Saturday, November 2, 2013

Jeshi la Kongo laanzisha 'awamu ya mwisho' ya kuwang'oa M23



Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limeanzisha kile wanachokiita "awamu ya mwisho" kuwamaliza wapiganaji waliobakia wa M23 , baada ya kuichukua ngome ya mwisho katika hatua ya kuuvunja kabisa uasi huo.
Wanajeshi wa Kongo wakiwa katika matayarisho ya kufanya mashambulizi 'ya mwisho' dhidi ya M23.

Mkaazi mmoja wa mji wa Jomba ulio mpakani mwa Kongo na Uganda, ameliambia shirika la habari la AFP kwa njia ya simu kwamba sasa "wanajeshi wa Kongo wanaendesha operesheni zao dhidi ya waasi"kwenye eneo hilo.

Mkaazi huyo aliyekataa kutaja jina lake amesema amemuona msichana mmoja akiwa amejeruhiwa kwa risasi katika mapigano ya hivi karibuni kabisa, ingawa hakufafanua zaidi. "Wanajeshi wa serikali walitumia usiku wao (wa kuamkia Ijumaa ya tarehe 1 Novemba) hapa na sasa wamekwenda mstari wa mbele wa mapigano," amesema mtu huyo.

Shirika la habari la AFP limeripoti kwamba hata wakati wa mazungumzo hayo ya simu, milio ya risasi ilikuwa inasikikana waziwazi, ambapo chanzo hicho cha habari kilisema kwamba pande zote mbili za mapigano zilikuwa zikitumia silaha nzito. Mwandishi wa AFP aliyeko upande wa Uganda aliweza pia kusikia milio hiyo ya risasi.

MONUSCO yasaidia
Mkuu wa MONUSCO, Martin Kobler. Mkuu wa MONUSCO, Martin Kobler.

Chanzo kimoja kutoka Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Kongo (MONUSCO), ambacho kinalisaidia jeshi, amesema mashambulizi hayo dhidi ya M23 ni "awamu ya mwisho," baada ya jeshi hilo kukichukua kituo kikuu cha waasi cha Bunagana hapo Jumatano.

Lakini wapiganaji wenye msimamo mkali wa M23, wanaokisiwa kufikia 100, wanasemekana kujificha kwenye eneo hilo lenye milima mitatu umbali wa kiasi cha kilomita 80 kaskazini mwa mji wa Goma, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Kivu ya Kaskazini.

"Jeshi la Kongo limewazunguka wapiganaji hawa wachache wa M23 ili kuwamaliza. Operesheni inaendelea," kilisema chanzo hicho.

Tangu mapigano kuanza tena mnamo tarehe 25 Oktoba, baada ya mazungumzo ya amani kuvunjika nchini Uganda, hakuna wanajeshi wa Umoja wa Mataifa waliojihusisha moja kwa moja kwenye mashambulizi, lakini MONUSCO imekuwa ikiwasaidia wanajeshi wa serikali kwa taarifa za kiintelijensia na vifaa.

Kabila awataka M23 wajisalimishe
Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa katika operesheni za kulinda amani Kongo. Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa katika operesheni za kulinda amani Kongo.

Baada ya waasi kupoteza makao yao makuu ya Bunagana, siku ya Jumatano Rais Joseph Kabila aliwasihi tena wapiganaji hao wa M23 kusalimu amri kwa hiyari, akiwaonya kwamba wakishindwa kufanya hivyo, basi wanajeshi wake wangeliwalazimisha.

Maelfu ya watu wamekimbia mapigano kati ya wanajeshi wa serikali na wapiganaji wa kundi la M23, ambalo limeundwa na waasi wa zamani wa Kitutsi waliokuwa wameingizwa kwenye jeshi la Kongo chini ya makubaliano ya amani ya mwaka 2009, lakini kisha wakaasi mwezi Aprili 2012, wakidai kwamba makubaliano hayo hayakuwa yametekelezwa kikamilifu.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Saumu Yusuf

Hakuna mkutano bila upinzani wa Syria



Mjumbe wa amani Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Kiarabu Lakhdar Brahimi amesema leo kuwa kongamano linalopangwa la amani jijini Geneva ili kumaliza vita vya Syria huenda lisiandaliwe bila ya ushiriki wa upinzani.


