Thursday, August 29, 2013

Wabunge wa Tanzania nao wasusia kikao EALA



Arusha. Kikao cha Bunge la Afrika Mashariki (EALA), jana kilivunjika kwa mara ya pili baada ya Wabunge wa Tanzania, kutoka ndani ya ukumbi wakipinga kanuni kuvunjwa juzi.

Baada ya wabunge wa Tanzania kutoka nje, Spika wa Bunge hilo, Margareth Zziwa aliahirisha Bunge kwa dakika 15 ili kuweka mambo sawa, lakini jitihada za kuwashawishi ziligonga mwamba na kuamua kuahirisha Bunge hadi leo.
Hata hivyo, Mbunge wa Tanzania, Makongoro Nyerere hakuungana na wenzake kugoma kwani alibakia ukumbini na kuungana na wabunge 32 wa Burundi, Kenya, Uganda na Rwanda.

Awali, Mbunge Abdullah Ali Hassan Mwinyi alitoa msimamo wa wabunge wa Tanzania kuwa walitoka, kupinga kitendo cha wabunge wengine kudharau kiti cha Spika juzi na kutoka nje ili kushinikiza hoja yao.

Mwinyi alisema ili kushinikiza kuheshimiwa kiti cha Spika, wameamua kutoka nje ya ukumbi huo kwa kuonyesha hawaungi mkono, tabia ya baadhi ya wabunge kushinikiza hoja zao, kujadiliwa na Bunge hata kwa kukiuka kanuni na taratibu.

“Jana(juzi) ilikuwa ni mara ya pili wenzetu, kudharau kiti cha Spika na kutaka kutoa hoja na kujadiliwa bila kufuata kanuni, sasa tumeona ni vizuri na sisi kwa kupinga kuvunjwa kanuni, tutoke ili kuonyesha tunapinga mchezo huu,” alisema Mwinyi.

Mwinyi alisema kitendo cha wabunge wenzao kutoka nje ya ukumbi kwa kukataliwa kuvunja taratibu, kinadhalilisha kiti cha Spika na hata wabunge wenyewe.
Mbunge mwingine wa Tanzania, Twaha Taslima alisema kanuni zipo wazi kuwa kama mbunge ana hoja na kutaka Bunge lijadili mambo ambayo si ya dharura ni lazima aiwasilishe saa 24 kabla kwa Spika.

“Sasa jana(juzi), Mbunge wa Kenya, Peter Mathuki alitaka hoja yake ya kutaka utaratibu wa kufanyika bunge kwa mzunguko ijadiliwe kitu ambacho hakikuwa sahihi,” alisema Taslima.

Muthuki, juzi aliungwa mkono na nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), isipokuwa Tanzania.
Jana aliwasilisha hoja hiyo kwa kufuata utaratibu lakini haikujadiliwa baada ya wabunge wa Tanzania kutoka nje.

Katika hoja hiyo, msimamo wa wabunge wa Tanzania na Kamati ya Uongozi ya Bunge ni kuwa vikao vyote vifanyike katika ukumbi wa Bunge, Arusha baada ya kukamilika.
Wabunge wa Tanzania ambao jana walitoka ni Shyrose Bhanji, Profesa Nderakindo Kessy na Taslima. Wabunge wanne hawakuwapo.

Kwa mujibu wa kanuni za Bunge hilo, kama wabunge watatu wa nchi moja, wakitoka nje kupinga jambo lolote basi kikao kinaahirishwa kwa dakika 15 na wasiporejea bunge linaahirishwa.

Akizungumzia mgogoro huo, Ofisa Habari wa EALA, Bobi Odiko alisema kilichotokea jana si ukiukwaji wa taratibu na kuongeza kuwa ana imani mambo yatakuwa sawa na vikao vitaendelea leo kwa amani.
Source: Mwananchi

Ponda asimamisha shughuli Morogoro Wakati wa kusikilizwa Kesi yake



Morogoro. Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda jana alisababisha kusimama kwa shughuli za Serikali wilayani Morogoro baada ya ofisi kadhaa ikiwamo ya Mkuu wa Wilaya na baadhi ya mitaa kufungwa ili kupisha kusikilizwa kwa kesi inayomkabili katika Mahakama ya Mkoa wa Morogoro.
Tofauti na Agosti 19, mwaka huu wakati aliposafirishwa kwa helikopta, jana Sheikh Ponda alisafirishwa kwa barabara kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro akiwa chini ya ulinzi.

