwenye system (mfumo) ya Bunge. Wabunge waliopitisha sheria hiyo hawakutimiza wajibu wao vizuri.
“Wenzao wa upinzani waliuona upungufu huo mapema na kuusema lakini wakazidiwa na self interest (masilahi binafsi) ya CCM.Sasa unarudishwa bungeni kwa agizo la Rais, waliopitisha wanajisikiaje?”

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Mstaafu Amir Manento aliungana na Rais Kikwete akisema: “Katiba ni suala la wananchi wote, halipaswi kuwa la kikundi cha watu au chama cha siasa.

“Ninachoona, ndicho Rais alichoona na sasa anataka kuweka mambo sawa. Ukipeleka suala la Katiba kwa kuegemea upande fulani unaweza usipate matunda uliyotegemea. Suala hili ni nyeti kidogo na busara inatakiwa zaidi.”

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Eugenia Kafanabo alisema hashangazwi na muswada huo kurejeshwa bungeni kwa sababu ulipitishwa huku baadhi ya wabunge wakiupinga baada ya kuona makosa na kwamba Rais Kikwete ameona upungufu huo.

“Ulipitishwa kwa kulazimishwa, baadhi ya wabunge walisema uko sahihi, wengine wakitaka ufanyiwe marekebisho. Katiba ni sheria mama lazima upatikanaji wake uwe wa maridhiano, lazima wanaotengeneza Katiba husika waridhiane na kusiwe na malalamiko,” alisema Kafanabo.

Hata hivyo, akizungumzia suala hilo, Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe alisema suala la Rais kusaini muswada huo, kisha kurudishwa bungeni ni utaratibu wa kawaida.

Alikanusha taarifa kwamba hakuna mawasiliano baina ya Rais na mawaziri wake na kwamba suala la sheria kurejeshwa bungeni ni la kawaida. “Ni utaratibu wa kawaida tu kurekebisha sheria ambayo imeshasainiwa, hakuna kitu kipya hapo unaweza kufanyiwa marekebisho mpaka mara tatu.”

Kuhusu kile ambacho Rais Kikwete alikizungumza kwenye hotuba yake ya Septemba, waziri huyo alisema wanasubiri maelekezo yake ambayo ni dhahiri yatatokana na mwafaka utakaopatikana kwenye mazungumzo baina yake na viongozi wa upinzani.

Bunge la Katiba
Uamuzi wa Rais Kikwete kukutana na wapinzani kujadili suala hilo, pia umezua hofu ya kuchelewa kwa Bunge la Katiba ambalo linapaswa kufanyika mwezi ujao.
Hofu hiyo inatokana na suala la marekebisho ya sheria ambayo ilipitishwa na Bunge kutokuwamo katika ratiba ya sasa ya vikao vya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala ambayo inakutana kwa siku ya tano leo. Kamati hiyo ndiyo yenye dhamana ya kupitia na kuifanyia uchambuzi miswada ya sheria kabla ya kufikishwa Bungeni.

Juzi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliwasilisha mbele ya kamati hiyo miswada ya sheria ambayo inapaswa kupelekwa katika Mkutano wa Bunge unaotarajiwa kuanza Oktoba 29, mwaka huu lakini marekebisho ya sheria iliyozua mvutano si sehemu ya miswada hiyo. Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee alisema ikiwa marekebisho yanayokusudiwa kufanywa hayatapelekwa katika mkutano ujao wa Bunge, basi ni ishara kwamba Bunge la Katiba litachelewa.

“Bunge la Katiba haliwezi kufanyika bila sheria husika kukamilika. Kwa hiyo kama Serikali itaamua kuurejesha muswada huo bungeni lazima liwe ni Bunge hili linalofuata, tofauti na hapo utaathiri Ratiba ya Bunge la Katiba,” alisema Mdee.

Kwa upande wake, Chikawe alisema hata kama Rais ataamua kurejesha sheria hiyo Bungeni, hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi kuhusu muda wa Bunge la Katiba kwani kila kitu kitaenda kama ilivyopangwa... “Tusubiri maelekezo kwanza hakuna haja ya kuwa na wasiwasi. Kama kutakuwa na maelekezo kuna uwezekano wa kurekebisha na kila kitu kitaenda kama kilivyopangwa.

Miongoni mwa mambo ambayo yanalalamikiwa na wapinzani ni pamoja na madaraka ya Rais ya kuteua wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, kuvunjwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba baada ya kuwasilisha rasimu badala ya kuendelea kuwapo hadi kura ya maoni na utaratibu wa kufikia uamuzi katika Bunge la Katiba.

Rais Kikwete katika hotuba yake alionekana kukubaliana na baadhi ya hoja za wapinzani huku akitaka suala la Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kutofanya vikao na wadau wa Zanzibar lirejeshwe bungeni kwa lengo la kupata mwafaka wa pamoja.

Kuhusu kura katika Bunge la Katiba, Rais Kikwete alisema wingi wa wabunge wanaotoka pande za muungano siyo hoja, kwani Katiba ya sasa iko wazi kwamba masuala yote ya muungano yatapitishwa kwa kuungwa mkono na theluthi mbili ya wabunge kutoka kila upande. 