Wakati akikamilisha ziara yake mjini Damascus, Lakhdar Brahimi alitoa wito kwa pande zote mbili, serikali ya Syria na upinzani kuhudhuria mkutano unaopangwa wa amani. Mjumbe huyo wa amani amesema kabla ya kurejea mjini Beirut, kuwa mazungumzo hayo yanayotarajiwa kuandaliwa baadaye mwezi huu jijini Geneva, hayawezi kuendelea kama upinzani Syria utasusia.

Nayo Urusi imesema inataraji kuwa mkutano huo wa amani utaandaliwa kabla ya kumalizika mwaka huu, licha ya tofauti zilizopo na Marekani kuhusu uwakilishi wa upinzani. Waziri Mkuu Dmitry Medvedev ameziomba pande zote katika mzozo wa Syria kulegeza msimamo wakati akiushutumu upinzani kwa kumtaka Rais Bashar al-Assad aondoke kama masharti ya kabla ya mazungumzo.
Ndege za Israel zashambulia kambi ya jeshi la Syria Ndege za Israel zashambulia kambi ya jeshi la Syria

Ombi la Brahimi na Medvedev, limekuja saa chache tu baada ya maafisa kusema kuwa Israel imefanya shambulizi la kutokea angani katika kituo kimoja cha jeshi la Syria ili kusitisha usafirishaji wa silaha kwa kundi la Hezbollah. Kituo cha televisheni cha Al- Arabiya kimesema kuwa Israel imeipiga kambi ya jeshi la angani la Syria katika mkoa wa Latakia, wakati ikiyalenga makombora ya Urusi yanayotumiwa katika mashambulizi ya ardhini yaliyokusudiwa kupewa kundi la wanambambo wa Hezbollah. 

Afisa wa Marekani amethibitisha kwa shirika la habari la AFP kuwa “kulikuwa na shambulizi la Israel“ lakini hakutoa maelezo zaidi kuhusu eneo na kilicholengwa, wakati nao maafisa wa Syria wakikataa kuzungumzia habari hizo. Mwezi Mei, Israel ilifanya mashambulizi mawili ya kutokea angani ndani ya Syria, na afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Israel akasema mashambulizi hayo mawili yalizilenga silaha zilizoundwa nchini Iran ambazo zilikusudiwa kupewa Hezbollah.

Hayo yanajiri wakati Shirika la Kupambana na Matumizi ya Silaha za Sumu likisema kuwa silaha zote za sumu nchini Syria zimedhibitiwa. Msemaji wa shirika hilo Michael Luhan amesema “silaha zote zimewekwa katika mifuko ambayo haiwezi kupasuliwa“. Amesema kuna tani 1,000 ya sumu inayoweza kutengeneza silaha, pamoja na tani 290 za silaha za sumu. Shirika hilo pia limesema vifaa vyote vya kutengenezea silaha za sumu vimeteketezwa.

Wakaguzi wana hadi leo kuzuru maeneo yote na kuharibu vifaa vyote vya kutengeneza silaha za sumu kwa mujibu wa muda uliowekwa kwenye azimio la Shirika la OPCW na Umoja wa Mataifa.Katika uwanja wa mapambano, jeshi la Syria limesema majeshi yameutwaa mji wa Sfeira katika mkoa wa Aleppo baada ya kuuzingira kwa siku 27, huku kukiwa na ripoti kuwa waasi wameondoka kabisa katika eneo hilo.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri: Josephat Charo

Nishati mbadala yagubika mazungumzo Berlin



Wawakilishi wa tume ya nishati kutoka vyama ndugu vya Christian Democratic CDU na Social Democratic SPD wazungumzia mageuzi katika sekta ya nishati
Waziri wa mazingira Peter Altmeier wa chama cha CDU na waziri mkuu wa jimbo la Northrhine Westfalia,bibi Hannelore Kraft wa chama cha SPD

Matumizi ya nishati mbadala nchini Ujerumani ndio yaliyogubika mazungumzo ya kuunda serikali kuu ya muungano mjini Berlin.Mada kuu ni kuhusu namna ya kupunguza kupanda bei ya nishati wakati Ujerumani inajiandaa kuondokana na nishati ya makaa mawe na kuingia katika enzi za nishati inayotokana na nguvu za upepo na mwangaza wa jua.

