Friday, November 1, 2013

KIDATO CHA NNE, SITA NJIA NYEUPE


                         Muundo wa Matokeo ya sasa Picha ya pili na kwa sasa picha ya kwanza



Serikali imefanya marekebisho ya upangaji wa viwango vya alama kwa wanafunzi wa kidato cha nne, sita pamoja na matumizi ya alama endelevu ya mwanafunzi kwa ajili ya kuamua kiwango cha ufaulu wa wanafunzi.
Marekebisho hayo yametokana na maoni ya wadau wa elimu ambapo kwa muda mrefu sasa, upangaji viwango vya alama vinavyotumika katika mitihani ya kuhitimu kidato cha nne na sita, haufanani wakati mitihani yote ni ya sekondari.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari na kufafanua kuwa, muundo huo utatumika kwa miaka minne.

"Utatumika kwa miaka minne kabla haujahuishwa ili kuupa muda wa kutosha kuona aina ya changamoto zinazojitokeza na jinsi ya kuzishughulikia," alisema Prof. Mchome.
Marekebisho hayo ni utekelezwaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa katika sekta hiyo (Big Results Now), ambapo daraja sifuri, limefutwa na kuwekwa daraja ambalo litafahamika kama daraja la tano.

"Daraja la tano ndio la mwisho kabisa katika ufaulu, mabadiliko haya yatapunguza idadi ya wanafunzi wa wanaofeli kuanzia 2013 (kidato cha nne) na kidato cha sita 2014.
"Kuanzia sasa, daraja la kwanza I, litaanzia pointi 7-17, II (18-24), III (25-31), IV (32-47) na daraja la V (48-49)," alisema.

Awali, katika muundo wa zamani, daraja la I lilianzia pointi 7-17, ambayo haijabadilishwa, II (18-21), III (22-25), IV (26-33) na daraja sifuli lilianzia pointi 34-35.
Alifafanua kuwa, daraja la kwanza ni kundi la ufaulu ambao umejipambanua na bora sana, II ufaulu mzuri sana, III ufaulu mzuri na wastani, IV ufaulu hafifu na V ufaulu usioridhisha.

Aliongeza kuwa , alama endelevu mwaka 2013 kwa wanafunzi wa kidato cha nne, tayari zimewasilishwa Baraza la Mitihani nchini (NECTA), ambapo alama hizo zichangie asilimia 40 katika mtihani wa kidato cha nne mwaka huu.
Prof . Mchome alisema , wataalamu wa mifumo ya mitihani, watalifanyia kazi zaidi suala la madaraja liweze kutumika kwa ufanisi katika kipindi hiki cha mpito.

"Mabadiliko hayo yamefanyika ili kuendelea kuimarisha mfumo wa elimu, kuweka wazi taratibu mbalimbali kwa ajili ya mitihani na masuala mengine.
"Sera ya elimu na mafunzo ya 1995 imeelekeza kwamba, katika kuamua kiwango cha ufaulu wa mwanafunzi wa sekondari, alama za tathmini endelevu ya mwanafunzi zitachangia asilimia 50 na mtihani wa mwisho asilimia 50.

"Upande wa Zanzibar, alama hizi zimekuwa zikiandaliwa kwa mfumo wa asilimia 40 na mtihani wa mwisho asilimia 60," alisema na kuongeza kuwa, wadau wengi walishauri muundo uliopo sasa wa madaraja, uimarishwe na kuanza kutumia muundo wa wastani wa alama katika ufaulu (GPA) ambao ni rahisi kueleweka.
Alisema matumizi ya muundo wa GPA ni rahisi kukadiria uwezo wa mwanafunzi kielimu na kufanya maamuzi yakiwemo ya kuendelea na masomo katika ngazi mbalimbali za elimu.

"Kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi walio katika mfumo wa elimu wapo katika ufaulu hafifu, Serikali imeona kuna mambo mengi ambayo hayana budi kuendelea kuimarishwa," alisema.
Mambo hayo ni pamoja na mfumo wa mitaala, walimu, mazingira ya kujifunzia, kufundishia, vitabu na vifaa vingine muhimu.
Katika hatua nyingine, Wizara hiyo imesema mtihani wa kidato cha nne na mtihani wa maarifa mwaka huu, unatarajiwa kufanyika nchini kote kwa siku 18 kuanzia Novemba 4 hadi 21.