Hata hivyo, msimamo huo wa Rais unapingana na kile kilichopitishwa na Bunge ambacho ni nyongeza ya kipengele kinachoeleza kwamba, ikiwa kura zitapigwa mara mbili na jambo linalobishaniwa likakosa kuungwa mkono kwa theluthi mbili ya kura, basi suala hilo litapitishwa kwa kuangalia idadi ya kura kwa maana ya wingi pekee (simple majority).

Wakili wa kujitegemea, Alex Mgongolwa anapinga wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuteuliwa na Rais, kupendekeza ufanyike uchaguzi... “Wanatakiwa wawepo wajumbe ambao hawafungamani na upande wowote, akiwamo Rais.

CCM wabadili msimamo
Msimamo wa Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, unaonekana kuwagawa wanachama wa chama hicho wakiwamo wabunge ambao wanalaumiwa kwamba walipitisha muswada wa sheria husika kwa kuweka mbele masilahi ya chama badala ya mustakabali wa Taifa.

Msingi wa lawama hizo ni vurugu zilizotokea bungeni Septemba 6, mwaka huu na kusababisha wabunge wa Chadema, NCCR Mageuzi na CUF kususia mjadala wa sheria husika, hivyo kuwapa mwanya wenzao wa CCM.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Emmanuel Mallya alisema kitendo cha mawaziri na wabunge kupitisha muswada huo, kinaonyesha jinsi wanavyothamini masilahi ya chama chao kuliko ya taifa.

“Walipitisha muswada ule kwa kutazama zaidi Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, wao nia yao ni kuendelea kukaa madarakani. Katika suala hili, Rais lazima asimame kidete maana yeye hana cha kupoteza, ” alisema Mallya.

Wakili wa Kujitegemea, Karoli Muluge alisema mvutano uliopo sasa unatokana na muswada huo kuandaliwa na watu wa CCM, hivyo kuweka vipengele ambavyo vitakibeba chama hicho.

“Viongozi wanatakiwa kuwasikiliza wananchi na kujua kitu gani kinatakiwa kufanyiwa marekebisho katika muswada husika. Watu wasikilizwe kwa sababu wameeleza wazi upungufu uliopo,” alisema Muluge.

Katika vikao vyake vya juu, CCM kilifikia uamuzi wa kupinga mapendekezo ya Serikali tatu yaliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, uamuzi ambao ulifuatiwa na baadhi ya makada wake kuwakejeli wajumbe wa tume hiyo, akiwamo Mwenyekiti wake, Jaji Mstaafu Joseph Warioba.

Hata hivyo, Rais Kikwete katika hotuba yake alizipa kisogo kejeli hizo, pale aliposema kuwa tume hiyo ilifanya kazi nzuri, kwani ilizingatia masilahi mapana ya nchi kwa kuwasemea watu wote bila ya kubagua.

“Natambua kuwapo kwa baadhi ya watu ambao hawafurahii msimamo huo na matokeo ya kazi yao. Watu hao kuwalaumu Wajumbe wa Tume kwa ajili hiyo ni kuwaonea na kutowatendea haki. Tunataka watakaokuwa Wajumbe wa Bunge Maalumu nao waige mfano huu mzuri. Wajali masilahi mapana ya taifa letu na watu wake badala ya kujali yale ya taasisi zao au makundi yao,” alisema Kikwete.

Kauli hii inatafsiriwa kuwa ndiyo msingi wa msimamo wa CCM uliotangazwa na Katibu wake wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye ambaye alisema licha ya baadhi ya wanachama wake kuonekana kuilaumu na kuiponda Tume ya Warioba, chama chenyewe “kinaikubali na kuiunga mkono.

“CCM ina wanachama zaidi ya milioni sita, huwezi kuchukua maoni ya mmoja wa wanachama wake ukayachukulia kama msimamo wa chama. CCM kama taasisi kina msimamo wake unaotolewa na msemaji wake ambao ndiyo huu. Nakuambia sisi tunaiunga mkono Tume ya Jaji Warioba na tunaikubali.”

Wabunge wa CCM
Mbunge wa Bukoba Vijijini (CCM), Jason Rweikiza alimshauri Rais asaini muswada huo mara moja ili mchakato wa Katiba uendelee kama kawaida.
“Hawa wenzetu, wao waliamua kutoka nje ya ukumbi badala ya kukaa wakawasilisha hoja zao. Sisi tulijadili na kufuata taratibu zote, kwa hivyo Rais ana haki kabisa ya kusaini na kama kuna marekebisho atarejesha tena bungeni.

Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu alisema anaunga mkono hoja ya Rais Kikwete ya kufanyiwa marekebisho katika sheria hiyo kwani nia ni kupatikana kwa Katiba itakayosaidia nchi.

“Kama zipo hoja tuungane tuzizungumze na kuja na kitu kimoja kitakachokuwa na masilahi ya taifa. Tusivutane bila sababu za msingi, kwa sababu tunajenga nyumba moja.” Alisema wapinzani walipaswa kujenga hoja zao ndani ya Bunge badala ya kutoka nje na kususia vikao.“Sasa marekebisho yanategemea na uhitaji, sioni shida, kama Rais ameusoma na kuona kama kuna marekebisho hakuna tabu…

Sheria hizi zinatarajia utashi, kitu ambacho sisi tumetunga na kukipitisha kinaweza kuwa sahihi lakini mtu mwingine anaweza kuangalia akaona siyo sahihi,” alisema Mpina.
Imeandikwa na Tausi Mbowe, Joyce Mmasi, Fidelis Butahe na Fredy Azzah (Dar), Daniel Mjema (Moshi) na Sheilla Sezzy (Mwanza).
                                         Chanzo: Mwananchi

