Thursday, October 31, 2013

Operesheni dhidi ya ujangili iungwe mkono



Kwa wiki kadhaa hapa nchini inaendeshwa operesheni ya kupambana na ujangili wa tembo na wanyama wengine chini ya kikosi maalumu kinachoundwa na maofisa kutoka katika vyombo vya dola, maarufu kwa jina la Operesheni Tokomeza.

Taarifa mbalimbali zimekuwa zikiripotiwa kuhusiana na utekelezaji wa majukumu ya kikosi hiki, ikiwamo watu mbalimbali kukamatwa wakidaiwa kuhusika na ujangili, hasa wa meno ya tembo, uhalifu ambao kwa siku za karibuni umeichafua sana nchi yetu kimataifa.

Watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa umma na wa kisiasa wamekamatwa katika maeneo ya Serengeti, Ngorongoro, Arusha, Ruaha, Iringa, Mahenge, Maswa, Meatu na kwingineko ambako pia, ushahidi wa aina tofauti umepatikana kuhusiana na vitendo vya ujangili.

Kukamatwa kwa watuhumiwa katika maeneo yote hayo ni ushahidi kwamba majangili wana mtandao mpana unaotumia nguvu za kifedha, kisiasa au za ulinzi wa dola kujiimarisha katika maeneo mengi ya nchi, na kuendelea kuhujumu maliasili za taifa.
Hata hivyo, pamoja na lengo zuri la operesheni hiyo, yapo madai ya kikosi hicho kutumia mabavu na ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwamo kupiga watu ovyo, kujeruhi na hata kuua watu kadhaa wanaotuhumiwa kujihusisha na ujangili.

Pamoja na kwamba malalamiko dhidi ya operesheni hiyo yanatakiwa kushughulikiwa na ukiukwaji huo wa haki za binadamu kukomeshwa, madai hayo yanatakiwa kutazamwa kwa umakini kulingana na unyeti wa tukio na mazingira yake.
Ni kweli, operesheni hiyo inatakiwa isiwe ya mateso, unyanyasaji, ukatili wala fursa ya ulipaji wa visasi, bali inatakiwa kuendeshwa kwa umakini, weledi na haki ili kuhakikisha kila mmoja anatendewa kadri ya matendo yake.

Tunatambua kuwa operesheni yoyote inayowahusisha watu wazito inakuwa na changamoto na vikwazo vingi, hali inayowasukuma hata wabunge kuanza kushinikiza Serikali kutoa orodha ya vigogo wanaodaiwa kujihusisha na vitendo vya ujangili.
Kwa mujibu wa madai ya wabunge hao na taarifa za vyombo vya habari, biashara hiyo haramu inawahusisha baadhi ya wabunge, mawaziri, watumishi wa Serikali na maofisa katika vyombo vya dola.

Jeshi la Polisi limetajwa kuongoza miongoni mwa makundi manne ya majeshi, ambayo watumishi wake wamekamatwa wakijihusisha na ujangili katika matukio saba ya ujangili. Wengine ni kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Magereza.

Mathalan, kwa jinsi tatizo hilo lilivyo kubwa, katika matukio ya karibuni yaliyohusisha maofisa wa vyombo vya dola, jumla ya meno ya tembo 686 yaliyotokana na kuuawa kwa tembo 343 yalikamatwa, na vipande vingine 447 vilipatikana.
Kwenye operesheni ya namna hii ambayo Serikali imekiri kuwapo fununu za wanasiasa kuwa miongoni mwa majangili, ni lazima kuwepo vikwazo na shinikizo la kuizuia au kukwamisha, kwa vitisho au malalamiko ya umma kutoka kila kona ili kuhakikisha operesheni husika haifanikiwi.