Mbali ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro kufungwa, nyingine ni Hazina Ndogo, Madini, Posta, Vipimo, Ukaguzi na Maktaba ya Mkoa.
Sababu za kufungwa kwa ofisi hizo pamoja na Mtaa wa Stesheni na maeneo ya Posta ni kuwa jirani na Mahakama hiyo. Magari yalizuiwa kutembea katika njia na maeneo ya karibu na ofisi pamoja na Mahakama hiyo huku kukiwa na idadi kubwa ya askari polisi na magereza kwa muda wote wa takriban saa mbili.

Alifikishwa mahakamani hapo saa 4:10 asubuhi akiwa katika basi la Magereza ambalo lilisindikizwa na jingine dogo, huku magari mengine yakisimamishwa kupisha msafara huo. Mahakama hiyo ilifurika umati wa wafuasi wa kiongozi kiasi cha kuwalazimu polisi na wana usalama wengine kuweka utepe kuwazuia wengi wao kufika katika jengo lililokuwa likitumika kuendesha kesi hiyo.

Shughuli katika eneo hilo zilirejea katika hali yake ya kawaida saa 6:25 mchana baada kesi yake kuahirishwa na msafara wa Sheikh Ponda kurejea katika Gereza la Segerea, Dar es Salaam ambako yuko rumande.

Muda wote tangu kuwasili mpaka kusikilizwa kwa kesi hiyo, wafuasi hao walikuwa kimya hadi pale ilipoahirishwa na hasa baada ya Sheikh Ponda kuwapungia mkono alipokuwa akielekea kwenye basi ambako walisikika wakisema: “Takbriir na kuitikia Allahu Akbar – (Mungu Mkubwa).”

Kesi yenyewe
Katika kesi hiyo, Wakili wa Serikali, Benard Kongola alisema mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Morogoro, Richard Kabate kuwa Sheikh Ponda alitenda makosa ya uchochezi Agosti 10, mwaka huu saa 11.45 jioni kwenye maeneo ya Kiwanja cha Ndege, Morogoro.

Alisema siku hiyo, Sheikh Ponda alialikwa kutoa maelezo machache kwenye Kongamano la Eid lililoandaliwa na Umoja wa Wahadhiri Mkoa wa Morogoro (Uwamo) na kwamba akiwa hapo alitamka maneno: “Ndugu Waislamu, msikubali uundwaji wa kamati za ulinzi na usalama za misikiti kwani kamati hizo zimeundwa na Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), ambao ni vibaraka wa CCM na Serikali na kama watajitokeza kwenu watu hao na kujitambulisha kwamba wao ni kamati za ulinzi na usalama za misikiti, fungeni milango na madirisha ya misikiti yenu na muwapige sana,” huku akijua kutoa maneno hayo ni kosa kisheria.

Alisema kwa kufanya hivyo, Sheikh Ponda anayetetewa na mawakili watatu wanaoongozwa na Juma Nassoro, alivunja masharti ya Mahakama ya kifungo cha nje iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya Mei 9, mwaka huu iliyokuwa imetamka kuhubiri amani.

Katika shtaka la pili, Sheikh Ponda anadaiwa kuwashawishi wafuasi wake kutenda kosa la jinai kwa kuwaambia: Serikali ilipeleka jeshi Mtwara kushughulikia suala la vurugu iliyotokana na gesi kwa kuwaua, kuwabaka na kuwatesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Waislamu, lakini haikufanya hivyo kwa wananchi wa Loliondo waliokataa Mwarabu asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji baada ya kudai ni mali yao kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Wakristo.” Shtaka la tatu ni kudaiwa kutamka maneno yaliyoumiza imani ya watu wengine kama yalivyo katika shtaka la pili.

Baada ya kusoma mashtaka hayo, Kongola alisema walikuwa na mashahidi 15 na vielelezo vitatu ambavyo ni DVD mbili na kibali kilichotolewa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Morogoro(OCD), Agosti Mosi, 2013 cha kongamano husika na hati ya hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Kisutu, Mei 9, 2013.