MWANANCHI; Tumetoka kifungoni na hamasa kubwa



Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications limited (MCL)Tido Mhando akizungumza na waandishi wa habari jijini kuhusu kuanza uchapishaji leo wa gazeti la Mwananchi lililokuwa limefungiwa kwa wiki mbili. Kulia ni Mhariri Mtendaji wa gazeti hilo Denis Msacky. PICHA | FIDELIS FELIX 

Kwa ufupi
Hatua ya kulifungia gazeti hili kwa sababu za kufikirika imesababisha maumivu kwa watu wengi. Vijana (vendors) waliokuwa wakiuza na kusambaza gazeti hili pamoja na familia zinazowategemea wameumia. Waandishi wa kujitegemea wanaolipwa kutokana na habari wanazotuma gazetini wameumia pamoja na familia zao.

Habari kamili
Hata hivyo, huu hakika sio wakati wa kumtafuta mchawi, kwa maana ya kutaka kujua nani hasa serikalini alitoa amri ya kulifungia gazeti hili kwa sababu ambazo sisi tunaona hazikuwa na chembe ya mashiko. Tulishangazwa kuona amri hiyo ya Serikali ikitolewa wakati mkuu wa nchi, Rais Jakaya Kikwete akiwa nje ya nchi, tena akiwa katika majukumu mazito ambayo dunia nzima ilikuwa ikiyafuatilia kwa shauku na umakini mkubwa.

Kulifungia gazeti wakati huo hatuoni kama ilikuwa kwa masilahi ya taifa kwa sababu hatua hiyo iliichafua taswira ya nchi yetu na bila shaka Rais Kikwete alijikuta katika wakati mgumu kila alipoulizwa kuhusu hatua hiyo iliyochukuliwa na Serikali yake.
Ni habari zipi zilizolipeleka gazeti hili kifungoni? Habari ya kwanza ilikuwa juu ya waraka kuhusu mishahara mipya ya watumishi wa Serikali ambayo tuliithibitisha pasipo kuacha shaka yoyote kutoka katika vyanzo vyetu vya habari vya kuaminika katika mamlaka za juu serikalini.

Tuliuchukulia kama taarifa muhimu sana kwa watumishi wa Serikali na wananchi kwa jumla na hatukuona sababu ya Serikali kutaka wananchi wafichwe kuhusu kuwapo kwa mishahara mipya kwa watumishi wake.

Itakumbukwa kuwa, wiki chache kabla ya gazeti hili halijachapisha habari hiyo, lilikuwa pia limechapisha habari kuhusu mishahara mipya katika sekta binafsi kwa mujibu wa waraka wa Serikali uliotolewa na Wizara ya Kazi na Ajira. Swali linalojitokeza hapa ni hili: Inakuwaje mishahara mipya ya watumishi wa Serikali iwe siri na mishahara mipya kwa sekta binafsi iwe kinyume chake?

Tunaamini kwamba utamaduni wa Serikali kuficha habari na taarifa zenye manufaa kwa umma siyo utawala bora hata kidogo. Ni hivi majuzi tu Rais Kikwete alipomwagiwa sifa na Rais Barrack Obama kwa kutia saini mkataba wa uendeshaji wa shughuli za Serikali kwa uwazi.

Habari ya pili iliyochapishwa Agosti 17 mwaka huu na kusababisha gazeti hili kufungiwa ilihusu Serikali kuimarisha ulinzi katika maeneo ya karibu na misikiti jijini Dar es Salaam jana yake kufuatia kuwapo tetesi kwamba waumini wa Kiislamu siku hiyo wangeandamana kupinga kitendo cha Jeshi la Polisi kumuweka mahabusu Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda. Baadhi ya waumini walikuwa wameonyesha kukasirishwa na kitendo cha polisi kumwondoa Sheikh Ponda katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi) na kumpeleka katika Gereza la Segerea, jijini Dar es Salaam.

Habari hiyo yenye kichwa cha habari; ‘Waislamu wasali chini ya ulinzi mkali wa polisi’ ilichapishwa ikiwa na mmoja wa mbwa waliokuwa na polisi katika doria kutokana na hofu ya kuzuka vurugu baada ya Swala ya Ijumaa, Agosti 16. 

Habari hiyo ilisema Waislamu hawakuandamana na waliswali kwa amani na utulivu na kwamba polisi hao waliokuwa na mbwa, huku wengine wakitumia pikipiki kufanya doria walitanda katika mitaa mbalimbali kwa lengo la kuimarisha ulinzi. 

Lakini kwa mshangao wetu, Serikali katika kujaribu kuhalalisha kulifungia gazeti hili ilitoa tafsiri ya uongo kwamba habari tuliyochapisha ilisema kwamba mbwa walipelekwa katika maeneo ya ibada, wakati habari hiyo haikuwa na kitu kama hicho. 

Serikali ilidai katika taarifa hiyo, kwamba lengo la habari hiyo lilikuwa kuichonganisha na waumini wa Kiislamu ili waichukie pamoja na vyombo vyake vya ulinzi na usalama, kwani kwa Waislamu mbwa ni haramu na picha hiyo iliudhalilisha Uislamu. Taarifa hiyo potofu ya Serikali imetuthibitishia pasipo kuacha shaka kwamba haikuwa na nia njema na gazeti hili.

