Friday, November 1, 2013

Polisi mbaroni kwa kupora Sh220 mil



Moshi. Askari polisi wawili wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), wametiwa mbaroni kwa tuhuma za kula njama na kushiriki katika uporaji wa Sh220 milioni za Kampuni ya Dot Services ya mjini Moshi.

Habari za uhakika zilisema baada ya kubanwa na makachero, askari hao walirejesha Sh60 milioni na watuhumiwa wengine wawili ambao ni raia, walirejesha Sh23 milioni. Askari hao ni wale walioko katika Kikosi cha Polisi wa doria wanaotumia pikipiki na jana watuhumiwa wote walitawanywa katika vituo mbalimbali ili wahojiwe kwa nyakati tofauti tofauti.

Habari za kipolisi zilisema askari hao hawakwenda eneo la tukio lakini walifahamu mpango mzima kuhusu uporaji huo uliowawezesha kupata mgawo wa fedha hizo.
Waliotiwa mbaroni wana vyeo vya Constable (majina tunayo) na inaelezwa kuwa tukio hilo limewachukiza baadhi ya polisi wakidai ni kuwa mfululizo wa matukio yanayochafua sura ya jeshi hilo.

Habari hizo zimebainisha kuwa tukio hilo ni mpango mahususi uliowashirikisha watu wasiopungua 10 wakiwamo baadhi ya watumishi wa Kampuni ya Dot Services waliovujisha mpango wa kuhamisha fedha hizo.
Kulingana na vyanzo vya habari, idadi ya walioshiriki katika mpango wa kupora fedha hizo ni kati ya watu wanane na 10 na tayari polisi wameanzisha msako mkali wa kuwatafuta.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa Kilimanjaro, Robert Boaz alikaririwa akisema kuwa fedha hizo ziliporwa Jumanne asubuhi katika makutano ya Barabara za Arusha na Boma mjini Moshi.
Kwa mujibu wa Kamanda Boaz, baada ya kufika katika makutano hayo, wafanyakazi wa Kampuni ya Dot Services waliokuwa na gari aina ya Toyota Hilux T.864 AZM walisimama kuruhusu pikipiki ipite.

Kamanda Boaz alisema wakati wakisubiri pikipiki ipite, ghafla walijitokeza watu wawili wakafungua milango na kuingia ndani ya gari na kuwateka wafanyakazi na kuwaamuru waelekee eneo la Shanty Town.

Hata hivyo mkurugenzi wa Fedha wa kampuni hiyo ya ujenzi yenye makao yake makuu nchini Uganda, Shuresh Bab alifanikiwa kuruka kwenye gari hilo na kutoa taarifa polisi.
Kamanda Boaz alifafanua kuwa msako wa kuwatafuta wahusika ulianza mara moja ambapo polisi walifanikiwa kulipata gari hilo na wafanyakazi wakiwa wametelekezwa mto Karanga mjini Moshi.
Chanzo: Mwananchi


Ripoti yaonyesha wizi wa fedha wa kutisha



Benki Kuu ya Tanzania.PICHA|MAKTABA
Na Florence Majani, Mwananchi

Kwa ufupi
Ripoti hiyo ya Uhalifu wa Kiuchumi ya mwaka 2013 iliyotolewa na Kampuni ya Uchunguzi wa Huduma ya Delloite imebaini kuwa watendaji wa ngazi za juu wanahusika zaidi na uhalifu huo ukilinganisha na watendaji wa ngazi za chini.
Dar es Salaam.Taasisi za Fedha nchini zimepoteza kiasi cha Sh34.4 bilioni kuanzia kipindi cha Oktoba mwaka jana hadi Oktoba mwaka huu kutokana na wizi wa fedha katika taasisi hizo,ripoti mpya imebainisha.

Utafiti huo uliofanyika katika nchi za Kenya,Tanzania na Uganda umebainisha kuwa,Taasisi za Fedha za Afrika Mashariki zimepoteza zaidi ya Sh471 bilioni sawa na (USD 30 milioni) kwa mwaka.

Hata hivyo benki hizo ziliweka wazi upotevu wa Sh126.9 bilioni tu ambao ni robo ya upotevu huo wa zaidi ya Sh471 bilioni kwa kile kinachodaiwa kuhofia kupoteza wateja.
“Taasisi za fedha zinapoteza fedha nyingi kutokana na teknolojia na watendaji wa ngazi za juu kuhusika kwa kiwango kikubwa lakini hazitaki kukiri kwa sababu ya kuhofia kukosa wateja,” alisema Robert Nyamu, Mkurugenzi wa Delloite, Afrika Mashariki.