Prof. Mchome alisema watahiniwa walioandikishwa kufanya mtihani huo ni 427,906 kati yao 367,399 wa shule 60,507 watahiniwa wa kujitegemea.
Aliwataka walimu, wasimamizi wa mitihani, wakuu wa shule, viongozi na jamii kuhakikisha mitihani inafanyika katika hali ya amani, utulivu na asitokee mtu akajaribu kuharibu taratibu kwani ni kosa la jinai na atachukuliwa hatua.

"Uharibifu wa taratibu hauna faida katika jamii kwani mitihani ya kidato cha nne ni muhimu katika Taifa kwa maendeleo ya jamii na sekta ya elimu.
"Natoa wito kwa kamati za mitihani mikoa yote, kuhakikisha taratibu zote za utunzaji, uhifadhi na usafirishaji wa mitihani zinazingatiwa," alisema.

Alisema hadi sasa maandalizi na usafirishaji mitihani hiyo ngazi ya Mkoa, yamekamilika pamoja na usalama wa mitihani ambapo hakuna uliovuja katika ngazi yoyote kuanzia NECTA, mikoa na halmashauri
Chanzo: Majira

Meya wa Morogoro aonya samaki wabovu



Morogoro. Meya wa Manispaa ya Morogoro, Amiri Nondo amewatahadharisha wananchi kutonunua samaki kwa muda kutokana na kuwapo kwa wimbi la samaki wabovu wanaosadikiwa wana madhara kwa afya.
Akifunga kikao cha Baraza la madiwani juzi, Nondo aliwataka wananchi wa manispaa hiyo kusitisha ulaji samaki kwa muda.

Hata hivyo, Nondo aliwaagiza maofisa wa afya wa manispaa hiyo kufuatilia suala hilo haraka, ili kubaini wafanyabiashara wasio waaminifu.
“Wale Samaki tuliotangaziwa hivi karibuni siyo salama sasa wameingia manispaa yetu, tusitishe kula samaki kwa muda,” alisema. Pia, alisema mfanyabiashara atakayebainika kuuza samaki hao achukuliwe hatua za kisheria.

Makinda: ‘Siogopi hoja ya kung’olewa’



Mbunge wa Mfenesini (CCM), Suleiman Nassib Omar akiweka saini baada ya Mbunge wa Nzega, Dk Hamisi Kigwangala (kushoto) kuanza kukusanya saini za wabunge kwenye ukumbi wa bunge jana akitafuta kuungwa mkono katika hoja ya kutokuwa na imani na Spika wa Bunge, Anne Makinda.PICHA NA EDWIN MJWAHUZI

Na Neville Meena na Sharon Sauwa, Mwananchi
Dodoma: Spika wa Bunge, Anne Makinda amesema hatishwi na mchakato wa kumng’oa katika nafasi yake ambao umeanzishwa na Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangalla kutokana na tuhuma za kukiuka kanuni za Bunge.

Kadhalika Spika Makinda amepuuza hoja za Dk Kigwangalla akisema kuwa yeye hajavunja kanuni yoyote, lakini akaweka bayana kuwa mbunge huyo wa Nzega ana haki kwa mujibu wa Kanuni za Bunge kuendelea na kile anachokifanya.
“Kanuni si zinamruhusu, utaratibu upo kwenye kanuni za Bunge kwa hiyo aendelee na mchakato lakini mimi ninachosema sitetereki maana hakuna kanuni yoyote ambayo nimeivunja,” alisema Makinda katika mahojiano maalumu na Mwananchi ofisini kwake jana.

Wakati Spika akitoa kauli hiyo, jana, Dk Kigwangalla alianza harakati zake za kukusanya saini za wabunge, akitafuta kuungwa mkono katika hoja ya kutokuwa na imani naye kwa madai kwamba amekuwa akikiuka kanuni.