Hatua ya kulifungia gazeti hili kwa sababu za kufikirika imesababisha maumivu kwa watu wengi. Vijana (vendors) waliokuwa wakiuza na kusambaza gazeti hili pamoja na familia zinazowategemea wameumia. Waandishi wa kujitegemea wanaolipwa kutokana na habari wanazotuma gazetini wameumia pamoja na familia zao. 

Hivyo hivyo, watoa matangazo na wasomaji waliokuwa wakilitegemea gazeti hili kwa habari za uhakika nao pia wameumia. Hasara ambayo MCL imepata kutokana na hatua hiyo ya Serikali haitamkiki.

Pengine huu ni wakati mwafaka wa kuikumbusha Serikali kwamba, gazeti hili pamoja na mengine yanayochapishwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), ni magazeti makini sana yenye waandishi wa habari wanaoheshimu maadili ya taaluma yao. Hatusemi kwamba hatuwezi kufanya makosa, kwani sisi ni binadamu.

Hata hivyo, inapotokea tukafanya makosa tunafanya masahihisho stahiki haraka kwa lengo la kupunguza maumivu kwa yeyote tuliyemkosea. Makosa ya makusudi kama kuandika habari za uongo hayavumiliki na kila mwandishi wa kampuni yetu anatambua fika kwamba kufanya hivyo ni kujitakia kiama.

MCL imeweka miongozo ya sera na malengo ya uhariri kwa waandishi. Lengo ni kuhakikisha habari zinazochapishwa ni sahihi, zinatenda haki na haziegemei upande wowote. Kwa maana hiyo, vyombo vyake vya habari vinasimamia ukweli na haki na waandishi wake wana jukumu la kuhakikisha wanakuwa na kiwango cha juu cha weledi na maadili ili kuwawezesha kutoa habari kwa umma.

Tumetoka kifungoni tukiwa na somo muhimu. Kwamba sheria kandamizi kama Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 haisimamii masilahi ya taifa, bali kundi la watu wachache. Ni sheria kandamizi ambayo kwa umoja wetu tunaweza kuifuta. Tungependa kuwashukuru wasomaji wetu na wananchi kwa jumla kwa kuwa nasi katika kipindi kigumu tulichokuwa kifungoni. Vilevile, tunavishukuru kwa namna ya pekee vyombo vyote vya habari vya ndani na nje ambavyo vilisimama imara kupinga hatua ya Serikali kufungia magazeti.

Tutakuwa watu wasio na shukurani kama hatutatambua mshikamano mkubwa ulioonyeshwa na asasi za kiraia, mabalozi na watu mbalimbali kupinga matumizi ya sheria hii kandamizi. Hatujakata tamaa, bali tumetoka kifungoni tukiwa na hamasa kubwa kuendelea kuwapa habari wananchi pasipo woga wala upendeleo.

Hatupambani na Serikali, lakini tutaendelea kuikosoa pale inapofanya makosa na tutaipongeza pale inapotimiza wajibu wake. Tunawaomba wasomaji wetu mwendelee kutuunga mkono.
                                                               Chanzo: Mwananchi

Hotuba za marehemu Baba wa Taifa sasa kupatikana kiganjani



Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiki akisisitiza jambo wakati wa uzinduzi wa huduma ya kupata hotuba za Marehemu baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliyofanyika kwenye hotel ya Double Tree jana. Ili kuweza kupata hotuba za maneno na picha za video unatakiwa kutuma neno Hotuba kwenda namba 15678, pia unaweza kupata huduma hiyo kwa kutumia www.simu.tv/nyerere mobile tv. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Push Media Mobile Freddie Manento.

Na Mwandishi Wetu
WATANZANIA watapata fursa ya kuangalia na kupata hotuba za marehemu Baba wa Taifa, Julius Kambarage Nyerere kupitia mpango ulioanzishwa na taasisi ya Mwalimu Nyerere Foundation kwa kushirikiana na kampuni ya Push Mobile Media.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Foundation, Joseph Butiku alisema kuwa wameamua kuanzisha mpango huo ili kuwawezesha watanzania, waafrika na dunia kwa ujumla kujua kazi alizozifanya marehemu Baba wa Taifa kwa jamii.

Butiku Alifafanua kuwa ili kuweza kupata hotuba hizo kupitia simu ya mkononi unatakiwakutuma neno Hotuba kwenda namba 15678 . Vile vile unaweza kupata picha nyingi zaidi kwa kuingia www.simu.tv/nyereremobile tv.

Alisema kuwa mpango huo upo kwa njia ya CD na DVD ambazo watanzania wengi wameanza kuzichangamkia kupata nakala.

"Huu ni mpango maalum wa kuhakikisha kumbukumbu za marehemu baba wa Taifa zinapatikana kiganjani na muda wowote, tumeingia makubaliano maalum na kampuni ya Push Media Mobile ili kuendeleza juhudi hizi za kuenzi enzi zake," alisema Butiku.
Alisema kuwa marehemu Mwalimu amefanya kazi kubwa za kuelimisha kwa kutunga vitabu mbali mbali ambavyo vingi vimekuwa vikutumika kusaidia mambo mbali mbali ya kisiasa na uchumi.