Kutokana na hali hiyo, tunaunga mkono kauli ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha aliyoitia juzi bungeni akiwataka wanasiasa kuacha kushikiza kwa kutumia nguvu zao za kisiasa, kusitishwa kwa operesheni hiyo kwa sababu yoyote, kwa kuwa tunaamini shughuli kama hii haiwezi kufanikiwa iwapo itaendeshwa kama lelemama.
Chanzo: Mwananchi

MAGAZETINI LEO ALHAMISI 31 OKTOBA 2013 NA Chiwambo's Blog











Saini zakusanywa kumng’oa Makinda



Spika wa Bunge, Anne Makinda (kulia) akizungumza na Mbunge wa Viti Maalumu, Clara Mwatuka na Mbunge wa Kilolo, Profesa Peter Msola katika Viwanja vya Bunge, mjini Dodoma jana.PICHA NA EDWIN MJWAHUZI

Na Sharon Sauwa,Mwananchi
Kwa ufupi
“Si kweli kwamba Kamati ya Bajeti inalipwa fedha za ziada kila wakati, hapana, ni pale tu wanapoomba malipo hayo kutokana na sababu ambazo lazima Spika aridhike nazo. Ieleweke kuwa siyo kamati hiyo tu, kwa sasa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ambayo inachambua miswada mingi nayo imekuwa ikiomba na baada ya Spika kuridhia basi nao wanapewa,”

Dodoma. Mbunge wa Nzega, Dk Khamis Kigwangalla, (CCM), leo anatarajiwa kuanza kukusanya saini za wabunge akitafuta kuungwa mkono katika hoja ya kutokuwa na imani na Spika wa Bunge, Anne Makinda kwa madai kwamba amekuwa akikiuka kanuni za Bunge.

Dk Kigwangalla aliibua hoja ya kutokuwa na imani na Spika katika kikao cha wabunge wote cha kuelezea shughuli zitakazofanywa na Bunge katika mkutano wa 13, kilichofanyika juzi jioni kwenye ukumbi wa Pius Msekwa.

Mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, jana alithibitisha kuwapo kwa mjadala huo katika kikao cha wabunge, lakini hakuwa tayari kueleza kwa undani na badala yake alisema kwamba leo ataanza kukusanya saini za wabunge kwa ajili ya kukamilisha hoja ya kutokuwa na imani na Spika Makinda.

Chanzo chetu kutoka katika kikao hicho cha wabunge kilibainisha kuwa Kigwangalla alihoji kuhusiana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge (CCM-Bariadi Magharibi) kuteuliwa na Spika wakati katika kamati nyingine wenyeviti na makamu huchaguliwa na wajumbe wa kamati husika.

Pia Dk Kigwangala alisema Spika Makinda alivunja kanuni kwa kuwapa posho ya Sh430,000 kwa siku wajumbe wa kamati inayoongozwa na Chenge wakati wajumbe wa kamati nyingine wamekuwa wakipewa Sh130,000.

“Anachokifanya Spika ni matumizi mabaya ya fedha za umma, inakuwaje wengine wafanye kazi hata bila posho lakini wao (Kamati ya Bajeti), walipwe posho ya Sh430,000 kwa siku?” chanzo hicho kilimkariri Dk Kigwangalla akihoji. Hata hivyo, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah akizungumza na gazeti hili jana alisema mazingira ya kamati fulani kupata malipo ya ziada tofauti na viwango vya kawaida hutokea pale uongozi wa kamati husika unapoomba kwa Spika.

“Si kweli kwamba Kamati ya Bajeti inalipwa fedha za ziada kila wakati, hapana, ni pale tu wanapoomba malipo hayo kutokana na sababu ambazo lazima Spika aridhike nazo. Ieleweke kuwa siyo kamati hiyo tu, kwa sasa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ambayo inachambua miswada mingi nayo imekuwa ikiomba na baada ya Spika kuridhia basi nao wanapewa,” alisema Dk Kashililah.

Katibu huyo wa Bunge alieleza kuwa zaidi ya kamati nane zimewahi kuomba malipo ya ziada kwa maana ya kutaka posho zaidi, ulinzi, usafiri na hata chakula, ikiwa zinakabiliwa na majukumu ya ziada pia katika mazingira tofauti nje ya utaratibu wa kawaida.

“Kimsingi, kamati nyingi zinapewa malipo tofauti, watu wanaweza kuwa na kazi mpaka saa saba au nane usiku, au wanakwenda kufanya kazi katika mazingira yasiyokuwa ya kawaida, taratibu zinamruhusu Spika kama akiridhika na maelezo ya kazi husika, basi anaruhusu kutekelezwa kwa maombi hayo,” alisema Dk Kashililah.