Msemaji wa Benki Kuu ya Tanzania,Loy Nabeta hakuwa tayari kuzungumzia upotevu huo na kusema kuwa ni suala linalohitaji majadiliano ya kina na utendaji wa ngazi za juu.
Wimbi la wizi wa fedha katika benki lilianza kupata umaarufu mwaka 2010 na Oktoba 2012 hadi Februari 2013, inakadiriwa kuwa jumla ya Sh700 milioni zimeibwa katika benki mbalimbali kwa nyakati tofauti.

Ripoti hiyo ya Uhalifu wa Kiuchumi ya mwaka 2013 iliyotolewa na Kampuni ya Uchunguzi wa Huduma ya Delloite imebaini kuwa watendaji wa ngazi za juu wanahusika zaidi na uhalifu huo ukilinganisha na watendaji wa ngazi za chini.
“Wanapofanya uhalifu hujua namna ya kuuficha na kuujadili na wasimamizi wa ndani bila kubainika.Wanajua mbinu na mifumo yote ya kifedha na wanatumia fursa hiyo kuiba,” alisema Nyamu.

Watendaji waliotajwa kuhusika zaidi na wizi huo wa fedha ni wale wa ngazi za juu wakiwamo wakurugenzi watendaji, ofisa operesheni, wakurugenzi wa fedha, vitengo vya teknolojia na wakuu wa vitengo wanatumia nafasi zao kufanya uhalifu wa fedha ukilinganisha na wafanyakazi wa kati na ngazi za chini.

Wizi unaofanyika zaidi katika nchi za Afrika Mashariki unatajwa kuwa ni wa fedha halali ambao ni zaidi ya asilimia 70 ya uhalifu wa aina zote wa kifedha.
Hata hivyo Nyamu alisema watendaji wa ngazi za chini wanaweza kufanya uhalifu wa kiasi kikubwa cha fedha iwapo wanajua namna ya kufanya hivyo.

Mtaalamu wa Uchumi na Mhadhiri wa Chuo cha usimamizi wa Fedha(IFM), Dk Eliamani Sedoyeka alisema ni kweli kuwa watu wa ngazi za juu wanatumia nafasi zao kufanya uhalifu wa kifedha kwa sababu wanaelewa kwa undani mfumo unavyofanya kazi na kutolea mfano i wizi wa Benki ya Stanbic .


Chanzo: Mwananchi

Mugabe anaweza 'kutusiwa' au kukosolewa



Watu kadhaa wameshitakiwa nchini Zimbabwe kwa kumtusi Rais Robert Mugabe
Mahakama ya kikatiba nchini Zimbabwe imebatilisha sheria inayosema kuwa ni uhalifu kumtusi Rais wa nchi.

‘‘Viongozi wa mashitaka hawapaswi kuwa na tamaa sana ya kuwashitaki watu wanaomkosoa Rais Mugabe katika kumbi za ulevi na maeneo mengine ya kijamii,’’ iliamua mahakama ya kikatiba.

Angalau watu 80 wameshitakiwa chini ya sheria hiyo katika miaka ya hivi karibuni.
Mnamo mwezi Mei, mwanaharakati Solomon Madzore alikamatwa baada ya kudaiwa kumuita Mugabe 'Punda anayechechemaa.'

Alikanusha kosa la kumtusi Rais.
Chini ya kifungu cha 33 cha sheria ya uhalifu nchini Zimbabwe, mtu anaweza kufungwa jela hadi mwaka mmoja au kutozwa faini ya dola 100 kwa kumtusi Rais.
Sheria hiyo ilipingwa na watu kadha nchini humo akiwemo mkaazi mmoja wa mji wa Bulawayo Kusini mwa nchi, Tendai Danga, aliyekamatwa miaka miwili iliyopita kwa madai ya kumtusi Mugabe wakati alipozozana na polisi ndani ya baa.

Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC mjini Harare, Brian Hungwe, majaji tisa waliotoa uamuzi huo, walikubaliana kwa kauli moja kuwa sheria hiyo inahujumu uhuru wa kujieleza na kuifanya vigumu kwa serikali kukata rufaa dhidi ya uamuzi wao.
Hata hivyo, mahakama hiyo ilimpa waziri wa sheria, Emmerson Mnangagwa hadi tarehe 20 Novemba kukata rufaa.

Mwezi Agosti mahakama ilimwachilia huru mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 26 Takura Mufumisi, aliyeshitakiwa kwa kuwa na nia ya kutumia bango la karatasi lenye picha ya Mugabe kama karatasi ya kujipangusia chooni ndani ya baa moja.
Katika kura ya maamuzi iliyofanyika mwezi Machi, wananchi walipitisha katiba mpya ambayo inawapa uhuru zaidi wa kujieleza.