"Nakumbuka alisema kuwa mawazo haya yapo kwenye vitabu na kanda mbali mbali, yatumike katika kuchangia maendeleo ya binadamu, alikuwa mwangalifu sana kwani yamezingatia hali halisi ya jana na leo, natoa ushauri kwa watanzania kutumia mpango huu ili kusaidia taifa," alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Push Mobile Media Freddie Manento alisema kuwa wameingia makubaliano na Taasisi ya Mwalimu Nyerere na lengo kubwa ni kurahisisha kupatikana busara za Mwalimu kwa watanzania wote, ikiwa pamoja na vizazi vya sasa.
Manento alisema kuwa huduma hii moja ya njia ya kuendelea kumkumbuka Marehemu Baba wa Taifa ambaye pia ni muasisi wa Taifa hili.

Alisema kuwa sababu nyingine ya kuanzisha huduma hiyo ni kuwakumbusha Watanzania, Waafrika na dunia kwa ujumla busara zake na hasa kwa njia ya hotuba zake ambazo si za kawaida kwani bado zinaendelea kuzungumzia mambo mbali mbali yanayotokea sasa.

Aliongeza kuwa mpango huo pia utaendeleza njia nyingine za kuenzi heshima ya marehemu Baba wa Taifa katika mchango wake wa kulikomboa taifa hili na mpiganaji wa haki za binadamu duniani.

Alisema kuwa hakuna asiyejua kuwa marehemu Baba wa Taifa ni mkombozi wa haki za wanyonge na alikuwa mstari wa mbele katika kupigiania Uhuru wa Tanzania na mataifa mengine katika bara la Afrika.

Alisema kuwa mchango wake hauwezi kusaulika na vizazi vilivyopo wakati wa uhai wake na vizazi vipya vitakuwa na hamu kubwa ya kupata falsafa zake kupitia hotuba mbali mbali ambazo zimekuwa zikitumika katika nyanja nyingi hapa nchini.

"Ili kurahisisha upatikanaji wa hotuba hizo, tumeamua kushirikiana na Taasisi ya Mwalimu Nyerere Foundation na kuanzia sasa, unatweza kupata hotuba yake kwa njia ya televisheni na kwa njia ya meseji kwa kupitia simu ya mkononi na kuendelea kumuenzi marehemu Baba wa Taifa," aliongeza.

Alisema kuwa huduma hii ni ya mara ya kwanza kutokea hapa nchini ambapo Watanzania watapata fursa ya kuona na kusoma hotuba ya marehemu baba wa Taifa kwa njia ya mtandao wa simu ya mkononi.
Chanzo: Mjengwablog

Gazeti la “Mwananchi” kuingia mtaani Leo oktoba 11



Kampuni ya Mwananchi Communications Limited, wachapishaji na wauzaji wa magazeti ya MWANANCHI, MWANASPOTI, na THE CITIZEN leo imetoa ufafanuzi katika mambo mawili, kuhusiana na tukio lililotokea hivi karibu. Kwanza ni gazeti lake mama la MWANANCHI ambalo halikuchapishwa wala kuuzwa kwa takribani majuma mawili kwa agizo la serikali. Kuhusiana na hilo, wamechukua fursa na kuongelea kuhusu KUREJEA KWA UCHAPISHWAJI WA GAZETI HILO na KUUSHUKURU UMMA kwa kuwa nao bega

KUREJEA KWA UCHAPISHAJI WA GAZETI
Kwa mujibu wa agizo la Serikali, kutochapishwa kwa gazeti la Mwananchi kunakwisha leo, na kuanzia kesho tarehe 11.10.2013 gazeti litakuwa mitaani kama kawaida. Kwa hiyo kuanzia kesho wasomaji wa gazeti hilo maarufu wataendelea kupata gazeti lenye habari za uhakika zinazojikita kwenye umahiri, uhuru, na weledi wa uandishi na uhariri.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Bw Tido Mhando, magazeti hayou yataendelea kusambazwa nchi nzima na kufika mapema kabisa kote, kupitia kwa mawakala na wauzaji wake walioenea kote Tanzania.

Kwa wapenzi wa gazeti la Mwananchi waliopo jijini Dar es Salaam, kesho watauziwa magazeti na waandishi wa gazeti hilo ambao kuanzia asubuhi watakuwa mtaani wakisherehekea uhuru wao kwa kukutana na wasomaji wao moja kwa moja.

PROMOSHENI YA CHOMOKA NA MWANANCHI
Kutochapishwa kwa gazeti la MWANANCHI kwa majuma mawili kulisababisha ile promosheni ya CHOMOKA NA MWANANCHI isimame kwa muda huo huo. Tido alichukua Fursa kuwajulisha wasomaji wake kwamba promosheni hii sasa inarudi tena na inaendelea kuanzia ilipokuwa imekomea.

Zawadi za shilingi milioni moja kila siku, na zawadi za magari mapya, zitaendelea kushindaniwa na kutolewa ili kutimiza ile ahadi yetu ya kutoa zawadi zenye thamani ya jumla ya shilingi 250,000,000/=.



PICHANI JUU:Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited(MCL)Tido Mhando akizungumza na waandishi wa habari jijini kuhusu kuanza uchapishaji leo wa gazeti la Mwananchi lililokuwa limefungiwa kwa wiki mbili.

Mkurugenzi wa Mwananchi, Tido Mhando akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (Hawapo pichani) kuhusiana na kuanza kwa uchapishwaji wa gazeti hilo.
 

