Friday, February 15, 2013

HAYA NDIYO YALIYOZUNGUMZWA NA MTANZANIA UGAIBUNI ATISHIWA KUUAWA


NA EVARIST CHAHALI, USKOCHI

Makala yangu katika RAIA MWEMA Tole la Feb 13 "Tishio la uhai mlangoni kwangu"

JUMAMOSI Februari 2 mwaka huu itabaki katika kumbukumbu zangu kwa muda mrefu, pengine katika uhai wangu wote.

Majira ya saa 3 asubuhi nilikurupushwa usingizini na kelele za mlango uliokuwa ukigongwa kwa nguvu. Wakati ninajiandaa kwenda kufungua mlango, nikasikia sauti yenye dharura ikisema, “bwana Chahali, polisi hapa, tafadhali fungua mlango.”
Nilichanganyikiwa kwani tangu nifike nchi hii zaidi ya miaka 10 iliyopita sijawahi kufanya kosa lolote au kukwaruzana na vyombo vya dola/sheria.

Baada ya kufungua mlango, askari waliovalia kiraia walijitambulisha na kuonyesha vitambulisho vyao. Pia walinisihi kuwa nisiwe na hofu ya kudhani kwamba nimefanya kosa lolote.

Kwa kifupi, walinieleza kuwa wamepewa ujumbe kutoka moja ya taasisi za intelijensia za hapa kuwa kuna tishio la uhakika dhidi ya maisha yangu. Hata hivyo, walieleza kuwa kwa vile wao walipewa tu ujumbe huo na kutakiwa kuuwasilisha kwangu, hawakuwa na maelezo ya ziada. Walisisitiza kuwa nichukue tahadhari muhimu na kunipa maelekezo ya mawasiliano ya dharura.

Kwa vile nilikurupushwa usingizini, awali taarifa hiyo ilionekana kama ndoto iliyokuwa inaendelea hata baada ya kutoka usingizini. Ilinichukua takriban saa tatu kuzinduka kutoka katika mshituko huo, na kutambua uzito wa taarifa niliyopewa na polisi hao.
Nikaamua kwenda kituo kimoja cha polisi kupata ufafanuzi zaidi. Mara baada ya kujitambulisha, mazingira ya namna suala hilo lilivyokuwa likishughulikiwa kituoni hapo lilinipa picha kuwa jambo hilo lina uzito. Kwa kifupi, baada ya kitambo nilipewa ufafanuzi ambao haukutofautiana na maelezo niliyopewa awali na polisi walionitembelea katika makazi yangu.

Kikubwa ni kuwa taarifa hiyo ilionyesha kuwa tishio hilo dhidi ya maisha yangu linatokea huko nyumbani. Swali linaloendelea kunisumbua kichwa ni KWA NINI iwe hivyo.
Wakati si vigumu kwangu kuhisi wahusika wa mpango huo wa kijahili, napata shida kuelewa kwanini wahusika hao watumie fedha za walipakodi kuandaa operesheni ya kutaka kunidhuru ilhali ninaamini kwa asilimia 100 kuwa mimi si tishio kwa usalama wa Taifa letu.

Ndiyo, baadhi ya ninayoandika kwenye makala zangu na tweets zangu huko kwenye mtandao wa kijamii wa twitter yanaweza kuwachukiza baadhi ya watu, lakini kwa hakika kuchukizwa huko si sababu ya kutaka kunidhuru.

Hadi wakati ninaandika makala hii nimekuwa nikiishi kwa tahadhari kubwa. Faraja kubwa kwangu inatokana na sababu tatu za msingi. Kwanza, kwa vile nilizaliwa na kukulia katika familia inayomtanguliza Mungu katika kila jambo, nina imani kubwa kuwa mamlaka pekee kuhusu uhai wangu (yaani kuwa hai au kufa) ni Mungu pekee. Hakuna mwanadamu anayeweza kupora jukumu hilo la Mungu na kufanikiwa kufupisha uhai wa yeyote.

Pili, nina imani kubwa na taasisi za usalama za hapa Uingereza. Kimsingi, wenzetu hawa wanathamini sana usalama na uhai wa binadamu pasi kujali mhusika ni mzaliwa wa hapa au ni ‘mgeni’ kama mimi. Ushauri na sapoti ninayoendelea kupata inanipa matumaini makubwa kuwa nipo kwenye ‘mikono salama.’