Miongoni mwa madai ya Dk Kigwangalla ni hatua ya Makinda kufanya uteuzi wa Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, tofauti na kanuni zinazotaja wenyeviti kuchaguliwa na wajumbe wa kamati.
Hoja nyingine ni kamati hiyo ya bajeti kulipwa posho ya Sh430,000 wakati wajumbe wa kamati nyingine wamekuwa wakipewa Sh130,000 pamoja na kumteua Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba kuingia katika kamati hiyo ya bajeti wakati mbunge huyo ni Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu.

Jana Dk Kigwangalla aliwasilisha hoja yake kwa Katibu wa Bunge na kuongeza madai mapya yakiwamo ya kuagiza kwa mabavu majedwali ya mabadiliko ya sheria kwenda kwenye kamati ya bajeti, kuvunja masharti ya kanuni ya 48 inayotoa maelekezo ya namna ya kuwasilisha na kujadili jambo la dharura na kutumia madaraka yake vibaya kwa kuvunja masharti ya Sheria ya The National Assembly (Administration) Act (Cap.115) ya mwaka 2008.

Makinda akijibu hoja hizo jana alisema alifanya uteuzi wa Chenge kuongoza Kamati ya Bajeti kwa sababu kamati hiyo ni mpya na haikuwapo katika kamati za awali, hivyo ni wazo ambalo lilitokana na mawazo ya Bunge la sasa.

“Tulikuwa tunafikiria jinsi Bunge linavyoweza kuisadia Serikali ipate vyanzo vipya vya mapato. Kwa hiyo tumehitimisha wazo hili kwa kuamua kuwa na Kamati ya Bajeti. Kamati hii haikuwapo na wala utaratibu wake wa kikanuni haukuwapo. Niliamua na kanuni zinanipa uwezo huo kwamba niteue mtu ambaye ninaamini anaweza kuisimamia katika hatua za mwanzo ili tuone uzoefu utatufikisha wapi,” alisema Makinda na kuongeza:

“Kamati hii hata Serikali ilikuwa haikubaliani na sisi, lakini katika muda mfupi wa utendaji wake umefanya kazi kubwa na kama tusingekuwa na Mzee Chenge ambaye ni mzoefu na anafahamu vizuri utendaji wa Serikali basi tungeshindwa na mimi siko tayari kuanzisha kitu halafu nikashindwa”.

Kuhusu posho, Spika aliungana na kauli ya Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah kwamba si wakati wote Kamati ya Bajeti imekuwa ikipewa malipo zaidi, bali ni pale tu wanapofanya kazi nje ya siku na saa za kazi tena kwa kibali chake.

“Lazima walete maombi na waeleze kwa nini wanapaswa kufanya kazi kwa muda wa ziada au siku za mapumziko na mimi nikisharidhia basi wanalipwa mara mbili ya viwango vya kawaida na hiyo ni kwa mujibu wa taratibu na Kanuni zetu,” alisema.
Kadhalika alizungumzia suala la wabunge wengine kuteuliwa kuingia kwenye kamati ambazo si zao ambapo alisema, suala hilo pia ni la kawaida kwani hata katika mjadala unaoendelea wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ameongeza wajumbe wa ziada.

“Ninafanya hivyo kupanua wigo wa mjadala na mara nyingi kwa mfano kwenye kamati yetu ya Katiba nimeongeza wabunge wenye uelewa wa masuala ya sheria ili watusadie kufanya uchambuzi, maana unaweza kukuta kwenye kamati, watu wenye utaalamu kuhusu suala husika ni wachache. Kwa hiyo siyo kosa kwa mujibu wa Kanuni zetu,” alisema Makinda.

Ukusanyaji saini
Kwa upande wake Dk. Kingwangalla jana alikuwa akiendelea na ukusanyaji wa saini za wabunge huku akisema kuwa amewasilisha kwa Katibu wa Bunge kusudio la kupeleka bungeni hoja yake.