Thursday, October 10, 2013

TIDO MHANDO; Mwananchi haitarudi nyuma katika utendaji wake, Litaendelea kusimamia haki sheria na ukweli daima.

                                  
Tido Mhando


Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya kuchapisha magazeti ya mwananchi Bw Tido Mhando amesema licha ya kufunguiwa na serikali kwa kipindi cha wiki mbili haitarudi nyuma katika utendaji wake na kuahidi kuendelea kusimamia haki sheria na ukweli daima.

Mkurugenzi huyo ameyasema hayo alipokutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam akiwa kaambatana na mhariri mtendaji wa gazeti la Mwananchi Bw Denis Msaki ambapo amesema kwa kipindi cha majuma mawili wamepata hasara ya zaidi ya shilingi milioni 400.
Chanzo: ITV DAIMA

Chuji awekewa ulinzi wa kutisha Bukoba



BENCHI la Ufundi la Kagera Sugar, limeweka wazi kuwa limemwandalia ulinzi mkali kiungo wa Yanga, Athuman Iddi ‘Chuji’ wakati timu hizo zitakapocheza Jumamosi mjini Bukoba.

Yanga ambayo inasafiri leo Alhamisi kuelekea Bukoba ikiwa na kiungo wake Haruna Niyonzima aliyeunguliwa na nyumba yake hivi karibuni, imecheza mechi mbili nje ya Dar es Salaam dhidi ya Mbeya City na Prisons. Zote ilitoka sare ya bao 1-1.

Kocha Msaidizi wa Kagera Sugar, Mlage Kabange, aliliambia Mwanaspoti kuwa: “Tahadhari yetu kubwa ambayo tutaingia nayo kwenye mchezo huo ni kuhakikisha Chuji (Athuman) hatembei.

“Kuna vijana watatu wameandaliwa kwa ajili ya kufanya kazi hiyo ya kumwekea ulinzi mkali na kuhakikisha hapati nafasi ya kupiga zile pasi zake kwa (Mrisho) Ngassa wala (Simon) Msuva.

“Tunaamini kwa kufanya hivyo Yanga hawatatembea kabisa. Chuji amekuwa akitumika sana kuwachezesha Ngassa na Msuva, hata ukiangalia mechi walizoshinda mipira mingi imekuwa ikianzia kwake.”

Alifafanua kuwa wameifuatilia Yanga na kugundua inatengeza mashambulizi yake kupitia winga za kulia na kushoto ikiwatumia Ngassa na Msuva.
“Hata ukifuatilia matokeo yao katika ushindi wa mechi mbili zilizopita dhidi ya Ruvu na Mtibwa utabaini hilo. Chuji amekuwa akiwachezesha vizuri Ngassa na Msuva, lengo letu kumwekea Chuji ulinzi wachezaji watatu ni kwamba Ngassa pamoja na Msuva wasipate mipira, nafikiri tukifanikiwa kwa hilo tutakuwa tumewamaliza kabisa.”

Hata hivyo, Kabange amegoma kuweka hadharani majina ya wachezaji walioandaliwa kwa ajili ya shughuli hiyo.
“Hatuwezi kuwataja majina, nafikiri hii ni kama vita, huwezi kumpa mpinzani wako mbinu zako,” alisema.

Yanga itakuwa ikicheza kwenye Uwanja wa Kaitaba huku ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza msimu uliopita ingawa ilisawazisha makosa hayo na kulipa kisasi kwenye mchezo wa marudiano jijini Dar es Salaam.
Bao la Kagera likifungwa na Themi Felix wakati Nizar Khalfan akifunga la Yanga.
Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

CHICHARITO ATAJA SABABU KWA NINI ATAONDOKA MAN U



MSHAMBULIAJI Javier Hernandez amesema anaweza kuondoka ManchesterUnited ili kusaka timu ambayo atapata nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza. 


Mshambuliaji huyo anayefahamika kama Chicharito hapewi nafasi kubwa katika klabu ingawa mwezi uliopita aliifungia timu hiyo bao la ushindi katika Kombe la Ligi, maarufu kama Capital One dhidi ya Liverpool na zaidi ya mechi hiyo alianza katika mechi nyingine moja tu, United ikifungwa nyumbani na West Brom.

Hernandez amesema kwamba wakati akiwa ana furaha kuchezea klabu kubwa kama hiyo, pia anataka nafasi zaidi za kucheza na anaamini anaweza kuwa nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza iwe Old Trafford au katika klabu yoyote.

"Nasotea hiyo [kuanza katika mechi zaidi],"alisema Hernandez akihojiwa na kituo cha Televisheni cha Mexico, Deportes Telemundo.
"Nafanyia kazi hilo- kupata nafasi kikosi cha kwanza. Nafahamu kwamba kiwango changu uwanjani kitaniruhusu kutimiza lengo hilo siku fulani, aidha hapa [Manchester] au popote katika klabu yoyote.

"Naelekea kutimiza miaka minne hapa [Manchester United] na kweli, kama ambavyo wakati wote nimesema, nina furaha kuwa tayari nimechezea moja ya klabu bora duniani, nafanya vizuri kila siku kutafuta muda zaidi uwanjani,".

"Nahitaji kupewa nafasi zaidi kuonyesha uwezo wangu, kwa sababu kati yetu sote tunataka kutoa mchango wetu ili hii timu ishinde ubingwa,".
Hernandez amekuwa akisotea namba kikosi cha kwanza United kutokana na kuzidiwa kete na akina Wayne Rooney, Robin van Persie na Danny Welbeck, lakini Mmexico huyo amesema hiyo inaweza kuwa nzuri kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu England.