Lakini tatu ni ukweli kwamba takriban miaka mitano sasa nimekuwa nikiishi na uelewa kwamba kuna baadhi ya watu huko nyumbani wanaoniona kama kimelea cha maradhi hatari ambacho kikiachwa bila kudhibitiwa kitazua balaa.

Kwa sababu hiyo, tangu wakati huo nimekuwa nikiishi kwa tahadhari japo si kubwa kama hii ninayolazimika kuichukua sasa. Lakini ili uweze kuchukua tahadhari ni lazima uwe na mbinu na ujuzi wa kuchukua tahadhari husika. Kwa bahati nzuri, watu hao wanafahamu fika kuwa nina ujuzi wa kutosha na kuelewa na kumudu fika mbinu za kuishi kwa tahadhari.

Hata hivyo, kumudu mbinu ni suala moja na kuishi kwa kutumia mbinu hizo ni kitu kingine. Si jambo la kupendeza hata kidogo kuishi ukiwa na uelewa kuwa siku moja, mahala fulani unaweza kukumbana na madhara fulani. Lakini kadri unavyolazimika kuishi kwa namna hiyo inakuwa kama sehemu muhimu ya maisha yako, na ndivyo ilivyo kwangu.

Pamoja na kuchukulia kwa uzito taarifa hizo za tishio dhidi ya uhai wangu, nimechukua hatua nyingine kadhaa ikiwa ni pamoja na kuwafahamisha watu ninaohisi kuwa ndio wahusika wa mpango huo dhalimu kwamba ni ukosefu wa busara wa hali ya juu kupoteza fedha za walipa kodi kutaka kunidhuru.

Ingekuwa vema raslimali zinazotumika kufanikisha mpango huo zikaelekezwa kwenye uchunguzi wa mabilioni ya fedha za Watanzania yaliyofichwa kwenye mabenki nchini Uswisi huku nchi yetu ikikabiliwa na deni kubwa la ndani na nje la zaidi ya shilingi trilioni 30!

Licha ya kuwa na mwangaza kuhusu mahala linakoanzia tishio hilo kutoka huko nyumbani, sina hakika kama ni mkakati wa kitaasisi au ndiyo yaleyale niliyowahi kuandika katika makala yangu moja huko nyuma juu ya kuwapo kwa rogue elementskatika taasisi zetu nyeti.

La muhimu kwangu kwa sasa ni kuhakikisha kuwa majahili hao hawafanikiwi katika azma yao. Pia sioni haja ya kuvifahamisha rasmi vyombo vya dola huko nyumbani. Itoshe tu kusema hapa kwamba mipango kama hii katika zama hizi haina tena tija.

Hakika suala hili limenikera sana lakini ninajitahidi kuzingatia busara za mwandishi wa Laws of Power, Robert Greene, ambapo kanuni ya 21 inausia kuwa “Play a Sucker to Catch a Sucker – Seem Dumber than your Mark” (yaani, kwa tafsiri isiyo rasmi, jifanye mjinga kumnasa mjinga).

Kanuni hii inasema, ninanukuu, “No one likes feeling stupider than the next persons. The trick, is to make your victims feel smart – and not just smart, but smarter than you are. Once convinced of this, they will never suspect that you may have ulterior motives” (hakuna mtu anayependa kuonekana mpumbavu zaidi ya mtu mwingine. Ujanja ni kumfanya mlengwa wako ajione mwerevu, na si mwerevu tu bali mwerevu zaidi yako. Pindi akaamini hivyo, hatohisi kuwa una nia kubwa zaidi yake).

Nimalizie makala hii kwa kusisitiza kuwa vitisho kama hivi kamwe havitonizuwia kusimamia ukweli na kuuhubiri pasi kumhofia mtu au taasisi.
Ninatambua yaliyowakumba baadhi ya waandishi wa habari wa nyumbani.
Kwangu hizo ni chachu za kuendeleza walichoanzisha.

Kadhalika, ni vema walioandaa mpango huo dhalimu wakatambua kuwa licha ya kitendo hicho kuwa na uwezekano wa kuharibu ‘mahusiano ya kiusalama’ kati ya nchi yetu na Uingereza (kwa kuwatwisha mzigo usio wa lazima kuhakikisha mimi kama mkazi wa nchi hii sidhuriwi), lakini pia kinakwaza kiapo changu cha utii kwa nchi yangu (nilipokuwa mtumishi wa umma) ‘kuyaacha mambo fulani yaendelee kubaki yasiyopaswa kuongelewa hadharani.’ Laws of Power ya 19 inasisitiza, “Never offend a wrong person” (kamwe usimkorofishe mtu asiyestahili).