Kuhusu Serukamba
Aidha, Dk Kigwangalla alinukuliwa akisema Spika amekiuka kanuni kwa kumchagua Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Peter Serukamba (Kigoma Mjini-CCM), kuwa mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Bajeti.

“Hakuna mbunge yeyote aliyepo katika kamati mbili lakini hata kungekuwa na sababu maalumu basi wa kuteuliwa angekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, Mahmoud Mgimwa (Mufindi Kaskazini-CCM) ambaye TRA (Mamlaka ya Mapato Nchini) ipo chini ya kamati yake,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kilisema Dk Kigwangalla alisema badala ya kumweka karibu katika ushiriki, Mgimwa alipokwenda katika kamati hiyo aliambulia kufukuzwa.
Akizungumzia suala hilo, Dk Kashililah alisema Serukamba pamoja na wabunge wengine kadhaa waliteuliwa na Spika kwa ajili ya kuongeza nguvu katika kamati hiyo wakati wa kipindi cha Bajeti Kuu ya Serikali.

Aliwataja wabunge wengine walioteuliwa kushiriki katika Kamati ya Bunge ya Bajeti kuwa ni John Cheyo (Bariadi Mashariki-UDP), Salahe Pamba (Pangani - CCM) na Hamadi Rashid Mohamed (Wawi - CUF).

Kanuni za Bunge
Kwa mujibu wa kanuni za Bunge katika toleo la mwaka 2007, kifungu cha 137(1), ili kumwondoa Spika madarakani, mbunge anayetaka kuwasilisha hoja hiyo atatakiwa kuwasilisha taarifa ya maandishi ya kusudio hilo kwa Katibu, akieleza sababu kamili ya kutaka kuleta hoja hiyo.

Kifungu kidogo cha pili kinasema baada ya kupokea taarifa ya maandishi ya kusudio la kumwondoa Spika kwenye madaraka, Katibu atapeleka taarifa hiyo kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa ajili ya kujadiliwa.

Kifungu cha tatu kinabainisha kuwa endapo kamati hiyo itaridhika kuwa zipo tuhuma mahususi dhidi ya Spika zinazohusu uvunjaji wa masharti ya ibara husika za Katiba, sheria au kanuni zinazoongoza shughuli za Bunge, basi kamati hiyo itaidhinisha hoja hiyo ipelekwe bungeni ili iamuliwe.

Kanuni zinasema Naibu Spika, atakalia Kiti cha Spika wakati wa kujadili hoja ya kutaka kumwondoa Spika madarakani na Spika atakuwa na haki ya kujitetea wakati wa mjadala na kwamba ili kumwondoa zinahitajika kura zisizopungua theluthi mbili ya idadi ya wabunge wote.
Chanzo: Mwananchi

magufuli bado alia na wenye malori



WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli amesema tatizo la uzidishaji wa mizigo unaofanywa na magari makubwa iwapo litaendelea, barabara zote zitaharibika. Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo bungeni jana, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF). 

Katika swali lake, Hamad alitaka kujua sababu ya barabara zinazojengwa kuharibika ndani ya kipindi kifupi.
Dk. Magufuli alisema tatizo la kuharibika kwa barabara linasababishwa na ujenzi duni wa wakandarasi, lakini kwa kiasi kikubwa huharibiwa na magari yanayozidisha mizigo.
"Kwa mfano katika Barabara ya Dar es Salaam hadi Dodoma tayari upande wa kushoto wa barabara umeshabonyea.

"Kwa Tanzania uzito unaotakiwa kupita barabarani hautakiwi kuzidi tani 56, lakini magari yanazidisha hadi kati ya tani 90 na 98, tukiendelea hivyo si tu barabara zitavimba bali zitapasuka kabisa," alisema.

Alitoa viwango vya uzito unaotakiwa katika nchi kama Marekani kuwa ni tani 36.2, Uingereza Tani 44, Ufaransa Tani 40 na Ujerumani ni Tani 40.
Awali akijibu swali la msingi la Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige, Dk. Magufuli alisema Mkoa wa Geita umeingia mkataba na Mhandisi Mshauri kwa ajili ya kuifanyia marekebisho barabara ya Geita, Bukoli hadi Kahama.