"Ushindani ndani ya timu wakati wote umekuwa mkubwa na ninafikiri hiyo inaisaidia timu kwa kiasi kikubwa, kwa sababu kuna wachezaji wengi bora ambao kila mmoja kati yao anataka nafasi kikosi cha kwanza,".

"Mazoezi na mechi zinazokuja zitatulazimisha kusimama imara kuisaidia timu kuimarika kwa vyote, kwa uchezaji binafsi na kitimu kwa ujumla,".
Chanzo: sportmail

BERGKAMP ATAKA KUREJEA ARSENAL KUPIGA KAZI



GWIJI wa Arsenal, Dennis Bergkamp ameelezea nia yake ya kujiunga na dawati la makocha la timu ya Arsene Wenger.


Mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 44 alunga mabao 87 katika miaka yake 11 ya kuchezea Arsenal na amesema klabu hiyo ina nafasi maalum moyoni mwake.
Robert Pires amekuwa akisaidia kuendesha mazoezi katika Uwanja wa Gunners, London Colney na Bergkamp, ambaye aliichezea timu hiyo kuanzia mwaka 1995 hadi2006, anaweza kuungana naye.

"Hisia alizonazo Johan Cruyff kwa Barcelona, nami ninazo hizo hizo kwa Arsenal," Bergkamp aliiambia Telegraph.
"Nikiwa Arsenal ilikuwa babu kubwa. Wakati wote nafurahia. Sijawahi kuwa na siku mbaya humo. Ipo katika fikra zangu wakati wote. Ni sehemu ya malengo yangu kurejea huko.

"Naona kama naweza kuwa sehemu ya makocha. Nafurahia hiyo kazi, hususan kufundisha vitu binafasi kwa washambuliaji,".
Bergkamp alijipatia sifa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kucheza soka, ubunifu na maarifa ya kisoka alipokuwa Arsenal.

Mchezaji mpya ghali wa Arsenal, Mesut Ozil amekuwa akifananishwa na Mholanzi huyo, lakini mchezaji huyo wa zamani wa Uholanzi amesema kila mchezaji ni wa kipekee.
Sasa akiwa kocha Msaidizi wa Ajax, Bergkamp amevutiwa na mwanzo mzuri wa Arsenal msimu huu na kusema Ozil ni kipaji maalum.

"Pamoja na heshima zangu zote kwa wachezaji wengine wote wa Arsenal, nafikiri ni mmoja ambaye anaweza kutengeneza tofauti,"alisema.
"Wachezaji wengine ni wazuri katika kiungo. Lakini unahitaji mtu mmoja fulani wa kiwango cha juu ambaye anaweza kuhaha Uwanja mzima,". 
Chanzo: binzubeiry



Obama ataka suluhisho la bajeti haraka



 Rais Obama amesema yuko tayari kuzungumza na wajumbe wa chama cha Republican kuhusu kitu chochote, lakini baraza la wawakilishi linatakiwa kwanza lipitishe mswaada kuzifungua tena shughuli za serikali.


Rais wa Marekani, Barack Obama, ameonya kwamba viongozi wa dunia wana wasiwasi wabunge wa chama cha Republican nchini humo huenda wakauvuruga kabisa uchumi wa taifa na kuapa kutotetereka katika msimamo wake wa kutaka kiwango cha fedha Marekani inazoweza kukopa kulipa madeni yake kiongezwe bila masharti yoyote.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari katika ikulu yake mjini Washington hapo jana, rais Obama amewataka wabunge wa chama cha Republican waache vitisho na waupigie kura muswaada wa sheria kuidhinisha fedha kwa ajili ya serikali, ambao ikiwezekana huenda ukapitishwa leo.

"Baraza la wawakilishi linatakiwa kupiga kura leo. Kama wanasiasa wa chama cha Republican na spika Boehner wanasema hakuna kura za kutosha. Basi wanatakiwa wathibitishe. Acha muswada upigiwe kura halafu tuone kitakachotokea. Wasiwasi wangu mkubwa ni kwamba kuna kura za kutosha."

Boehner akataa kujisalimisha bila masharti
Spika wa bunge la Marekani, John Boehner, amesisitiza hakutakuwa na 'kujisalimisha bila masharti' kwa chama cha Republican. Boehner amesema bunge litairuhusu Marekani ikope fedha zaidi kama rais Obama atakubali kubana matumizi. Hata hivyo kulikuwa na ishara ya matumaini ya kuutanzua mgogoro mkali wa bajeti ambao umesababisha baadhi ya shughuli za serikali kufungwa kwa zaidi ya wiki moja na hivyo kuibua hofu kwamba Marekani huenda ikashindwa kulipa madeni yake kama kiwango hicho hakitaongezwa kufikia tarehe 17 mwezi huu.

Obama amesema kukiwa na haja atakubali makubaliano ya muda mfupi kuongeza kiwango cha fedha serikali inazoweka kukopa na kufungua tena shughuli zilizofungwa, hatua ambayo itauahirisha mkwamo huo kwa wiki kadhaa. Wakati huo huo, rais Obama amewashutumu wabunge wa chama cha Republican kwa kuutumia mkwamo wa bajeti kama chombo cha shinikizo kwa lengo la kuyahujumu mageuzi ya bima ya afya.

