maandamano dhidi ya gesi asilia ya Msimbati mkoani Mtwara.
VURUGU za kupinga ujenzi wa bomba la
kusafirisha gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam uliotulia kwa takriban wiki
mbili sasa, umeibuka upya.
Vurugu hizo ziliibuka upya juzi baada ya jengo la Ofisi ya Chama cha Mapinduzi
(CCM), kata ya Majengo Mtwara Mjini, kuchomwa moto usiku wa kuamkia juzi na
kundi la watu wasiojulikana.
Habari zinasema kuwa hakukuwa na madhara makubwa ya tukio hilo kutokana na
umati mkubwa wa watu kujitokeza kuzima moto huo.
Hadi moto huo unazimwa, milango na madirisha ya ofisi hiyo, ilikuwa imeteketea
kabisa.
Mbali ya kuchoma jengo hilo, kundi hilo lilichoma matairi ya magari katika
mitaa mbalimbali ya eneo hilo na kusababisha hofu kubwa kwa wananchi hao.
Hata hivyo uchunguzi wa gazeti hili, umebaini kuwa chanzo cha chokochoko hizo
mpya ni viongozi wa muungano wa vyama vya upinzani kushindwa kuwapa wananchi
majibu ya kikao chao cha siri cha hivi karibuni kati yao na Waziri Mkuu Mizengo
Pinda, kilichofanyika kwa zaidi ya saa sita nyumbani kwake, jijini Dar es
Salaam.
Habari zinasema kuwa viongozi hao waliporudi Mtwara hawakusema yaliyojiri Dar
es Salaam kitendo kilichochochea fujo na kusababisha kiongozi wa msafara huo, Hamza
Masudi Licheta kupigwa na wananchi wa Mtwara kwa tuhuma kuwa amewasaliti.
Hivi karibuni, viongozi wa muungano wa vyama vya TLP, NCCR Mageuzi, CHADEMA,
Sau, APPT Maendeleo, DP, UDP, na ADC, walishiriki mkutano na Waziri Mkuu Pinda
usiku kujadili suala la mzozo wa gesi ya Mtwara.
Haikubainika sababu hasa zilizofanya mkutano huo ufanyike usiku nyumbani kwa
Waziri Mkuu na ambao haukuripotiwa na chombo chochote cha habari.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi wenzake, mwenyekiti wa umoja huo, Hamza
Masudi Licheta, alisema:
“Sisi tulisafiri toka Mtwara kuja Dar es Salaam kuonana na Waziri Mkuu kwa
sababu alipokuwa Mtwara aliondoka kabla hatujafikia muafaka, hatukukubali kama
Waziri Mkuu alivyosema, aliondoka mapeka kuwahi Dodoma na sababu aliyotoa
alipokuwa Mtwara alisema anawahi Dodoma kwa kuwa uwanja wa ndege wa Dodoma
hauna taa, jambo lililomlazimu kuondoka Mtwara kwa harakaharaka.”
Alipoulizwa na gazeti hili nani aliratibu safari yao kuja Dar es Salaam
alisema, “Utaratibu wetu uliratibiwa na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, na
tulikuja tukafanya mkutano kuanzia saa mbili hadi saa saba usiku.”
Uchunguzi wa gazeti hili unaonyesha kuwa viongozi hao walisafiri toka Mtwara
kuja Dar es Salaam na walilala katika nyumba ya kulala wageni inayoitwa Kisuma,
iliyoko jijini Dar es Salaam.
Aliongeza: “Sisi hatukuitwa na Waziri Mkuu, sisi ndio tulitaka kuonana naye
kumwambia kuwa wananchi wa Mtwara hawajamwelewa katika taarifa yake aliyotoa
bungeni Dodoma, pili tulimtaka yeye aondoe ile marufuku ya mikutano ya hadhara
kwani Waziri wa Mambo ya Ndani amepiga marufuku mikutano yote ya hadhara huko
na sasa tunashindwa kuwaelimisha wananchi kuhusu suala hilo na kadiri wananchi
wanavyokosa taarifa ndio hali inazidi kuwa mbaya sasa wananchi wameanza
kutupiga na kututuhumu kuwa tumehongwa kwa kuwa hatuwezi kufanya mikutano
kuelezea kilichotokea katika mkutano tuliofanya usiku nyumbani kwa Pinda Dar es
Salaam.”
Hamza aliongeza, “Tumeenda kwa Waziri Mkuu ili kumwambia kuwa hatumtaki mkuu wa
mkoa, hata kama aliomba radhi, sisi wananchi wa Mtwara hatuko tayari kufanya
naye kazi, hatutampa ushirikiano, hivyo tulitegemea kuwa Waziri Mkuu
angemwambia Rais, na kesho (leo) tumeambiwa Balozi wa Nigeria nchini anakuja
Mtwara, hivyo hatutaki aandamane na mkuu wa mkoa.
Alipoulizwa nani aliwalipia gharama za safari toka Mtwara kuja Dar es Salaam na
kurudi pamoja na malazi, alisema: “Huwa tuna utaratibu wa kuomba wananchi,
hivyo tuna mfuko wa muungano wa vyama vya upinzani.”
Hata hivyo uchunguzi wa gazeti hili, umebaini kuwa kauli ya Waziri Mkuu kuwa
wananchi wa Mtwara wameelewa suala la gesi kupitia viongozi wao imeongeza utata
kutokana na mkutano huo wa usiku na viongozi wa vyama vya siasa.
Mwanasiasa mmoja maarufu nchini ambaye hakutaka kutajwa jina amehoji, “Kama
Waziri Mkuu alieleweka Mtwara, kikao cha usiku na viongozi wa vyama vya
upinzani ulikuwa wa nini? Kulikuwa na kitu gani cha kujadili kwa siri hadi
viongozi waliporudi Mtwara hawakutoa taarifa kwa wananchi?”
Taarifa ya Waziri Mkuu aliyoitoa Bungeni, Januari 31, 2013 ilionyesha kuwa
amefanikiwa kumaliza mgogoro wa gesi Mtwara, kitendo ambacho kilisifiwa na
wananchi wengi akiwemo Rais Jakaya Kikwete.
Wakati akitoa taarifa Bungeni, Pinda alisema kuwa amekutana na makundi
mbalimbali Mtwara na baada ya kufanya nao mazungumzo, wamemuelewa na kuacha
vurugu.
“Mheshimiwa Spika, kama utakavyoona, kiwango cha vurugu na uharibifu wa mali za
serikali na raia kilikuwa kikubwa. Kufuatia hali hiyo, Januari 27, 2013,
nililazimika kukatisha safari yangu ya kuja Bungeni Dodoma na kwenda mkoani Mtwara,”
alisema.
Kwa mujibu wa Pinda, lengo la ziara
yake ilikuwa kujionea hali halisi ya ulinzi na Usalama mkoani Mtwara, kupata
taarifa rasmi za matukio mbalimbali yaliyotokea katika siku za hivi karibuni
mkoani humo.
Kutoka Juma Mtandablog