Alisema mkataba huo ni kwa ajili ya kuifanyia upembuzi yakinifu pamoja na usanifu wa kina barabara hiyo kwa gharama ya Sh milioni 403.9 katika kipindi cha miezi 13.
Katika swali lake, Maige alitaka kujua lini utekelezaji wa kuiwekea lami barabara hiyo utaanza. Chanzo: mtanzania

wapinzani kusimamisha mgombea mmoja 2015



UPEPO wa mabadiliko ya kisiasa unaovuma kuelekea kambi ya upinzani, sasa unaonekana kuwaamsha viongozi wa vyama hivyo baada ya kutolewa kwa taarifa kuwa wanafikiria kusimamisha mgombea mmoja wa urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. 

Taarifa zilizolifikia gazeti hili kabla ya kuthibitishwa na mmoja wa viongozi hao, zilieleza kuwa hatua ya vyama hivyo imekuja baada ya ushirika wao waliouunda kupinga upungufu uliokuwemo kwenye Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kuzaa matunda.

Pamoja na hilo, inaelezwa kuwa maamuzi hayo magumu ya wapinzani yametiwa chachu na kauli aliyoitoa Rais Jakaya Kikwete ya hivi karibuni ya kukitabiria anguko Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi wa mwaka 2015 au ule wa 2020, kutokana na kile alichodai kuwa viongozi wa chama hicho kuendekeza rushwa.

Mmoja wa viongozi wanaounda ushirika huo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia alithibitisha taarifa hizo huku akisisitiza kuwa nia ya kufanya hivyo ni kuhakikisha wanaiondoa madarakani CCM mwaka 2015.
Kwa mujibu wa Mbatia, walichokifanya kwenye Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba si nguvu ya soda na badala yake wataendeleza hadi kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Mbatia alisema kuwa uongozi wa vyama vya upinzani unatarajia kuungana na kumsimamisha mgombea mmoja, ili kuhakikisha wanaiondoa madarakani CCM.
Mbatia ambaye alikuwa akizungumza katika mahojiano maalumu na RAI Jumatano, alisema hatua hiyo pamoja na ushirika wao unalenga kudumisha amani na uzalendo kwa kuweka utaifa mbele.

Alisema umoja wanaoendelea kuuonyesha kwenye mchakato wa Katiba Mpya, ambao unalenga kuweka mbele maslahi ya Taifa ili kuhakikisha inapatikana Katiba bora yenye kushirikisha Watanzania wote, wataufanya pia kwenye chaguzi mbalimbali.
"Ili jambo lolote litokee lazima kuwepo na chanzo, mwanzo wetu wa ushirikiano ulioanza Septemba mwaka huu ndani ya ukumbi wa Bunge, tutauendeleza.

"Tupo kwenye maridhiano zaidi, hata muungano wetu wa Tanzania bara na Zanzibar si wa kisheria, viongozi wetu Nyerere na Mzee Karume walikaa na kuzungumza, hata sisi tunafanya hivyo, tunatakiwa kuzungumza kwa maslahi ya nchi," alisisitiza Mbatia.
Alisema vyama vyao viliamua kuwa na ushirikiano wa pamoja kutokana na kubaini kwamba, bila umoja hakuna kitakachofanikiwa.

"Tumeshaanza kuzungumza kwa mapana juu ya ushirikiano wetu, ukweli ni kwamba kuna mwelekeo mzuri," alisema.
Alisema hatua ya vyama kujadili kwa pamoja mchakato wa Katiba ni dalili njema za kuelekea kwenye mafanikio na ndio maana wanaona ipo haja ya kuuendeleza ushirika huo hadi kwenye chaguzi mbalimbali nchini.
"Tunapaswa kuvifanya vyama vyetu viwe vya maslahi mapana kwa taifa, ili visionekane vipo kwa ajili ya maslahi ya viongozi.