Wachambuzi wanasema hiyo ni mbinu mpya ya chama cha Republican kumbana Obama. Mwanauchumi Steven Ricciuto anasema, "Nadhani huo utakuwa mkakati wa chama cha Republican ambao kwa kiwango fulani unaweza kukubalika na Wamarekani; kwamba hupaswi kushindwa kulipa madeni. Lakini katika miswaada yote ya bajeti huenda kuna masharti yaliyofungamanishwa, ambayo huenda yakauendeleaza mkwamo uliopo."

Lakini rais Obama ameshikilia msimamo wake kwamba katu hatokubali makubaliano yoyote kuhusu kukakataa kuzikubali nadharia za chama cha Republican ili apate mamlaka zaidi kukopa fedha kugharamia kifedha majukumu ya Marekani. 

Obama amesema bunge lina kazi mbili za msingi - kupitisha bajeti na kuhakikisha Marekani inalipa madeni yake. Ameonya kwamba wabunge hawakudai walipwe fidia na kusisitiza msimamo wake kuwa atafanya mazungumzo na Warepublican mara tu kiwango cha fedha kitakapoongezwa na shughuli za serikali zilizofungwa zitakapofunguliwa.

Spika Boehner alijitokeza kwenye televisheni muda mfupi baada ya Obama kumaliza mkutano wake na waandishi wa habari na kusema mazungumzo yatafanyika. Spika huyo pia ameukosoa msimamo wa Obama akisema sivyo serikali ya Marekani inavyofanya kazi. Obama ambaye alizungumza na Boehner hapo kabla kwa njia ya simu, anahoji kuongeza kima cha fedha serikali inazoweza kukopa ni muhimu kwa uaminifu wa taifa hilo kuweza kukopa fedha na hakupaswi kuvurugwa na wasiwasi wa kisiasa.

Mwanamke wa kwanza kuingoza benki kuu ya Marekani
Wakati mzozo wa bajeti ukiendelea, rais Obama leo atamteua Janet Yellen kama mwanamke wa kwanza kuiongoza benki kuu ya Marekani. Obama atampendekeza Yellen kwa awamu ya miaka minne kuchukua mikoba kutoka kwa Ben Bernanke, ambaye sera zake za miaka minane zilihusishwa na kukabiliana na mzozo wa kiuchumi ulioikabili dunia na kutafuta njia za kuufufua uchumi.

Afisa wa Marekani amesema tangazo hilo litafanywa katika ikulu ya Marekani leo usiku katika tukio litakalohudhuriwa na Bernanke, na hivyo kufungua mlango kwa mchakato wa kuthibitishwa katika nafasi hiyo. Yellen, mwenye umri wa miaka 67, amekuwa akishikilia nafasi ya pili ya uongozi wa benki hiyo.

Yellen alizaliwa New York na ameolewa na mshindi wa tuzo ya uchumi ya Nobel, profesa George Akerlof na ni mama wa profesa wa uchumi, Robert Akerlof. Alisomea uchumi katika chuo kikuu cha Brown na baadaye katika chuo kikuu cha Yale, ambako alipata shahada yake ya uzamili. Yellen amekuwa profesa katika chuo kikuu cha Havard na hivi karibuni katika chuo kikuu cha California, Berkeley, ambako mume wake pia hufundisha na kufanya utafiti.

Mwandishi: Josephat Charo



Rais Morsi kufunguliwa mashtaka Novemba



Aliyekuwa Rais wa Misri Mohammed Morsi aliyeng'olewa mamlakani atafunguliwa mashtaka mwezi Novemba tarehe nne.
Bw Morsi atashatakiwa kwa kosa la uchochezi na mauaji pamoja na wanachama kumi na wanne wa kundi Muslim Brotherhood.

Mashtaka hayo yanahusiana na mauaji ya waandamanaji saba wakati wa vurugu kati ya wafuasi wa upinzani na wafuasi wa Muslim Brotherhood nje ya ikulu ya rais mjini Cairo mwaka uliopita.

Kupinduliwa kwa bwana Morsi kumesababisha maandamano ya kupinga na kumuunga mkono kutoka kwa wafuasi na wapinzani na wafuasi wake na baadhi wameuawa na vikosi vya kijeshi.

Morsi atashtakiwa na viongozi wengine kumi na wanne wa vuguvugu la Brotherhood.
Amekuwa akizuiliwa katika eneo lisilojulikana tangu alipoondolewa mamlakani tarehe 3 mwezi Julai.

Mamia ya watu wanataka arejeshwe mamlakani na wengi wao wakiwa wafuasi wa vuguvugu la Brotherhood. Wengi wa wafuasi hao wameuawa kwenye makabiliano na vikosi vya usalama tangu Morsi alipong'olewa madarakani.

Zaidi ya watu hamsini walifariki kutokana na ghasia hizo siku ya Jumapili.
Mahakama ya rufaa mjini Cairo iliamua kuwa Morsi na wenzake 14 akiwemo Mohammed al-Beltagi na Essam al-Erian, wanaweza kufunguliwa mashtaka katika mahakama ya uhalifu.

Wendesha mashtaka walitangaza kuwa mwezi jana walifunguliwa mashtaka ya uchochezi kuhusiana na ghasia nje ya ikulu ya Rais mjini Cairo.