Ukusanyaji wa saini ulifanywa kwa kupitia fomu maalumu na kutoa taarifa kwamba wabunge wa CUF na NCCR-Mageuzi, wote wameshasaini katika fomu hizo.
Akizungumza jana katika viwanja vya Bunge, Dk Kigwangallah, alisema wabunge wa Chadema, walimweleza kuwa watafanya hivyo baada ya kukutana katika kikao cha pamoja.

Hata hivyo Kiongozi wa Upinzani Bungeni ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alikiri kusikia taarifa hizo lakini akasema walikuwa bado hawajaketi kama kambi ili kuwa na msimamo wa pamoja kuhusu suala hilo.
Jana asubuhi wakati wa kipindi cha maswali na majibu, Dk. Kingwangalla alionekana akipita katika baadhi ya meza za wabunge akiwashawishi kusaini fomu za kumuunga mkono.

Hadi jana mchana wabunge wa CCM, na CUF wapatao 30 tayari walikuwa wamesaini fomu hizo, wakimuunga mkono mbunge huyo.
Alipoulizwa ulazima wa kukusanya saini za wabunge wakati kanuni hazimtaki kufanya hivyo alisema, hilo linamwezesha kujua nguvu aliyonayo katika kumuunga mkono kuhusiana na suala hilo.

Hoja zake
Katika taarifa ya kusudio lake ambalo Mwananchi imebahatika kuliona, Dk. Kingwangalla alisema uteuzi wa Serukamba ni kinyume na masharti ya kanuni ya 116(3) na (4).

Alisema Juni 27, 2013, wakati wa kutunga sheria ya fedha, Spika aliagiza kwa mabavu kuwa wabunge wote wenye majedwali ya mabadiliko waende kwenye kamati ya bajeti.
“Uamuzi huu wa Spika ni wa kidikteta na unapingana na masharti ya kanuni ya 88 ya kanuni za kudumu za Bunge ambapo kwa ufupi ni kwamba majedwali ya mabadiliko hujadiliwa bungeni wakati wa kamati ya Bunge zima na huamuliwa kukubaliwa ama kukataliwa na Bunge zima na si kamati yoyote ya Bunge,” alisema.

Alisema hatua hiyo ya kuipa mamlaka makubwa kamati hiyo ni kuondoa mantiki ya uwepo wa Bunge lilopewa mamlaka ya kutunga sheria zote za nchi na Katiba ibara ya 63 (3) ( c) na (d ).

Pia alisema Spika Makinda amekuwa wa kwanza kuvunja masharti ya kanuni anazopaswa kuzitilia nguvu kama anavyoelekezwa na kanuni ya 5 (2). Amevunja pia kanuni na hivyo anastahili kuhukumiwa na kuadhibiwa kwa mujibu wa masharti ya kanuni hizi ili kukidhi masharti ya Ibara ya 84 (7) (d) ya katiba ya kumwondoa madarakani.

Alitoa mfano wa hoja ya dharura iliyotolewa wakati MV Skagit ilipozama Julai 18, 2012 na siku zilipowasilishwa hoja mbili zinazohusiana na mauaji ya kwenye vurugu zinazohusu migogoro baina ya jamii za wakulima na wafugaji na wanyang’anyi wa mali na unyanyasaji wa wafugaji unaofanywa kwenye operesheni tokomeza ujangili.

Katika kuhitimisha taarifa hiyo, Dk Kingwangalla alisema: “Ni maoni yangu binafsi na ya wabunge wengi wanaoniunga mkono kuwa Spika wa Bunge Anne Makinda apumzishwe kazi kwa tuhuma nilizozitaja hapo juu.”
Chanzo: Mwananchi

Zitto, Lema katika vita ya maneno



Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu hali ya vurugu  zinazoendelea Mtwara katika sakata la mradi  Gesi asilia kuja Dar es Salaam.PICHA NA VENANCE NESTORY
Na Neville Meena, Mwananchi

Dodoma: Wabunge Wawili Maarufu wa Chadema, Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini) na Godbless Lema (Arusha Mjini) wameingia katika vita ya maneno ambayo chanzo chake ni kauli ya Lema aliyotoa katika kikao cha wabunge (briefing) kilichofanyika mjini Dodoma Jumanne wiki hii.