Watu wengi wamepongeza uamuzi wa mahakama wakiamini kuwa sheria ilikuwa imemlinda rais dhidi ya kukosolewa.
Chanzo: BCSwahili

Wakamatwa kwa kashfa ya ARV's A. Kusini



Maafisa wawili wa afya nchini Afrika Kusini wamekamatwa baada ya kuwauzia wagonjwa dawa za kupunguza makali ya Ukimwi.
Kwa mujibu wa polisi, dawa hizo hazipaswi kuuzwa bali hutolewa bila malipo kwa waathiriwa wa virusi vya HIV katika hospitali za umma.

Polisi wa kitengo maalum, walifanya uchunguzi baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wagonjwa.
Wanaume hao watashitakiwa kwa makosa ya wizi na kupatikana na dawa zinazopaswa kutolewa bure kwa wagonjwa.

"Wagonjwa walilazimika kutoka hospitalini bila dawa katika hospiali ya Esselen baada ya kuambiwa kuwa hakuna dawa za ARV. Kisha baadaye walishauriwa na maafisa wawili wa afya waliowaambia kuwa wanaweza kuwauzia dawa hizo,’’ shirika la habari la Sapa lilimnukuu msemaji wa kitengo hicho maalum cha polisi, kapteni Paul Ramaloko.
Bwana Ramaloko alisema kuwa washukiwa walikuwa wanauza dawa hizo kwa dola sita kwa boxi moja ndogo na waliwambia wagonjwa kuwa dawa hizo zilikuwa zimehifadhiwa kwa wakati wa dharura.

Maafisa hao watafikishwa mahakamani Ijumaa. Uchunguzi ulianza mnamo mwezi Mei na kukamilishwa Septemba.
Mwandishi wa BBC mjini Johannesburg amesema kuwa ukubwa wa operesheni ya polisi dhidi ya madai hayo haujulikani wala ukubwa wa kashfa hiyo.

Wanaume hao, walikamatwa Jumatano, baada ya kuwauzia dawa maafisa wa ujasusi.
"Wale waliokamatwa lazima wakabiliwe na sheria kwa vitendo vyao," alisema Simon Zwane, msemaji wa idara ya afya katika mkoa wa Gauteng,’’ liliripoti gazeti la Sapa.
Afrika Kusini ni moja ya nchi zenye idadi, kubwa ya waathiriwa wa virusi vya HIV duniani na maafisa wa afya nchini humo wanasema kuwa ina mpango mkubwa zaidi wa kutoa dawa za ARV duniani.
Chanzo: BBCSwahili

ICC yaahirisha kesi dhidi ya Rais Kenyatta



Uamuzi huu umetolewa huku AU ikifanya juhudi za kidiplomasia kutaka kesi hiyo kuahirishwa kwa mwaka mmoja

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC imeahirisha kesi ya rais wa Kenya Uhuru Kenyatta katika mahakama hiyo hadi tarehe 5 mwezi Februari mwaka 2014.
Uamuzi huo umefikiwa hii leo ikiwa siku moja kabla ya upande wa mashitaka kuashiria kuwa hawatapinga ikiwa kesi hiyo kuahirishwa kwa mwaka mmoja hadi Novemba mwaka 2014

Pia unakuja huku juhudi za kidipmolasia za viongozi wa Afrika kushinikiza baraza la usalama la Umoja wa Mataifa zikishika kasi kulitaka baraza hilo kukubali kesi dhidi ya Rais Kenyatta na naibu wake William Ruto kuakhirishwa.
Rais Kenyatta alikuwa ameiomba mahakama hiyo kuakhirisha kesi dhidi yake hadi Februari mwaka ujao huku upande wa mashitaka ukitaka ukahirishaji kutozidi Februari tarehe tatu mwaka 2014.

“Majaji wamekubaliana na upande wa mashitaka kuahirisha kesi dhidi ya Rais Kenyatta hadi Februari mwaka 2014 ili kuupatia upande wa mashitaka muda wa kutosha kufanya uchunguzi zaidi kutokana na tuhuma dhidi ya upande wa mashitaka kutoa taarifa zisizo za kweli, '' majaji walisema katika uamuzi wao.

Upande wa utetezi nao ulitaka tarehe ya kesi hiyo kuahirishwa ili majaji waweze kushughulikia baadhi ya malalamiko yao, kuhusu Kiongozi wa mashitaka kuhujumu mfumo wa kesi dhidi ya Kenyatta. Malalamiko hayo waliyawasilisha Oktoba tarehe kumi na kuwasilisha ombi la kutaka kesi dhidi ya Rais Kenyatta kufutiliwa mbali.
Chanzo: BBCSwahili