Baada ya kusomewa, Sheikh Ponda alikana mashtaka yote matatu huku akikubali kuwemo kwenye kongamano hilo. Alikiri kukamatwa na polisi Agosti 11, Dar es Salaam.
Wakili wa utetezi, Nassor aliwasilisha ombi la dhamana kwa mteja akisema mashtaka hayo yote kisheria yana dhamana. Pia aliwasilisha ombi la kupatiwa hati yenye maelezo ya mlalamikaji ambaye ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani alisema kuwa kutokana na upelelezi upande wa mashtaka kukamilika, wanahitaji maelezo hayo kwa ajili ya kuandaa utetezi.

Hata hivyo, Wakili Kongola aliiomba Mahakama kutompa dhamana mshtakiwa kutokana na cheti kilichotolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kupinga dhamana ya mshtakiwa huyo kwa masilahi ya usalama wa nchi.

Akitoa mwongozo wa maombi yaliyowasilishwa na pande zote mbili, Hakimu Kabate aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 11, mwaka huu itakapotajwa tena na kwamba Septemba 17, mwaka huu Mahakama itatoa uamuzi endapo mshtakiwa atapewa dhamana au la wakati itakapoanza kusikilizwa.
Chanzo: Mwananchi

Wednesday, August 28, 2013

Miaka 50 ya "I have a dream" Martin Luther King alipotoa hotuba yake ya kihistoria





Imetimia miaka 50 tangu Martin Luther King alipotoa hotuba yake ya kihistoria. King aliyekuwa mwanaharakati wa kupigania haki za watu weusi Marekani, alizungumzia ndoto yake ya kuwa na nchi yenye usawa kwa wote.

"Nina ndoto kwamba siku moja watoto wangu wanne wataishi kwenye nchi ambapo hawatatathminiwa kulingana na rangi ya ngozi yao bali kulingana na tabia yao." Ilikuwa tarehe 28 Agosti mwaka 1963, pale ambapo Martin Luther King na maelfu ya Wamarekani weusi waliandamana mjini Washington kudai uhuru na haki sawa ya kupata ajira kwa watu weusi. King alikuwa miongoni mwa waandalizi wa maandamano hayo na mmoja wa watu waliotoa hutoba siku hiyo. Hotuba yake ya I have a dream - yaani nina ndoto - inaelezea mustakabali anaoutamani kwa nchi yake. Alitaka Marekani iwe na umoja na watu wasibaguliwe kwa sababu ya rangi ya ngozi yao.

"Hatuwezi kuridhika iwapo mtu mweusi kutoka Mississippi hana haki ya kupiga kura na mtu mweusi anayeishi New York haoni sababu ya kupiga kura," alisema King katika hotuba yake. Miaka hamsini baadaye, sehemu fulani ya ndoto ya Martin Luther King imetimia. Kwa mara ya kwanza Marekani inaongozwa na rais mweusi.


Ubaguzi bado tatizo sugu
Barack Obama ni rais wa kwanza mweusi wa Marekani Barack Obama ni rais wa kwanza mweusi wa Marekani

Barack Obama leo ataongoza maadhimisho ya miaka 50 ya hotuba ya King. Atatoa hotuba kwenye jengo la kumbukumbu ya Lincoln mjini Washington - mahali pale pale ambapo King alielezea ndoto yake miaka 50 iliyopita.

Obama ameeleza kuwa mafanikio yake kama mwanasiasa mwenye mamlaka makubwa zaidi Marekani, yamejengwa juu ya misingi ya juhudi za Martin Luther King na wenzake. Anaamini kwamba asingekuwa rais wa Marekani leo, kama wanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi wasingekuwa tayari kuvumilia vitisho, mateso na hata kufungwa jela.

Hata hivyo, ubaguzi wa rangi bado ni tatizo sugu kwenye baadhi ya maeneo ya Marekani. Kisa cha kijana Trayvon Martin aliyepigwa risasi na Mmarekani mwenye ngozi nyeupe aliyehisi kuwa Treyvon ni kibaka kiliweka wazi kwamba bado yapo maoni potofu juu ya watu weusi. Suala lililozusha mjadala mkubwa zaidi ni kwamba aliyempiga risasi kijana huyo hakupewa hukumu yoyote mahakamani.

