Maafisa
wa Umoja wa Mataifa na wanaharakati kutoka Jumuiya za kiraia wamesema sera madhubuti
kuzungumzia umaskini, njaa na uharibifu wa mazingira ni njia pekee ya
kuondokana na baa la njaa na umaskini.
Katibu
mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon ametaja kuwa zaidi ya watu bilioni moja
bado wanaishi katika umaskini wa kupindukia na zaidi ya watu milioni 840
wanakabiliwa na njaa.
Danielle
Nierenberg, mmoja wa waanzilishi wa shirika lisilokuwa la kiserikali
linaloshughulikia masuala ya chakula lenye makao yake nchini Marekani, amesema
inapaswa kutafuta njia za haraka za kuondokana na baa la njaa na umaskini,
duniani.
Wakati
wa mkutano kupanga mpango wa maendeleo endelevu ya milenia utakaozinduduliwa
rasmi mwakani, maafisa hao wamesema kuwa bado kuna nafasi kubwa ya kukabiliana
na mzizi unaosababisha umaskini na ukosefu wa chakula na njia sahihi za kuzuia
uharibifu wa mazingira.
Hivyo
basi serikali, wafanyabishara, wakulima na mashirika ya kiraia, watambue kwamba
wakati wa kuchukua hatua ni sasa, hususan katika kipindi hiki ambapo mabadiliko
ya tabia nchi yanachukua nafasi katika dunia nzima, anasema Nierenberg ambaye
pia ni mkurugenzi wa zamani wa mpango wa chakula na kilimo, mjini Washington.
2030
kikomo cha umaskini na njaa?
Mkutano
wa viongozi wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa chini ya uenyekiti wa wakuu wa
nchi kutoka Indonesia, Liberia na Uingereza mwaka jana ulitoa mwongozo uliolenga
kuondoa umaskini na njaa hadi ifikapo mwaka 2030, lakini ni namna gani lengo
hilo litafanikiwa iliachwa mikononi mwa kamati maalum iliyoundwa ikijumusha
nchi 30 mwanachama wa Umoja wa Mataifa, ambayo inatarajia kuwasilisha
mapendekezo yake mwakani.
Mpango
wa maendeleo ya milenia; unalenga kupunguza hadi kufikia nusu ya idadi ya watu
wanaoishi katika umaskini wa kupindukia na baa la njaa ifikapo mwaka 2015,
ingawa lengo hilo linaweza lisifikiwe na mataifa mengi maskini, hasa kutoka
Bara la Afrika.
Ingawa
kwa mujibu wa mkurugenzi msaidizi wa Shirika la Kilimo na Chakula, Jomo Kwame
Sundaram, ameliambia shirika la habari la IPS kuwa shirika hilo bado
linajitolea kusimamia lengo lake kuhusu usalama wa chakula na lishe, ikiwa ni
pamoja na kuondoa umaskini na utapiamlo na kwamba ni vigumu kubainisha ni kwa
vipi malengo ya maendeleo ya milenia yamechangia kupunguza idadi ya watu
wanaoishi kwenye umaskini.
Wasi
wasi kufikiwa lengo la milenia
Kufuatia
kuundwa kwa kamati ya ngazi za juu kuangalia usalama wa chakula duniani na
ikizingatiwa kupanda kwa bei ya vyakula mapema mwaka 2008, katibu mkuu wa Umoja
wa Mataifa Ban Ki-Moon alionyesha wasi wasi wake kuhusu kufikiwa kwa lengo hilo
la milenia la kuondokana na njaa.
Mwaka
jana katibu mkuu huyo alimteua mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kilimo na Chakula,
Jose Graziano da Silva alipozindua kampeni ya kutokomeza baa la njaa, wakati wa
mkutano wa 20 mwaka jana kuhusu masuala ya chakula.
Maafia
hao wamesema kuwa mapambano dhidi ya ukosefu na uharibifu wa chakula ni mfano
mzuri wa namna wakulima, wafanyabiashara na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali
yanavyoweza kufanya kazi kwa pamoja kutengeneza miundo mbinu iliyo bora, kulinda
mazao, na kuwa na njia bora za upatikanaji wa chakuala ambacho kingeweza
kuharibiwa.
Wamesema
kuna umuhimu mkubwa kuzingatia suala la kilimo na njia mbadala za kutatua
matatizo kama vile changamoto za kimazingira na kijamii ikiwa ni katika ukosefu
wa ajira, migogoro,ongezeko la watu mijini na hata mabadiliko ya tabia nchi,
wakati wa mikutano kutathimini malengo ya maendeleo ya milenia mwakani.
Mwandishi:
Flora Nzema/IPS
Mhariri:
Mohamed Abdul-Rahman
No comments:
Post a Comment