"If you're not ready to die for it, take the word 'freedom' out of your vocabulary" ~ Malcom X

Souece: Gazeti la Raia Mwema & www.chahali.com

Katibu wa Bunge, Spika Makinda wapingana Juu ya Kutorusha Runingani Vipindi Vya Bunge


Katibu wa Bunge, Thomas Kashilillah.

KATIBU wa Bunge, Thomas Kashilillah amepingana hadharani na bosi wake Spika wa Bunge, Anne Makinda kuhusu kurushwa moja kwa moja matangazo ya Vipindi vya Bunge.
Juzi katika mkutano na waandishi wa habari katika Ofisi za Bunge, Kashilillah alisema kuwa ofisi yake inakusudia kutoonyesha matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge vinavyofanyika mjini Dodoma kutokana na baadhi ya wabunge kukiuka kanuni za kibunge kwa kuvunja maadili.
Hata hivyo, kauli ya Kashilillah inapingana na ile ya Makinda aliyoitoa mjini Dodoma, Februari 8 wakati wa kuahirisha kikao cha 10 cha Bunge aliposema: “Naipongeza TBC (Shirika la Utangazaji la Taifa) kwa kuonyesha moja kwa moja matangazo na yote yanayoendelea bungeni.
“Kutokana na vurugu zilizotokea, ninaiomba Serikali kuiongezea ruzuku TBC ili kupata mitambo ya kisasa waweze kuonyesha vizuri matangazo yake, safari hii matangazo yalikuwa yanakatika katika sana,” alisema Makinda.
Hata hivyo, kauli hiyo wakati wa kufunga Bunge ilikuwa ni ya pili kwa Makinda kwani baada ya kutokea vurugu zilizoongozwa na baadhi ya viongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Makinda aliisifu TBC kwa kuonyesha kila kilichotokea bungeni na kuweka msisitizo kuwa lazima TBC isaidiwe ili kila kinachotokea ndani ya Bunge kionekane kwa wananchi.
Akizungumza jana kwenye Ofisi za Bunge, Kashilillah alisema kuwa vikao vinavyofanyika sasa mara nyingi vinakiuka kanuni na maadili ya shughuli za Bunge, jambo ambalo limesababisha baadhi ya wabunge kuinuka na kutoa kauli mbalimbali wakati mijadala ikiendelea.
Kashilillah alisema, utaratibu unafanyika na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ili kuangalia namna ambavyo wataweza kuonyesha shughuli za Bunge kwa vipande vipande vilivyorekodiwa kwa maeneo yanayofuata kanuni na maadili ili kuficha taswira mbaya itakayojitokeza kwa wananchi.
“Kuna ukiukwaji mkubwa wa kanuni na maadili ya vikao vya Bunge, na si kwamba wanaofanya hivyo hawafahamu, isipokuwa wanafanya makusudi au wanatafuta umaarufu kupitia vikao hivyo. Kutokana na hali hiyo, tumeamua kukaa na TCRA ili kuangalia namna ambavyo tunaweza kurusha vikao vilivyorekodiwa badala ya moja kwa moja,” alisema.
Simu za matusi na kashfa
Akizungumzia suala la Spika Makinda kutukanwa na kukashifiwa, Dk Kashililah alisema kuwa, kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali ameshawafahamu wote waliofanya hivyo na taratibu za kuwakamata zinaandaliwa.
“Tumeshawabaini, tunafahamu wanakoishi na namba zao tayari zimeanza kushughulikiwa. Hasa wale wote waliotuma ujumbe wa matusi au kupiga simu,” alisema.
Kuvunjwa kwa kamati
Kuhusu kuvunjwa kwa baadhi ya Kamati za Bunge, alisema kuwa Spika wa Bunge anaweza kuzivunja kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo utendaji wake au ushauri unaotoka kwa viongozi wa vyama vyenye uwakilishi bungeni.
Alisema kutokana na hali hiyo, waliangalia kamati ambazo zinafanya kazi kwa mwingiliano na kuhamishia shughuli zile kwenye kamati nyingine kama ilivyokuwa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ambayo shughuli zake zimehamishiwa kwenye Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC).
“Kabla ya kufanya uamuzi wa kuvunja kamati hizo, tulishirikiana na viongozi wa vyama vyote vyenye uwakilishi bungeni, hii ilisaidia kumpa mamlaka Spika Makinda kutangaza kuvunjwa kwa kamati hizo, huku baadhi majukumu yake kuhamishiwa kwenye kamati nyingine,” alibainisha.
Alisema kutokana na hali hiyo, kamati hiyo itaongezewa nguvu ili ziweze kufanya kazi kwa mujibu wa kanuni kama ilivyokuwa awali, jambo ambalo ni sawa na uboreshaji wa kazi zao.
“Hii si mara ya kwanza kufanyika suala hilo, hata kipindi cha Spika Adam Sapi aliwahi kuvunja kamati hizo na kuhamishia shughuli zake kwenye kamati nyingine.”
Hoja ya Mnyika
Alisema kuwa kitendo cha Spika Makinda kuiondoa hoja ya Mbunge wa Ubungo, John Mnyika si ukiukwaji wa kanuni, bali hoja yake ilijibiwa na Waziri wa Maji, Prof Jumanne Maghembe.
“Wakati Mnyika anawasilisha hoja yake, anayejibu hoja ni mwakilishi wa Serikali na wakati ule alikuwa Waziri Maghembe na kusema kuwa, hoja ya hiyo tayari imo kwenye mpango mkakati wa utekelezaji wa mradi wa maji wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mnyika alipaswa kuwasilisha mabadiliko ya hoja ili iweze kuzaa  hoja, lakini alishindwa badala yake Spika akaiondoa mezani,”alifafanua.