Lema akizungumza katika kikao hicho, anadaiwa kutoa maneno ambayo yalitafsiriwa na wabunge wengi kuwa yalikuwa yakimlenga Zitto kuhusu hatua yake ya kukataa posho na kumtuhumu kwamba ana ukwasi ambao unapaswa kuhojiwa.
Gazeti hili lilimtafuta Lema likirejea taarifa iliyotolewa na Zitto akilalamika kwamba Lema alimshambulia katika kikao hicho cha wabunge wote na kwamba alikuwa akimlenga yeye.

Lema, hata hivyo, alikiri kuzungumzia suala hilo akisema:
“Mimi sikumtaja mtu, kwahiyo kama kuna mtu analalamika hilo ni suala jingine, ila mimi nilimaanisha nilichokisema”.

Hata hivyo, Zitto alieleza kuwa msimamo wa Lema ulikuwa unapingana na wabunge wengine wa Chadema, ambao waliwahi kupendekeza kuwa posho zifutwe.
Zitto alisema kuwa yeye mwenyewe, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika waliwahi kupendekeza kuwa posho zifutwe.
“Mimi sipokei posho kabisa, posho za vikao na ndiye mbunge pekee ambaye hapokei posho ya vikao tangu mwaka 2011,” aliongeza Zitto, ambaye anahudhuria mkutano unaozungumzia uendeshaji wa Serikali kwa uwazi huko London, Uingereza.

Zitto alisema malipo ya wabunge mpaka sasa ni makubwa sana ukilinganisha na hali ya wananchi wakati Serikali ikishindwa kulipa vizuri walimu na wauguzi.
“Hatuwezi sisi kama wabunge kuanza kulilia posho, wakati wananchi wetu hawana maji, hatuwezi kulilia posho. Mbunge anayetaka posho zaidi akafanye kazi nyingine na awaachie wanaoweza kuwakilisha watu waendelee,” alisema Zitto.

Lema, hata hivyo, alisema kwamba katika mkutano huo aliweka bayana kwamba umasikini siyo uzalendo na kusisitiza kuwa wabunge wanapaswa kuwa na maslahi bora na wakati huohuo wana wajibu wa kuwatetea watumishi wengine wa umma.
“Nilisema huwezi kuzuia taasisi moja kupewa maslahi bora eti tu kwa sababu watumishi wengine hawalipwi vizuri, ni haki wabunge kulipwa vizuri na wakati huo wapiganie maslahi ya watumishi wengine,” alisema Lema na kuongeza:

“Kwahiyo nikasisitiza kwamba nawashangaa wale ambao wanakataa posho ya Sh80,000 na ukienda kuchunguza wanakatwa fedha zote kutokana na mikopo waliyochukua, lakini bado wakija sehemu kama Arusha wanalala kwenye hoteli ya gharama kubwa kati ya Dola za Marekani 150 na 600”.

Alisema katika mazingira hayo kunakuwapo maswali mengi yasiyokuwa na majibu na kwamba mbunge wa aina hiyo alitakiwa anapokuwa katika mji wowote nchini aishi katika hoteli yenye thamani kati ya Sh20,000, 30,000 na hata Sh50,000.
“Kwa hiyo ikiwa unakataa posho ya Sh80,000 halafu unalala chumba cha Dola 600 hustahili kupata credibility (sifa) stahili, ni unafiki tu na kutafuta sifa za kipuuzi,”alisema Lema.

Alisisitiza kwamba wabunge wa Tanzania hawalipwi ipasavyo na kwamba kudai malipo ya ziada hakuwaondolei wajibu wao wa kuwatetea watumishi wengine wa umma ambao pia malipo yao ni kidogo.

“Kuna hatari ya kuona kwamba Sh80,000 au Sh200,000 ni fedha nyingi, ni kwamba kama sisi wabunge tutalipwa Sh50,000 basi maana yake ni kwamba walimu au polisi tutaridhika wakilipwa hata Sh10,000,”alisema
Chanzo: Mwananchi