"Kwa kuwa tumeweka maslahi ya taifa mbele kwenye suala la Katiba, tumeona tuwe na mfumo ambao utalisaidia taifa, ndio maana hata tulipotoka Ikulu tumekubaliana kuwa Tanzania kwanza vyama baadaye, naamini kwa nia njema hata ule ushirikiano wetu utaendelea mbele zaidi kwa maslahi mapana ya taifa letu, tunategemea hivyo... tuna mategemeo mazuri, lazima tufikirie chanya," alisema Mbatia.

Kauli ya Mbatia imeungwa mkono na Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Julius Mtatiro ambaye ameeleza kuwa chama chao hakina tatizo kwenye suala la kumsimamisha mgombea mmoja na wako tayari kwa sababu ushirikiano ni suala la msingi na lenye maana.

"Kulingana na upepo wa kisiasa ulivyo sasa, ni dhahiri tunahitaji kushirikiana ili kukiondoa chama tawala madarakani, kwa sababu mahali tulipo sasa ni pagumu.
"Tunachosubiri sasa ili kukamilisha muungano wetu ni tamko la pamoja kutoka kwa viongozi wa juu wa vyama vyote, lakini naamini nia ya kusimamisha mgombea mmoja itakubalika bila kupingwa," alisema Mtatiro.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Habari kutoka Chadema, John Mnyika, alisema ushirikiano kwa sasa umejikita kwenye suala la kunusuru mchakato wa Katiba na kuwezesha nchi kupata Katiba bora.
Alisema ushirikiano katika masuala mengine ikiwamo pendekezo la kushirikiana katika uchaguzi, litatafakariwa kwa kuzingatia mafanikio katika ushirikiano kwenye suala la mchakato wa Katiba Mpya ambao tunaendelea nao kwa sasa.

"Huu ndio msimamo ambao naamini pia viongozi wote wanao.
"Kwa kuzingatia kauli zilizotolewa na wenyeviti wote watatu Septemba 15 mwaka huu kwenye mkutano na waandishi wa habari, wakati wa kutoa tamko la pamoja la ushirikiano," alisema.

Hata hivyo, mchambuzi wa masuala ya siasa nchini, Dk. Benson Bana ameukosoa uamuzi huo kwa kudai kuwa hawawezi kuungana kwa sababu hawana kiwango cha kuing'oa CCM madarakani.

Dk. Bana aliweka wazi kwamba, hadhani kama vyama hivyo vitafaulu kuitoa CCM madarakani, kwa sababu havina mtaji wa kutosha wa wanachama.
Alieleza kuwa vyama vyote vitatu vinavyojiona vinaisumbua CCM, ambavyo ni CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi, havijafanya utafiti wa kutosha kubaini mtaji wa wapiga kura walio nao.

Alisema Chadema ina nguvu ndogo Bara hasa kwenye maeneo ya mijini, CUF ina nguvu Zanzibar na NCCR-Mageuzi haina nguvu ya aina yoyote jambo linaloashiria udhaifu wa vyama hivyo, ambapo alivitaka kujipa muda wa kujipanga kabla ya kufikiria kuing'oa CCM.

Wenye mtazamo tofauti na huo wanasema kuwa endapo hatua hiyo ya vyama vya upinzani itafanikiwa, ni wazi itathibitisha kauli ya Mwenyekiti wa CCM kwamba chama hicho kijiandae kung'oka mwaka 2015 au 2020.
Hata hivyo bado kuna shaka juu ya maamuzi hayo ya vyama vya upinzani, kutokana na yale ambayo yamepata kushuhudiwa katika chaguzi nyingine zilizotangulia hususani zile za viti vya ubunge.

Imeshuhudiwa katika chaguzi kadhaa vyama hivyo vikisigana kufikia maamuzi ya kuachiana maeneo ya kusimamisha wagombea wenye nguvu.
Mwaka 2010 kwenye uchaguzi Mkuu, CUF kilikitaka Chadema kutosimamisha mgombea kwenye Jimbo la Tunduru kutokana chama chao kuwa na nguvu, hata hivyo wenzao walikataa.

Hali hiyo pia ilijitokeza kwenye Jimbo la Kiteto, Chadema iliitaka CUF kutosimamisha mgombea jambo ambalo halikutekelezwa.
Chanzo: mtanzania