Sherehe za leo za mjini Washington zitahudhuriwa pia na marais wa zamani wa Marekani. Bill Clinton na Jimmy Carter ni miongoni mwa wale watakaotoa hotuba.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/Reuters/ap

Mhariri: Josephat Charo

MAGAZETINI LEO JUMATANO TAREHE 28-08-2013 NA Chiwambo's Blog





kikosi cha AZAM FC kitakachoteremka Dimbani leo Jumatano kuikabili Mtibwa


Operesheni ya kijeshi yanukia Syria bila UN



Uwezekano wa Umoja wa Mataifa kuidhinisha mashambulizi dhidi ya Syria ni mdogo sana, lakini tayari Marekani na washirika wake wanafanya maandalizi ya mashambulizi kupitia dhana ya uwajibikaji wa kimaadili.

Wiki moja baada kutokea shambulio linalodaiwa kuwa la kemikali nchini Syria, mataifa kadhaa yameanza kupeleka vikosi kujiandaa na mashambulizi. Siku ya Jumatatu waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza William Hague alielezea uhakika kwamba gesi ya sumu ilitumiwa na vikosi vitiifu kwa rais Assad. Uchunguzi wa karibu juu ya shambulio hilo unaendelea kufanywa na wakaguzi wa Umoja wa Mataifa. Iwapo watabainisha kuwa kweli gesi hii ilitumiwa na upande wa serikali, hakuna kitakachozuia mashambulizi ya kijeshi.

Rais wa Marekani Barack anasema utawala wa Assad laazima uwajibishwe. ***FREI FÜR SOCIAL MEDIA*** Rais wa Marekani Barack anasema utawala wa Assad laazima uwajibishwe.


                                                      RAIS WA MAREKANI OBAMA



Muungano wa hiari
Kulingana na muktadha wa sheria hata hivyo, mashambulizi hayo yatakuwa yanakiuka sheria za kimataifa, kwa kuwa uhalali wake unaweza kutokana tu na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, ambako China na Urusi zinaweza kuzuia mpango huo kwa kutumia kura zao za turufu. Kwa nchi hizo mbili, uingiliaji kijeshi kutoka mataifa ya nje siyo njia ya kuleta suluhu.

Kama litafanyika shambulizi la kijeshi, haitakuwa mara ya kwanza kwa Marekani kuchukua hatua kama hiyo pasipo idhini ya Umoja wa Mataifa. Rais wa zamani wa Marekani George W. Bush, kupitia kile alichokiita muungano wa hiari, aliyaongoza mataifa kadhaa kuivamia Iraq mwaka 2003, kwa madai ya kuikomboa kutoka mikononi mwa Saddam Hussein.

Kabla ya uvamizi huo, Marekani ilijaribu kupitisha hoja yake ndani ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, kuonyesha kuwa kulikuwepo silaha za maangamizi nchini Iraq, ambapo waziri wa ulinzi wa wakati huo Collin Powell aliwasilisha ushahidi wa madai hayo katika baraza.

Hata hivyo, kulikuwa na mashaka makubwa kwa upande wa Ufaransa, Urusi na Ujerumani kuhusiana na ushahidi huo, na waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Joschker Fischer, alieleza bayana kuwa hakuridhika na ushahidi wa Marekani. Na kwa hakika mashaka yake yalikuja kutimia, baada ya kubainika kwamba ushahidi uliyowasilishwa katika umoja wa mataifa ulikuwa wa kughushi. Collin Powell alikiri kufanya makosa na kujiondoa katika ulingo wa siasa.

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron anakutana na maafisa wa juu serikalini na jeshi kujadili mikakati. Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron anakutana na maafisa wa juu serikalini na jeshi kujadili mikakati.


                                                      Rais wa Ufaransa Francois Hollande



Ulinganisho na Kosovo
Lakini kwa Manfred Eisele, Meja Jenerali mstaafu wa jeshi la Ujerumani Bundeswehr, mazingira ya uingiliaji kati nchini Iraq siyo sawa na yaliyopo nchini Syria hivi sasa. Lakini anaona ulinganifu kati ya Syria na Kosovo mwaka 1999, ambako waasi wa kabila la Albania walipigana vita vya kujitenga na serikali ya Yugoslavia.

Wakati wa mgogoro huo zilijitokeza ripoti za mara kwa mara juu ya ukiukaji wa haki za binaadamu na mauaji ya kimbari yaliyokuwa yakifanywa na jeshi la Yugoslavia. Urusi ilikubali katika baraza la usalama lakini ilipinga uingiliaji kati wa vikosi vya kimataifa, hali iliyoilaazimu jumuiya ya kujihami NATO kuingilia kati bila idhini ya Umoja wa Mataifa.