Waziri mkuu wa jimbo lenye wakaazi wengi zaidi la Ujerumani-Northrhine Westfalia,bibi Hannelore Kraft wa kutoka chama cha Social Democratic-SPD pamoja na waziri wa nishati wa serikali kuu inayomaliza wadhifa wake Peter Altmeier wa chama cha Christian Democratic Union CDU ndio wanaoongoza mazungumzo ya tume inayaoshughulikia mageuzi katika sekta ya nishati.

Alipoteremka ndani ya gari tu bibi Hannelore Kraft alitambua nini kinamsubiri.Wanaharakati wa shirika la usafi wa mazingira Green Peace wamekusanyika mbele ya wizara ya mazingira katika uwanja wa Postdam na magari matano yaliyojaa makaa mawe na karibu na hapo sampuli za mitambo ya nishati ya upepo."Nishati mbadala badala ya kugharimiwa makaa mawe" ndio ujumbe wa wanaharakati hao kwa waziri mkuu huyo wa jimbo la Northrhine Westfalia.
Nishati mbadala inayotokana na nguvu za upepo-mradi unaoendeshwa katika jimbo la Schleswig-Holstein

Sheria ya mageuzi kufanya kazi mwaka 2015

Saa sita nzima walihitaji wajumbe wa tume ya mazungumzo kujadiliana kuhusu nishati mnamo duru hiyo ya kwanza .Magharibi ilipoingia matokeo yakatangazwa:Vyama ndugu vya CDU na CSU vinavyoongozwa na kansela Angela Merkel na kile cha Social Democratic vinataka mswaada wa sheria mpya ya mageuzi ya nishati ifikiwe hadi msimu wa kiangazi mwakani .Bunge la shirikisho Bundestag na baraza la wawakilishi wa majimbo Bundesrat,yakiidhinisha mswaada huo ,sheria ya mageuzi ya nishati ianze kufanya kazi mapema mwaka 2015.

Pande zote mbili zinaonyesha kuridhika na maridhiano yaliyofikiwa katika duru hiyo ya kwanza ya mazungumzo.Waziri mkuu wa jimbo ambalo kijadi ndio shina la migodi ya makaa mawe,bibi Hannelore Kraft amekanusha tuhuma kwamba anayapigania mashirika ya makaa mawe .Waziri wa mazingira Peter Altmaier anayataja mageuzi ya sekta ya nishati kuwa "mradi mkubwa zaidi wa serikali kuu ya muungano."Anasema "Ujerumani inabidi iutanabahishe ulimwengu kwamba nishati mbadala inaweza kupatikana kwa bei nafuu".

Hapo waziri wa nishati alikuwa akijibu hoja kwamba licha ya kuporomoka bei jumla ya umeme,majumbani watu wanalipa bei kubwa kabisa kufidia nishati mbadala.
Mgodi wa makaa mawe huko Garzweiler katika jimbo la Northrhine Westfalia

Kipindi cha mpito kipite salama

Waziri mkuu Hannelore Kraft,anaeshirikiana serikalini na walinzi wa mazingira die Grüne mjini Dusseldorf amekanusha tuhuma kwamba anayapigania mashirika ya makaa mawe."Tunataka kipindi cha mpito kuelekea nishati mbadala kifanyike salama,watu wamudu na kiambatane na usafi wa mazingira" amesema.

Mkuu wa chama cha walinzi wa mazingira Simone Peter aliwaonya CDU/CSU na SPD dhidi ya kile alichokiita kurejea nyuma na kutoa ruzuku kwa migodi isiyokuwa na tija ya makaa ya mawe.