Source: www.mwananchi.co.tz

Ashangaa Serikali kutumia takwimu za kale



MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba amesema ni aibu kwa Tanzania kutumia takwimu za miaka ya nyuma ambazo zinatumia gharama kubwa kifedha na muda mwingi badala ya kuwa njia mbadala na rahisi ya kupata takwimu kwa wakati.

Lipumba alisema hayo juzi wakati akizungumza machache kwenye hafla fupi ya uzinduzi wa Mpango wa Sauti za Wananchi ambapo alitoa pongezi kwa Taasisi ya Twaweza kwa juhudi zao za kutumia simu za mkononi ili kupata maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi.

Profesa huyo alisema jitihada hizo zitawawezesha kukusanya taarifa kwa njia ya simu ambayo itatumia gharama ndogo lakini kwa ufanisi pia ina uwezo wa kuwafikia Watanzania waishio kila upande wa nchi. “Tunahitaji kujua taarifa halisi zinazogusa maeneo ya wananchi ambayo Serikali inatakiwa kuyafanyia kazi kupitia sera zake,mfano Sera ya Serikali ya wazee ambayo inawataka wapate matibabu bila malipo, je inafanya hivyo…,hivyo kupitia mpango huu tunaweza kupata taarifa halisi,”alisema.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kariuki alitoa pongezi kwa niaba ya Serikali kwa Twaweza ambao ndio waandaaji wa mpango huo akisema una umuhimu kwa wananchi na kwa Serikali pia katika kupata maoni yao na kuandaa sera ambazo zinakidhi haja na matakwa ya wananchi.

Kariuki alisema mpango huu ni wakupata maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi hususani yanayohusu afya,elimu na maji, ili kujua ni jinsi gani sekta hizi zinatoa huduma kwao namna ambavyo Serikali inawajibika.
Source: www.mwananchi.co.tz

MAGAZETINI LEO IJUMAA, 15, 2013 NA chiwambo's Blog






Thursday, February 14, 2013

NAFASI ZA UALIMU 26,537 ZATANGAZWA


Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dk. Shukuru Kawambwa.(Picha na Maktaba).


Jumla ya waalimu 26,537 wameajiriwa na serikali kwa mwaka wa fedha 2012/13. Walimu wa ngazi ya cheti walioajiriwa ni 13,568. Kati yao walimu 13,527 wamepangiwa kufanya kazi katika shule za msingi zilizopo kwenye halmashauri na walimu 41 wamepangwa katika shule za msingi za mazoezi zilizopo chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Jumla ya walimu wa sekondari na vyuo vyuo vya ualimu walioajiriwa ni 12,973 wakiwemo walimu walimu wa shahada 8,887 na wa stashahada ni 4,086.