Andreas Bock, mtaalamu wa siasa kutoka chuo kikuu cha Augsburg anakubaliana na maoni ya Eisele, na anasema Kosovo kulikuwepo na ukiukaji wa dhahiri wa haki za binaadamu uliohalalisha uingiliaji kati. Anasema hata kama hatua hii ilikuwa inakwenda kinyume na sheria za kimataifa, kulikuwepo na wajibu wa kimaadili kwa jamii ya kimataifa kusimama pamoja.

Haki dhidi ya maadili
Hata hivyo, uingiliaji wa namna hiyo kwa misingi ya ubinaadamu bila idhini ya Umoja wa Mataifa ulisitishwa mwaka 1990, pale vikosi vya jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika magharibi ECOWAS, vilipoingilia kati nchini Liberia vikiongozwa na Nigeria. Eisele anasema wakati huo dunia haikuwa na maslahi na kilichokuwa kinaendelea nchini Liberia, kwa sababu mauaji yalikuwa yakitokea barani Afrika. Lakini anasema hali iliyokuwepo wakati huo ilikuwa inalinganishwa na hali ya Kosovo.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande alisema hata bila idhidi ya Umoja wa Mataifa laazima Assad achukuliwe hatua. Rais wa Ufaransa Francois Hollande alisema hata bila idhidi ya Umoja wa Mataifa laazima Assad achukuliwe hatua.

 

                                                 Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron





Sheria mpya

Ili jamii ya kimataifa iweze kuingilia kati hali kama hizo bila kuzuiwa na kura za turufu za wanachama watano wa kudumu wa baraza la usalama, serikali ya Canada ilianzisha dhana ya sheria ya wajibu wa ulinzi mwaka 2001, na kuendelezwa na kamati ya wataalamu wa sheria za kimataifa. Kulingana na dhana hiyo, kanuni ya kutoingilia kati masuala ya ndani ya nchi nyingine inasita kutumika pale unapotokea ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu. Kwa kuwa hakuna msimamo wa pamoja katika baraza la usalama, Marekani, Uingereza na Ufaransa zinaweza kutumia dhana hii kuingilia kati nchini Syria.

Mwandishi: Marcus Lütticke
Tafsiri: Iddi ISmail Ssessanga
Mhariri: Daniel Gakuba

PT
Rais Barack Obama wa Marekani na waziri mkuu wa Uingereza, David Cameron wameafikiana kuwa ni dhahiri silaha za kikemikali zilitumika katika mashambulio ya wiki jana nchini Syria na kwamba serikali ya rais Bashar Al Assad ndiyo iliyohusika.
Hata hivyo waziri mkuu David Cameron hajatoa ishara yoyote ikiwa watatumia nguvu za kijeshi kutatua mzozo huo Syria .
Lakini katika mahojiano na BBC na vyombo vingine vya habari alisisitiza kuwa hatua yoyote itakayochukuliwa italenga kujibu matumizi ya silaha za kemikali.
Licha ya kwamba chama cha upinzani cha Labour kimeonysha ishara kwamba kinaweza kuunga mkono uingiliaji kati wa jeshi nchini Syria wengi wa wanasiasa bado hawajaamua.
Balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa anatarajiwa kuwasilisha azimio kuhusu Syria wakati wa mkutano wa Baraza la usalama wa Umoha wa Mataifa
Cameron amesema azimio hilo ni la kulaani serikali ya rais Bashar Al Assad kwa kutumia silaha za kemikali dhidi ya raia wake na pia kuidhinisha mikakati maalum ya kulinza raia wa Syria.
Bwana Cameron amesema serikali yake inataka Umoja wa Mataifa kuwajiabika katika mzozo huo wa Syria.
Tangazo hilo limetolewa baada ya rais Obama kushauriana kwa njia ya simu na rais Barrack Obama wa Marekani.
Marekani bado haijatoa ripoti yake ya ujasusi kuhusu shambulio hilo, lakini vyombo vya habari nchini marekani vinadai kuwa uchunguzi huo ulidukua mawasiliano kati ya maafisa wa wizara ya ulinzi nchini Syria wakikubali kutekeleza shambulio hilo.