Duru ya pili ya mazungumzo ya tume inayoshughulikia masuala ya nishati itaendelea jumatatu ijayo mjini Berlin.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/AFP

Mhariri:Yusuf Saumu

Marekani yakiri huenda udukuzi ukawa umevuka mipaka



Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry akiri udukuzi huenda ukawa umekwenda mbali sana, haya yanajiri wakati bado mvutano unaendelea kati ya taifa hilo na mataifa ya ulaya juu ya madai ya udukuzi

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry
Baada ya siku kumi za mvutano juu ya udukuzi huo taarifa ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry ndio ya kwanza ya kukiri kuwa huenda ikawa maafisa wa Ujasusi wa Marekani wamevuka mipaka katika suala hilo la udukuzi.

Kerry pia ametetea mpango huo na kusema kwamba tangu kutokea kwa mashambulizi ya septemba 11 mwaka wa 2001 nchini Marekani, na mashambulizi mengine jijini London na Madrid, Marekani na nchi nyengine ni lazima zisimame pamoja katika kuwadhibiti magaidi ambao nia yao ni kuuwa watu na kushambulia idara za serikali.
Kerry amesema tangu mwaka huo kumekuwa na uchunguzi wa mawasiliano na kukiri kwamba uchunguzi mwengine huenda ulikuwa unavuka mipaka.

Hata hivyo Kerry hakutoa maelezo yoyote juu ya tamko lake hilo, lakini akasema kwamba tukio ambalo kwa sasa linaleta mvutano na washirika wake wa karibu kama Ujerumani halitarejelewa tena.
Waziri huyo wa nchi za nje wa Marekani licha ya kukiri kwamba huenda udukuzi unaofanywa ukawa unapita mipaka pia amehakikisha kuwa hakuna mtu yoyote anayehujumiwa katika mpango huo wa kukusanya habari.

Wiki hii Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alihamaki na kumuweka sawa Rais wa Marekani Barrack Obama kuhusu madai kwamba maafisa wa Ujasusi wa Marekani wamekuwa wakichunguza mawasiliano yake ya simu na kusema kwamba iwapo hilo litathibitishwa basi hii itaondoa imani ya Ujerumani kwa Marekani.

Wabunge wa Ulaya wataka kujua zaidi juu ya udukuzi
Siku ya Jumatano wiki hii kundi la wabunge wa Ulaya walikuwa mjini Washington Marekani kutaka kujua zaidi juu ya uchunguzi wa Marekani kwa washirika wake.
Huku hayo yakiarifiwa kamati ya baraza la seneti inayohusika na masuala ya Ujasusi nchini Marekani ilipitisha mswada hapo jana unaodhibiti kiwango cha kufanya uchunguzi kwa kutumia vyombo vya elektroniki lakini ikakubali udukuzi huo kuendelezwa.
Katika mswada huo imekubalika uchunguzi wa mawasiliano unaweza kufanyika kwa miaka mitano tu. Mswada huo umepingwa vikali na kampuni za teknologia pamoja na makundi ya kiraia nchini Marekani.

Wakati huo huo mbunge mmoja wa Ujerumani amekutana na mfichua siri za kijasusi za Marekani Edward Snowden mjini Moscow, na kusema mfanyakazi huyo wa zamani wa shirika la Ujasusi la NSA yuko tayari kuja Ujerumani kusaidia katika uchunguzi wa udukuzi wa mawasiliano ya simu ya mkononi ya Kansela Angela Merkel.

Hans-Christian Stroebele mbunge wa upinzani wa chama cha walinzi wa mazingira ameliambia shirika la habari la Ujerumani la ARD kwamba inaonekana Edward Snowden anajua mengi juu ya sakata hiyo na kusema kuwa atatoa habari zaidi leo katika barua aliyoiandikia serikali ya Ujerumani na mwendesha mashtaka mkuu wa Ujerumani.

Bunge la Ujerumani hata hivyo limepanga kufanya kikao maalum Novemba 18 kuzungumzia juu ya udukuzi huo huku chama cha walinzi wa mazingira kikitaka mashahidi kama Edward Snowden kuitwa kueleza wanachokijua juu ya udukuzi huo.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu